Kwa nini India iko mbioni kusaka madini chini ya bahari?

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

India inachukua hatua nyingine katika harakati zake za kutafuta madini ya thamani kwenye kina kirefu cha bahari ambayo yanaweza kuwa yenye umuhimu mkubwa kwa mazingira safi siku zinazokuja.

Nchi hiyo ambayo tayari ina leseni mbili za utafiti wa kina cha bahari katika Bahari ya Hindi, imetuma maombi ya kupata nyingine mbili huku kukiwa na ongezeko la ushindani kati ya mataifa makubwa duniani kupata madini muhimu.

Nchi za china, Urusi na India zinawania kufikia hifadhi kubwa ya rasilimali za madini yakiwemo cobalt, nickel, shaba na manganese - ambayo yako maelfu ya mita chini ya uso wa bahari.

Madini haya hutumika kuzalisha nishati mbadala kama vile nishati ya jua na upepo, magari ya umeme na teknolojia ya betri inayohitajika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mamlaka ya Kimataifa ya Bahari inayoshirikiana na Umoja wa Mataifa (ISA) imetoa leseni 31 za utafutaji hadi sasa, ambapo 30 kati ya hizo zinatumika. Nchi wanachama wake wanakutana nchini Jamaica wiki hii kujadili kanuni za utoaji wa leseni za uchimbaji madini.

Ikiwa ISA itaidhinisha maombi mapya ya India, idadi ya leseni yake itakuwa sawa na ile ya Urusi na moja chini ya China.

Mojawapo ya maombi ya India inalenga kuchunguza vilima vinavyofanana na bomba la moshi karibu na matundu ya hewa yanayopitisha maji yenye shaba, zinc, dhahabu na fedha - katika eneo la Carlsberg ya Bahari ya Hindi ya Kati.

Tume ya sheria na kiufundi ya ISA imetuma orodha ya maoni na maswali kuhusu hili kwa serikali ya India, kulingana na waraka ulioonekana na BBC.

Kwa kujibu maombi mengine - kuchunguza maganda ya ferromanganese yenye utajiri wa cobalt ya Bahari ya Afanasy-Nikitin katika Bahari ya Hindi ya Kati - tume imebainisha kuwa nchi nyingine ambayo haijatajwa imedai eneo la bahari (ambalo India imeomba) kama sehemu ya rafu yao iliyopanuliwa ya bara na kuuliza India kwa majibu.

Bila kujali matokeo ya maombi hayo, jambo moja ambalo liko wazi ni kwamba India haitaki kurudi nyuma katika mbio za kupata madini muhimu kutoka chini ya bahari.

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

India, China, Ujerumani na Korea Kusini tayari zina leseni za kutafuta madini katika Bahari ya Hindi.

Mnamo mwaka wa 2022, Taasisi ya Kitaifa ya Teknolojia ya Bahari ya India ilifanya majaribio ya mashine yake ya kuchimba madini katika kina cha mita 5,270 katikati mwa bonde la Bahari ya Hindi na kukusanya vinundu vya polymetallic (miamba yenye umbo la viazi ambayo iko kwenye sakafu ya bahari na ina utajiri wa manganese, cobalt, nickel na shaba).

Wizara ya sayansi ya ardhi ya India haikujibu maswali ya BBC kuhusu mipango ya uchimbaji madini katika bahari kuu ya nchi hiyo.

Marekani haiku kwenye mbio za kuchimba katika Bahari za kimataifa kwani haijaridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari, makubaliano ambayo yalisababisha kuundwa kwa ISA. Badala yake, inalenga kutafuta madini kutoka katika bahari yake ya ndani na kusindika yale yanayochimbwa na washirika wake kutoka kwenye maji ya kimataifa.

Wanaounga mkono uchunguzi wa kina kirefu wa bahari wanasema kuwa uchimbaji madini kwenye ardhi karibu umefikia kiwango cha mwisho, na kusababisha uzalishaji duni, na kwamba maeneo mengi ya vyanzo vya madini yamekumbwa na migogoro au masuala ya mazingira.

Lakini wanaharakati wa mazingira wanasema kina kirefu cha bahari ni mpaka wa mwisho katika sayari ambayo bado haijasomwa na haijaguswa na binadamu na uchimbaji madini huo unaweza kusababisha uharibifu usioweza kurekebishwa.

Nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ujerumani, Brazil na Kanada pia zinataka kusitishwa kwa muda uchimbaji wa madini ya bahari kuu, kutokana na kile wanachosema ni ukosefu wa habari kuhusu mazingira ya baharini.

xx

Benki ya Dunia imekadiria kuwa uchimbaji wa madini muhimu utahitaji kuongezeka mara tano ifikapo mwaka 2050 ili kukidhi mahitaji ya teknolojia ya nishati safi.

India ina malengo ya muda mfupi ya kuongeza uwezo wake wa nishati safi hadi gigawati 500 ifikapo 2030, na kukidhi asilimia 50 ya mahitaji yake ya nishati kutoka kwa nishati mbadala kufikia wakati huo, kwa lengo la muda mrefu la kufikia uzalishaji wa sifuri kwa gesi chafu ifikapo 2070.

Ili kufikia malengo haya, wataalam wanasema India itahitaji kupata madini muhimu kutoka kwa vyanzo vyote vinavyowezekana ikiwa ni pamoja na kina cha bahari.

Hivi sasa, nchi chache zinatawala uzalishaji wa madini muhimu kwenye ardhi. Australia ni mzalishaji mkuu wa lithium, wakati Chile ni mzalishaji mkuu wa shaba. Uchina huzalisha zaidi graphite na mawe adimu (yanayotumika katika simu na kompyuta).

Lakini kuna wasiwasi wa kijiografia juu ya kutawala kwa Uchina katika usindikaji wa madini haya kabla ya kuingia kwenye mkondo wa usambazaji.

Uchina - ambayo imeboresha teknolojia na utaalam wa usindikaji kwa miongo kadhaa - kwa sasa inadhibiti asilimi 100 ya usambazaji uliosafishwa wa graphite asilia na dysprosium, kwa asilimia 70 ya cobalti na karibu asilimi 60 ya lithium na manganese iliyochakatwa, kulingana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati Mbadala.

Zaidi ya hayo, Beijing imepiga marufuku usafirishaji wa baadhi ya teknolojia zake za usindikaji.

Ili kukabiliana na China Marekani na nchi kadhaa za magharibi zilizindua Ushirikiano wa Usalama wa Madini - ili kuchochea "uwekezaji katika minyororo muhimu ya usambazaji wa madini" mwaka 2022. India sasa ni mwanachama.

India pia imetia saini makubaliano na Urusi kuendeleza teknolojia ya uchimbaji madini kwenye kina kirefu cha bahari.

Pia uanaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi