Siri ya kisiwa cha maisha marefu

    • Author, Na Andrew Bomford
    • Nafasi, BBC

Wakazi wa kisiwa kidogo nchini Ugiriki wanaishi kwa wastani wa miaka 10 zaidi ya watu wengine wa Ulaya Magharibi. Kuna siri gani katika kisiwa hiki cha maisha marefu?

Inaweza kuwa hewa safi. Inaweza kuwa mboga safi na maziwa ya mbuzi. Kila sehemu ya kisiwa hiki ni kukavu, hivyo kutembea kunaweza kuchangia kujenga mwili wenye afya. Inaweza hata kuwa mionzi ya asili ya miamba ya mawe ya granite. Lakini Stamatis Moraitis anadhani anajua sababu ya maisha marefu ya watu wa kisiwa hiki.

"Ni kinywaji tunachotengeneza hapa," anasema, akiwa na glasi ya kinywaji juu meza ya jikoni , majira ya asubuhi. "Kinywaji safi, hakuna kilichoongezwa. Vinywaji vya kibiashara vimeongezwa vitu vingine visivyofaa kwa afya. Lakini hiki ni safi na tunakitengeneza wenyewe."

Stamatis alisherehekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 98 - Januari 1. Anasema yeye ni mzee kuliko hati zake zinavyosema, kwamba alizaliwa Januari 1, 1915. Nje ya nyumba yake kuna mizaituni, miti ya matunda, na mizabibu. Hutengeneza takriban lita 700 za juisi ya zabibu kwa mwaka.

"Unakunywa peke yako?" Nikauliza. "Hapana!" Alisema, na kushangazwa na swali. "Ninakunywa na marafiki zangu."

Stamatis hunywa zabibu na kupumzika na marafiki na familia. Yeye ni nembo ya uponyaji hapa. Miaka 45 iliyopita, alipokuwa akiishi Marekani, aligunduliwa na saratani ya mapafu na kuambiwa ana miezi tisa tu ya kuishi.

"Wakati huo ilikuwa ghali sana kufanya mazishi huko," anakumbuka. "Kwa hiyo nikamwambia mke wangu, 'naenda nyumbani kwetu Ikaria walikozikwa wazazi wangu.'

Ni hadithi ambayo ameisimulia mara nyingi, na hajachoka kuisimulia. "Niliwakuta marafiki zangu kijijini nilikozaliwa na tukaanza kunywa zabibu. Nikifikiri nitakufa kwa amani."

"Kila siku tulikusanyika, tukanywa pamoja. Muda ulipita na nilihisi nguvu. Miezi tisa ilipita nilihisi afya. Miezi kumi na moja ilipita - nilihisi vizuri. Sasa miaka 45 baadaye, bado niko hai!"

"Miaka michache iliyopita nilirudi Marekani na kujaribu kutafuta madaktari wangu. Lakini sikuweza kuwapata. Wote walikuwa wamekufa."

Kuna hadithi nyingi kama hizi katika kisiwa hiki. Katika miaka ya hivi karibuni wanasayansi na madaktari wamekwenda kwenye kisiwa ambacho si mbali sana na pwani ya Uturuki ili kujua ukweli.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa Chuo Kikuu cha Athens, Dk Christina Chrysohoou, ambaye aliwachunguza watu wa kisiwa hiki, alisema, ‘wanakabiliwa na magonjwa ya saratani na matatizo ya moyo sawa na watu wengine, lakini wanakabiliwa na magonjwa hayo katika sehemu ya mwisho ya maisha yao.’

"Ikaria inatupa fursa ya kujifunza kwa nini watu hawa wanafurahia faida hizi, hatuwezi kuepuka magonjwa haya, lakini wanafanikiwa kudumisha ubora wa maisha yao kwa miaka mingi. Wastani wa umri wa ugonjwa wa moyo ni kati ya miaka 55 hadi 60. Lakini Ikaria hufikia miaka 70."

Pia, kuna utafiti wa vinasaba unaowalinganisha watu wanaoishi kisiwani humo na waliozaliwa kisiwani humo lakini wakahama na hivyo kuishi maisha tofauti na ya watu ambao bado wanaishi Ikaria.

Kukutana na baadhi ya wakazi wakongwe wa kisiwa hiki kutakufanya uvutiwe na maisha yao marefu.

Meza ya chakula imejaa vyakula vya Ikarian. "Ni vitafunio," alisisitiza Voula, mke wa George Kassiotis mwenye umri wa miaka 102, alipotoa kitambulisho chake kinachoonyesha tarehe yake ya kuzaliwa ni 1910 na kusimulia maisha yake ya utotoni.

Kwenye ukuta mmoja kuna picha yake akiwa katika kikosi cha wapanda farasi cha Ugiriki mwaka 1931. Alipigana nchini Italia dhidi ya Albania katika Vita vya Pili vya dunia, kisha akasaidia kujenga barabara ya kwanza ya chuma kisiwani humo kabla ya kustaafu mwaka wa 1970.

"Sili chakula kilichosindikwa, sivuti sigara, sina wasiwasi," George Kasiotis alisema. "Sina wasiwasi na kifo. Najua sote tutakufa."

Kizazi cha vijana hujaribu kushika mila. Tulipata mlo mwingine nyumbani kwa Nikos Karoutsos, mmiliki wa mkahawa mwenye umri wa miaka 50, na tuliona marafiki na familia nyingi wakija kwenye mkahawa huo kwa ajili ya vinywaji na chakula.

"Hatuna vilabu vya usiku wala sehemu za kucheza," alisema, huku watu wakigonganisha glasi zilizojaa maji ya zabibu nyekundu kutoka kwenye chupa kubwa za plastiki. "Mlango uko wazi kila wakati, hakuna haja ya kupiga simu na kuuliza ikiwa uingie."

Tukiwa njiani kuelekea nyumbani tulimpita Stamatis Moraitis mwenye umri wa miaka 98, akiwa anapanda ngazi hadi kwenye mzaituni wake mmoja ili kuchuma matunda.

"Nimefurahi bado ninaweza kufanya hivi," alisema huku akicheka. "Ninahisi afya zaidi hapa."