Je, ACT Wazalendo kinaweza kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania?

- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Wakati chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT Wazalendo kikijiandaa kufanya Mkutano Mkuu maalumu jijini Dar es Salaam Januari 29 mwaka huu, swali moja kubwa ambalo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanajiuliza ni iwapo chama hicho kinaweza kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika miaka michache ijayo.
Mkutano Mkuu huo unatarajiwa kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali ikiwemo ya Mwenyekiti wa chama hicho - kuziba nafasi iliyoachwa wazi na gwiji wa siasa za Tanzania, Maalim Seif Shariff Hamad, aliyefariki dunia Februari 17, 2021. Huu ni uchaguzi muhimu kwa sababu chama hicho kitaaanza maisha mapya bila ya mwanasiasa aliyekuwa kete muhimu zaidi ya kisiasa kwenye chama hicho katika kipindi kifupi alichokuwa Mwenyekiti.
Kwa sasa, ACT Wazalendo kinachukuliwa kama chama cha tatu kwa ukubwa nchini Tanzania; kikiwa nyuma ya chama tawala -CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Hata hivyo, ACT kilianzishwa takribani miaka saba tu iliyopita, na kupanda kwake kumekifanya kiwe mbele ya vyama vingine mashuhuri vilivyowahi kuwa vikubwa kabla yake; NCCR -Mageuzi, Civic United Front (CUF) na Tanzania Labour (TLP).
Kabla ya kuingia kwenye mjadala kama hatimaye ACT Wazalendo kinaweza kuja kuwa chama kikuu cha upinzani au la, ni muhimu kwanza kutazama ni mambo gani ambayo kihistoria yamekuwa yakiamua umaarufu wa vyama vya upinzani katika kipindi cha takribani miaka 30 iliyopita - muda ambao siasa za vyama vingi zilirejeshwa rasmi kisheria nchini Tanzania Julai mosi, 1992.
Rais aliye madarakani
Katika historia ya vyama vingi nchini Tanzania, vyama vinne vimewahi kuwa vinara wa upinzani. Vyama hivyo ni NCCR-Mageuzi, TLP, CUF na Chadema. Kimsingi, vyama hivyo - kuondoa CUF upande wa Zanzibar na Chadema, vimekuwa na utamaduni wa kudumu kwa walau uchaguzi mmoja na kisha kutoa nafasi ya kuibuka kwa chama kingine.
Jambo la kwanza linaloamua hatma ya kukua kwa chama cha upinzani nchini Tanzania limekuwa ni aina ya Rais aliye madarakani. Ukuaji wa siasa za upinzani umekuwa ukitegemea kuwepo kwa Rais kutoka CCM anayeamini katika demokrasia na siasa za ushindani au vinginevyo.
Marais wawili wa Tanzania wanaweza kuingia katika kundi hili; Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliongoza Tanzania katika mfumo wa chama kimoja miaka 20 akiwa Rais kuanzia mwaka 1965 hadi anastaafu 1985 japo aliendelea kuwa Mwenyekiti wa CCM hadi 1990. Benjamin Mkapa hakuwa mvumilivu na mstahamilivu wa kiwango cha wawili hao na John Magufuli - kwa kukosa maneno ya kumweleza, abaki kuwa John Magufuli.
Mwinyi ndiye aliyeruhusu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi na kutoa fursa kwa wasomi na wanasiasa kuendesha mijadala na mikutano ya kuhamasisha watu kujiunga na siasa za upinzani. Chama kilichonufaika na kukua zaidi wakati wake ni NCCR Mageuzi. Kwa sababu hiyo, ukuaji wa NCCR unaweza kuhusishwa moja kwa moja na urais wa Mzee Mwinyi.
CUF ilianzishwa na kukua, kwa upande wa Zanzibar, wakati wa Mwinyi pia. Hata kama Zanzibar kulikuwa na mazingira na utamaduni tofauti wa kisiasa ukilinganisha na Tanzania Bara, Rais Salmin Amour wa visiwa hivyo, asingeweza kuiwekea vikwazo ambavyo Rais wa Tanzania - Mzanzibari mwenzake, alikuwa ameamua visiwepo.
Chadema ilikuwa kwa kasi kubwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 hadi 2015. Huu ni wakati ambapo Kikwete alikuwa Rais wa Tanzania. Kwa sababu hiyo, ukuaji wa Chadema - pamoja na sababu nyingine nitakazozieleza katika makala haya, unaweza kuhusishwa moja kwa moja na urais wa Kikwete.
Kwa kifupi, kama Rais wa Tanzania angekuwa Magufuli katika wakati wa Kikwete au Mwinyi, historia ya vyama vya upinzani isingekuwa hii ya leo. Kuweka hoja hii katika muktadha sahihi, hakuna chama chochote cha upinzani kinachoweza kusema kilikua wakati wa Magufuli.
Sababu nyingine za ziada
Uchambuzi wowote kuhusu siasa za Tanzania, ni muhimu uzingatie kigezo kimoja kikubwa kuliko vyote katika siasa za nchi hiyo - CCM. Ukuaji wa upinzani hutokana pia na mnyukano au mgawanyiko wa aina fulani; maslahi, itikadi, fursa na vitu vingine ndani ya chama tawala.
Wakati wa Mzee Mwinyi, upinzani ulipata pia nguvu kwa sababu ndani ya CCM kuna waliokuwa wakiamini kwamba Rais huyo wa pili alikuwa anakitoa chama kwenye misingi ya kijamaa na kukipeleka kwenye ubepari. Kwenye nyakati za Kikwete, CCM ilipitia katika wakati mgumu kwa sababu ya makundi kiasi kwamba mara mbili ilikaribia kugawanyika huku yakiibuka visifa kama 'CCM magamba' ikimaanisha baadhi ya wanachama waliotuhumiwa kuchafua sura ya chama sababu ya mienenendo yao. Kwa sababu hiyo, ukuaji wa NCCR na Chadema kwa nyakati tofauti - ni muhimu ikahusishwa pia na minyukano ndani ya CCM.
Kuna msemo mmoja maarufu ambao hutumiwa sana kama kauli mbiu kwenye mikutano ya CCM - kwamba CCM ikiwa imara, upinzani hauwezi kupata nafasi. Kwa maneno mengine - nikinukuu maneno mashuhuri ya Nyerere; ili CCM ishindwe kwenye uchaguzi, ni lazima kwanza ipasuke.
Upinzani wa Tanzania pia umekuwa ukikua kwa sababu ya kuwa na kiongozi kipenzi cha wananchi. Ukuaji wa CUF unahusishwa na Maalim Seif, NCCR-Mageuzi na Augustine Mrema. Ni Chadema pekee ambayo ilikua pasipo kuwa na kiongozi mmoja kipenzi cha watu na jambo hili nitalitolea pia maelezo kwenye makala haya.
Sababu nyingine ni uwepo wa kikundi cha wanamikakati wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, kuwa na ushawishi kwenye vyombo vya habari na kuwa na kizazi cha viongozi kinachobadilika kutoka kimoja kwenda kingine. Hii ndiyo ilikuwa nguvu kubwa ya NCCR Mageuzi na Chadema - ingawa kwa viwango tofauti.

Chanzo cha picha, CHADEMA
NCCR ilijengwa na wasomi na wanaharakati mashuhuri kama vile akina Dkt. Masumbuko Lamwai, Dkt. Ringo Tenga, Mabere Marando, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwage - wakiungwa mkono na vijana kama vile James Mbatia, Anthony Komu na Msafiri Mtemelwa. Vikao vya juu vya chama cha NCCR-Mageuzi vilikuwa chemchem ya fikra na mikakati mikubwa. Mgogoro uliokimaliza chama hicho ulisababisha kundi hili muhimu kupoteza hamu ya siasa na wengine kuamua kuhamia Chadema.
Chadema - katika kilele cha ubora wake, kilikuwa na watu kama Prof. Mwesiga Baregu, Marando, Profesa Kitila Mkumbo, Bob Makani, Dk. Wilbrod Slaa, Freeman Mbowe - na vijana kama Zitto Kabwe, John Mnyika, Halima Mdee na wengine waliokifanya kiwe kama mashine inayofanya kazi pasipo kutegemea mtu mmoja - a political juggernaut- nikiazima msemo wa lugha ya Kiingereza.
Ukuaji wa chama cha upinzani nchini Tanzania unategemea pia uwezo wa kifedha wa chama husika. NCCR ilinufaika kwanza na ukweli kwamba waasisi wake hawakuwa watu "wenye njaa"- baadhi wakiwa wahadhiri wa vyuo kikuu na wengine wakiwa na mapato kutoka shughuli zao binafsi. Chadema ilifaidika na kuungwa mkono na matajiri kama Philemon Ndesamburo waliokuwa na uwezo wa kuingia mfukoni kuifanya Chadema ijiendeshe. Haikuwa ajabu kwamba - kwa kuchanganya uwezo wa kifedha na ubunifu, kiliweza kuagiza helikopta za kampeni na kufanya siasa za kisasa miaka 15 iliyopita.
Changamoto na fursa za ACT Wazalendo
Wakati huu, ACT ina faida mbili kubwa kisiasa; mosi ni kwamba Rais Samia Suluhu Hassan anaonekana kama ni aina ya Rais anayeweza kufananishwa zaidi na Kikwete na Mwinyi kuliko Magufuli, Nyerere au Mkapa. Kama ataendelea kuachia uhuru wa vyama kufanya siasa, hilo litatoa fursa ya kuibuka kwa chama kingine kama ilivyotokea kwa watangulizi wake wawili hao.
Pili ni kwamba kama ilivyokuwa wakati wa Mwinyi na Kikwete; hali haionekani kama ni shwari ndani ya CCM. Matukio ya karibuni na kauli kama za aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, na wana CCM wanaohusishwa na utawala wa Magufuli, zinaonyesha CCM si moja. Haya ni aina ya mazingira yaliyoruhusu kukua kwa upinzani kwenye miaka ya nyuma. Kuna fursa ya kukua au kuibuka kwa chama kingine.
ACT ina faida ya kuwa na wanasiasa kama Zitto, Ismail Jussa Ladhu, Othman Masoud Othman, Eddy Riyami, Joran Bashange, Mansour Himidi na Juma Duni Haji lakini pia vijana wanaoibuka kama Abdul Nondo, Ado Shaibu na Bonifacia Mapunda. Chama kinaweza kukosa mwanasiasa wa aina ya Maalim Seif au Mrema lakini ikatengeneza mmfumo thabiti wa kisiasa isiyomtegemea mtu mmoja - kama ambavyo Chadema ilifanya hapo awali.

Chanzo cha picha, IKULU Tanzania
Zitto hana ushawishi kama wa Mrema au Maalim Seif ambao kwanza walipata nafasi ya kutumika serikalini - lakini kwenye mitandao ya kijamii - yeye ndiye mwanasiasa wa Kitanzania anayefahamika na mwenye wafuasi wengi zaidi - akizidiwa na Kikwete pekee. Katika siasa za sasa za kidijitali, huu ni mojawapo ya msingi wa ukuaji wa chama.
ACT ina changamoto mbili kubwa; mosi haionekani kuwa na uwezo wa kifedha - walau kwa sasa, wa kuweza kujitanua na kukua. ACT haina 'Ndesamburo' wake au maprofesa na wanaharakati wa kukisaidia kifedha. Katika siasa za kisasa, unahitaji fedha kujiongezea umaarufu na kukua. Wapinzani walioshinda katika chaguzi zilizopita Kusini mwa Afrika; Hakainde Hichilema wa Zambia na Lazarus Chakwera wa Malawi ni wanasiasa matajiri waliokuwa na ukwasi wa kutosha kufadhili shughuli zao za kisiasa.
Marekani wanajua kwamba mgombea atakayekuwa Rais baada ya Joe Biden ni yule atakayekuwa na fedha nyingi za kufanya kampeni za uchaguzi. Barack Obama, Donald Trump, Bill Clinton na George Bush wote waliongoza kwa kukusanya fedha za kampeni kabla ya kushinda uchaguzi. Kama kuna udhaifu katika siasa za kiliberali ni huu wa matumizi na umuhimu wa fedha katika siasa. Kwa hali yake ya sasa, ni vigumu kwa ACT kuipiku Chadema.
Jambo la pili ni kutegemea mambo yaliyo nje ya uwezo wake. Kwa mfano, Rais Samia ni lazima awe mwanademokrasia ili ACT ikue. La pili ni kwamba ni lazima Chadema ifanye makosa ya kisiasa ndiyo yenyewe ikue zaidi - walau nje ya Zanzibar. Chadema ilikua kwa sababu ya mgogoro wa NCCR na ili kuipiku ni lazima nayo ifanye makosa.
Kwa mfano, kama Chadema itaamua kususia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuiacha ACT Wazalendo ishindane peke yake na CCM, na Rais Samia akawa ameendelea kuatamia demokrasia na uhuru wa kutoa maoni, njia ya ACT Wazalendo kuwa chama kikuu cha upinzani itakuwa nyeupe.
Angalizo ni moja; ni lazima hali hii ya sasa iendelee kama ilivyo. Uchambuzi huu haujazingatia uwepo wa tukio la kisiasa lisilo la kawaida linaloweza kutokea wakati wowote kuelekea mwaka 2025 au mwaka 2030.












