Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka 20 ya Facebook: Jinsi ilivyoubadili ulimwengu kwa njia nne
Angalia picha hapo juu. Hivi ndivyo Facebook, au The Facebook kama ilivyojulikana wakati huo, ilivyoonekana wakati Mark Zuckerberg na marafiki wachache walipoizindua baada ya uvumbuzi wa wao wakiwa shuleni miaka 20 iliyopita.
Tangu wakati huo, mtandao maarufu zaidi wa kijamii ulimwenguni umekarabatiwa mara kadhaa.
Lakini lengo lake limebaki sawa: kuunganisha watu mtandaoni. Na kutengeneza mabilioni na mabilioni ya pesa kutokana na matangazo ya kibiashara.
Kama jukwaa linatimiza miaka 20, na hizi hapa ni njia nne ambazo Facebook imeubadilisha ulimwengu.
1. Facebook ilileta mabadiliko katika media ya kijamii
Mitandao mingine ya kijamii, kama MySpace, ilikuwepo kabla ya Facebook - lakini tovuti ya Mark Zuckerberg iliiondoka mara moja wakati ilipozinduliwa mwaka 2004, ikithibitisha ni jinsi gani tovuti ya mtandaoni ya aina hii inaweza kushika kasi.
Chini ya mwaka mmoja Facebook ilikuwa na watumiaji milioni moja, na ndani ya miaka minne ilikuwa imezidi MySpace - iliyochochewa na ubunifu kama vile uwezo wa 'kuwaweka' watu kwenye picha.
Kuchukua kamera ya kidijitali hasa nyakati za usiku, kisha 'kuwatumia kwa pamoja ' marafiki zako picha kadhaa ilikuwa ni kitu muhimu kwa vijana wanaopendelea starehe za usiku. Kubadilishwa kwa mara kwa mara kwa shughuli za Facebook kuliwavutia watumiaji wa kwanza wa mtandao huu wa kijami.
Kufikia mwaka wa 2012, Facebook ilikuwa ina watumiaji zaidi ya bilioni moja kwa mwezi na, mbali kipindi kifupi cha mwishoni mwa 2021 - wakati watumiaji wa kila siku walipungua kwa mara ya kwanza hadi kufikia bilioni 1.92, jukwaa limeendelea kukua.
Kwa kupanua huduma yake katika nchi ambazo awali hazikuunganishwa na mtandao huo na kutoa huduma za kimtandao za bure, kampuni hiyo imedumisha na kuongeza idadi ya watumiaji wa Facebook. Mwishoni mwa 2023, Facebook iliripoti kuwa ilikuwa na watumiaji zaidi ya bilioni mbili kila siku.
Kwakweli, Facebook kwa sasa si maarufu sana kama ilivyokuwa kwa vijana ilipoanzishwa. Lakini, unabaki kuwa mtandao maarufu zaidi wa kijamii ulimwenguni, na imeleta enzi mpya ya shughuli za kijamii mtandaoni.
Baadhi wanaiona Facebook na washindani wake kama vyombo vinavyoboresha mawasiliano huku wengine wakiwaona kama mawakala wanaochochea uraibu unaosababisha uharibifu.
2. Facebook ilifanya data zetu kuwa za thamani... na kusifanya zisiwe za kibinafsi
Facebook ilithibitisha kuwa kukusanya maoni ya kupenda kwetu ( likes)na kutokupenda (dislikes) ni faida kubwa.
Siku hizi, kampuni mama ya Facebook, Meta, ni kampuni kubwa ya matangazo ambayo, pamoja na Google, inachukua hisa kubwa ya pesa za matangazo ya kimataifa.
Meta iliripoti mapato ya karibu $ 34bn (£ 26.7bn) katika robo ya tatu ya 2023, ambayo yalitokana hasa na utoaji huduma za matangazo zinazolengwa sana; $ 11.5bn zilitangazwa kuwa faida.
Lakini Facebook pia imeonyesha ni vipi ukusanyaji wa data unaweza kuwa tatizo.
Meta imetozwa faini mara kadhaa kwa kutoshughulikia data za kibinafsi.
Kesi iliyotangazwa zaidi ilikuwa kashfa ya Cambridge Analytica mwaka 2014, ambayo ilisababisha Facebook kulipa $725m (£600m) ili kutatua hatua za kisheria kutokana na ukiukaji mkubwa wa data.
