Milipuko ya vifaa vya mawasiliano yawaua tisa na kuwajeruhi takriban 300 katika mashambulizi mapya kote Lebanon

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Galant anasema nchi hiyo "inafungua awamu mpya katika vita"

Muhtasari

  • Rais wa Iran azilaumu Israel na Marekani kwa shambulio la Lebanon
  • Kampuni ya Taiwan yashtushwa kuhusishwa na shambulio la Lebanon
  • Blinken anasema Marekani haikujua au kuhusika katika milipuko ya 'pager' za Hezbollah
  • Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu 12 wameuawa wakiwemo watoto wawili
  • Milipuko ya pager Lebanon: Urusi yalaani 'mashambulizi dhidi ya Lebanon'
  • Hezbollah iligeukia pager baada ya kupiga marufuku simu za rununu
  • Urusi yaamuru watu kuhamishwa baada ya shambulio la Ukraine la ndege zisizo na rubani
  • Milipuko ya Pager Lebanon: Tunachojua kufikia sasa
  • Israel ililipua pager mapema kuliko ilivyopangwa awali - ripoti
  • Korea Kaskazini yarusha makombora ya masafa mafupi kwa mara ya pili ndani ya wiki moja
  • Israel 'ilitega vilipuzi ndani ya Pager 5,000' za Hezbollah - Reuters
  • Kuonekana kwa mwezi mkuu (Super Moon) na kupatwa kwa mwezi kwawafurahisha watazamaji
  • Watoto wanne waliokwama kwenye jokofu nchini Namibia wafariki
  • Bingwa wa ndondi wa Ukraine Usyk aachiliwa baada ya kuwekwa kizuizini kwenye uwanja wa ndege – Zelensky
  • Tazama: Video ikionyesha mlipuko wa kifaa cha mawasiliano cha pager kwenye duka kubwa la Lebanon
  • Hezbollah yailaumu Israel baada ya milipuko ya kifaa cha mawasiliano kuwajeruhi maelfu nchini Lebanon

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi, Yusuf Jumah & Dinah Gahamanyi

  1. Kwaheri

    Na hadi hapo tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja leo. Asante sana kwa kufuatilia taarifa hizi .

    Kumbuka pia unaweza kuendelea kuzipata habari zetu kupitia Chaneli yetu ya WhatsApp kwa kubofya hapa

    Tukutane kesho alfajiri panapo majaaliwa.

    th
  2. Habari za hivi punde, Milipuko ya vifaa vya mawasiliano yawaua tisa na kuwajeruhi takriban 300 katika mashambulizi mapya kote Lebanon

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu tisa wameuawa na wengine zaidi ya 300 wamejeruhiwa katika milipuko ya hivi punde, wizara ya afya ya Lebanon inasema.

    Awamu mpya ya vita imeanza, waziri wa ulinzi wa Israel asema

    Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Galant anasema nchi hiyo "inafungua awamu mpya katika vita" - na "kituo cha nguvu cha mvuto wote unahamia kaskazini kupitia uelekezaji rasilimali na nguvu huko".

    Alitoa maoni hayo wakati wa ziara ya kambi ya jeshi la Israel ya Ramat David kaskazini mwa Israel.

    "Tutahitaji uthabiti , vita hivi vinahitaji ujasiri mkubwa, dhamira, na uvumilivu," aliongeza.

    Maoni hayo yatachukuliwa kama dalili kwamba Israel inaelekeza mkazo wake kuelekea Hezbollah na mzozo unaozunguka mpaka na Lebanon.

    Takriban Waisrael 60,000 wamekimbia makazi yao kaskazini mwa nchi kutokana na mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani kutoka kwa Hezbollah.

    Mapema wiki hii, serikali ya Israel ilifanya kurejea kwao kuwa lengo kuu la vita na Gallant alisema hatua ya kijeshi itakuwa chaguo pekee iwapo diplomasia itashindwa, na hivyo kuongeza matarajio ya kuongezeka kwa migogoro na Hezbollah.

  3. Rais wa Iran azilaumu Israel na Marekani kwa shambulio la Lebanon

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian sasa ameunga mkono shutuma za Hezbollah zinazodai kuwa Israel ndiyo iliyopanga ulipuaji wa vifaa vya mawasiliano vya kundi hilo.

    Katika chapisho lililowekwa kwenye tovuti yake rasmi, rais wa Iran pia anaishutumu Marekani na washirika wengine kwa kuchangia "mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni".

    Pezeshkian analaani matumizi ya vifaa "vilivyotengenezwa kwa ajili ya ustawi wa binadamu" kuwapiga watu wanaochukuliwa kuwa mahasimu kama "ishara ya kuporomoka kwa utu pamoja na utawala wa kishenzi na ukatili".

    Maoni hayo yanakuja chini ya saa moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken kukanusha kuhusika kwa Marekani katika shambulio hilo. Israel imekataa kuzungumzia milipuko hiyo.

    Maelezo zaidi:

  4. Kampuni ya Taiwan yashtushwa kuhusishwa na shambulio la Lebanon

    xx

    Chanzo cha picha, Joy Chiang/BBC

    Kampuni ya Taiwan Gold Apollo inadai vifaa vilivyotumiwa katika shambulio la jana huko Lebanon zilitengenezwa na kampuni ya Hangary iitwayo BAC Consulting.

    Mwanzilishi wa Gold Apollo Hsu Ching-Kuang alisema kampuni yake ilitia saini makubaliano na BAC miaka mitatu iliyopita, akiongeza kuwa uhamishaji wa pesa kutoka kwao umekuwa "ajabu sana".

    Kumekuwa na matatizo na malipo ambayo yalikuja kupitia Mashariki ya Kati alisema, lakini hakuingia kwa undani zaidi.

    Gold Apollo pia iliongeza kuwa ingawa BAC imetoa leseni kwa jina lao, "haikuhusika katika utengenezaji wa bidhaa".

    Mfumo wa utengenezaji wa Taiwan ni mchanganyiko tata wa kampuni ndogo, ambazo nyingi hazitengenezi bidhaa wanazouza.

    Wanaweza kumiliki jina la chapa, hati miliki na kuwa na idara za utafiti na usanifu.

    Lakini sehemu kubwa ya utengenezaji halisi hufanywa katika viwanda vya China au Asia ya Kusini-mashariki.

    Takriban watu 12 wamefariki wengine na takriban 3,000 kujeruhiwa katika milipuko ya Jumanne iliyowalenga wanangambo wa kundi la Hezbollah, ambalo limezua taharuki katika eneo la Mashariki ya Kati.

  5. Blinken anasema Marekani haikujua au kuhusika katika milipuko ya 'pager' za Hezbollah

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wakati wa zamu yake akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Antony Blinken anasema Marekani "haijui kuhusu" na "wala haikuhusika" katika kile kilichotokea nchini Lebanon na Syria siku ya Jumanne.

    Kisha anasema Marekani imekuwa wazi kuhusu umuhimu wa kuepuka hatua zinazoweza kuzidisha mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Blinken kisha anasisitiza kwamba Marekani inasalia imara katika kupata makubaliano ya kusitisha mapigano .

    Anajibu swali la pili kuhusu suala hilo, na anasema wakati safari yake ya Cairo imejikita zaidi katika "mazungumzo ya kimkakati" kati ya Marekani na Misri. ".

    "Mazungumzo ya kina" yamefanyika na Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi, Blinken anaongeza.

    Maelezo zaidi:

  6. Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu 12 wameuawa wakiwemo watoto wawili

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Afya wa Lebanon Firass Abiad anasema watu 12 wameuawa, akiwemo msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka 11.

    Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Abiad anaongeza kuwa wahudumu wa afya walikuwa miongoni mwa waliouawa katika milipuko ya 'pager' iliyotokea kote nchini Lebanon hapo jana.

    Lebanon huenda ikalazimika kupeleka baadhi ya waliojeruhiwa nje ya nchi ili kupokea matibabu maalumu.

    Akizungumza baada ya kuwatembelea waliojeruhiwa hospitalini siku ya Jumatano, Waziri wa Afya Firass Abiad anasema kuwa watu 2,750 wamesalia hospitalini baada ya kulipuliwa kwa mamia ya 'pager' za mawasiliano.

    Anaongeza kuwa baadhi ya majeruhi wamehamishiwa Iran na Syria ili kutibiwa, lakini asilimia 98 ya waliojeruhiwa wataendelea kutibiwa ndani ya nchi hiyo.

  7. Milipuko ya pager Lebanon: Urusi yalaani 'mashambulizi dhidi ya Lebanon'

    Zakharova said Moscow viewed the attack as 'another act of the hybrid war against Lebanon'

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Zakharova alisema Moscow inachukulia shambulio hilo kama 'kitendo kingine cha vita mseto vinavyohusisha makabiliano ya kisiasa na mapigano ya kutumia silaha'.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova anasema shambulio la Jumanne huko Lebanon "linawakilisha changamoto kubwa kwa sheria za kimataifa".

    Bi Zakharova anaongeza "watekelezaji wa shambulio hili la teknolojia ya hali ya juu walitaka kuchochea makabiliano makubwa ya silaha wakitaka kuibua vita vikubwa katika Mashariki ya Kati".

    Kwingineko, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameelezea kusikitishwa kwake na shambulio hilo wakati alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati, kwa mujibu wa shirika la habari la Uturuki Anadolu.

    Naibu Waziri Mkuu wa Ireland anasema anachukulia milipuko hiyo kuwa ukiukaji wa Mkataba wa Geneva.

    "Hii ni aina mpya ya vita, nadhani tunapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa na kuwa na wasiwasi kuhusu hilo na jumuiya ya kimataifa inahitaji kutafakari juu ya asili ya shambulio hilo," Micheál Martin aliwaambia waandishi wa habari huko Dublin.

    Maelezo zaidi:

  8. Hezbollah iligeukia pager baada ya kupiga marufuku simu za rununu

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kama tulivyoripoti hapo awali ni vigumu kufuatilia mawasiliano ya pager ukilinganisha na simu za rununu.

    Vyanzo vya habari viliiambia shirika la habari la Reuters kwamba Hezbollah, mapema mwaka jana, ilianza kushuku kuwa Israel ilikuwa ikifuatilia simu zao. Hivyo kufikia Februari mwaka huu, kundi hilo lilipiga marufuku matumizi ya simu zao za mkononi walipokuwa wakiendesha operesheni.

    Wanasiasa wakuu wa Hezbollah pia walikwepa kuleta simu kwenye mikutano, na kiongozi wa kundi hilo alionya kuwa simu ni hatari zaidi kuliko majasusi wa Israeli.

    Katika hotuba ya televisheni, Hassan Nasrallah aliwaambia wafuasi kuvunja, kuzika au kufunga simu zao kwenye sanduku la chuma. Badala yake waliamua kutumia pager.

    Lakini mchambuzi mmoja anasema onyo la Hezbollah kuhusu matumizi ya simu ya mkononi lilikuwa hadharani sana.

    "Hezbollah kimsingi ilitangaza kwa ulimwengu kwamba walikuwa wakipunguza kiwango cha matumizi ya simu za rununu hadi wapeja," Joseph Steinberg, mwandishi wa Cybersecurity for Dummies, aliiambia Reuters.

    "Kimsingi unamwambia adui na wapinzani wengine wowote- na( Hezbollah ina wengi tu) ni aina gani ya teknolojia unataka kutumia."

    Pager ni nini?

    Hadi tukio la jana, pager zilikuwa teknolojia ya mawasiliano iliyosahaulika.

    Zilikuwa zikionekana mara kwa mara katika hospitali na huduma za dharura lakini sasa hazizungumziwi sana, baada ya nafasi yake kunyakuliwa miaka ya 2000 na simu za rununu.

    Pager ni kifaa chenye ukubwa wa pakiti ya sigara kawaida huunganishwa kwenye vifungo vya mikanda kwa kumbukumbu ya haraka.

    Zinafanya kazi kwa kusawazisha na visambaza sauti vinavyotumia nguvu nyingi - huhitaji nyingi kati ya hizo ili kufikia eneo kubwa, tofauti na milingoti ya simu za mkononi.

    Watumiaji wa pager kila wakati wanapokea ujumbe mpya unaotumwa mara kwa mara na zinaweza kupokea taarifa za pekee - kwani hazitoi mawimbi ya mawasiliano.

    Hii ndio sababu Hezbollah iliripotiwa kuzipendelea zaidi ya simu za rununu, kwani watumiaji wa pager hawawezi kupatikana kupitia GPS au njia zingine.

    Peja inapopokea ujumbe, hutoa mlio fulani na maandishi mafupi huonyeshwa - kwa kawaida humwomba mpokeaji ampigie simu mtu huyo au aende mahali alipo.

  9. Urusi yaamuru watu kuhamishwa baada ya shambulio la Ukraine la ndege zisizo na rubani

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wakazi katika baadhi ya sehemu za eneo la Tver nchini Urusi wameamriwa kuhama baada ya shambulio "kubwa" la Ukraine ya ndege zisizo na rubani kuzua moto, gavana wa eneo hilo amesema.

    Igor Rudenya alisema wafanyakazi wa huduma za dharura katika mji wa Toropets wamekuwa wakijaribu "kuzima" moto uliosababishwa na kuanguka kwa mabaki ya ndege zisizo na rubani. Hakusema iwapo kuna majeruhi.

    Wakati huo huo, picha ambazo hazijathibitishwa zimeibuka zikionyesha mlipuko mkubwa katika mji huo.

    Kanda za video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha milipuko na moshi mkubwa ukitanda angani.

    Mashirika ya habari ya AFP na Reuters yamenukuu vyanzo vya Ukraine vikisema ghala la risasi lilipishambuliwa.

    Mkuu wa Kituo cha Ukraine cha Kukabiliana na taarifa za upotoshaji Andriy Kovalenko, alisema kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba pamoja na silaha zake kama vile roketi za Grad na makombora mbalimbali, Urusi pia imeanza kuhifadhi makombora ya Korea Kaskazini katika eneo la Toropets.

    BBC haijathibitisha madai yoyote yaliyotolewa.

    Toropets iko karibu kilomita 380 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Urusi Moscow, na kilomita 470 kaskazini mwa mpaka na Ukraine.

    Soma pia:

  10. Habari za hivi punde, Jeshi la Israel Iinasema limeshambulia wanachama wa Hezbollah usiku kucha

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema lilishambulia jengo ambalo idadi ya wanachama wa Hezbollah walikuwa jana usiku.

    Katika chapisho kwenye X, inasema vikosi vyake " vilitambua idadi ya magaidi kutoka shirika la kigaidi la Hezbollah " ambao walikuwa "wakifanya kazi karibu na kijiji cha kusini mwa Lebanon cha Majdal Salem.

    "Zikifunga duara kutoka angani, ndege za kivita zilishambulia jengo ambalo magaidi walikuwa wakiendesha shughuli zao."

    Ndege za kivita za IDF pia zilishambulia majengo ya Hezbollah katika maeneo matano ya kusini mwa Lebanon, taarifa hiyo inaongeza.

  11. Milipuko ya 'pager' Lebanon: Tunachojua kufikia sasa

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Magazeti yakionyesha vichwa vya habari kuhusu milipuko ya pager kote Lebanon siku ya Jumanne huko Beirut

    Tumekuwa tukifuatilia matukio ya Lebanon kwa karibu asubuhi ya leo baada ya watu kadhaa kufariki na maelfu ya wengine kujeruhiwa wakati pager zinazotumiwa na wanamgambo wa kundi la Hezbollah zilipolipuka siku ya Jumanne. Haya ndio mambo ambayo yamekuwa yakitokea tangu wakati huo:

    • Chanzo kikuu cha usalama cha Lebanon na chanzo kingine kimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba Mossad - wakala wa kijasusi wa Israeli - walitegaidadi ndogo ya vilipuzi ndani ya sager 5,000 za Taiwan zilizoagizwa na Hezbollah.
    • Mwanzilishi wa kampuni hiyo ya Taiwan amekana kuhusika na milipuko hiyo. Haya yanajiri baada ya picha za waigizaji kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii - ambazo zilionekana kuashiria kuwa huenda zilitengenezwa na kampuni ya Gold Apollo Company Ltd yenye makao yake Taiwan.
    • Hezbollah, pamoja na waziri mkuu wa Lebanon, wanailaumu Israel kwa shambulio hilo. Wanajeshi wa Israel wamekataa kutoa maoni yao kuhusiana na tukio hilo
    • Balozi wa Iran mjini Beirut ni mmoja wa waliojeruhiwa jana mchana. Mke wake amesema anaendelea vizuri
    • Tumesikia pia kutoka kwa watu kadhaa walioshuhudia matukio huko Lebanon na kuelezea matukio "ya kutisha"

    Unaweza pia kusoma:

  12. Israel ililipua 'pager' mapema kuliko ilivyopangwa awali - ripoti

    g

    Chanzo cha picha, social media

    Kama tulivyoripoti hapo awali, chanzo cha Lebanon na chanzo kingine kimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba Mossad - wakala wa kijasusi wa Israeli - waliweka vilipuzi katika maelfu ya pager za Hezbollah, ambazo ziliingizwa nchini miezi kadhaa iliyopita.

    Kando, vyanzo vya Israel na Marekani vinaiambia Axios na Al-Monitor kwamba milipuko hiyo ilipangwa mapema kama hatua ya kwanza katika vita vikubwa dhidi ya Hezbollah.

    Lakini katika siku za hivi majuzi, Israel iliingiwa na wasiwasi kwamba Hezbollah walikuwa wamefahamu mpango huo - hivyo walilipuwa pager hizo mapema.

    "Ilikuwa ni kulipua ama kupoteza fursa hiyo ," afisa wa Marekani anaiambia Axios.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Korea Kaskazini yarusha makombora ya masafa mafupi kwa mara ya pili ndani ya wiki moja

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Korea Kaskazini imerusha makombora mengi ya masafa mafupi siku ya Jumatano kuelekea pwani yake ya mashariki, Korea Kusini na Japan zilisema.

    Hii inajiri siku chache baada ya Pyongyang kuzindua kituo cha kurutubisha uranium na kuapa kuimarisha silaha zake za nyuklia.

    Makombora hayo yalirushwa kutoka Kaechon, kaskazini mwa mji mkuu Pyongyang, mwendo wa saa 12:50 asubuhi (sawa na 21:50 GMT Jumanne) kuelekea kaskazini-mashariki na kuruka takriban umbali wa kilomita 400 (maili 249), Wakuu wa wafanyakazi wa Korea Kusini (JCS) walisema, bila kubainisha makombora mangapi yalifyatuliwa na ni mangapi yalitua.

    "Tunalaani vikali kurushwa kwa kombora la Korea Kaskazini kama uchochezi wa wazi ambao unatishia pakubwa amani na utulivu wa rasi ya Korea," JSC ilisema katika taarifa, na kuapa majibu makubwa kwa uchochezi wowote zaidi.

    Takriban dakika 30 baada ya taarifa yake ya kwanza ya kombora, mlinzi wa pwani ya Japan alisema Korea Kaskazini ilirusha kombora jingine la ballistic.

    Waziri wa Ulinzi wa Japani Minoru Kihara alisema walau moja ya makombora hayo ililianguka karibu na pwani ya mashariki ya kaskazini mwa nchi kavu na kwamba ufyatuaji huo wa makombora "hauwezi kuvumiliwa."

    Kituo cha Marekani kinachotoa amri na muongozo wa usalama katika maeneo ya Bahari ya Hindi na Pacific (Indo-Pacific )kilisema kwenye ujumbe wake wa X kwamba kinafahamu ufyatuaji huo wa makombora na kinashauriana kwa kwa karibu na utawala wa Seoul na Tokyo.

    Korea Kaskazini ilirusha makombora kadhaa ya masafa mafupi siku ya Alhamisi iliyopita, ikiwa ni mara ya kwanza kwa makombora ya aina hiyo kurushwa katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili.

    Marekani, Korea Kusini na Ukraine, miongoni mwa nchi nyingine, zimeishutumu Pyongyang kwa kusambaza maroketi na makombora kwa Moscow kwa ajili ya matumizi katika vita vya Ukraine, ili kupata misaada ya kiuchumi na kijeshi.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Habari za hivi punde, Israel 'ilitega vilipuzi ndani ya vifaa 5000 vya 'Pager' za Hezbollah - Reuters

    .

    Chanzo cha picha, Matt De Thomiere

    Maelezo ya picha, Kifaa cha mawasiliano cha Pager

    Shirika la habari la Reuters linaripoti, kwamba shirika la kijasusi la Israel la Mossad lilitega vilipuzi ndani ya peja 5,000 zilizotengenezwa na Taiwan na kununuliwa na kundi la Lebanon la Hezbollah - miezi kadhaa kabla ya mashambulizi ya Jumanne, likinukuu chanzo kikuu cha usalama cha Lebanon na chanzo kingine.

    Reuters pia inaongeza kuwa njama hiyo inaonekana kuwa imechukua miezi mingi kufanywa, ikinukuu vyanzo kadhaa.

    Shambulio hilo lililenga Hezbollah na limeziacha hospitali nchini Lebanon zikiwa zimezidiwa - baadhi ya waathiriwa wamepofushwa, huku wengine wakihitaji kukatwa viungo.

    Kwa mujibu wa BBC Wanachama wa Hezbollah walilipuliwa kwenye maduka makubwa, barabarani, kwenye magari yao, majumbani mwao na karibu na watoto wao.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Kuonekana kwa mwezi mkuu (Super Moon) na kupatwa kwa mwezi kwawafurahisha watazamaji

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Super Moon na kupatwa kwa mwezi kwa sehemu kulionekana ulimwenguni kote - na picha hii iliyochukuliwa kutoka Jerusalemu

    Mwezi mkuu na kupatwa kwa mwezi kwa sehemu ilionekana ulimwenguni kote - na picha hii iliyochukuliwa kutoka Yerusalemu

    Mwezi umeangaza anga katika maeneo mbali mbali kote ulimwenguni sanjari na tukio la nadra la kupatwa kwa mwezi.

    Mwezi umeweza kuonekana uking'aa zaidi na zaidi Jumanne usiku.

    Miandamo mikubwa hutokea wakati Mwezi unapokuwa karibu zaidi na dunia katika mzunguko wake.

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ndege inaruka mbele ya Mwezi Toronto

    Kupatwa kwa mwezi kwa nadra kwa sehemu hutokea wakati kivuli cha dunia kinapofunika sehemu ya mwezi ambako pia kulitokea na takriban 4% ya sehemu ya mwezi ulifunikwa na giza.

    Kupatwa kwa sehemu ya mwezi kulionekana kote ulimwenguni -Usiku kutoka Jumanne hadi Jumatano, na tukio hili lilionekana wazi zaidi nchini Uingereza na Marekani.

    Kupatwa kwa jua pia kulionekana katika Amerika Kusini, Ulaya na Afrika, na vile vile sehemu ndogo za Asia na Mashariki ya Kati.

  16. Watoto wanne waliokwama kwenye jokofu nchini Namibia wafariki

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jokofu la zamani lisilofanya kazi ilikuwa nje ya nyumba (picha ya faili)

    Polisi nchini Namibia wanachunguza kifo cha watoto wanne waliokuwa wakicheza kwenye jokofu tupu katika mkoa wa Zambezi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

    Watoto hao waliokuwa na umri wa kati ya miaka mitatu na sita, walipatikana ndani ya jokofu lililotumika katika eneo lenye watu wengi katika mji wa Katima Mulilo siku ya Jumatatu alasiri.

    Polisi wanaamini kuwa watoto hao walikwama kwenye jokofu kwa bahati mbaya walipokuwa wakicheza lakini uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo.

    Kati ya watoto hao wanne, wawili walikosa hewa hadi kufa kwenye jokofu huku wengine wawili wakifia hospitalini wakipokea matibabu, shirika la utangazaji la umma liliripoti.

    "Nilipoingia, niliwaona wahudumu wa afya wakihudumia binti yangu na msichana mwingine. Waliwakimbiza hospitalini, huku wengine wawili wakiwa wamepakiwa kwenye magari ya polisi ya kuhifadhia maiti,” Aranges Shoro, mmoja wa baba wa watoto hao, aliliambia gazeti la kibinafsi la The Namibian.

    "Kulikuwa na ndoano kwenye jokofu ambayo inaweza kufunguliwa kutoka nje tu," kamanda wa polisi wa eneo la Zambezi Andreas Shilelo alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema.

    "Walikwama kwa muda wa saa moja na nusu na kukosa hewa."

  17. Bingwa wa ndondi wa Ukraine Usyk aachiliwa huru baada ya kuwekwa kizuizini kwenye uwanja wa ndege – Zelensky

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Oleksandr Usyk alishinda medali ya dhahabu baada ya kushinda ndondi za uzani wa juu mjini London 2012

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema kuwa bingwa wa ndondi za uzani juu Oleksandr Usyk ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa katika uwanja wa ndege nchini Poland.

    Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha Usyk akitolewa akiwa amefungwa pingu na maafisa waliovalia sare.

    "Nilizungumza kwa simu na Oleksandr Usyk alipokuwa kizuizini," Zelensky aliandika kwenye Telegram.

    "Nilikasirishwa na tabia hii kwa raia na bingwa wetu. "Nimewaagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Ihor Klymenko wapate mara moja maelezo yote ya tukio hilo kwenye uwanja wa ndege wa Krakow.

    "Mara tu nilipofahamishwa kuwa kila kitu kiko sawa, bingwa wetu aliachiliwa na hakuna mtu anayemshikilia tena."

    Bingwa huyo wa uzani wa juu wa mashindano ya WBC, WBA na WBO Usyk anatarajiwa kuwa London wiki hii kupambana na Daniel Dubois akitetea ubingwa wake wa IBF dhidi ya Anthony Joshua kwenye Uwanja wa Wembley.

    Unaweza pia kusoma:

  18. Tazama: Video ikionyesha mlipuko wa kifaa cha mawasiliano cha pager kwenye duka kubwa la Lebanon

    Maelezo ya video, Tazama : Mlipuko mdogo kwenye duka kubwa la bidhaa Lebanon

    Video hii, iliyoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii, inaonekana kuonyesha wakati kifaa cha mawasiliano kinachofahamika kama pager kikilipuka katika duka kubwa nchini Lebanon Jumanne alasiri. Inaonyesha mlipuko mdogo unaomjeruhi mtu mmoja anayeanguka chini.

    Maelfu ya watu walijeruhiwa na takriban wanane kufariki wakati vifaa vya mawasiliano ya ujumbe vya wanachama wa Hezbollah vilipolipuka karibu kwa wakati mmoja kote nchini Lebanon.

    Uchunguzi wa BBC Verify unaonyesha kuwa video hiyo ilipakuliwa baada ya milipuko hiyo, na tarehe na wakati ulioonyeshwa kwenye ripoti za video za CCTV za unaendana na wakati halisi wa milipuko hiyo.

    Kufikia sasa haijawezekana kuthibitisha eneo ilikochukuliwa video.

    Unaweza pia kusoma:

  19. Hezbollah yailaumu Israel baada ya milipuko ya vifaa vya mawasiliano kuwajeruhi maelfu nchini Lebanon

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Jamaa wa waliojeruhiwa na milipuko ya kifaa cha mawasiliano cha pager wakiwa katika hospitali za Beirut na kwingineko

    Watu tisa, akiwemo mtoto, wameuawa baada ya vifaa vya mikononi vinavyotumiwa na wanachama wa kundi la Hezbollah kwa mawasiliano kulipuka kote Lebanon, waziri wa afya wa nchi hiyo anasema.

    Balozi wa Iran nchini Lebanon alikuwa miongoni mwa watu wengine 2,800 waliojeruhiwa na milipuko hiyo iliyotokea kwa wakati mmoja huko Beirut na maeneo mengine kadhaa.

    Hezbollah, ambayo inaungwa mkono na Iran, ilisema vifaa hivyo vinavyofahamika kama pager ni vya "wafanyakazi wa vitengo na taasisi mbalimbali za Hezbollah" na kuthibitisha vifo vya wapiganaji wanane.

    Kundi hilo liliilaumu Israel kwa kile lilichokiita "uchokozi huu wa uhalifu" na kuapa kwamba "italipiza kisasi". Jeshi la Israel lilikataa kutoa maoni kuhusu tuhuma hizo.

    Saa chache kabla ya milipuko hiyo, baraza la mawaziri la usalama la Israel lilisema kusitisha mashambulizi ya Hezbollah kaskazini mwa nchi hiyo ili kuruhusu kurejea usalama kwa wakaazi waliokimbia makazi yao ni lengo rasmi la vita.

    Kumekuwa na kurushiana risasi walau kila siku katika mpaka wa Israel na Lebanon tangu siku moja baada ya kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza tarehe 7 Oktoba.

    Hezbollah imesema kuwa inaunga mkono kundi la Wapalestina linaloungwa mkono na Iran. Makundi hayo kwa pamoja yamepigwa marufuku na Israeli, Uingerezapamoja na nchi nyingine zikiyatambua kama mashirika ya kigaidi.

    Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema matukio ya hivi punde nchini Lebanon "yanatia hofu sana, hasa ikizingatiwa kuwa haya yanafanyika katika mazingira ambayo ni tete sana".

    Unaweza pia kusoma:

  20. Uhali gani?...Tunakualika kwa matangazo haya ya moja kwa moja ya leo Jumanne kwa habari za kikanda na kimataifa tukisema shukran kwa kujiunga nasi.