Trump kusalimu amri vita vya ushuru? Ishara zinajionyesha

Trump kusalimu amri vita vya ushuru? Ishara zinajionyesha
    • Author, Faisal Islam
    • Nafasi, Mhariri Masuala ya Uchumi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kutoka Arizona, Washington DC nchini Marekani, hadi Saskatchewan nchini Canada, kuna ushahidi wa wazi wa mabadiliko ya kihistoria katika uchumi wa dunia. Mashaka yaliyopo yanamaanisha hakuna anayejua uchumi unaelekea wapi.

Kutembea kutoka bustani ya White House hadi Makao Makuu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) huchukua dakika 9 pekee. Katika mikutano ya IMF ya wiki tatu zilizopita, iliyojumuisha wanachama wa G7 na G20 - wawakilishi wa Marekani walikumbana na ukosoaji wa wazi, hasira, mshangao na wasiwasi mkubwa, kutoka karibu ulimwengu wote, kwa kuutia uchumi wa dunia kwenye shida, kama vile ilivyokuwa miaka minne ya janga la Corona.

Wasiwasi ulionyeshwa kwa ukali zaidi na nchi za Asia Mashariki, ambazo mwanzoni mwa Aprili ziliorodheshwa kama "waporaji" wa kazi za Marekani kwa sababu ya ukweli kwamba chumi hizi, nyingi ni washirika wakuu wa Marekani, na zinasafirisha bidhaa nyingi kwenda Marekani kuliko Marekani inavyosafirisha kupeleka huko.

Mazungumzo ya G7 yalikuwa ya utulivu lakini Japan ilionyesha hasira yake, wanahisi kusalitiwa na Marekani katika biashara. Waziri wa fedha wa Japan, Katsunobu Kato aliiambia meza ya duara, ushuru wa Marekani "unatamausha sana," na kuumiza ukuaji na uimara wa soko.

Sababu za kurudi nyuma

Katika masoko ya dhamana wiki hii, msukosuko wa vita vya kibiashara vya Marekani ulitoa ishara kuwa nchi hiyo itarudi nyuma. Kauli za kuonekana kuheshimu mafanikio ya kiuchumi China na kutaka kuunda uwiano wa biashara, ni tofauti za zile kauli za kuwa China inapora.

Hata hivyo mkutano uliotarajiwa kati ya Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent na mwenzake wa China haukufanyika.

Na kuna maoni kwamba hakuna haja ya nchi nyingine kulipiza kisasi kwa ushuru, kwani Wakuu wa Walmart na Target wanamwambia Rais Trump faraghani kwamba maduka ya Marekani yatakuwa matupu kuanzia mapema mwezi Mei.

Kupungua kwa idadi ya makontena ya bidhaa kutoka China katika bandari ya Los Angeles - mshipa mkuu wa uchumi wa dunia kwa robo ya kwanza ya karne ya 21 – hilo linatia wasiwasi.

IMF inasema imeanza kuona athari ya ushuru wa Trump kutoka anga za juu, kwani satelaiti zinaona meli chache na zikiwa tupu zikiondoka kwenye bandari za China.

Ni kweli kwamba kulikuwa na utulivu mwingi zaidi mwishoni mwa Mikutano ya IMF ikilinganishwa na mwanzo. Kwa nini? Kwa sababu Waziri wa Hazina wa Marekani Scott Bessent amechukua udhibiti wa ajenda ya ushuru na kujaribu kutuliza hali. Wanadiplomasia wa fedha wanaamini Bessent alihusika katika kuhakikisha ushuru unasitishwa kwa siku 90.

Taarifa zinasema aliweza kuzungumza na Trump kuhusu hali ya soko na athari zitokanazo na ushuru wake, baada ya mshauri mwingine wa uchumi wa Ikulu ya Marekani, kuitisha mkutano wa uongo ili kumwondoa msuka ushuru wa Trump. bwana Peter Navarro.

Wkuu wa Wall Street wanaamini kumfukuza kazi Peter Navarro, mshauri mkuu juu ya ushuru, hilo pekee ndilo linaweza kuifanya hali kurudi kama kawaida. Taarifa za ndani zinasema Trump hatamfukuza mshauri wake wa huyo wa biashara, kwani alitumikia kifungo baada ya ghasia za Januari 6 za kumuunga mkono Rais.

Hakuna anayepiga goti

Siku ya wikiendi Bessent alisema kwa namna ya kutuma ujumbe, "wawekezaji wanahitaji kujua kuwa soko la dhamana la serikali ya Marekani ndio soko salama zaidi ulimwenguni."

Waziri mwingine wa fedha aliniambia kuhusu wenzake wa kimataifa kwamba "hakuna mtu anayekwenda Marekani kupiga goti kutokana na ukweli kwamba Marekani inapaswa kupambana na soko lake lenyewe la dhamana.

Pia kuna afueni kwamba Marekani imebakia kushirikiana na Benki ya Dunia na IMF. Ripoti juu ya Mradi wa 2025 ambayo ilichapishwa Aprili 2023 na taasisi ya wataalam ya The Heritage Foundation – iliweka matarajio kuwa muhula wa pili wa Trump huenda Marekani ikaondoke kwenye mashirika hayo ya kimataifa, na Gavana wa Benki ya Uingereza hivi karibuni alinieleza wasiwasi wake juu ya hilo.

Marekani, China na Washirika wao

Lakini bado kuna maswali. Je, Marekani itatumia vita hivi vya kibiashara ili kujaribu kuuweka ulimwengu mzima upande wake katika vita dhidi ya China? Ikiwa hilo ndilo lengo la Marekani, inashangaza kuona imeweka ushuru mkubwa kwa washirika wape pia. Uhispania, inakabiliwa na ushuru wa 20% kama nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU).

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alikutana na Rais Xi huko Beijing wiki mbili zilizopita. Uhispania ina uchumi unaokuwa kwa kasi.

Uchumi huo umejengwa juu ya nishati ya kijani, upatikanaji wa kazi, utalii na uwekezaji mkubwa na teknolojia kutoka China. Marekani iliichukulia ziara hiyo kwa uzito na kufanya majadiliano ya "wazi" na waziri wake wa fedha Carlos Cuerpo.

Lakini katika Mkutano wa Kilele wa Uchumi wa Dunia wa Semafor huko DC, Cuerpo alinambia: "Kuna upungufu mkubwa wa biashara na China, na tunahitaji kurekebisha hilo kwa kufanya biashara zaidi na China, kwa kuvutia pia uwekezaji kutoka China, ndani ya mwavuli wa usalama wa kiuchumi. Na hilo linaweza tu kufanyika kwa kuzungumza na China."

Uhispania imepata uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha magari ya umeme cha China na kupata teknolojia hiyo. Marekani haipendi hilo. Lakini ikiwa Marekani ilitaka kuizuia Uhispania na EU kutoshirikiana na China, ni ngumu kuona mkakati wa ushuru ukifanya kazi.

Yeyote atakayeshinda katika uchaguzi wa Canada ataupeleka uchumi wa nchi hiyo ya G7 katika mjadala wa kuufanyia mageuzi katika ngazi ya ulimwengu.

Waziri Mkuu mpya wa Canada ataongoza Mkutano wa G7 nchini Canada mwezi Juni – baada ya makataa ya siku 90 ya Rais Trump yatakapokuwa yameisha. Inakisiwa Donald Trump atasafiri kwenda Alberta, katika nchi anayodai inapaswa kuwa jimbo la Marekani.

Mkutano huo unaweza kuwa chanzo cha biashara ya amani, utulivu bila mivutano. Lakini pia unaweza kuwa chanzo cha vita vingine vya kibiashara. Hizi ni nyakati muhimu kwa uchumi wa dunia.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi