Shabiki wa Uganda apigwa risasi akisherehekea Arsenal kuifunga Manchester United

Muda wa kusoma: Dakika 2

Shabiki wa klabu ya Arsenal ya Uingereza, ambaye alikuwa akishangilia ushindi wa timu hiyo dhidi ya Manchester United, anadaiwa kupigwa risasi na mlinzi mmoja nchini Uganda.

Shabiki mwingine alijeruhiwa wakati mlinzi huyo alipoufyatulia risasi umati mkubwa wa wafuasi waliokuwa wakishangilia katika mgahawa mmoja katika mji wa Lukaya katikati mwa Uganda, yapata kilomita 100 kutoka mji mkuu Kampala.

Tukio hilo lilifanyika kuelekea mwisho wa mechi, ambayo Arsenal ilishinda 2-0.

Mwandishi wa habari wa eneo hilo aliambia BBC kwamba meneja wa jengo hilo alikasirishwa na kelele ambazo wafuasi hao waliokuwa wakishangilia walikuwa wakipiga na akamwomba mlinzi huyo kuingilia kati.

Hatahivyo mashabiki hawakuzingatia onyo la kunyamaza.

Walioshuhudia tukio hilo walimweleza mwandishi wa habari hizi, Farish Magembe kuwa mmiliki alizima umeme katika mgahawa huo hali iliyowakasirisha mashabiki ambao walijibu kwa kupiga kelele zaidi.

Hapo ndipo mlinzi huyo anadaiwa kufyatua risasi kadhaa.

Mwathiriwa aliyetambulika kwa jina la John Ssenyonga mwenye umri wa miaka 30 alifariki katika eneo la tukio. Shabiki mwingine wa muda mrefu wa Arsenal, Lawrence Mugejera, alipelekwa hospitali kwa matibabu.

Mlinzi na meneja wa jengo hilo wamekuwa mafichoni baada ya tukio, huku polisi wakiwatafuta.

Msemaji wa Jeshi la Polisi mkoani, Twaha Kasirye, alinukuliwa na gazeti la Daily Monitor akisema walipata bunduki katika eneo la tukio.

“Tunalaani tukio hilo na tunaomba yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia polisi kumfikisha mtuhumiwa huyo ili aweze kuzungumza,” alisema.

Pia aliwataka mashabiki kudhibiti msisimko wao.

Mvutano na vurugu za kusikitisha zinazotokana na matokeo ya mechi za soka hasa baina ya klabu za Uingereza si jambo la kawaida katika nchi hiyo ambayo Ligi Kuu ya England inafuatiliwa kwa karibu.

Mwezi Oktoba, shabiki wa Arsenal alimdunga kisu shabiki wa Manchester United baada ya wawili hao kuzozana kuhusu matokeo ya pambano kati ya Arsenal na Liverpool.

Januari mwaka jana, diwani mmoja kijana alifariki kutokana na majeraha ya kuchomwa visu mjini Kampala baada ya kuingilia kati pambano lililotokea baada ya Arsenal kushindwa na Manchester City.

Wiki moja tu kabla ya hapo, shabiki wa Arsenal alikuwa amepigwa na kifaa kutu hadi kufa huko Adjumani, katika wilaya ya Nile Magharibi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla