Jenerali wa Bolivia Gary Prado Salmon aliyemkamata mwanamapinduzi wa Cuba afariki dunia

Che Guevara

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Che Guevara kwenye picha hii nchini Cuba mwaka 1965 - alikuwa waziri wa viwanda wakati huo

Jenerali wa Bolivia aliyemteka mwanamapinduzi wa Cuba Ernesto "Che" Guevara na kuwa shujaa wa taifa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84.

Mnamo mwaka wa 1967 Gary Prado Salmon aliongoza operesheni ya kijeshi huko Bolivia, akiungwa mkono na mawakala wa huduma ya siri ya Marekani, ambayo ilishinda uasi wa kikomunisti ulioandaliwa na Che Guevara.

Wakati huo Bolivia ilikuwa na serikali ya kijeshi ya mrengo wa kulia.

Afisa wa jeshi alimuua Guevara mzaliwa wa Argentina siku moja baada ya kukamatwa kwake.

Vita Baridi kati ya Marekani na Muungano wa Kisovieti vilikuwa katika kilele chake na Washington ilikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ushawishi wa kikomunisti katika Amerika ya Kusini, ikiwa ni pamoja na shughuli za Che Guevara.

Alikuwa ameondoka Cuba baada ya ushindi wa mapinduzi ya 1959, kuongoza harakati za msituni katika nchi zingine. Alikuwa mshirika mkuu wa kiongozi wa kikomunisti wa Cuba Fidel Castro na akawa shujaa wa wakomunisti duniani.

Mtoto wa Jenerali Prado alimuelezea baba yake kama "mtu wa ajabu", ambaye aliacha "urithi wa upendo, uadilifu na ujasiri".

Pia uanaweza kusoma:

Afisa wa Bolivia aliyempiga risasi na kumuua Che Guevara alikuwa Mario Terán, aliyefariki mwaka jana.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kuvizia kundi la waasi la Guevara Jenerali Prado alifanywa kuwa shujaa wa taifa kwa kutetea utawala wa kijeshi wa Bolivia.

Alikuwa ameiongoza Bolivian Rangers iliyofunzwa na Marekani katika eneo la msituni ambako kundi la Che Guevara, ambalo awali lilikuwa na takriban 120, lilipungua hadi 22 tu.

Tangu mwaka wa 1981 Jenerali Prado amekuwa mtumiaji wa kiti cha magurudumu, baada ya risasi kumpiga kwa bahati mbaya kwenye uti wa mgongo. Aliandika kitabu kuhusu ushindi wake wa 1967, kinachoitwa How I Captured Che.

Kulingana na mwanawe, "kwake kumkamata Che halikuwa jambo muhimu zaidi alilofanya maishani mwake - badala yake, ilikuwa ni kuchangia kufanya jeshi kuwa taasisi ya kidemokrasia ambayo ingeheshimu katiba na sheria".

Che Guevara aliuawa katika kijiji cha La Higuera huko Bolivia , 830km (maili 516) kusini mwa La Paz, na mwili wake ulizikwa mahali pa siri. Mnamo 1997 mabaki yake yaligunduliwa, yakafukuliwa na kurudishwa Cuba, ambapo alizikwa tena.