Kawira Mwangaza :Mfanyakazi wa zamani wa nyumbani ambaye sasa ni gavana
Anne Ngugi
BBC Swahili

Nyumbani kwa Kawira Mwangaza gavana mteule wa Kaunti ya Meru nchini Kenya bado kuna hali ya vifijo na nderemo , baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho huku watu wengi wakiwa wamefika kumpa pongezi ,vile vile mitaani Meru ushindi wake ni moja ya gumzo za mitaani kwani watu wanajiuliza ni mbinu ipi ambayo aliitumia kumuondoa mwanasiasa mkongwe na ambaye amebobea katika siasa za Meru kwa miongo mingi Kiraitu Murungi.
“Tangu tulipoanza kampeini , nilisikia jinsi mpinzani wangu kisiasa alivyokuwa akinipapura kwa majina yasio ya kupendeza , ila mimi nilitabiri na kumweleza kwamba nitahakikisha nimembwaga , sasa ukitizama matokeo , mpinzani huyo Kiraitu Murungi alikuwa wa tatu na sasa atajibu nini ? ”Mwangaza alisnahoji wakati akihojiwa na BBC.
Kiongozi huyu ameweka historia katika siasa za eneo hilo la Meru , kwanza ni mwanamke wa pili kuchaguliwa katika nyadhifa za kisiasa katika eneo hili ambazo kwa miongo mingi zimekuwa zinatawaliwa na wanaume, vile vile ametwaa ushindi yeye mwenyewe akikiri kwamba kutoka kwa jamii ya Meru ambayo wanawake hawajapewa sauti kutokana na mila ila sasa anasema kwamba mambo yamebadilika .
Kawira Mwangaza hakuwa kwenye kinyang’anyiro cha wadhifa wa ugavana na tiketi ya chama chochote kikuu cha kisiasa aliamua kuwa mgombea huru , jambo ambalo limeendelea kuwashangaza wengi ni vipi aliwashawishi wapiga kura kumpigia kura kwa wingi .

“Jambo ambalo ningetaka watu wafahamu ni kwamba mimi nimekuwa mtumishi wa watu hata kabla ya kuwa katika nafasi ya uongozi , nilikuwa naingia kwenye vijiji baada ya vijiji na kuwaambia wenyeji wawachague watu ambao wana umasikini mkubwa kwa mfano wale ambao wanaishi kwa ufukara , hapo tulikubaliana nao tuwape ng’ombe , wengine tuliwapa chakula na wengine blanketi ”anakumbuka Mwangaza
Kitendo hiki anasema alikianza miaka mitatu iliyopita , ni hali iliyomleta karibu na wananchi wengi wa eneo hili la Meru , na kwa hivyo alipoanza kujinadi kwa watu kuhusu azma yake ya kuwa gavana anasema kwamba yeye hakutumia hela ila watu walimpa hela za kampeini , anasema kwamba hakuchapisha hata bango moja kujinadi ila kazi yake na wenyeji wa chini ilimtambulisha hadi kwenye debe .
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maisha yake Kawira Mwangaza hayajakuwa na mwangaza miaka ya kuzaliwa kwake hadi utu uzima .Gavana huyu mteule anasema kwamba alizaliwa katika mazingira ya umasikini mkubwa , na ilipowadia wakati wake kujiunga na shule ya sekondari ilikuwa vigumu na ilibidi awe mfanyikazi wa ndani kwa mwaka mzima huku jamii yake ikitafuta namna ya kuendeleza masomo yake
“Nakumbuka wakati nilikuwa mfanyikazi wa ndani katika nyumba ya shangazi wangu huko Marsabit , sikuwahi kata tamaa kwamba wakati mmoja ningefaulu kimaisha’ anasema Mwangaza
Ilibidi aondoke kwao Timau,Kenya hadi Kaskazini mashariki mwa Kenya eneo la Marsabit .Japo baadaye alijiunga na shule ya wasichana ya Moyale , alijitahidi kusoma kwa bidii na akaibuka wa kwanza katika mtihani wa kitaifa wa kuhitimisha masomo ya sekondari eneo hilo akipata alama ya C+.
Mwangaza anasema kwamba baada ya kukamilisha shule alihangaikia biasdhara mbalimbali za uchuuzi na kufaulu kujilipia karo wakati alijiunga na chuo kimoja Kampala Uganda
Safari ya kujitosa katika siasa
Mwaka wa 2013 aliamua kujiunga na siasa , kuwania kiti cha eneo bunge huko Timao , japo alitumia hela nyingi kitita cha shilingi milioni ishirini nza Kenya , hakuchaguliwa kama mbunge , hali hii ilipelekea jamii yake kutumbukia katika hali ya madeni na ufukara .Yeye na mumewe walijipata katika hali ya ufukara mkuu na kuanza maisha ya kuwa mchuuzi wa mboga , vitunguu na nyanya mitaani Nairobi .
Hakukata tamaa , wakati mmoja yeye na mumewe waliamua kuanzisha televisheni ambayo ingepeperusha matamgazo yake kwa lugha yake ya asili ya Kimeru .Televisheni yao ilianza na wafanyikazi wawili yeye na mumewe .Mwangaza alikuwa ni mtangazaji na mumewe alikuwa mpiga picha .

“Tulikuwa tunaingia vijijini kuangazia shida tofauti za jamii hapa meru ,Televisheni yetu tuliipa jina Baite TV, watu walikuwa wanatizama na kusisimuliwa na taarifa zetu zilizokuwa zinaangazia sana maisha ya Meru .Hapo ndipo watu walianza kunifahamu , na mimi nikaanza kufahamu shida za jamii yangu ”Mwangaza anakumbuka
Uzoefu wake kama mwanahabari wa mashinani ulimuongezea njaa ya kuwa kiongozi atakayeshughulikia shida za watu wake.Pamoja na hayo Mwangaza na mumewe ni wahubiri na vile vile walikuwa na kanisa ambalo wao ni waanzilishi
Safari ya kuwa gavana ,anasema kwamba imekuwa ni ndefu , anaamini kwamba hakuna haraka katika kuafikia makubwa anaelewa fika kwamba ana mtihani mkuu uliyo mbele yake wa kuhakikisha Kaunti ya Meru inasonga mbele kimaendeleo.
Wakati wa mahojiano haya alikuwa ameketi huku mumewe Mwarega Baichu akiwa pembeni. Mumewe alimsaidia katika kampeini kwa kutumia talanta yake ya uimbaji na weledi wake wa kupiga gita kuwarai wananchi kumchagua mke wake. Gavana huyo mteule ana sifa kedekede kwa mumewe kwa kuwa nguzo muhimu wakati wa kampeini na hata wakati wa mahangaiko yake mengi .
Mwangaza Kawira ni mama ya watoto wawili .















