Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump atafanya nini siku ya kwanza Ikulu?
- Author, Laura Blasey & Jessica Murphy
- Nafasi, BBC News World
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Donald Trump na Chama chake cha Republican wana udhibiti wa Bunge la Marekani. Timu yake ya kampeni imesema kutarajiwe msururu wa maagizo kutoka kwa rais wa Marekani katika wiki ya kwanza.
Wataalamu wa sera na wanasheria tayari wanatayarisha maagizo hayo kama sehemu ya mabadiliko ya utawala.
Vikundi vya utetezi na magavana wa majimbo yanayosimamiwa na Democratic wameapa kupinga baadhi ya maagizo hayo.
Uhamiaji na mpaka
Katibu wa masuala ya habari wa Trump, Karoline Leavitt aliiambia Fox News siku ya Jumapili "tunajua aliahidi kutia saini agizo la kulinda mpaka wa kusini."
"Tunajua atazindua operesheni kubwa ya kuwahamisha wahamiaji wengi sana katika historia ya Marekani," alisema.
Ndani ya wiki moja tangu kuchaguliwa tena, Trump ameanza kujaza nafasi za uongozi ambazo zitasimamia suala uhamiaji, na anajiandaa kushughulikia mipango yake juu ya sera ya mpaka mapema.
Amemteua afisa wa zamani wa jeshi la uhamiaji Tom Homan kusimamia mipaka, amemchagua Gavana wa Dakota Kusini, Kristi Noem kusimamia usalama wa nchi, na kumteua Steven Miller kama naibu mtendaji mkuu katika Ikulu ya White House katika kusimamia sera.
Bw Miller anafahamika kwa kuunda sera za Trump zinazoweka vikwazo juu ya wahamiaji haramu katika muhula wake wa kwanza.
Sera yoyote ya uhamisho wa watu wengi inaweza kukabiliwa na changamoto za kimipango na msururu wa changamoto za kisheria kutoka kwa wahamiaji na wanaharakati wa haki za binadamu.
Trump pia anapanga kutekeleza tena sera yake ya "Baki Mexico" ambayo inawataka wanaotafuta hifadhi kusubiri Mexico wakati madai yao yanashughulikiwa.
Rais Joe Biden aliuita mpango huo "usio wa kibinadamu" na kujaribu kuuondosha katika siku yake ya kwanza ofisini, lakini alikabiliwa na changamoto za kisheria. Mwaka 2022, Mahakama ya Juu ilimruhusu kuuondoa.
Wakati wa utawala wa Trump, takribani waomba hifadhi 70,000 walirudishwa Mexico kusubiri kesi zao kusikilizwa wakiwa makwao.
Ahadi nyingine ni kukomesha uraia wa kuzaliwa – sheria iliopo kwa miaka 150, inasema mtu yeyote aliyezaliwa katika ardhi ya Marekani ni raia wa Marekani.
Haijulikani wazi jinsi Trump anavyopanga kutekeleza sera hii. Uraia wa kuzaliwa ni haki iliyo wazi katika Katiba ya Marekani, kumaanisha kuwa inaweza tu kubadilishwa kwa sababu maalum.
Atahitaji majimbo kukubaliana au kura ya thuluthi mbili ya kuunga mkono katika Bunge la Congress – ambalo limegawanyika, ili kupitisha mabadiliko, kisha kuidhinishwa na robo tatu ya mabunge ya majimbo - ambayo Republican wanadhibiti zaidi ya nusu yake.
Januari 6
Trump hakutaja msamaha katika hotuba yake ya ushindi, lakini kwa muda mrefu anataka kuwasamehe wale waliopatikana na hatia ya kuvamia Capitol mwaka 2021.
"Oh, kabisa, nitawasamehe. Ikiwa hawana hatia, nitawasamehe," Trump alisema wakati wa mkutano na Chama cha Kitaifa cha Wanahabari Weusi.
Marais wa Marekani wana mamlaka makubwa ya kusamehe watu waliopatikana na hatia ya uhalifu wa shirikisho au kumaliza vifungo vyao gerezani.
Waendesha mashtaka pia wanaweza kuamua kufuta kesi zinazosubiri kusikilizwa - kutegemea nani rais anataka kumsamehe.
Jambo lisilo wazi ni nani atapata msamaha huo.
Trump aliiambia CNN: "Nitawasamehe wengi wao. Siwezi kusema kila mmoja, kwa sababu baadhi yao, labda walivuka mstari."
Bi Leavitt aliliambia gazeti la Washington Post kwamba ataamua "kwa msingi wa kesi kwa kesi atakaporudi White House."
Zaidi ya watu 1,500 walikamatwa kuhusiana na ghasia za Capitol. Zaidi ya 750 kati yao walihukumiwa kwa uhalifu kuanzia kuingia bila ruhusa hadi kuwashambulia maafisa wa polisi na njama za uchochezi.
Jack Smith
Trump pia anakabiliwa na changamoto zake za kisheria baada ya uchaguzi wa 2020 na kesi juu ya hati za siri.
Wakili Maalumu Jack Smith, ni mwendesha mashtaka wa zamani ambaye aliteuliwa na Idara ya Haki ya Marekani, kusimamia uchunguzi dhidi ya Trump. Lakini rais mteule anakana kesi zote.
Trump amesema kumfukuza kazi Jack Smith itakuwa moja ya vipaumbele vyake vikubwa.
"Nitamfukuza kazi ndani ya sekunde mbili. Atakuwa mojawapo ya mambo ya kwanza kuyashughulikia," alisema katika mahojiano mwezi Oktoba.
Kesi hiyo tayari ilikuwa inakabiliwa na mustakabali usio na uhakika. Mahakama ya Juu zaidi iliamua mwezi Julai kwamba marais wana kinga fulani ya kutoshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa matendo yao wakiwa ofisini, na hilo limehujumu kesi ya Smith.
Ushindi wa Trump katika uchaguzi pia unampa mamlaka ya kujisamehe makosa yoyote ya shirikisho, ingawa hakuna rais aliyefanya hivyo hapo awali.
Inaelezwa kuwa Idara ya Haki iko katika mazungumzo na Smith kuhusu kumaliza kesi hizo. Haijulikani iwapo Trump anaweza kwenda mbali zaidi na kumwadhibu Smith.
Trump amekuwa akimsuta mara kwa mara wakili huyo katika mahojiano, akimtaja kuwa "mtu mpotovu", "mpumbavu" na matusi mengine.
Mkataba wa Paris
Katika kampeni yake ya 2016, Trump aliweka ahadi ya kujiondoa katika makubaliano ya tabia nchi ya Paris. Ndani ya miezi sita baada ya kuchukua madaraka, Marekani iliondoka kwenye mkataba huo muhimu.
Rais Joe Biden alijiunga tena na kuufanya mkataba huo kuwa mojawapo ya sera muhimu alipochuana na Trump mwaka 2020. Biden alitia saini barua ya kutaka Marekani irejeshwe kwenye mkataba siku yake ya kwanza ofisini.
Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa timu ya Trump inaandaa maagizo ya kujiondoa kwa mara nyingine atakapoingia madarakani mwezi Januari.
Kuondoka kwenye mkataba huo kutamaanisha Marekani haipo tena kwenye malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.
Miongoni mwa vipaumbele vya Trump vinavyokinzana na mkataba wa Paris, ni kutaka kuzalisha mafuta na gesi.
"Tutachimba, tutachimba, tutachimba," alimwambia mtangazaji wa Fox News, Sean Hannity mwaka jana.
Trump pia amekosoa mipango ya utawala wa Biden ya kuongeza uzalishaji wa nishati ya upepo na kuongeza uzalishaji wa magari ya umeme, huenda akayalenga mambo hayo mapema katika utawala wake mpya.
Urusi na Ukraine
Katika kampeni, Trump alisema anaweza kumaliza vita vya Urusi na Ukraine "kwa siku moja." Pia amekuwa akikosoa uungaji mkono wa serikali ya Marekani kwa Ukraine, akisema vita hivyo vinakausha rasilimali.
Bado hajatoa maelezo kuhusu atakavyojadiliana ili kumalizika vita hivyo - zaidi ya kusema atasaidia nchi hizo mbili kufikia makubaliano.
Tangu kuchaguliwa tena, Trump alizugumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika simu ambayo ilidumu "karibu nusu saa," huku bilionea Elon Musk pia akishiriki. Chanzo kimoja kiliiambia BBC "hayakuwa mazungumzo ya mambo muhimu."
Ikulu ya Kremlin ilikanusha kuwa Trump alifanya mazungumzo na Vladimir Putin, ingawa ripoti za vyombo vya habari zilisema Trump alimuonya rais wa Urusi dhidi ya kuzidisha vita nchini Ukraine.
Biashara na uchumi
Uchumi ni suala ambalo Trump alilifanyia kampeni sana, akiapa kukomesha mfumuko wa bei mara tu atakapoingia madarakani.
"Tutashughulikia kila kitu kuanzia uwezo wa kumudu gari hadi kumudu nyumba, gharama za bima hadi masuala ya ugavi," alisema Trump.
"Nitaliambia baraza langu la mawaziri kwamba natarajia matokeo chanya ndani ya siku 100 za kwanza, au mapema zaidi kuliko hapo."
Alisema atatia saini amri ambayo inaelekeza kila katibu wa baraza la mawaziri na mkuu wa shirika "kutumia mamlaka waliyo nayo" kuondoa mfumuko wa bei na kupunguza bei kwa watumiaji.
Mpango wa Trump ni pamoja na kutoza ushuru wa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, haswa zile zinazoingia kutoka China, akisema ushuru huu utawezesha utengenezaji wa bidhaa nchini Merika.
Bado haijulikani ni kiasi gani cha ushuru ataweka, lakini matarajio ni 10% ya ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, na ushuru wa 60% kwa bidhaa kutoka China.
Pia ameapa kuilenga Mexico na ushuru.
"Nitamfahamisha (rais wa Mexico) siku ya kwanza au mapema, ikiwa hawatakomesha uvamizi huu wa wahalifu na dawa za kulevya zinazoingia nchini mwetu, nitaweka ushuru wa 25% kwa kila kitu wanacholeta Marekani,” alisema.
Ushuru huu hautahitaji idhini ya bunge. Kifungu cha 232 cha Sheria ya Upanuzi wa Biashara cha 1962, kinampa rais mamlaka ya kutoza ushuru kwa bidhaa ambazo zinaweza kuathiri usalama wa taifa la Amerika.
Rais mteule pia ameapa kumfuta kazi Gary Gensler, mwenyekiti wa Tume ya Usalama na Ubadilishanaji fedha, siku ya kwanza. Gensler, aliyeteuliwa na Biden, alipendekeza sheria za kuweka wazi uzalishaji wa hewa chafu kwa makampuni na utekelezwaji wa kanuni kali kuhusu sarafu ya mtandaoni.
Trump ametetea sarafu ya mtandaoni, na ushindi wake uliifanya thamani ya Bitcoin kupanda kwa 30%, kutokana na matarajio kwamba utawala wake utakuwa na sera rafiki zaidi.
Title X
Donald Trump ameapa kutengua mabadiliko yaliyofanywa na Rais Biden kwa Title X, mpango pekee wa kitaifa wa kupanga uzazi unaofadhiliwa na serikali.
Mwaka 2019, wakati wa muhula wake wa kwanza, utawala wa Trump ulitekeleza sheria mpya ambayo ilikataza mtoa huduma yeyote wa afya katika mtandao wa Title X kutaja utoaji wa mimba kwa wagonjwa, hata kama mgonjwa aliuliza yeye mwenyewe kuhusu hilo.
Mabadiliko hayo yaliondoa mamilioni ya dola kutoka katika mashirika kama vile Planned Parenthood ambayo hutoa huduma au kuelekeza wagonjwa kuhusu uavyaji mimba.
Lakini miezi michache baadaye, Biden alipochukua madaraka, alibadilisha sera hiyo. Sasa, inatarajiwa Trump ataibadilisha sheria hiyo tena.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa ana Ambia Hirsi