Kombe la Dunia 2022: Uamuzi wa Kuipa Qatar nafasi ya kuwa mwenyeji ilikuwa 'kosa'-Blatter

Rais wa zamani wa Fifa Sepp Blatter

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa zamani wa Fifa Sepp Blatter anasema uamuzi wa kuipa nafasi Qatar kuhodhi michuano ya Kombe la Dunia la 2022 ulikuwa "kosa".

Blatter mwenye umri wa miaka 86, alikuwa rais wa shirikisho la soka duniani wakati Qatar ilipotunukiwa kandarasi ya kuhodhi mashindano hayo mwaka 2010.

Nchi hiyo ya Ghuba imekosolewa kwa msimamo wake kuhusu mahusiano ya watu wa jinsia moja, rekodi ya haki za binadamu na kuwatendea isivyo haki wafanyakazi wahamiaji. " Nchi ni ndogo sana . Kandanda na Kombe la Dunia ni kubwa mno," aliliambia gazeti la Uswizi la Tages Anzeiger.

Kombe la Dunia la Qatar, ambalo ni la kwanza kuandaliwa Mashariki ya Kati katika historia ya miaka 92 ya michuano hiyo na la kwanza wakati wa majira ya baridi kali ya Ukanda wa Kaskazini, litafanyika kuanzia tarehe 20 Novemba hadi 18 Desemba.

Blatter alisema Fifa ilirekebisha vigezo vilivyotumika kuchagua nchi zinazoandaa kombe la dunia mwaka 2012 baada ya kuibuliwa wasiwasi kuhusu jinsi wanavyotendewa wafanyakazi wahamiaji wanaojenga viwanja vya Kombe la Dunia nchini Qatar. "Tangu wakati huo, masuala ya kijamii na haki za binadamu yanazingatiwa," aliongeza.

Sepp Blatter alijiunga na Fifa kama mkurugenzi wa ufundi kwa mara ya kwanza mwaka 1975 na alichaguliwa kuwa rais mwaka 1998.

Chanzo cha picha, Getty Images

Blatter alitumia miaka 17 akiwa rais wa Fifa lakini alilazimika kuachia ngazi mwaka 2015 kwa madai kwamba alipanga kinyume cha sheria uhamisho wa faranga milioni mbili za Uswizi ($2.19m; £1.6m) kwa rais wa zamani wa Uefa Michel Platini, ambaye pia alilazimika kujiuzulu nafasi yake kwenye Fifa.

Awali alifungiwa kwa miaka minane, baadaye ikapunguzwa hadi sita, kutokana na malipo ya Platini. Mnamo Machi 2021 alipokea marufuku ya ziada hadi 2028 kwa "ukiukaji mbalimbali" wa kanuni za maadili za Fifa.

Blatter na Platini walishtakiwa kwa ulaghai Novemba mwaka jana lakini hawakupatikana na hatia katika kesi nchini Uswizi mwezi Julai.

Uamuzi wa kutoa kandarasi ya Kombe la Dunia la 2018 na 2022 kwa Urusi na Qatar mtawalia umegubikwa na tuhuma za ufisadi ulioenea, huku uchunguzi ukizinduliwa na waendesha mashtaka wa Uswizi na Idara ya Sheria ya Marekani mnamo 2015.

Qatar na Urusi siku zote zimekuwa zikikanusha makosa yoyote, na zote zilifutiliwa mbali na uchunguzi wa Fifa mnamo 2017.