Luhaga Mpina kuwania Urais Tanzania
Mamia ya wafuasi na wasio wafuasi wa Chama ACT Wazalendo walikuwepo katika Mahakama Kuu, Masijala kuu ya Dodoma kufuatilia uamuzi wa shauri la Luhaga Mpina.
Muhtasari
- Mahakama Afrika Kusini yaamua kuwa mwanaume anaweza kutumia majina ya baba mkwe
- Ufaransa inashuku ujasusi wa kigeni umehusika na vichwa vya nguruwe vilivyoachwa nje ya misikiti
- Luhaga Mpina kuwania Urais Tanzania
- Israeli yatishia kuwaua viongozi wa Hamas waliosalia Qatar
- Chelsea yakabiliwa na mashtaka 74 kuhusu malipo ya wakala
- Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa dharura kuhusu droni za Urusi nchini Poland
- Qatar yasema 'tumesalitiwa'
- Arusha: Mwendesha mashtaka aomba Kabuga arejeshwe Rwanda
- Kwa picha: Ethiopia yasherehekea mwaka mpya
- Trump alaani mauji ya mshawishi wa kisiasa na mshirika wake aliyepigwa risasi
- Ghana yakubali kuwapokea raia wa Afrika Magharibi waliofukuzwa kutoka Marekani
- Qatar yasema msako unaendelea katika eneo la mashambulizi ya Israel yaliyoyowalenga viongozi wa Hamas
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma
Mahakama Afrika Kusini yaamua kuwa mwanaume anaweza kutumia majina ya baba mkwe

Chanzo cha picha, Visual Ideas/Getty Images
Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini imeamua kuwa wanaume wanaweza kutumia jina la ukoo la wake zao, na kubatilisha sheria iliyowazuia kufanya hivyo.
Katika ushindi wa wanandoa wawili walioleta kesi hiyo, Mahakama ya Kikatiba iliamua kwamba sheria hiyo ilikuwa "ungiaji wa kikoloni" ambao ulilingana na ubaguzi wa kijinsia.
Henry van der Merwe alinyimwa haki ya kutumia jina la ukoo la mke wake Jana Jordaan, wakati Andreas Nicolas Bornman hakuweza kujumuisha Donnelly, jina la ukoo la mkewe, Jess Donnelly-Bornman, kituo cha habari cha SABC, kinaripoti.
Bunge sasa litalazimika kurekebisha Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, pamoja na kanuni zake, ili uamuzi huo uanze kutekelezwa.
Ufaransa inashuku ujasusi wa kigeni umehusika na vichwa vya nguruwe vilivyoachwa nje ya misikiti

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi wa Ufaransa wanashuku kuwa watu walioweka vichwa vya nguruwe nje ya misikiti ya Paris Jumatatu usiku walikuwa wakifanya kazi chini ya maagizo kutoka kwa idara ya kijasusi ya kigeni, pengine Urusi.
Vichwa hivyo vilipatikana Jumanne asubuhi nje ya misikiti tisa katikati mwa Paris na vitongoji vya jirani, na kusababisha wimbi la hasira na lawama.
Lakini wachunguzi sasa wamesema watu wawili waliohusika waliendesha gari lililosajiliwa na Serb, walitumia simu ya rununu ya Croatia, na kuvuka hadi Ubelgiji saa chache baadaye.
Tukio hilo lina mfanano wa kushangaza na uchochezi mwingine wa hivi majuzi - haswa ule unaojulikana kama Star of David kwenye kuta za Paris mnamo Oktoba 2023, na uchoraji wa mikono rangi nyekundu kwenye ukumbusho wa Maangamizi ya Wayahudi mnamo Mei 2024.
Pia unaweza kusoma:
Habari za hivi punde, Luhaga Mpina kuwania Urais Tanzania

Chanzo cha picha, ACT
Luhaga Mpina ameshinda shauri la kupinga kuenguliwa kugombea urais wa Tanzania kwa tikiti ya ACT Wazalendo.
Uamuzi huo umetolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dodoma muda mfupi uliopita.
Mamia ya wafuasi na wasio wafuasi wa Chama ACT Wazalendo walikuwepo katika Mahakama Kuu, Masijala kuu ya Dodoma kufuatilia uamuzi wa shauri la Luhaga Mpina.
Baadhi ya wanasiasa mashuhuri akiwemo kiongozi mkuu wa zamani wa ACT, Zitto Kabwe ni miongoni mwa waliofika kufuatilia uamuzi wa shauri lililofunguliwa na ACT Wazalendo dhidi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania.
Shauri hilo ambalo lilifunguliwa na bodi ya wadhamani ya ACT Wazalendo na mgombea mteule wa kiti cha urais kupitia chama hicho lilipinga kuondolewa kwa Mpina kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu kwa kuzuiwa kurejesha fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea nafasi ya urais.
Shauri hili ambalo lilifunguliwa kwa hati ya dharura lilisikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza.
Soma zaidi:
Israeli yatishia kuwaua viongozi wa Hamas waliosalia Qatar

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ametishia kuwaua tena viongozi wa Hamas walioko nchini Qatar iwapo Doha haitawafukuza maafisa hao, na kusababisha majibu makali kutoka kwa serikali ya Qatar.
Pamoja na ukosoaji huo wa kimataifa kuhusu shambulio lililotokea katika mji mkuu wa Qatar inaarifiwa kuwa Netanyahu hajatetereshwa kwa namna yoyote.
Netanyahu amesema siku ya Jumatano kwamba mataifa yanapaswa “kuipongeza” Israel kwa mashambulizi yake ya mabomu na mauaji katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
Kauli hizo zilitolewa siku moja baada ya Israel kufanya shambulio lisilo la kawaida ndani ya Qatar, kwa kuwalenga viongozi waandamizi wa Hamas walioko Doha, wakati mazungumzo kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano lililoungwa mkono na Marekani yakiendelea.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani vikali kauli za Waziri Mkuu huyo wa Israeli, ikizitaja kama “jaribio la aibu ... la kuhalalisha shambulio la kinyonge dhidi ya ardhi ya Qatar, pamoja na vitisho vya wazi vya kuvunja tena mamlaka ya kitaifa ya nchi.”
“Netanyahu anafahamu vyema kuwa ofisi ya Hamas ilifunguliwa nchini Qatar katika muktadha wa juhudi za upatanishi zilizopigiwa chapuo na Marekani pamoja na Israel,” Taarifa hiyo imeeleza.
“Kauli kama hizi si jambo la kushangaza kutoka kwa mtu anayejiegemeza katika misimamo mikali ili kupata ushindi wa kisiasa, huku akiwa anatafutwa na vyombo vya sheria za kimataifa, akikabiliwa na vikwazo vinavyozidi kuongezeka kila uchao hali inayozidi kumtenga katika jukwaa la kimataifa,” Taarifa hiyo iliongeza.
Wakati hayo yakijiri, ikumbukwe kwamba ndani ya kipindi cha siku tatu pekee, Israel imefanya mashambulizi katika maeneo ya Gaza, Lebanon, Yemen, Syria, Tunisia na Qatar, huku ikiendeleza uvamizi wa kila siku katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na siku ya Jumatano, Israeli iliwaua watu 35 katika shambulio nchini Yemen.
Soma zaidi:
Chelsea yakabiliwa na mashtaka 74 kuhusu malipo ya wakala

Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea imeshtakiwa na Chama cha Soka kwa madai ya kukiuka sheria 74 zinazohusiana na malipo kwa mawakala kati ya 2009 na 2022.
Gharama hizo kimsingi zinalenga matukio yaliyotokea kati ya misimu ya 2010-11 na 2015-16.
Bwenyenye wa Urusi Roman Abramovich alikuwa akiidhibiti klabu hiyo kuanzia 2003 hadi 2022, kabla ya kuiuza Chelsea kwa muungano ulioongozwa na mwekezaji Mmarekani Todd Boehly na kampuni ya kibinafsi ya Clearlake Capital.
Sheria hiyo inadaiwa kukiuka mawakala, wapatanishi na uwawekezaji wengine kwa wachezaji.
Chelsea, ambao walisema wameripoti ukiukaji wa sheria unaowezekana kwa FA wenyewe, wana hadi Septemba 19 kujibu.
Kuna machaguo mawili ya kuiadhibu Chelsea, ikiwa ni pamoja na faini, vikwazo vya uhamisho na kukatwa pointi. Hata hivyo, ushirikiano wa hali ya juu wa The Blues utazingatiwa.
Soma zaidi:
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa dharura kuhusu droni za Urusi nchini Poland

Chanzo cha picha, Sumy OVA / BBC RUSSIAN
Kwa ombi la Poland, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kujadili ukiukaji wa Urusi wa anga ya Poland, Reuters iliripoti, ikiinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland.
Hatua hiyo ilikuja kujibu oparesheni ya usiku moja ambayo Warsaw, ikisaidiwa na washirika wa NATO, ilitungua ndege kadhaa zisizo na rubani za Urusi ambazo zilikiuka anga yake siku ya Jumatano.
Katika siku ya shambulizi wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema haikupanga kushambulia maeneo yoyote nchini Poland, baada ya Warsaw kusema ndege 19 zisizo na rubani za Urusi ziliingia kwenye anga yake wakati wa mashambulizi ya usiku magharibi mwa Ukraine
Aidha wizara ya Mambo ya nje ya Urusi ilisema Poland imekuwa ikieneza "simulizi za uwongo" kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani ili "kuzidisha mzozo wa Ukraine". ."Hata hivyo, tuko tayari kufanya mazungumzo na wizara ya ulinzi ya Poland kuhusu suala hilo."
Unaweza pia kusoma:
Qatar yasema 'tumesalitiwa'

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilisema matamshi ya Netanyahu "hayashangazi kutoka kwa mtu anayetegemea matamshi ya itikadi kali ili kupata kura za uchaguzi." Qatar ilitoa taarifa yenye maneno makali mapema Alhamisi asubuhi ikilaani matamshi ya Netanyahu kuhusu uwepo wa ofisi ya Hamas, na kuyaita "ya kutojali."
Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alisema: "Siwezi kupata maneno ya kuelezea kiwango cha hasira zetu. Huu ni ugaidi wa serikali. Tumesalitiwa."
Qatar imesema kuwa "Netanyahu anajaribu kuharibu kila fursa kwa utulivu na amani," baada ya kufanya "shambulio la wazi" dhidi ya viongozi wa Hamas huko Doha.
Qatar iliongeza kuwa ni "ufahamu wa umma" kwamba maafisa wa Qatar wanakutana na viongozi wa Hamas, kama sehemu ya jukumu la Qatar kama mpatanishi katika mzozo unaoendelea wa Mashariki ya Kati.
Doha ilifafanua kuwa "kila kitu kuhusu mkutano huu kinajulikana kwa Waisraeli na Wamarekani, si jambo tunaloweza kuficha... Hakuna sababu ya kuuchukulia kuwa unahifadhi ugaidi.''
Haya yanajiri huku mamlaka ya Qatar ikisema bado inawasaka watu wawili waliotoweka na kuyatambua mabaki ya miili ya binadamu baada ya shambulio la Israel kuwalenga viongozi wakuu wa Hamas mjini Doha siku ya Jumanne.
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa kuna wasiwasi katika duru za kijeshi za Israel kwamba shambulio hilo lenye utata mkubwa halikufanikiwa.
Wizara ya mambo ya ndani ya Qatar imeitambua miili ya wanachama watatu kati ya watano wa ngazi ya chini wa Hamas ambao kundi lenye silaha la Palestina lilisema waliuawa pamoja na afisa wa usalama wa Qatar.
Unaweza pia kusoma:
Arusha: Mwendesha mashtaka aomba Kabuga arejeshwe Rwanda

Chanzo cha picha, Live Event
Maelezo ya picha, Félicien Kabuga akiwa katika mahakama ya The Hague, Uholanzi, mwaka jana Mwendesha mashitaka wa kitengo cha Mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda (ICTR) kilichosalia kusikiliza kesi zilizoachwa na Mahakama hiyo ya Arusha amekitaka kitengo hicho kufanya utafiti wa kuachiwa kwa muda kwa Félicien Kabuga na kuhamishiwa Rwanda, nchi alikozaliwa ambayo "ndio pekee imeonyesha nia ya kumpokea", kwa mujibu wa waraka kutoka katika kitengo hicho.
Kwa sasa Kabuga anazuiliwa katika gereza la The Hague, Uholanzi, baada ya chumba cha taasisi inayofanya kazi huko mnamo mwezi Septemba, 2024 kuamua kusitisha kwa muda usiojulikana kesi ya Kabuga mwenye umri wa miaka 90 kwa misingi ya afya, na kwamba ataachiliwa kwa dhamana.
Kabuga alishtakiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kifedha kwa mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda, mashtaka aliyoyaita "uongo".
Jumanne mjini Arusha, Tanzania, jopo la majaji watatu; Iain Bonomy, Mustapha El Baaj na Margaret M. deGuzman na ripota Bw. Abubacarr M. Tambadou msajiliwa mahakama walijadili kuhusu kuachiliwa kwa muda kwa Kabuga na kurejeshwa Rwanda.
Hati hiyo ya mahakama inasema kwamba kutokana na matukio ya miaka miwili iliyopita, “Kabuga akiachiliwa atakwenda Rwanda pekee”.
Redio ya Ufaransa RFI inaripoti kwamba wakili wa Kabuga alijaribu kuuliza moja ya nchi za Ulaya kumkubali. Lakini , hata Ufaransa, nchi ambayo alikamatwa mwezi Mei, 2020 baada ya miaka 26 ya kuwa mafichoni haijakubali kumkaribisha.
Unaweza pia kusoma:
Kwa picha: Ethiopia yasherehekea mwaka mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Barabara hupambwa kwa taa za kuvutia Wakati majira ya baridi kali yanapoisha, hali ya hewa ya baridi inafifia, nuru huanza kuangaza, na dunia kupambwa na kijani kibichi na maua, Waethiopia waanza mwaka wao mpya.
Sherehe hii hupambwa kwa maua ya Adai, ambayo huashiria mwisho wa mwaka wa awali na mwanzo wa mpya.
Mwewe, ambao huashiria mwisho wa majira ya baridi na mwanzo wa enzi mpya, pia huanza kuonekana akiwa na manyoya yake mapya.
Waethiopia wanasherehekea mwaka wao mpya mnamo Septemba 1, wakikamilisha miezi 13 inayoufanya mwaka wao kuwa wa kipekee tofauti na maeneo mengine duniani ambako mwaka huwa na miezi 12.
Muda nao uhesabiwa tofauti
Muda unahesabiwa tofauti -ambapo siku ikiwa imegawanywa sehemu mbili za masaa 12 kuanzia 06:00, ambayo inafanya mchana na usiku wa manane saa sita kwa wakati wa Ethiopia.
Kwahiyo ukipanga kikao na mtu aliyeko Addis Ababa saa nne asubihi kwaajili ya kahawa-usishangae ukamuona huyo mtu akitokea saa sita.
Hizi ni baadhi ya picha za sherehe za Mwaka mpya wa Ethiopia:

Maelezo ya picha, Masoko hufurika wanyama wanyama wanaochinjwa kwa ajili ya sherehe za mwaka mpya 
Maelezo ya picha, Kuku pia ni kitoweo kinachopendwa na Waethiopia katika sherehe za mwaka mpya 
Chanzo cha picha, Getty Images


Maelezo ya picha, Maua haya huashiria kipindi cha Mwaka mpya 

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Waromania huvaa mavazi ya ngozi ya dubu kuadhimisha Mwaka Mpya 
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa maelezo zaidi ya taarifa hii unaweza kusoma:
Trump alaani mauaji ya mshawishi wa kisiasa na mshirika wake aliyepigwa risasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Charlie Kirk alipigwa kupigwa risasi alipokuwa akizungumza katika hafla katika Chuo Kikuu cha Utah Valley. Rais wa Marekani amelaani kifo cha Charlie Kirk Kirk aliyekuwa alikuwa mmoja wa wanaharakati wahafidhina (Conservative) mashuhuri na mwanahabari nchini Marekani na mshirika wa kutumainiwa wa Rais Donald Trump.
Ameyataja mauaji ya Charlie Kirk 'wakati wa giza kwa Marekani' huku msako mkali ukiendelea kuwapata wahusika wa shambulio hilo, lililowashutua Wamarekani.
Charlie Kirk , 31, aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akizungumza katika hafla katika Chuo Kikuu cha Utah Valley.
Kirk alipigwa risasi moja shingoni, video iliyothibitishwa na kitengo cha uhakiki wa habari cha BBC -BBC Verify, imeonyesha.
Hakuna mtu mwingine aliyepigwa risasi wakati wa tukio hilo. Mshambuliaji bado hajakamatwa.
Mke na watoto wa Kirk walikuwepo wakati wa ufyatuaji risasi, kulingana na Seneta wa Oklahoma Markwayne Mullins
Bado hakuna sababu inayojulikana ya upigaji risasi huo
Mnamo 2012, akiwa na umri wa miaka 18, alianzisha shirika la Turning Point USA, shirika la wanafunzi ambalo linalenga kueneza maadili ya kihafidhina katika vyuo vya Marekani.
Mitandao yake ya kijamii na podikasti ya kila siku iliyojulikana mara nyingi alikuwa akijadiliana na wanafunzi kuhusu masuala kama vile utambulisho wa watu waliobadili jinsia, mabadiliko ya hali ya hewa, imani na maadili ya familia.
Kirk alikuwa ameoa na alikuwa na watoto wawili wadogo, ambao walikuwa naye wakati wa tukio la ufyatuaji risasi.
Mauji yake pia yamelaaniwa na viongozi mbali mbali wa kisiasa wa Marekani na nje ya nchi, walioyataji kama yasiyokubalika na kutoa wito wahusika waadhibiwe ili kuyakomesha.
Ghana yakubali kuwapokea raia wa Afrika Magharibi waliofukuzwa kutoka Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais wa Ghana John Mahama Rais wa Ghana John Mahama amethibitisha kuwa nchi hiyo imekubali kuwapokea raia wa Afrika Magharibi waliofukuzwa kutoka Marekani.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Accra, Rais Mahama alifichua kuwa watu 14 waliofukuzwa, wengi wao wakiwa Wanigeria na mmoja wa Gambia, tayari wamewasili Ghana chini ya makubaliano ya nchi mbili.
Rais Mahama alieleza kuwa Marekani iliwasiliana na Ghana kukubali raia watatu kuondolewa Marekani, na Ghana ilikubali kuwakubali raia wa Afrika Magharibi, akitoa mfano wa Itifaki ya ECOWAS kuhusu uhuru wa harakati huru. Itifaki hiyo inaruhusu raia wa nchi wanachama kuingia na kuishi katika nchi nyingine za Afrika Magharibi bila viza kwa hadi siku 90.
"Hatuna shida kuwakubali," Rais Mahama alisema, akiongeza kuwa Ghana iliwezesha kurejeshwa kwa rais wa Nigeria waliofukuzwa nchini mwao kwa basi, wakati raia wa Gambia akisaidiwa na mamlaka ya Ghana na ubalozi wa Gambia nchini Ghana.
Hii ni sehemu ya juhudi za utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji ambao wako Marekani kinyume cha sheria, huku baadhi ya nchi za Kiafrika zikiwa tayari zinapokea wahamiaji waliofukuzwa. Rwanda, Sudan Kusini, na Eswatini zimekubali kuwapokea raia waliofukuzwa kutoka Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Qatar yasema msako unaendelea katika eneo la mashambulizi ya Israel yanayolenga viongozi wa Hamas

Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka ya Qatar inasema bado inawasaka watu wawili waliotoweka na kuyatambua mabaki ya miili ya binadamu baada ya shambulio la Israel kuwalenga viongozi wakuu wa Hamas mjini Doha siku ya Jumanne.
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa kuna wasiwasi katika duru za kijeshi za Israel kwamba shambulio hilo lenye utata mkubwa halikufanikiwa.
Wizara ya mambo ya ndani ya Qatar imeitambua miili ya wanachama watatu kati ya watano wa ngazi ya chini wa Hamas ambao kundi lenye silaha la Palestina lilisema waliuawa pamoja na afisa wa usalama wa Qatar.
Hamas imedai jaribio la kuua timu yake ya mazungumzo lilishindikana. Katika mahojiano na CNN, waziri mkuu wa Qatar hakufichua hatma ya mpatanishi mkuu wa Hamas Khalil al-Hayya.
"Hadi sasa... hakuna tamko rasmi," Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani alisema Jumatano jioni.
Pia alisema hatua ya Israel ni sawa na "ugaidi wa serikali" na kwamba anatumai washirika wa likanda wa Qatar watakubali "jibu la pamoja".
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara tukikuletea habari za kikanda na kimataifa.
