Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwandishi wa BBC: Jitihada zangu za kuweka familia salama nikiangazia vita vya Gaza
Kwa takriban miezi mitatu, Adnan El-Bursh aliripoti juu ya vita huko Gaza alipokuwa akiishi katika hema, akila mlo mmoja kwa siku, na kujitahidi kuweka mke wake na watoto watano salama. Mwandishi wa BBC Idhaa ya Kiarabu anasimulia nyakati za taabu alizokabiliana nazo akizungumzia vita vilivyomuathiri.
Onyo: Ripoti hii ina maelezo na picha ambazo huenda zikawahuzunisha baadhi ya wasomaji
Moja ya wakati mbaya zaidi wa miezi sita iliyopita ilikuwa usiku ambao sote tulilala mitaani. Nilitazama nyuso za mke wangu na watoto wangu, nikiwa nimejikunyata kwenye baridi kali huko Khan Younis kusini mwa Gaza, na kujihisi nikiwa mnyonge.
Pacha wangu wa umri wa miaka 19, Zakia na Batoul, walilala kwenye lami pamoja na binti yangu, Yumna, mwenye umri wa miaka 14, mwanangu Mohamed, mwenye umri wa miaka minane na msichana wangu mdogo, Razan, mwenye umri wa miaka mitano, pamoja na mama yao, Zaynab.
Tulipojaribu kupumzika nje ya makao makuu ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina, milio ya makombora ilirindima usiku kucha na ndege zisizo na rubani zilisikika angani.
Tulifanikiwa kupata nyumba ya kukodi, lakini mwenye nyumba alikuwa amepiga simu mapema siku hiyo, akisema jeshi la Israel lilikuwa limeonya kwamba jengo hilo lingepigwa kwa bomu. Nilikuwa nikifanya kazi wakati huo, lakini familia yangu ilichukua virago na kukimbia.
Tulikutana tena kwenye makao makuu ya Hilali Nyekundu, ambayo tayari yalikuwa yamefurika watu waliokimbia makazi yao.
Mimi na kaka yangu tuliketi kwenye masanduku usiku kucha, tukijadiliana tunapaswa kufanya nini.
Tulikuwa tumekimbia makazi yetu katika mji wa Jabalia siku chache zilizopita, tarehe 13 Oktoba, tukiacha nyuma mali zetu, baada ya jeshi la Israel kuamuru kila mtu kaskazini mwa Gaza kuhamia kusini kwa usalama.
Na sasa tulikuwa tumetoroka shambulio la bomu katika eneo tuliloambiwa tuhamie. Ilikuwa hali ngumu. Nilihisi hasira, unyonge na kusikitika kwamba sikuweza kutoa ulinzi wowote kwa familia yangu.
Hatimaye, familia yangu ilihamia kwenye orofa huko Nuseirat katikati mwa Gaza, huku mimi nikiishi na timu ya BBC kwenye hema katika hospitali ya Nasser huko Khan Younis. Niliwatembelea kila siku chache.
Mawasiliano yalikuwa magumu, na mtandao na mawimbi ya simu wakati mwingine hukatwa. Kuna kipindi sikuweza kuwasiliana na familia yangu kwa siku nne au tano.
Mji Khan Younis, timu ya BBC - watu saba - tuliishi kwa mlo mmoja kwa siku. Hata chakula kilipokuwa, nyakati zingine hatukukila kwa sababu ya changamoto ya kupata mahali pa kujisaidia.
Wakati huu rafiki yangu, mkuu wa ofisi ya Al Jazeera Wael Al-Dahdouh, alikumbwa na msiba mkubwa .
Nyumba ambayo familia yake ilikuwa inaishi ililengwa katika shambulio la anga la Israel. Mke wake, kijana wa kiume, binti yake wa miaka saba na mjukuu wa mwaka mmoja waliuawa.
Jeshi la Israel linasema inachukua "tahadhari zinazowezekana" ili kupunguza vifo vya raia, na katika tukio hili "imeshambulia miundombinu ya kigaidi ya Hamas katika eneo hilo".
Nilitazama picha za rafiki yangu, ambaye nimemfahamu kwa miaka 20, akikumbatia miili ya watoto wake iliyofunikwa kwa sanda katikati mwa Gaza. Nilitamani ningekuwa naye pale kumfariji.
Habari hizo zilijiri huku kukiwa na msururu wa taarifa kuhusu vifo vya marafiki, jamaa na majirani wengine. Moyo wangu uliumia. Sasa nimepoteza takriban watu 200 katika vita.
Siku hiyo nililia hewani, nilipokuwa nikiripoti. Usiku niliamka huku machozi yananidondoka nisijue la kufanya. Picha ya Wael haikuondoka akilini mwangu.
Nimeangazia mizozo huko Gaza kwa miaka 15, lakini vita hivi ni tofauti, kutoka kwa shambulio ambalo halijawahi kutokea lililoianzishwa na Hamas dhidi ya Israel, hadi kiwango cha maafa yaliyotokana na mashambulizi ya kuliza kisasi yaliofanywa na Israel.
Saa 06:15 mnamo tarehe 7 Oktoba niliamshwa na milipuko mikubwa na watoto wangu wakipiga kelele. Nilipanda juu ya paa na kuona makombora yakirushwa kuelekea Israel kutoka Gaza.
Tulipogundua Hamas ilikuwa imevunja uzio ndani ya Israel - katika shambulio lake ambalo lilishuhudia watu wapatao 1,200 wakiuawa na 250 kutekwa nyara - tulijua jibu kutoka kwa Israel lingekuwa kalizaidi kuwahi kushuhudiwa.
Zaidi ya watu 34,000 sasa wameuawa huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas. Hatari ya majeruhi na vifo imekuwa ikiwakodolea macho wakazi kila uchao.