Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025: Kwa nini Mpina na Fatma Fereji 'watasumbua'?

Chanzo cha picha, ACT
Na Mwandishi Wetu
Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), alichukua uamuzi wa kushtua mwaka 2019 kwa kuhamia Chama cha ACT Wazalendo. Uamuzi huu wa Machi 19 ulibadilisha kabisa siasa za Tanzania Bara na Zanzibar. Ndani ya wiki moja, kilichokuwa chama kikuu cha upinzani Zanzibar kiligeuka kuwa cha tatu, huku ACT Wazalendo ikichukua nafasi yake kama chama kikuu cha upinzani.
Hali hiyo inafanana na matukio ya Agosti 2025. Aliyekuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameiunganisha nguvu na ACT Wazalendo na kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho kama mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29. Chama cha ACT Wazalendo kimechagua Mpina (50) kuwa mgombea urais na Fatma Alhabib Fereji (64) kuwa mgombea mwenza.
Ujio wa Mpina unaweza kuleta mabadiliko makubwa, ukifanana na ule wa "Shusha Tanga, Pandisha Tanga" wa wakati wa Maalim Seif, ambao uliibadilisha siasa za ACT Zanzibar. Sasa ni wazi kwamba Mpina anaweza kuathiri siasa za ACT Tanzania Bara na matokeo ya jumla ya chama hicho kwenye uchaguzi huu.
Tofauti na wagombea wengine wa vyama zaidi ya 15, Mpina na Fatma wamelazimika kuruka kiunzi cha kuenguliwa na Tume Huru ya Uchaguzi INEC, iliyokubaliana na uamuzi wa Msajili wa yama vya Siasa kuhusu Mpina na mgombea mwenza wake kukosa vigezo vya kuteuliwa.
ACT Wazalendo na Mpina waliamua kwenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo INEC na kuomba Mpina arejeshwe katika mchakato wa uchaguzi akiwa mgombea. Alhamisi Septemba 11, Jopo la majaji watatu; Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa, na John Kahyoza likakubaliana na hoja za msingi za walalamikaji dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na INEC, hususan kukiukwa kwa Katiba ya Tanzania, inayotoa uhuru kamili kwa INEC na kuzuiwa kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote na pia walalamikaji kutopewa fursa ya kusikilizwa. Hivyo jopo hilo likawapa ushindi walalamikaji.
Nini maana ya tiketi ya Mpina na Fereji?

Chanzo cha picha, ACT WAZALENDO/ Instagram
Tofauti ya tiketi ya Mpina na Fereji na ile ya Samia Suluhu Hassan na Dkt. Emmanuel Nchimbi ni kuwa wawili hawa wa ACT Wazalendo hawafahamiani wala hawana ukaribu wowote kiitikadi na kihaiba.
Fereji amejenga jina lake kama mwanasiasa jasiri, muungwana na aliye tayari kwa mazungumzo ya kutaka mwafaka wa kisiasa wakati wowote. Mojawapo ya sifa zake ni kuwepo kwenye kamati maalumu iliyosimamia utekelezwaji wa mwafaka baina ya CCM na CUF kuelekea mwaka 2010.
Kwa upande mwingine, Mpina ni mbunge ambaye amejipambanua kwa kuzungumza kwa uwazi kile anachokiamini, kutojali madhara ya matamshi yake na kwa ujumla, mwanasiasa asiyetabirika.
Kwa maana nyingine, tiketi ya Mpina na Fereji ni tiketi ya moto na maji. Kama ingekuwa ni CCM ya mwaka 2015 – tungesema Luhaga ni Magufuli na Fatma Fereji ndiye Samia Suluhu Hassan.
Uwezekano wa Mpina kuleta changamoto kubwa kwa CCM kwenye uchaguzi huu ni kwa sababu kubwa tatu – mosi aina yake ya siasa, muktadha wa siasa za kisasa na eneo anakotoka.
Aina ya siasa za Mpina

Chanzo cha picha, ACT
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kisiasa, Mpina ambaye kitaaluma ni mhasibu, akipata elimu yake ya Stashahada ya Juu kutoka Kilichokuwa chuo cha Uongozi wa Maendeleo (IDM) Mzumbe, sasa Chuo Kikuu Mzumbe na baadaye kupata Shahada ya Umahiri kutoka chuo Kiku cha Strathclyde nchini Scotland, anaangukia katika kundi la wanasiasa wasio wa kawaida ambao kwa lugha ya Kiingereza wanajulikana kwa jina la populists. Tabia zao, maneno na matendo yao si aina ya maneno ambayo watanzania wamezoea kuyasikia kwa wanasiasa wa kawaida.
Hii ni kwa sababu, huyu ni mwanasiasa ambaye wakati alipokuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, aliwahi kupima urefu wa samaki kwa kutumia rula ili kuhakikisha iwapo samaki hao hawakuwa wamekiuka urefu wa kuvuliwa unaokubalika kisheria.
Mpina na Fereji wanaweza kuleta changamoto kubwa kwa CCM kwenye uchaguzi huu kwa sababu ametoka ndani ya CCM, anaijua CCM na amekuwa sehemu ya CCM na harakati zake kwa muda mrefu.
Muktadha wa uchaguzi mkuu wa 2025 ni kwamba wagombea wa CCM kwa ujumla wanaonekana kuwa wanasiasa waungwana, waliopikwa na kujengwa kwenye mfumo wa demokrasia ya kiliberali. Pale ambapo wao watashindwa kudanganya hadharani au kusema kitu kisichotamkika, Mpina ataweza.
Iwapo ACT Wazalendo na Mpina wataamua kuendesha kampeni zenye kuendana na haiba ya mgombea wao, wanaweza kujikuta wakivutia kundi kubwa la vijana ambao wanaonekana kuvutiwa zaidi na wanasiasa wa aina ya Mpina ambao huonekana kama jasiri na watetezi wa wanyonge dhidi ya mfumo wa siasa unaokumbwa na na malalamiko ya kukumbatia kundi dogo la vongozi maarufu na familia za viongozi wastaafu wanaodaiwa kufaidi zaidi 'mema ya nchi' huku kundi kubwa likidhaniwa 'kutaabika'. Zimekuwepo njia rasmi na zisizo rasmi za kukanusha hali na kutoa maelezo kinzani, lakini mwangwi wa kuunga mkono hoja hiyo umekuwa ukiongezeka badala ya kupungua kadiri maelezo ya kupinga yanavyotolewa.
Siasa za Kikanda
CCM inaweza kujivuna kuwa chama chenye ufuasi nchi nzima – bila kujali dini, ukabila wala jinsi za Watanzania. Hata hivyo, msemo maarufu kuwa "All politics is local" kwa maana wema huanzia nyumbani, unaweza kutumiwa vema na Mpina na chama chake kipya, ACT Wazalendo.
Mgombea urais huyu anatoka katika eneo la Tanzania; Kanda ya Ziwa Victoria, lenye idadi kubwa ya wapiga kura na endapo wapiga kura wataamua kumpigia kura "mtu wao"– chama hiki cha upinzani kinaweza kuwashangaza wengi kwenye uchaguzi huu.
Watanzania huwa hawapigi kura kikabila lakini kama kuna kitu cha kujifunza kwenye uchaguzi nchini Tanzania, ni ukubwa wa ushindi alioupata Magufuli – kutoka Kanda ya Ziwa, katika eneo hilo wakati alipowania urais mwaka 2015 na 2020.
Kuna dalili kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi Tanzania, chama cha upinzani kitakuwa na upinzani dhidi ya CCM kwenye uchaguzi wa Muungano na ule wa Zanzibar – tofauti na miaka ya awali ambapo upinzani kwa kawaida huwa ni wa upande mmoja ndani ya mwaka husika wa uchaguzi. Kwamba unapokuwa upinzani mzito Zanzibar kwa upande wa Muungano hali ya ushindani hupwaya, vivyo hivyo na kinyume chake.
Changamoto kwa Mpina na ACT Wazalendo
Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na tatizo la watu wengi kutokujitokeza kupiga kura. Zipo taarifa kwamba CCM ilishangazwa na idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura mwaka 2020 kiasi kwamba kuna maeneo waliojitokeza walikuwa chini ya asilimia 40 ya waliojiandikisha.
ACT Wazalendo na Mpina watakuwa na kazi kubwa ya kuongeza morali ya wapiga kura – hasa katika mazingira ambayo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea na kampeni yake ya No Reforms No Election (Hakuna uchaguzi bila mabadiliko), inayohamasisha watu kutokujitokeza kupiga kura.
Mpina na chama chake watakuwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi endapo watu wengi watajitokeza kupiga kura. Uzoefu unaonesha kwamba upinzani huwa haufanyi vema pale ambapo wapiga kura huwa ni wachache.
Utumishi wa Mpina ndani ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi pia ulimtia doa Mpina baada ya kuhusishwa na uchomaji wa nyavu za wavuvi na vitendo vingine ambavyo havikupokewa vema na watu wa kipato cha chini, japo alijitetea mara kadhaa kuwa alikuwa akitekeleza matakwa ya sheria.
Jambo moja lililo wazi ni kwamba ujio wa Mpina katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umebadili kabisa upepo wa uchaguzi huo. Ni wazi kutakuwa na mpambano. Hiyo ndiyo maana ya tiketi hii ya Mpina na Fatma Fereji.
Imehaririwa na Florian Kaijage












