'Ilinibidi kuchagua kati ya wazazi wangu na mtoto wangu'

Tayeb ait Ighenbaz alilazimika kuchagua iwapo atamwokoa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 11 au wazazi wake waliponaswa na vifusi baada ya tetemeko la ardhi kutokea Morocco.

Mchungaji wa mbuzi kutoka jamii ndogo katika Milima ya Atlas anasema anasumbuliwa na uamuzi aliopaswa kufanya.

Tayeb alikuwa na mke wake, watoto wawili na wazazi siku ya Ijumaa usiku katika nyumba yao ndogo ya mawe wakati ilipokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini humo katika kipindi cha miaka 60.

Ananiongoza hadi kwenye nyumba yake ya zamani, ambayo sasa ni magofu.

Bado unaweza kuona sehemu ndani ya jengo na anaelekeza kwenye kifusi, akisema: "Hapo ndipo walipokuwa."

"Yote yalitokea haraka sana. Tetemeko la ardhi lilipotokea sote tulikimbilia mlangoni. Baba yangu alikuwa amelala na nilipiga kelele kwa mama yangu kuja, lakini alibaki nyuma kumngojea," anakumbuka.

Kwa upande mwingine, aliweza kuwaona tu mke wake na binti yake.

Alipokuwa akirudi kwenye jengo lililoanguka, Tayeb aliwakuta mtoto wake wa kiume na wazazi wake wakiwa wamenaswa chini ya vifusi. Aliweza kuuona mkono wa mwanawe ukipenya kwenye kifusi.

Alijua ni lazima achukue hatua haraka, akaelekea upande wa mwanaye Adam, akichimba kifusi kwa bidii ili amtoe.

Alipowageukia wazazi wake, wakiwa wamenaswa chini ya bamba kubwa la mawe, anasema alikuwa amechelewa.

"Ilinibidi kuchagua kati ya wazazi wangu na mwanangu," anasema huku akibubujikwa na machozi.

"Sikuweza kuwasaidia wazazi wangu kwa sababu ukuta ulianguka zaidi ya nusu ya miili yao. Inasikitisha sana. Niliwaona wazazi wangu wakifa."

Tayeb anaonyesha madoa kwenye nguo yake ya rangi nyepesi, akisema hii ni damu ya wazazi wake.

Nguo zake zote ziko ndani ya nyumba yake, na hajaweza kubadilishwa tangu tetemeko la ardhi.

Familia hiyo sasa inaishi na jamaa katika mahema ya muda karibu na nyumba yao ya zamani. Tayeb anasema pesa zake zote zilikuwa ndani ya nyumba na mbuzi wake wengi wameuawa.

"Ni kama kuzaliwa upya katika maisha mapya. Hakuna wazazi, hakuna nyumba, hakuna chakula, hakuna nguo," anasema. "Nina umri wa miaka 50 sasa na ni lazima nianze tena."

Hawezi kuanza kufikiria jinsi ya kusonga mbele, lakini anakumbuka masomo ambayo wazazi wake walimfundisha. "Mara zote walisema 'kuwa na subira, fanya kazi kwa bidii, usikate tamaa'."

Tunapozungumza, mwanawe Adam anakimbia, akiwa amevalia jezi ya mpira wa miguu ya Juventus yenye jina la Ronaldo mgongoni, na kumkumbatia baba yake.

"Baba yangu aliniokoa na kifo," anasema huku akimwangalia.

Dakika chache tu chini ya barabara kuelekea mji wa Amizmiz, baba mwingine na mwanawe wanasimama wakiwa wamekumbatiana.

Abdulmajid ait Jaefer anasema alikuwa nyumbani na mke wake na watoto watatu wakati tetemeko la ardhi lilipotokea na "sakafu ikaporomoka".

Mwanawe, Mohamed mwenye umri wa miaka 12, alitoka nje ya jengo hilo, lakini wengine wa familia walikuwa wamekwama.

Abdulmajid anasema miguu yake ilinaswa chini ya kifusi, lakini alitolewa nje na jirani. Kisha alitumia saa mbili kujaribu kuokoa mke wake na binti yake mmoja. Wote wawili walikuwa wamekufa alipowatoa kutoka kwenye vifusi.

Siku iliyofuata, mwili wa binti yake mwingine pia ulitolewa kwenye kifusi.

Abdulmajid, 47, sasa analala chini ya turubai kando ya barabara kutoka kwa nyumba yake.

Anaweza kuona jikoni, na friji bado imesimama na nguo zikining'inia kukauka.

Anasema hawezi kuondoka eneo hilo kwa sababu anahitaji "kulinda" mali yake, na kumbukumbu za maisha yake huko.

"Hilo ni jiko langu na friji yangu. Tulikuwa wote ndani. Sasa naangalia tu," anasema.

Kabla ya Ijumaa, Abdulmajid anasema "hajawahi hata kuota kuhusu tetemeko la ardhi. Hata sasa, siamini."

Tunapozungumza, magari yanasimama karibu nasi na watu wanaegemea kutoa rambirambi. Wengine wanaotembea barabarani wanasimama ili kuwakumbatia baba na mume wanaoomboleza.

"Kulikuwa na watu watano katika familia yangu. Sasa kuna wawili," ananiambia kwa huzuni.

"Kwa sasa, ninafikiria jambo moja tu: mwanangu."