Kwa nini nchi hii ina idadi kubwa ya wanawake walio na zaidi miaka 100?

Mshauri wa urembo Tomoko Horino mwenye umri wa miaka 100 akijirembua nyumbani kwake kabla ya kuelekea ofisini katika jiji la Fukushima.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo 2023, Tomoko Horino alitangazwa kuwa mshauri mkongwe zaidi wa masuala ya urembo akiwa na umri wa miaka 100.
    • Author, Jessica Rawnsley
    • Nafasi, BBC News
    • Author, Stephanie Hegarty
    • Nafasi, Mwandishi
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Idadi ya watu walio na umri wa miaka100 au zaidi nchini Japan imeongezeka kwa takriban 100,000, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali.

Hii inasadikiwa kuwa rekodi mpya kwa mwaka wa 55 mtawalio ya idadi ya vikongwe nchini Japan ambao walikuwa 99,763 kufikia mwezi Septemba, wizara ya Afya ilisema Ijumaa wiki iliyopita. Wanawake wanachangia asilimia 88 ya idadi hiyo kwa ujumla.

Waziri wa Afya Takamaro Fukoka aliwapongeza vikongwe wanawake 87,784 na wanaume 11,979 kwa kujaaliwa kuishi maisha marefu na kutoa "shukrani zake kwa mchango wao wa miaka mingi katika kuendeleza jamii".

Japan inaongoza duniani kwa kuwa na watu wanaoishi maisha marefu zaidi na inajulikana kuwa nyumbani kwa mtu mkongwe zaidi duniani - ingawa baadhi ya tafiti zinatilia shaka idadi kamili ya watu wazee zaidi kote duniani.

Pia ni mojawapo ya jamii zinazozeeka kwa kasi zaidi, huku wakazi mara nyingi wakiwa na lishe bora lakini kiwango cha chini cha uzazi.

Mtu mkongwe zaidi nchini Japan ni Shigeko Kagawa,114, mwanamke kutoka Yamatokoriyama, viungani mwa mji wa Nara. Huku mwanamume mkongwe zaidi akitajwa kuwa Kiyotaka Mizuno, 111, kutoka mji wa Iwata pwani ya Japan.

Takwimu hizo zilitolewa kabla ya Siku ya Wazee wa Japani tarehe 15 Septemba, sikukuu ya kitaifa ambapo watu wapya waliotimiza umri wa miaka mia moja hupokea barua ya pongezi na kikombe cha fedha kutoka kwa waziri mkuu.

Mwaka huu watu, 52,310 walistahiki kutambuliwa, wizara ya afya ilisema.

Wazee wakifanya mazoezi ya viung ya katika bustani siku ya Wazee

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wajapani wanazingatia sana lishe bora, sio rahisi kupatikana na magonjwa kwasababu wana utamaduni wa kufanya mazoezi ya pamoja
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika miaka ya 1960, Japan ilikuwa na idadi ndogo ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 100 ukilinganisha na mataifa mengine yaliyo na uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani - lakini hilo limebadilika kwa miongo kadhaa sasa.

Wakati serikali yake ilipoanza kufanya utafiti wa kubaini idadi ya wazee mwaka 1963, kulikuwa na watu 153 walio na umri wa miaka 100 au zaidi.

Idadi hiyo iliongezeka hadi 1,000 mwaka 1981 na kufikia 10,000 mwaka 1998.

Maisha haya marefu yanachangiwa zaidi na idadi ndogo ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo na aina fulani ya saratani ambayo kawaida huwaathiri watu wengi kama vile saratani ya matiti na ile ya tezi dume.

Japan ina kiwango cha chini cha watu walio na unene kupita kiasi, chanzo kikuu cha vitu vinavyochangia magonjwa yote mawili. Ulaji wa samaki na mboga mboga umewasaidia sana kudumisha afya bora.

Kiwango cha unene wa kupindukia ni cha chini sana kwa wanawake, jambo ambalo linaweza kueleza kwa nini wanawake wa Japani wana umri wa juu zaidi wa kuishi kuliko wenzao wa kiume.

Ulimwengu ulipoongeza kiasi cha matumizi ya sukari na chumvi kwenye vyakula, Japan iliamua kuachana na bidhaa hizo - huku ujumbe wa afya ya umma ukiwashawishi watu kupunguza matumizi ya chumvi.

Lakini sio lishe tu. Wajapani wanapendelea sana kufanya mazoezi, mtindo wa maisha ambao wanaukumbatia hadi uzeeni, wanatembea kwa miguu badala ya kutumia usafiri wa umma hali ambayo ni tofauti ukilinganisha na wenzao wa Marekani na Ulaya.

Radio Taiso, kundi la mazoezi ya pamoja kila siku limekuwa sehemu ya utamaduni wa Wajapani tangu mwaka 1928, lilibuniwa ili kuhimiza mshikamano katika jamii na kukuza afya ya umma. Utaratibu huo wa dakika tatu unatangazwa kwenye televisheni na kufanywa katika vikundi vidogo vya jumuiya kote nchini.

Hata hivyo, tafiti kadhaa zimetilia shaka uhalali wa idadi ya watu waliofikia umri wa miaka 100, zikipendekeza hitilafu za data, rekodi zisizotegemewa za umma na kukosa cheti cha kuzaliwa kunaweza kuchangia takwimu za juu.

Ukaguzi wa serikali wa sajili za familia nchini Japan mwaka wa 2010 ulifichua zaidi ya watu 230,000 walioorodheshwa kuwa na umri wa miaka 100 au zaidi ambao hawakujulikana waliko, wengine wanadaiwa kuwa walifariki miongo kadhaa iliyopita.

Ukosefu huo wa hesabu ulichangiwa na uwekaji mbaya wa rekodi na tuhuma kwamba huenda baadhi ya familia zilijaribu kuficha vifo vya jamaa zao waliozeeka ili kudai malipo yao ya uzeeni.

Uchunguzi wa kitaifa ulizinduliwa baada ya mabaki ya Sogen Koto, anayeaminika kuwa mzee zaidi huko Tokyo akiwa na umri wa miaka 111, kupatikana katika nyumba ya familia yake miaka 32 baada ya kifo chake.