'Israel imepata ushindi wa kimkakati, lakini hilo halitawazuia Hezbollah'

Chanzo cha picha, EPA
Israel imepata ushindi mkubwa wa kimkakati katika operesheni hii – ni kama aina fulani ya mapinduzi ya kuvutia ambayo ungesoma katika tamthilia ya kusisimua.
Bila shaka ni fedheha kwa Hezbollah, ambayo itaimarisha usalama wao na pengine kutekeleza mabaya zaidi.
Hata hivyo kuna uwezekano wa kujitokeza kwa athari mbaya za kimkakati kwa Israel, kwa sababu ingawa hii inafedhehesha wanamgambo wenye nguvu wa Lebanon na harakati za kisiasa, sio sababu ya kuwazuia.
Na haikaribii lengo la kimkakati la Israel la kusimamisha mashambulizi ya Hezbollah na kuruhusu Waisraeli zaidi ya 60,000 kwenye mpaka wa kaskazini ambao hawajakuwa kwenye nyumba zao kwa karibu mwaka mmoja kurejea majumbani mwao.
Waisraeli wametumia silaha muhimu, yenye ujasiri, ambayo ni wazi kuwa inafanyakazi kisawa sawa kulingana na wao.
Lakini ripoti katika Al Monitor, jarida linaloheshimika la Mashariki ya Kati, zinasema kwamba hawakuweza kuzitumia jinsi walivyotarajia.
Mpango wa awali, inasema, ulikuwa kwa Israel kufuatilia mashambulizi wakati Hezbollah ilikuwa bado inayumbayumba.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shambulizi la kutumia vifaa vya mawasiliano, ripoti zinasema, lilikuwa liwe jibu la mwanzo katika ongezeko la mashambulizi - kama sehemu ya mashambulizi ya kukabili adui au pengine uvamizi wa kusini mwa Lebanon.
Lakini ripoti hizi hizi zinasema kwamba Hezbollah ilikuwa inaendelea kushuku - na kulazimisha Israeli kuanzisha shambulio hili mapema.
Kwa hivyo Waisraeli wameonyesha kuwa wanaweza kuingia katika mawasiliano ya Hezbollah na kuonesha kwamba wanaweza kuwadhalilisha, lakini shambulizi hili haliondoi eneo hilo hata inchi moja kwenye vita. Badala yake inavichochea na kuvifanya vikaribie.
Kila kitu kwa sasa katika suala la kupungua kwa vita katika eneo la Mashariki ya Kati inategemea Gaza.
Wakati vita hivyo vikiendelea, iwe ni mgogoro na Lebanon, iwe ni mashambulizi katika Bahari ya Shamu kutoka kwa Wahouthi, iwe ni mvutano na Iraq; hakuna kitakachopungua.
Mjumbe wa Marekani nchini Lebanon Amos Hochstein amekuwa akifanya kazi kwa bidii kwa miezi kadhaa sasa - akizungumza na Walebanon, na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na Hezbollah na Waisraeli, kuhusu kujaribu kutafuta njia ya kumaliza migogoro hii kidiplomasia.
Na inasemekana, Waisraeli hawakuiambia Marekani kuhusu walichokuwa wakifanya katika mpango huu hadi dakika za mwisho - kwa hivyo hii pia, haitasaidia juhudi zake.

Chanzo cha picha, Reuters
Utabiri wa Marekani kwamba usitishaji vita huko Gaza unakaribia umewadia tena dhidi ya vitu viwili vinavyoonekana kuwa visivyoweza kutikisika.
Mmoja ni kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar, ambaye anataka Israeli iondoke kabisa katika Ukanda wa Gaza, pamoja na kuachiliwa kwa kiasi kikubwa kwa wafungwa wa Kipalestina katika mabadilishano ya mateka waliosalia wa Israel huko Gaza.
Mwingine ni waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye ameshikilia msimamo wake kwamba Israeli inaweza na itapata ushindi kamili dhidi ya Hamas.
Makubaliano huko Israeli ni kwamba ifaidike kutokana na kurefusha vita, licha ya shinikizo kutoka kwa familia za mateka na wafuasi wao ya kufikiwa kwa makubaliano ya kuwarudisha watu wao nyumbani.
Washirika wa waziri mkuu walio na msimamo mkali katika muungano wake pia wametishia kuiangusha serikali ikiwa atafikia makubaliano yoyote.
Israeli na washirika wake wanasisitiza kuwa kupeleka vita kwa maadui zake wa zamani kwa Hezbollah wa Lebanon ni kitendo halali kabisa cha kujilinda.
Kwa mara nyingine tena, kuna maswali mengi muhimu kuhusu jinsi shambulio la Israeli lilivyojeruhi na kuua raia waliokuwa karibu.
Picha za CCTV zilionyesha kifaa cha mawasiliano kikilipuka katika soko lililojaa watu wakati mmiliki wa kifaa hicho akinunua chakula. Ripoti nchini Lebanon zinasema msichana mdogo aliuawa wakati kifaa cha babake kilipolipuka.
Hezbollah itakuwa inayumbayumba kutokana na shambulio hilo, lakini itajipanga kwa haraka mno kama shirika na itatafuta njia nyingine ya kuwasiliana.
Lebanon ni nchi ndogo na ujumbe unaweza kubebwa na kuwasilishwa kwa mkono kwa urahisi.
Bila shaka Hezbollah na washirika wake nchini Iran, ambao balozi wao mjini Beirut alijeruhiwa katika shambulio hilo, watakuwa wanajiimarisha tena baada ya kudhalilika.
Lakini kwa mara nyingine tena eneo hilo limesukumwa hadi kwenye ukingo wa vita vya pande zote.
Hivi karibuni au baadaye, ikiwa hili litaendelea, watajipata wametumbukia kwenye shimo hilo.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Seif Abdalla








