Watoto wa Gaza wanaotafuta chakula ili kuokoa maisha ya familia zao

Na Fergal Keane

BBC News, Jerusalem

Katika maeneo fulani kwa nyakati fulani, kusalia tu hai ni jambo la kujivunia kwa mvulana - Kando na kwenda nje kila siku kutafuta chakula kinachozuia familia yako isife njaa.

Kila asubuhi, Mohammed Zo'rab, 11, hutoka nje katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah kwa misheni.

Anachukua bakuli kubwa la plastiki na kuelekea shule ambazo zimekuwa vituo vya wakimbizi, na kwenye kambi za muda kando ya barabara ambapo watu wanateseka kama familia yake lakini bado wanaweza kupata kitu cha kulisha mtoto wa wageni.

Mohammed pia huenda kwenye hospitali ambapo majeruhi hufika saa zote, na popote pengine ambapo kunaweza kuwa na sufuria inayochemka kwenye moto wa wazi.

"Ninaporudi kwa familia yangu na chakula hiki, wanafurahi na tunakula wote pamoja," anasema.

"Wakati mwingine mimi hurudi nyumbani mikono mitupu na nina huzuni."

Mohammed ndiye mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne na anaishi na mama yake, baba yake na ndugu zake katika makaziduni yaliyotengenezwa kwa plastiki na vyandarua .

Baba yake, Khaled, anazunguka zunguka Rafah akitafuta kazi za vibarua ili kuchangisha shekeli tano (kama dola 1.38; £1.08) kununua nepi kwa ajili ya binti yao wa miezi miwili, Howaida.

Mohammed ni mmoja wa maelfu ya watoto ambao wamekuwa watafutaji wa chakula kwa familia zao.

"Wakati foleni imejaa na kuna karibu watu 100 mbele yangu, mimi hupita kati kati ya watu," anasema, akijivunia ustadi wake wa kukwepa umati mkubwa bila kupigana.

Akiwa amerudi nyumbani, anakabidhi bakuli la maharagwe yaliyookwa kwa mama yake, Samar, ambaye anawagawia watoto wengine chakula hicho. Yeye dhaifu na hata hali.

"Nina saratani kwenye mifupa yangu," anafichua. "Nina umri wa miaka 31 lakini unaponiona unafikiri nina miaka 60. Siwezi kutembea.

"Nikitembea, ninachoka sana. Mwili wangu wote unauma na ninahitaji matibabu na lishe."

Kama wengine wengi, Samar na familia yake walifika Rafah kutoka nyumbani kwao kaskazini zaidi huko Khan Younis kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) liliwaambia kuwa itakuwa salama. Hiyo ilikuwa miezi mitatu iliyopita.

Tangu wakati huo, vita vimekaribia kwa kasi karibu na Rafah. Zaidi ya watu 70 waliuawa chini ya wiki mbili zilizopita wakati Israel ilipoanzisha msako kuwaokoa mateka wawili waliokuwa wakishikiliwa na Hamas.

Makazi ya familia ya Zo'rabu yanavuja na sakafu kujaa maji ya mvua. Wakati mwingine, mtoto Howaida hana nepi safi.

Kila siku ni ya mahaingaiko katika mahali ambapo watu milioni 1.5 - mara tano ya idadi ya watu wa kawaida - wamejaa karibu na mpaka wa Misri.

Huku 85% ya wakazi wa Gaza sasa wakiyahama makazi yao, kiasi cha misaada inayoingia katika eneo hilo hakiko karibu na kile kinachohitajika.

Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN), lori mia tano za msaada kwa siku zinahitajika. Wastani wa kila siku umekuwa lori tisini.

Hali kaskazini mwa Gaza ni mbaya sana.

Israel inasema Umoja wa Mataifa unashindwa kusambaza misaada kaskazini na kwamba misaada imerundikana - ikisubiri kuchukuliwa katika upande wa mpaka wa Gaza.

Shirika hilo limesitisha usafirishaji wa msaada wa chakula kaskazini mwa Gaza kwa sababu linasema hakuna ulinzi kwa madereva wa malori, ambao wamekabiliwa na mashambulizi ya magenge ya wahalifu na uporaji wa watu waliokata tamaa.

Lori moja lilipigwa na makombora, ambayo Umoja wa Mataifa inasema ilitoka kwa meli ya wanamaji wa Israel.

Aidha, jeshi la polisi linaloongozwa na Hamas huko Gaza haliko tayari tena kusindikiza malori ya chakula kwa sababu wanahofia kupigwa risasi na IDF.

'Turudishieni watu wetu'

Nchini Israeli, mwenendo wa kijeshi wa vita bado unaungwa mkono na wengi.

Hakuna maoni yoyote yanayoweza kutambulika ambayo yanaunga mkono kuongeza juhudi za misaada kwa raia huko Gaza. Katika kura moja ya hivi majuzi ya maoni 68% ya Wayahudi waliohojiwa walisema walipinga kuhamishwa kwa misaada ya kibinadamu hadi Gaza wakati Hamas bado inashikilia mateka wa Israeli.

Kinyume chake Waisraeli Waarabu waliohojiwa walikuwa 85% waliounga mkono misaada kwa watu wa Gaza.

Zvika Mor, ambaye mwanawe mkubwa, Eitan, ni mateka huko Gaza, anazungumzia mvulana ambaye alikuwa "mtu wa kwanza kuniita Daddy" na jinsi yeye, mke wake na watoto wao wengine saba wanamkosa kijana wao aliyetekwa nyara na Hamas. tarehe 7 Oktoba.

Eitan alikuwa akifanya kazi kama mlinzi katika tamasha la muziki la Nova, ambapo Hamas iliua takriban watu 360 ndani na karibu na eneo hilo.

Bw Mor anaongoza kikundi kidogo cha familia za mateka ambazo zinataka wapendwa wao warudishwe kabla ya mazungumzo yoyote na Hamas. Wanapinga serikali kufanya makubaliano ambayo yataweka masharti haya ya kusitisha mapigano, kuongezeka kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina.

"Israel inaunda [mzozo] wa kibinadamu huko Gaza. Kwa sababu lengo letu ni kuwaachilia watu wetu," Bw Mor anasema.

"Tunataka watu wetu, sawa? Na kwanza kabisa, kabla ya mazungumzo yote na mambo mengine, tupe watu wetu."

Alipoulizwa ikiwa hii haikuwana ukatili ikizingatiwa kwamba ni maisha ya raia wa Gaza ambayo yalikuwa hatarini, Bw Mor anajibu: "Ndiyo, lakini tuna watoto wachanga na wanawake na, na wazee, sawa?

"Ni jambo rahisi sana. Tupeni watu wetu na tutawapa chakula na dawa. Ni jambo rahisi sana."

Huko Gaza, mashirika ya kutoa misaada yanatumia chakula kilichosalia kutoa msaada.

Mahmoud Al-Quishawi wa shirika la uhisani la Pious Projects of America lenye makao yake makuu nchini Marekani alikuwa amesimama karibu na sufuria za maharagwe zinazochemka ambapo Mohammed alipokea chakula kwa ajili ya familia yake.

"Tunajaribu bila kuchoka kila siku kutoa usaidizi kwa watu hawa… kuwaambia 'tuko pamoja nanyi, hatutawaacha msimame peke yenu'," asema Bw Al-Quishawi.

Shirika hilo la misaada limeishiwa na gesi ya chupa ili kupasha moto chakula kwa hivyo watu wa kujitolea wanakusanya kuni na kuwasha moto.

"Hali sio nzuri," anasema. "Hali ni kama janga."

Kaskazini mwa Gaza, kumekuwa na ripoti za watoto kufariki kutokana na utapiamlo. Shirika la misaada la Uingereza Action Aid lilimnukuu daktari mmoja kaskazini mwa Gaza akisema kuwa idadi kubwa ya watoto wamefariki.

Katika rekodi ya video, Dk Hussam Abu Safiya - mkuu wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Kamal Adwan - alisema utapiamlo umeenea, pamoja na maambukizo ya mfumo wa usagaji chakula.

Kulingana na Action Aid, mtoto mmoja kati ya sita walio na umri wa chini ya miaka miwili "ambao walichunguzwa katika makazi ya IDP [wakimbizi wa ndani] na vituo vya afya mwezi Januari walipatikana kuwa na utapiamlo".

Hilo, linasema shirika la kutoa misaada, linawakilisha "kupungua kwa hali ya lishe ya idadi ya watu ambayo haijawahi kutokea ulimwenguni kote katika miezi mitatu."

Daktari mwingine katika Al-Shifa Medical Complex, pia kaskazini mwa Gaza, alisema alimtibu mvulana wa miezi miwili aitwaye Mahmoud Fatouh, ambaye alifariki mara baada ya kuwasili hospitalini.

"Mtoto huyu hakuweza kupewa maziwa. Mama yake hakupewa chakula ili kuweza kumnyonyesha," anasema Dk Amjad Aliwa.

"Alikuwa na dalili za upungufu mkubwa wa maji mwilini, na alikuwa akivuta pumzi zake za mwisho [alipokuja]".

Huko Gaza, raia wamekwama ambapo vita na njaa vimewakumba.

Ripoti ya ziada ya Alice Doyard, Haneen Abdeen, Gidi Kleiman na Stephanie Fried.