Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanasayansi aliyesaidia China kuwa nchi yenye nguvu duniani baada ya kufukuzwa na Marekani
Huko Shanghai, China, kuna jumba zima la makumbusho lenye vitu 70,000 vilivyowekwa kwa mtu mmoja: "mwanasayansi wa watu" Qian Xuesen.
Qian ndiye baba wa mpango wa sayansi ya anga na makombora wa China.
Utafiti wake ulisaidia kutengeneza roketi zilizorusha satelaiti ya kwanza ya China angani na makombora ambayo yalikuja kuwa sehemu ya silaha za nyuklia za China.
Kwa sababu hii, anaheshimiwa kama shujaa wa kitaifa.
Lakini huko Marekani, ambapo alisoma na kufanya kazi kwa zaidi ya muongo mmoja, michango muhimu ya Qian haitambuliki sana.
Kesi yake imeangaziwa katika vyombo vya habari kama vile New York Times katika siku za hivi karibuni, huku kukiwa na sera ya Rais Donald Trump ya kuwafukuza wahamiaji.
Mnamo Mei 28, waziri wa mambo ya nje Marco Rubio alitangaza kwamba utawala utafanya kazi "kufuta kabisa" visa kwa wanafunzi wa China, ikiwa ni pamoja na wale wanaohusishwa na Chama cha Kikomunisti au wanaosoma katika "maeneo nyeti."
Hatari za kufukuza, badala ya kukaribisha, talanta kama Qian zimeathiri nguvu hiyo hapo awali.
Je, Marekani inaweza kujikwaa tena na kuwaondoa watu mahiri kama mwanasayansi huyu wa Kichina na kurudia kile kinachojulikana kama moja ya makosa mabaya zaidi katika historia ya nchi?
Nyota yazaliwa
Qian alizaliwa mwaka wa 1911, wakati nasaba ya mwisho ya kifalme ya China ilikuwa karibu kubadilishwa na Jamhuri.
Baba yake, baada ya kufanya kazi huko Japan, alianzisha mfumo wa elimu wa kitaifa wa China.
Ilikuwa wazi tangu umri mdogo kwamba Qian alikuwa na vipaji vingi. Alihitimu katika kiwango cha juu cha darasa lake kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai Jiao Tong na akashinda udhamini adimu wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) nchini Marekani.
Mnamo 1935, kijana mtanashati, aliyevalia vizuri aliwasili Boston. Huenda Qian alikabiliwa na chuki na ubaguzi wa rangi, anasema Chris Jespersen, profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Georgia Kaskazini nchini Marekani.
Lakini pia kulikuwa na "hisia ya matumaini na imani kwamba China (ilikuwa) inabadilika kwa njia muhimu sana."
Kutoka MIT, Qian alikwenda kwenye Taasisi ya Teknolojia ya California (Caltech) kusoma chini ya mmoja wa wahandisi wa anga wenye ushawishi mkubwa wa wakati huo, Theodore von Karman mzaliwa wa Hungary.
Huko, Qian alikuwa ofisi moja na mwanasayansi mwingine mashuhuri, Frank Malina, mwanachama muhimu wa kikundi kidogo cha wavumbuzi kinachojulikana kama "Kikosi cha kifo."
Kundi hili lilipata jina lake la utani kwa sababu ya majaribio yake ya kutengeneza roketi chuoni, na pia kwa sababu baadhi ya majaribio yake ya kemikali tete yalikwenda vibaya sana, anaeleza Fraser Macdonald, mwandishi wa kitabu cha Escape from Earth: A Secret History of the Space Rocket.
Lakini hakuna mtu aliyekufa, mwandishi anasema.
Siku moja, Qian alivutiwa katika mjadala wa fumbo gumu la hisabati na Malina na washiriki wengine wa kikundi, na muda si mrefu akawa sehemu ya timu, akitoa utafiti wa kina kuhusu urushaji wa roketi.
Wakati huo, sayansi ya roketi ilikuwa "vitu vya watu wanaoota ndoto," Macdonald anasema. "Hakuna aliyeichukulia kwa uzito, na hakuna mhandisi mwenye mwelekeo wa hisabati ambaye angeweza kuhatarisha sifa yake kwa kusema huu ulikuwa wakati ujao."
Lakini hii ilibadilika haraka na kuzuka kwa Vita vya pili vya Duni (1939-45).
Kikosi cha Kifo kilivutia umakini wa wanajeshi wa Marekani, ambao walifadhili utafiti wa kupaa kwa kusaidiwa na ndege, ambapo visukuku viliunganishwa kwenye mbawa za ndege ili kuwaruhusu kuondoka kutoka kwa njia fupi za kuruka.
Ufadhili wa kijeshi pia ulisaidia kuanzisha Maabara ya Jet Propulsion (JPL) mnamo 1943 chini ya uongozi wa Theodore von Karman. Qian, pamoja na Frank Malina, walikuwa katikati ya mradi huo.
Qian alikuwa raia wa China, lakini ROC ilikuwa mshirika wa Marekani, kwa hivyo hakukuwa na "mashaka yoyote ya mwanasayansi wa Kichina katika biashara ya anga ya Marekani," Macdonald anasema.
Alipata kibali cha usalama cha kufanya kazi katika utafiti wa silaha zilizoainishwa na hata alihudumu katika Bodi ya Ushauri ya Sayansi ya serikali ya Marekani.
Kufikia mwisho wa vita alikuwa mmoja wa wataalamu wakuu wa ulimwengu wa uendeshaji wa ndege na alitumwa na Von Karman kwenye misheni isiyo ya kawaida hadi Ujerumani, akiwa na cheo cha muda cha luteni kanali.
Lengo lilikuwa kuwahoji wahandisi wa Nazi, akiwemo Wernher von Braun, mwanasayansi mkuu wa roketi wa Ujerumani.
Marekani ilitaka kujua nini hasa Wajerumani walichokijua.
Lakini mwishoni mwa muongo huo, kazi nzuri ya Qian nchini Marekani ilikatizwa ghafla na maisha yake huko yakaanza kuyumba.
Nchini China, kiongozi Mao Zedong alitangaza kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa Kikomunisti mwaka wa 1949, na Wachina haraka wakaja kuonekana Marekani kama "watu wabaya," anasema Jespersen wa Chuo Kikuu cha Georgia Kaskazini.
Wakati huo huo, mkurugenzi mpya wa JPL aliamini kuwa kulikuwa na kikundi cha kijasusi kwenye maabara na akaeleza tuhuma zake kuhusu baadhi ya wafanyakazi na FBI. "Wote walikuwa Wachina au Wayahudi," anasema Macdonald.
Vita Baridi kati ya Marekani na Muungano wa Kisovieti vilikuwa vikiendelea, na uwindaji wa wachawi dhidi ya ukomunisti wa enzi ya McCarthy ulikuwa ukishika kasi. Ni katika mazingira hayo ambapo FBI iliwashutumu Qian, Frank Malina na wengine kuwa wakomunisti na kuwa tishio kwa usalama wa taifa.
Mashtaka dhidi ya Qian yalitokana na hati ya Chama cha Kikomunisti cha Marekani ya mwaka wa 1938 iliyoonesha kuwa alikuwa amehudhuria mkusanyiko wa kijamii ambao FBI walishuku kuwa ni mkutano wa Chama cha Kikomunisti cha Pasadena.
Ingawa Qian alikanusha kuwa mwanachama wa chama, utafiti mpya umeonesha alijiunga wakati uleule kama Frank Malina, mwaka wa 1938. Lakini hiyo haimfanyi kuwa mtu wa Umaksi.
Kuwa mkomunisti wakati huo ilikuwa kauli ya kupinga ubaguzi wa rangi, anaeleza Macdonald.
Kundi hilo lilitaka kuangazia tishio la ufashisti, mtaalamu huyo anasema, pamoja na kutisha kwa ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Walikuwa wakifanya kampeni, kwa mfano, dhidi ya kutengwa kwa bwawa la kuogelea la eneo la Pasadena na walitumia mikutano ya Kikomunisti kulijadili.
Zuoyue Wang, profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha California Polytechnic State nchini Marekani, anasema hakuna ushahidi kwamba Qian aliipeleleza China au alikuwa wakala wa ujasusi alipokuwa Marekani.
Hata hivyo, alinyang'anywa kibali chake cha usalama na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani. Wenzake wa Caltech, akiwemo Theodore von Karman, waliiandikia serikali kutetea kutokuwa na hatia kwa Qian, lakini hawakufanikiwa.
Mnamo 1955, baada ya miaka mitano ya kifungo cha nyumbani, Rais Eisenhower aliamua kumfukuza hadi China. Mwanasayansi huyo aliondoka kwa boti akiwa na mke wake na watoto wawili wazaliwa wa Marekani, akiwaambia waandishi wa habari kwamba hatakanyaga tena Marekani. Na alitimiza ahadi yake.
"Alikuwa mmoja wa wanasayansi mashuhuri nchini Marekani. Alichangia mengi na angeweza kuchangia mengi zaidi. Kwa hiyo haikuwa tu unyonge bali pia hisia ya usaliti," anasema mwandishi Tianyu Fang.
Qian aliwasili China kama shujaa, lakini hakukubaliwa mara moja kwenye Chama cha Kikomunisti.
Rekodi yake haikuwa kamilifu. Mkewe alikuwa binti wa kiungwana wa kiongozi wa Kitaifa, na hadi Qian alipoanguka, alikuwa akiishi kwa furaha nchini Marekani. Mwanasayansi huyo alikuwa amechukua hata hatua za kwanza za kuomba uraia wa Marekani.
Hatimaye alipokuwa mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha China mwaka wa 1958, alikikubali na kuanzia hapo na kuendelea akajaribu kubaki upande wa kulia wa serikali.
Alipofika China, kulikuwa na ujuzi mdogo wa sayansi ya roketi, lakini miaka 15 baadaye alisimamia kurushwa kwa satelaiti ya kwanza ya China angani.
Kwa miongo kadhaa, alitoa mafunzo kwa kizazi kipya cha wanasayansi na kazi yake iliweka msingi wa Programu ya China ya Uchunguzi wa Mwezi.
Cha kushangaza, mpango wa makombora wa Qian ulisaidia China kuunda silaha zilizorushwa kuelekea Marekani.
Makombora ya Silkworm yaliyotengenezwa na Qian yalirushwa kwa Wamarekani katika Vita vya Ghuba vya 1991 na mnamo 2016 kwenye meli ya kivita ya USS Mason na waasi wa Houthi huko Yemen.
Waziri wa zamani wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani Dan Kimball, ambaye baadaye alikuja kuwa mkuu wa kampuni ya kurusha roketi ya Aerojet, aliwahi kusema kufukuzwa kwa Qian kilikuwa "kitu cha kijinga zaidi ambacho nchi hii imewahi kufanya."
Leo tena, kuna mvutano mkubwa kati ya China na Marekani. Wakati huu, sio juu ya itikadi, lakini juu ya biashara, usalama wa kiteknolojia na, kulingana na Trump, madai ya China kushindwa kudhibiti kuenea kwa Covid-19.
Ingawa Wamarekani wengi hawajui historia ya Qian na nafasi yake katika mpango wa anga za juu wa Marekani, Tianyu Fang anasema wanafunzi wengi wa China nchini Marekani wanajua kuhusu mwanasayansi huyo na kwa nini alilazimika kuondoka nchini humo.
"Uhusiano kati ya Marekani na China umezorota kiasi kwamba wanajua wanaweza kuwa kwenye tuhuma sawa na kizazi cha Qian," mwandishi wa habari analinganisha.