Waridi wa BBC: Walimu waliuliza huyu ‘bubu’ anafuata nini shuleni?
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mnamo mwaka 2009, jina la Aneth Gerena Isaya lilipasua vichwa vya Habari kadhaa nchini Tanzania, wakati wa sherehe za mahafali ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, kwa kuwa alikuwa mtu wa kwanza asiye na uwezo wa kusikia kufanikiwa kuhitimu shahada ya saikolojia chuoni hapo na vilevile kuwa mtu wa kwanza mwenye ulemavu wa aina hiyo kufika ngazi hiyo ya elimu ya juu kwa nchi nzima.
‘Siku ya mahafali yangu, chuo kiliniletea mkalimani toka nje ya chuo na leo simuiti mkalimani tena bali ndio mume wangu,’anasimulia Aneth.
Ili kuhakikisha anapata huduma zote za kitaaluma na kijamii akiwa mwaka wa kwanza, Aneth alianzisha msukumo wa ombi lake kuhakikisha anapata mkalimani kwa ajili ya kumtafsiria kile kinachofundishwa kwa kuwa alikuwa haelewi kitu katika ufundishaji wa elimu ya kawaida.
Waswahili wanasema safari ni hatua, pamoja na panda shuka ya kitaaluma na mazingira magumu kwa watu wenye ulemavu kupata ajira, Aneth sasa ni Mkurugenzi wa taasisi ya Furaha Ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi ijulikanayo kama FUWAVITA.
Taasisi ya FUWAVITA ikishirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) inatoa mafunzo ya ujasiriamli kwa wanawake viziwi wanaohitajika kuendesha biashara zao. Kwa sasa Aneth anajivunia kuwafikia wanawake 3500 ambao wanapata kipato kupitia bidhaa wanazotengeneza, kama vile mikate,siagi, mvinyo, keki na kadhalika.
Anasema taasisi hiyo imeweza kumkomboa mwanamke kiziwi kwa namna moja au nyingine , na pia imeweza kuongeza wigo mkubwa tangu mwaka 2018 alipoianzisha akiwa na wanawake watano, na sasa taasisi yake inafika mikoa mbalimbali kama Dodoma, Iringa, Mbeya, Shinyanga na maeneo mengine.
Hali ya kutosikia ilianzaje?
Chanzo cha picha, Aneth
Alizaliwa akiwa anasikia kama watu wengine, ila alipofika umri wa miaka mitano hali ilibadilika kwani alipata ugonjwa wa kuvimba mashavu na koo ambao ulimfanya awe na ulemavu wa kutosikia.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku ambayo alianza kutosikia , dada yangu hakuamini alinipiga hata makofi kwa kudhani kuwa anamfanyia ujeuri, wakati yeye mwenyewe alikuwa haelewi kilichokuwa kimemtokea.
“Kila nikiwaeleza walikuwa hawanielewi na hawaamini kile kilichonitokea.
Kwa vijijini huwa tunasaidiwa na dawa za kienyeji nikawa naweka maji ya moto kwenye masikio na baba yangu alikuwa ananipa matumaini kuwa nitapona tu.”
Anasema mpaka walipoamua kumpeleka hospitali ya kawaida, miaka miwili ilikuwa imeshapita.
Na madaktari wakasema wameshachelewa sana ni bora tu apelekwe shule ya viziwi.
Ila watu wake wa karibu ilikuwa ni vigumu kwa wao kuamini, “Walidhani nimerogwa tu, hali yangu iliwachukua muda mrefu sana kukubali uhalisia waliona ni jambo la ajabu sana”.
Jamii ya viziwi haikuwa inafahamika sana katika jamii aliyokulia, mpaka sasa wazazi wake hawaielewi.
“Zamani nilikuwa naweza kuongea ila kwa kuwa nimekuwa natumia lugha ya ishara kwa muda mwingi sauti ilianza kupotea kidogo kidogo mpaka sasa ni kama imepotea kabisa,”anasimulia Aneth.
Kuanza kutengwa na jamii haswa katika upande wa elimu
Chanzo cha picha, Aneth
Aneth anasema alianza kuona ananyanyapaliwa tangu akiwa mdogo,
“Watoto wenzangu walianza kuniita ‘bubu’ na kuacha kunitambulisha kwa jina langu na walikuwa hawataki kucheza na mimi tena. Nakumbuka jinsi nilivyokuwa napenda sana kucheza mchezo wa Kombolela lakini nilipoacha kusikia sikucheza tena mpaka nilipoenda shule ya viziwi ndio niliweza kucheza michezo mingine na viziwi wenzangu .”
Alipoingia sekondari ndio alianza kuingia darasani kusoma na watu wote, hali ilikuwa ngumu kwake lakini alifanikiwa kufaulu na kupata daraja la tatu licha ya kuwa walimu walikuwa hawaelewi lugha ya alama.
“Nilipopata barua kuwa nimechaguliwa kusomea ualimu Sumbawanga, nikasema Hapana kabisa, kupambana kote na nimefaulu kuingia kidato cha tatu na bado ninaambiwa kusomea kitu nisichotaka ni ngumu sana na nina hamu ya kwenda kidato cha tano na sita..
Walisema hamna kidato cha tano na sita chenye walimu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kusikia, na mimi niliuliza huko Sumbawanga kwani kuna walimu maalum, nao walijibu hakuna.
Nikasema sasa hali ni sawa, bora tu niendelee na sekondari badala ya kwenda chuo kwa kuwa kote ni sawasawa tu.”
Baada ya majadiliano hayo, mwishowe walimuandikia kumuandikia barua ya kupeleka wizara ya elimu.
Lakini shule aliyopangiwa huko Iringa, hali ilikuwa hiyohiyo ya kukataliwa.
“Siku nilipofika shule, mwalimu aliniangalia na kuuliza maswali kweli huyu anaweza huyu.
Mwalimu aliyenipokea aliniangalia juu mpaka chini na kuniangalia tena, huyu na kuuliza huyu kusoma anaweza kweli kwanza atasoma vipi?’
Shule hiyo iliandika tena barua wizarani kuwa arudi nyumbani, “nililia sana sana kwa kuwa niliona wanakatisha ndoto zangu.
Kwa sababu ya kulia sana, walinionea huruma, wakaniambia niwe naingia darasani ili waweze kujiridhisha.
Kila wakati walikuwa wanaulizana huyu ‘bubu’ anafuata nini shuleni.
Baada ya muda waliandika tena barua ,wizara ya elimu kuwa mtu waliomleta haingii darasani, analala tu hovyo.
Watu wa wizarani waliamua kuja wenyewe shuleni kuniona, na nikawaeleza ni kweli ninalala kwa kuwa sielewi licha ya kuwa na moyo wa kusoma.
Wakawa wananipa moyo, wakasema nikipata division 4, wataelewa na kunipa muda zaidi.
Ila nikapata nguvu mpya, baada ya kuniahidi kuniletea mkalimani ingawa nilikuwa siamini kama wataniletea, niliamua kutafuta rafiki wa kumfundisha lugha ya alama.
Nilipata rafiki anaitwa Clara ambaye alikuwa msaada mkubwa sana kwangu, nilimfundisha kwa juhudi zote ili aweze kujua lugha yangu .
Sikuletewa mkalimani mpaka namaliza kidato cha sita, na majibu yalipotoka nilipata daraja la pili.
Chanzo cha picha, Aneth
Wizara ya elimu hawakuamini kabisa na walisema walidhani ningepata daraja sifuri. Waliamua kunifanyiwa sherehe kubwa sana, waliwaza kuwa bora wafungue kitengo maalumu cha watu wenye ulemavu wa kusikia.’
Na hatimaye aliweza kuingia chuo kikuu cha Dar es salaam, ila anasikitika kuwa Rafiki yake aliyemsaidia kuelewa walichokuwa wanafundishwa alipata chuo kingine.
‘Wakati ninaingia chuo, kulikuwa hakuna kiziwi, kulikuwa na walemavu wengine.
Nilipofika chuo nilikuwa nazuga tu kuwa darasani, nilikuwa sielewi chochote, niliona wanaongea ongea tu.Nilikuwa naona aibu wenzangu wanaandika , hivyo nami nikawa ninazugazuga tu.
Nilienda kugonga mlango kwa mkuu wa chuo kumwambia hali yangu na changamoto niliyopitia.
Kwanza mkuu wa chuo alisema kukushauri ni uende Marekani chuo maalum ndio kuna chuo kizuri cha watu wa hali yangu.
Ila mimi nikamwangalia kwa mshangao, ‘mimi niende Marekani kwa gharama zipi’, nikawaambia njia ni moja tu, ajirini mkalimani.
Niliambiwa niende nikapumzike miezi miwili ila baada ya mwezi mmoja niliitwa kuwa ameajiriwa mkalimani mmoja.
Nilipofika mwaka wa tatu, mkalimani mwingine akaajiriwa.
Na mpaka namaliza chuo, viziwi wengi walijiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam na sasa wanakuja kwenye taasisi yangu kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Hivyo tunaendelea kushirikiana na chuo kikuu cha Dar es salaam katika kuwezesha mawasiliano yawe rahisi kwa viziwi.
Chanzo cha picha, Aneth
Maisha ya ujana na mahusiano
Chanzo cha picha, Aneth
Aneth anasema katika kipindi cha ujana wake, alikuwa anaogopa kuwa na mahusiano na watu ambao hawana ulemavu, “Ni kweli nilikuwa na mpenzi lakini alikuwa kiziwi kwa kuwa nilikuwa siamini kuwa mtu ambaye hana ulemavu anaweza kunipenda kabisa kabisa.
Nilikuwa naogopa wanaweza kunipa mimba na kuniacha bure.
Niliandikiwa barua nyingi za kuambiwa kuwa wananipenda, ila nilikuwa staki kulala na yeyote mpaka atakayefika nyumbani na kutoa mahari ndio nitamuamini.”
Anasema wakati anakuwa alikuwa ana hofu ya Mungu, na alielewa kuwa wanaume ni wengi na alijua ni muhimu kutimiza malengo yake kwanza.
Toka kuwa Mkalimani hadi kuwa mume wake ilikuwaje?
Siku ya mahafali yake, chuo kilileta mkalimani wa lugha ya alama kutoka nje kwa ajili ya siku hiyo moja.
Mtaalamu huyo wa lugha ya alama, ndio alikuja kuwa mume wake baada ya kuonana mara moja tu.
‘Wakati wa mahafali , mkalimani aliniuliza kama nina mchumba, nikamwambia sina, akasema sasa nimemaliza chuo si bora nikubali niolewe na yeye.
Alionesha kiu yake sana ya kuwa na mimi, alienda kwa wazazi .
''Jina langu lilikuwa linavuma sana yani moto kwelikweli umepamba kwa kuwa mtu wa kwanza kiziwi kupata shahada… wakati huo, naona aliona hii fursa ni vyema aitumie alipokutana na mimi kwa mara ya kwanza''.
Maisha yake ya sasa yakoje?
Chanzo cha picha, Aneth
Anneth kwa sasa ni mke na mama wa watoto wanne.
Anasema anamshukuru Mungu kwa kuwa mawasiliano yao ni mazuri sana na mume wake na ''ninamshukuru Mungu kwa kunipa yeye''.
“Amekuwa msaada mkubwa katika Maisha yangu binafsi na hata ya ofisi.
Anasaidia watoto kuweza kuwasiliana na mimi, maana watoto hawajui lugha ya alama.
Watoto wakubwa tunawasiliana kwa kuandika ila mtoto wangu mdogo mwenye miaka miwili anajaribu kuongea kwa alama.
Anaiga jinsi baba yake anavyoongea na mimi, kwa sasa anajua jinsi ya kuomba chakula kwa lugha ya alama na nina furaha sana.’
Aneth aliongeza kusema kuwa;
‘Mimi sikuwa nina uwezo wa kutumia shimisikio kwa kuwa ina kelele na ile ni kwa ajili ya wale ambao wanasikia kwa kiwango kidogo ila mimi sisikii kabisa, kwangu ni kelele tu haikuwahi nisaidia katika Maisha yangu yote.
Kwa sasa Aneth anaona kuwa kiziwi ni jambo analojivunia kwa kuwa kupitia changamoto alizopitia katika maisha yake katika kupata elimu na ajira, ameweza kuwa msaada kwa watu wengine viziwi.
Baada ya kumaliza chuo, alipata unyanyapaa wa kupata ajira kwa sababu ya hali yake ya kutosikia na sasa anatoa ajira kwa wasiosikia.
Imehaririwa na Munira Hussein
Habari kuu
Gumzo mitandaoni
Zinazovuma zaidi
Haipatikani tena