Mnamo 2022, Facebook pia ililipa faini ya € 265m (£ 228m) EU kwa kuruhusu data za kibinafsi kutolewa kutoka kwenye tovuti.
Na mwaka jana, kampuni hiyo ilitozwa € 1.2bnza faini na Tume ya Ulinzi wa Takwimu ya Ireland, kwa kuhamisha data za watumiaji wa Ulaya nje ya mamlaka. Facebook kwa sasa inapinga faini hiyo.
3. Facebook ilifanya mtandao kuwa wa kisiasa
Kwa kutoa matangazo yaliyolengwa, Facebook imekuwa jukwaa kuu la kampeni za uchaguzi duniani kote.
Kwa mfano, katika miezi mitano kuelekea uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2020, timu ya Rais Donald Trump ilitumia zaidi ya dola milioni 40 kwenye matangazo ya Facebook, kulingana na utafiti wa Statista.
Facebook imekuwa na mkono katika kubadilisha siasa za chini pia - kwa kuwezesha makundi tofauti ya watumiaji kukusanya, kampeni na kupanga hatua kwa kiwango cha kimataifa.
Facebook na Twitter zilisemekana kuwa muhimu wakati wa vuguvugu la mageuzi katika nchi za kiarabu katika kusaidia kuratibu maandamano na kueneza habari kuhusu kile kilichokuwa kikifanyika katika eneo hilo.
Lakini kupitishwa kwa Facebook kwa malengo ya kisiasa kumekosolewa kuhusu baadhi ya athari zake, ikiwa ni pamoja na athari zake kwa haki za binadamu.
Mwaka 2018, Facebook ilikubaliana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo ilisema imeshindwa kuwazuia watu kutumia jukwaa hilo "kuchochea ghasia za nje ya mtandao" dhidi ya watu wa Rohingya nchini Myanmar.
4. Facebook ilianza utawala wa Meta.
Kwa mafanikio makubwa ya Facebook, Mark Zuckerberg alijenga mtandao wa kijamii na himaya ya teknolojia ambayo bado haijawahi kutokea kwa watumiaji na nguvu zake za matokeo.
Kampuni zinazokuja, ikiwa ni pamoja na WhatsApp, Instagram na Oculus, zote zilinunuliwa na turbo chini ya mwavuli wa kampuni ya Facebook, ambayo ilibadilisha jina lake kuwa Meta mnamo 2022.
Meta sasa inasema zaidi ya watu bilioni tatu hutumia angalau moja ya bidhaa zake kila siku.
Na wakati haijaweza kununua wapinzani wake, Meta mara nyingi imekuwa ikishutumiwa kwa kuiga - ili kudumisha utawala wake.
Kipengele cha Hadithi za Facebook na Instagram (stories) kinachopotea baada ya muda ambacho ni sawa na kipengele muhimu kinachopatikana kwenye Snapchat; Instagram Reels ni jibu la kampuni kwa changamoto inayotokana na programu ya kushiriki video TikTok; Na Threads ni jaribio la Meta kuiga X, zamani inayojulikana kama Twitter.
Mbinu zimekuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali, kufuatia ushindani ulioongezeka na mazingira magumu zaidi ya udhibiti.
Mnamo 2022, Meta ililazimika kuuza Giphy ya GIF kwa hasara, baada ya wadhibiti wa Uingereza kuizuia kumiliki huduma hiyo kwa sababu ya hofu ya kwamba ingekuwa na umiliki wa juu zaidi katika soko la mtandaoni.
Kipi kitarajiwe katika miaka 20 ijayo?
Kuongezeka kwa Facebook na kuendelea kutawala ni ushahidi wa uwezo wa Mark Zuckerberg wa kuweka tovuti hiyo kuwa muhimu.
Lakini kudumisha taji lake kama mtandao maarufu wa kijamii itakuwa changamoto kubwa zaidi katika miaka 20 ijayo.
Meta sasa inaweka bidii sana katika mwelekeo wake wa kujenga biashara yake karibu na wazo la Metaverse, bila shaka ikitaka kuongoza makampuni makubwa ya teknolojia kama vile Apple.
Akili bandia pia ni kipaumbele kikubwa kwa Meta.
Kwa hivyo, kadri kampuni inaposonga mbali zaidi na mizizi yake ya Facebook, litakuwa ni jambo la kuvutia kuona nini mapya ya app hiyo yenye nembo ndogo ya ya bluu.
Taarifa ya ziada ya Iman Mohammed
Picha ya pamoja na Niall Kennedy.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi