Kwanini ugunduzi wa oksijeni kwenye 'kiza cha bahari' umewashangaza wanasayansi?

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hadi ugunduzi huu, iliaminika kuwa oksijeni haiwezi kuzalishwa bila jua
    • Author, Victoria Gill
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wanasayansi wamegundua oksijeni kwenye kina kirefu cha bahari, ikizalishwa na vipande vya mawe kwenye sakafu ya bahari.

Karibu nusu ya oksijeni tunayopumua hutoka baharini. Lakini, kabla ya ugunduzi huu, ilieleweka kuwa hutengenezwa na mimea ya baharini, inayofikiwa na mwanga wa jua.

Katika kina cha kilomita 5, ambapo hakuna mwanga wa jua unaoweza kupenya, oksijeni inaonekana kuzalishwa na vipande vya mawe.

Makampuni kadhaa ya uchimbaji madini yana mipango ya kukusanya mawe haya, lakini wanasayansi wa baharini wanahofia ukusanyaji huo unaweza kuvuruga maisha ya viumbe vya baharini ambavyo vinategemea oksijeni inayozalishwa.

Ugunduzi wenyewe

,j

Chanzo cha picha, NOC/NHM/NERC SMARTEX

Maelezo ya picha, Vinundu vya chuma vya ukubwa wa viazi huonekana kama miamba, iliyotapakaa sehemu za kina cha bahari

"Niliona jambo hili kwa mara ya kwanza mwaka 2013 - kiasi kikubwa cha oksijeni kinatoka kwenye sakafu ya bahari katika giza totoro," anaeleza mtafiti mkuu Prof Andrew Sweetman kutoka Chama cha Scotland cha Sayansi ya Bahari. "Nilipuuza, kwa sababu nilikuwa nimefundishwa - oksijeni inapatikana tu kupitia usanisinuru.”

Yeye na wenzake walifanya utafiti wao katika eneo la kina kirefu cha bahari kati ya Hawaii na Mexico - sehemu ya sakafu ya bahari ambayo imefunikwa na vipande hivi vya mawe.

Vipande hivi vya hujiunda vinapokusanyika na maganda magumu na uchafu mwingine. Ni mchakato unaochukua mamilioni ya miaka.

Kwa sababu vipande hivi vina lithiamu, kobalti na shaba - zote hizo zinahitajika kutengeneza betri - kampuni nyingi za madini zinaunda teknolojia ya kuvikusanya na kuvileta juu.

Ugunduzi uliochapishwa katika jarida la Nature Geoscience, unazua wasiwasi kuhusu hatari za uchimbaji wa mawe haya katika kina kirefu cha bahari.

Wanasayansi waligundua kuwa vipande hivi vinaweza kutengeneza oksijeni kwa sababu vina sifa kama betri.

"Ukiweka betri kwenye maji ya bahari, inaanza kutoa povu," anaeleza Prof Sweetman. "Kwa sababu mkondo wa umeme kwenye maji ya bahari hugawika kuwa oksijeni na hidrojeni [ambayo ni mapovu]. Tunaamini vipande hivi, hufanya mchakato kama huo lakini kwa njia ya asili.

p

Chanzo cha picha, Science Photo Library/NOAA

Watafiti katika maabara. Walipima nguvu ya umeme kwenye vipande hivyo. Waligundua kuwa umeme wake unakaribiana na umeme katika betri ya kawaida ya ukubwa wa AA.

Hii inamaanisha, vipande vya mawe vilivyokaa chini ya bahari vinaweza kuzalisha umeme mwingi.

Watafiti wanafikiri mchakato wa kuzalisha oksijeni ambayo haihitaji mwanga wa jua - unaweza kuwa unatokea kwenye sayari nyingine, na kuwa na mazingira yenye oksijeni ambapo maisha yanaweza kustawi.

Wanasayansi waonya

df

Chanzo cha picha, Camille Bridgewater

Maelezo ya picha, Watafiti walipima voltages kwenye nyuso za vinundu vya metali
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wasimamizi wa Kitaifa wa masuala ya Bahari na Anga kutoka Marekani (NOAA), wameonya uchimbaji wa mawe hayo unaweza "kusababisha uharibifu wa maisha na makazi chini ya bahari.”

Zaidi ya wanasayansi 800 wa baharini kutoka nchi 44 wametia saini onyo, linaloangazia hatari za kimazingira na kutaka kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji wa mawe hayo.

Spishi mpya zinagunduliwa katika kina kirefu cha bahari kila siku – na inaelezwa kuwa, tunajua zaidi juu ya uso wa mwezi, kuliko tunavyojua kuhusu kina cha bahari. Ugunduzi huu umefichua kwamba mawe yanayotoa oksijini yanasaidia maisha huko.

Prof Murray Roberts, mwanabiolojia wa baharini kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh ni mmoja wa wanasayansi waliotia saini ombi la kuzuia uchimbaji huo baharini.

"Tayari kuna ushahidi mwingi kwamba uchimbaji wa mawe hayo kwenye kina kirefu cha bahari utaharibu mifumo ya ikolojia ambao hatuielewi," aliiambia BBC News.

"Kwa sababu mashamba haya yanafunika maeneo makubwa kama haya ya sayari yetu, itakuwa ni wazimu kufanya uchimbaji baharini huku tukijua kuwa ni chanzo kikubwa cha uzalishaji wa oksijeni."

Prof Sweetman anaongeza: “Sioni utafiti huu kama jambo ambalo litakomesha uchimbaji.

"[Lakini] tunahitaji kuchunguza kwa undani na tunahitaji kutumia taarifa hizi na taarifa tutakazokusanya siku zijazo, ikiwa tutataka kwenda kwenye kina kirefu cha bahari kuchimba kwa njia ambazo ni rafiki zaidi kwa mazingira."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah