Mauaji ya Rwanda: Jinsi Felicien Kabuga alivyojificha kwa miaka 26

Mamlaka zimemtafuta Bwana Kabuga kwa miaka mingi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mamlaka zimemtafuta Bwana Kabuga kwa miaka mingi

Mfanyabiashara tajiri Félicien Kabuga aliwakwepa waendesha mashtaka wa jopo lililokuwa likichunguza mauaji ya kimbari nchini Rwanda kwa zaidi ya miongo miwili na nusu kwa kutumia majina 28 tofauti ya watu maarufu katika mabara mawili ili kutokamatwa.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 84 amekuwa mafichoni kwa muda mrefu hali ya kwamba jopo la kimataifa lililobuniwa kuchunguza mauaji hayo ya 1994 liliacha kufanya kazi yake.

Lakini hatimaye alisakwa katika maficho yake katika kijiji kimoja cha mji mkuu wa Ufaransa na kupatikana kufuatia uchunguzi ulioanzishwa na Serge Brammerts, mwendesha mashtaka wa Umoja wa mataifa akiongoza jopo linalosimamia uhalifu wa kivita nchini Rwanda na Yugoslavia.

''Tulijua mwaka mmoja uliopita kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa yeye kuwa nchini Uingereza, Ufaransa ama Ubelgiji na tuliamua miezi miwili iliopita kwamba alikuwa nchini Ufaransa'', alisema mwendesha mashtaka mkuu wa jopo hilo la kuchunguza mauaji nchini Rwanda.

Mamlaka nchini Ufaransa ilituonesha nyumba anayoishi kama maficho, hatua iliosababisha operesheni hiyo.

Mojawapo ya sababu kuu kwanini alifanikiwa kutoroka kwa muda mrefu ni kuhusishwa kwa watoto wake, alisema.

Félicien Kabuga alikuwa amejificha kwenye makazi ya eneo la Asnières-sur-Seine

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Félicien Kabuga alikuwa amejificha kwenye makazi ya eneo la Asnières-sur-Seine

Anajulikana kuwa na watoto watano - watoto wake wawili walikuwa wameolewa na watoto wa aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, ambaye kifo chake baada ya ndege yake kuangushwa tarehe 6 mwezi Aprili 1994 kilisababisha mauaji hayo ya kimbari.

Wachunguzi wa Kimataifa waliwachunguza watoto wake ili kubaini anakoishi baba yao, ambapo alikuwa anaishi kwa kutumia pasipoti kutoka kwenye taifa la Afrika lisilojulikana.

Kulingana na kanali Eric Emaraux, anayeongoza kitengo maalum cha polisi katika kukabiliana na uhalifu, mlipuko wa virusi vya corona pia ulisadia kwasababu amri ya kutotoka nje ilisitisha operesheni nyingi katika maeneo mengi ya Ulaya, na hivyobasi kutoa fursa ya kumsaka mtu anayedaiwa alikuwa mfadhili mkuu wa mauaji ya kimbari.

Katika siku 100 pekee mwaka 1994, takriban watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda na watu wa kabila la Wahutu ambao bwana Kabuga, mfanyabiashara ambaye alikuwa amejinufaisha kupitia sekta ya majani chai aliwaunga mkono.

Walikuwa wakiwalenga watu wasio wengi wa jamii ya Watutsi , pamoja na wapinzani wa kisiasa bila kuchagua kabila lao.

Marekani ilikuwa imetoa $5m (£4.1m) kama zawadi kwa taarifa zitakazosababisha kukamatwa kwa Kabuga.

Lakini ilikuwa inashangaza kwamba kwa miaka mingi mtu aliyekuwa anatafutwa sana Afrika, baada ya kushtakiwa kwa makosa saba ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu 1997, alifanikiwa kuishi mafichoni na kukwepa mkono wa sheria katika mataifa na mabara.

Je alikuwa akifichwa nchini Kenya?

Bwana Kabuga amedaiwa kuishi katika mataifa mengi ya Afrika mashariki , ikiwemo Kenya ambapo alikuwa na familia yake na maslahi ya kibishara.

Kenya ilisemakana kwa muda mrefu kumhifadhi mtoro huyo , huku wanasiasa wenye uwezo mkubwa wakidaiwa kuhujumu juhudi za kumkamata.

Je Filicien Kabuga ni nani?

Ndiye aliyekuwa mtu tajiri zaidi nchini Rwanda kabla ya mauaji ya 1994.

Akijipatia utajiri wake kupita bishara ya majani ya chai mwaka 1970 na alifanya biashara katika sekta chungu nzima nyumbani na katika mataifa ya kigeni.

Alikuwa mshirika wa karibu wa chama tawala cha MRND - na alikuwa na uhusiano na rais wa zamani Juvenal Habyarimana ambaye alifariki 1994.

Akituhumiwa kwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji hayo na kutumia biashara yake na uwezo wake kupanga na kufadhili mauaji.

Mmiliki wa kituo cha redio ya kibinafsi RTLM alishutumiwa kwa kuwachochea watu wa kabila la Hutu kuwaua Watutsi.

Mwaka 2006, jopo la kimataifa la Rwanda lililokuwa likichunguza mauaji hayo lilisema lina ushahidi kwamba bwana Kabuga alizuru nchini Kenya ama hata kuishi nchini humo, ambapo alikuwa akisimamia maslahi yake ya kibishara.

Miaka mitatu baadaye, Bwana Stephen Rapp, ambaye alikuwa balozi wa Marekani aliishutumu serikali ya Kenya kwa kukataa kumtoa bwana Kabuga.

Kulikuwa na ushahidi kwamba bwana Kabuga alihudhuria hafla zilizoshirikisha watu maarufu, alisema madai ambayo Kenya imekana.

Ni wazi kwamba familia ya bwana Kabuga ilikuwa ikimiliki mali nchini Kenya baada ya mali moja kuzongwa na kesi 2015 wakati mkewe, Josephine Mukazitoni , ambaye alikuwa mmiliki mwenza , alipojaribu kumiliki.

Kutafutwa nchini Kenya

Vyombo vya habari vilisema kwamba Bwana Kabuga alikuwa nchini Kenya katika maeneo tofauti , japokuwa havikutoa uthibitisho kwamba yeye ama mkewe waliishi nchini humo.

Alisemekana kutoroka mitego ya polisi mara kadhaa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.

Zaidi ya watu 800,000 waliuawa wakati wa mauaji ya kimbari

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 800,000 waliuawa wakati wa mauaji ya kimbari

Katika uvamizi mmoja wa Polisi tarehe 19 Mwezi Julai 1997 jijini Nairobi, wakati polisi walipowakamata washukiwa wengine saba wa mauaji ya Rwanda , bwana Kabuga alidaiwa kutoroka kufuatia onyo la mapema kutoka kwa afisa mkuu wa polisi.

Kwa waandishi waliokuwa wakimtafuta ilionekana kuwa biashara hatari sana.

Tarehe 16 Januari 2003, mwandishi huru William Munuhe alipatikana ameaga nyumbani kwake mjini Nairobi.

Nduguye Josephat Gichuki anasema kwamba baada ya kifo chake , aligundua kwamba Munuhe alikuwa ameanzisha operesheni kali na shirika la ujasusi nchini Marekani FBI kumkamata bwana Kabuga kwa kujifanya kuwa mfanyabiashara.

la kushangaza ni kwamba maafisa wa polisi walisema kwamba kifo cha Munuhe kilikuwa cha kujiua mwenyewe kutoka kwa moshi wa kaboni baada ya kuvuta moshi huo kutoka kwa stovu, bwana Gichuki aliiambia BBC.

''Akiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, mimi mwenyewe niliona shimo la risasi kichwani mwake na damu katika chumba chake''.

Mamlaka zimemtafuta Bwana Kabuga kwa miaka mingi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mamlaka zimemtafuta Bwana Kabuga kwa miaka mingi

Miaka minane baadae mwandishi John Allan Namu wa Kenya anaamini kwamba alidanganywa makusudi na chanzo kimoja nchini Kenya kwa mtu tofauti aliyedaiwa kuwa bwana Kabuga.

Anahisi kwamba hilo lilifanyika kwasababu baadhi ya watu hawakupendelea kile ambacho uchunguzi wake ulikuwa umebaini , ikiwemo ushahidi kwamba bwana Kabuga alikuwa na akaunti ya benki ambayo alikuwa akiitumia kufanyia biashara.

Suala lote hilo lilikuwa na utata hali ya kwamba yeye na familia walilazimika kwenda mafichoni kwa miezi kadhaa kutokana na vitisho vya kifo alivyokuwa akipokea.

Pale alipokamatwa ni thibitisho kwamba Kabuga alikwepa mitego ya serikali kutokana na ushirikiano wake na raia wa mataifa hayo duniani ikishirikisha Kenya, Namu aliambia idhaa ya BBC ya maziwa makuu.

Baada ya mauaji hayo ya halaiki , bwana Kabuga alitorokea nchini Switzerland lakini hakuruhusiwa kusalia nchini humo na aliripotiwa kurudi Afrika kupitia Kinshasa , mji mkuu wa DR Congo.

Ushahidi mwingi unaonesha akiwa Kenya, japokuwa bwan Brammertz anasema kwamba alionekana nchini Madagascar na Burundi.

Mawakili wa Kabuga wanasema, Kabuga anataka kushtakiwa nchini Ufaransa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mawakili wa Kabuga wanasema, Kabuga anataka kushtakiwa nchini Ufaransa

Lakini habari kama hizo hazikuwa na thibitisho lolote lililopelekea kukamatwa kwake , hivyobasi operesheni iliopelekea kukamatwa kwake ilikuwa siri kubwa huku akitafutwa maeneo kadha kwa pamoja, alisema.

Ilichukua takriban miaka miwili, kuanzia maficho yake ya mwisho - nchini Ujerumani ambapo alionekana mara ya mwisho wakati alipoenda kufanyiwa upasuaji 2007.

Uchunguzi wa simu zake na data yake ya kifedha uliwapeleka hadi mjini Paris Ufaransa.

Sio rahisi kufikiria kwamba angetorokea nchini Ufaransa bila ya usaidizi wa washirika wake, anasema Patrick Baudoing wa shirika la kimataifa la haki za kibinadamu.

Habari kuhusu uwepo wake kwa miaka mingi ulilifanya shirika la Human Rights Watch kuitisha uchunguzi kuhusu jinsi na nani aliyemsaidia.

Matembezi wakati wa amri ya kutotoka nje

Majirani zake wanasema mzee uyo aliishi katika eneo hilo kwa takriban miaka mitatu hadi minne.

Olivier Olsen, kiongozi wa muungano wa wamiliki wa nyumba katika mtaa huo aliokuwa akiishi, aliambia AFP kwamba bwana Kabuga alikuwa msiri mkubwa na mtu aliyetoa matamshi kwa kunong'ona alipokuwa akisalimia.

Kujificha kwa Kabuga kwa miaka 26 kulizua maswali mengi

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha, Kujificha kwa Kabuga kwa miaka 26 kulizua maswali mengi

'Kabla ya amri ya kutotoka nje alionekana akifanya matembezi ndani ya mtaa huo', alisema.

Bwana Kabuga kwa sasa anazuiliwa katika jela ya La Sante katikati mwa mji mkuu wa Paris , ambapo atasalia hapo hadi atakapohamishwa na kuzuiliwa na IRMCT.

Hatahivyo wakili wa Kabuga amesema kwamba mteja wao angependelea kufunguliwa mashtaka nchini Ufaransa.

Manusura wa mauaji hayo ya kimbari wanatumai kwamba kesi hiyo haitachukua muda na kwamba haki itapatikana kwa haraka.

Baada ya kukamatwa kwake Valerie Mukabayire , kiongozi wa wajane nchini Rwanda,aliambia BBC.

Kila manusura wa mauaji hayo ya 1994 nchini Rwanda anafurahia kukamatwa kwake.

'Kila mtu amekuwa akisubiri habari hizi. Ni kitu kizuri kwamba atakabiliwa na mkono wa sheria'.