George Weah anahitaji muda zaidi licha ya matatizo ya Liberia
Na Azeezat Olaoluwa & Yūsuf Akínpẹ̀lú
BBC News, Monrovia

Chanzo cha picha, EPA
Nyota wa zamani wa soka kimataifa, George Weah anagombea kuchaguliwa kwa muhula wa pili wa miaka sita kama rais wa Liberia, lakini anaonekana kujifunga goli mwenyewe kwa kushindwa kujihusisha na mada inayotawala mijadala kote mitaani - madai ya kuanzisha mahakama ya uhalifu wa kiuchumi na kivita.
Weah mwenye umri wa miaka 57 aliingia madarakani akiahidi kuunda nafasi za kazi, kubadilisha maisha na kuanzisha mahakama. Lakini baada ya kuchukua wadhifa wa urais mwaka wa 2018 alisema kutazama nyuma juu uhalifu wa zamani haingekuwa njia bora ya kupata maendeleo - jambo ambalo Frederick Tulay mwenye umri wa miaka 24 anahisi ni kosa.
"Kama mpiga kura kwa mara ya kwanza 2017, nilimwamini Rais Weah. Lakini amekataa kushughulikia ufisadi katika sekta ya umma. Vijana wengi wanatumia dawa za kulevya kwa sababu hawana kazi," aliiambia BBC, akisema hatampigia kura Bw Weah na chama chake cha Congress for Democratic Change.

Chanzo cha picha, FREDERICK TULAY
Bw Tulay alipoteza kazi yake katika kiwanda cha kampuni ya ujenzi miaka miwili iliyopita wakati mwajiri wake wa zamani hakuweza tena kumlipa mshahara wake. Sasa anafanya kazi kama dereva wa teksi lakini biashara haishamiri: "Barabara ni mbaya na gesi ni ghali. Ndoto yangu ni kuondoka nchini."
Maoni yake yanaonesha hasira waliyo nayo watu wengi - kwamba miaka 20 baada ya kumalizika kwa vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, ambapo takriban watu 250,000 walikufa, watu wengi bado wanapambana mno kuishi.
Nchi inaendesha mfumo wa sarafu mbili, ikimaanisha kwamba wale wanaolipwa kwa dola za Liberia mara nyingi wanahitaji kulipia chakula kutoka nje au bidhaa nyingine kwa dola za Marekani - na kufanya maisha kuwa ghali. Kashfa mbili za kifedha katika miaka michache iliyopita pia zimewashtua Waliberia, na kusababisha Marekani kuwawekea vikwazo maafisa kadhaa, akiwemo mkuu wa majeshi wa Bw. Weah.
Kwa Sonyah Peterson mwenye umri wa miaka 49, kushindwa kushughulikia majeraha ya siku za nyuma kumesababisha utamaduni huu wa kutokujali.
Mtu aliyenusurika katika mauaji ya kutisha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kanisa moja katika mji mkuu, Monrovia, sasa anatumia muda wake kufanya kampeni dhidi ya wahusika wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na wale waliofaidika kifedha kutokana na vita hivyo, washtakiwe.
Akiwa na umri wa miaka 16 alikimbilia kanisani kwa baba yake, ambaye alikuwa mmoja wa watu wapatao 600 waliouawa na wanajeshi mnamo 1990.
"Askari walipoishiwa risasi, baadhi yao walikwenda kuchukua risasi zaidi hivyo watu wajaribu kutumia fursa hiyo kutoroka lakini askari walianza kuwashambulia kwa mapanga," anakumbuka alipokuwa akionesha kwa vidole matundu ya risasi madirishani katika Kanisa la Kilutheri la St Peter.

Chanzo cha picha, BBC/GIFT UFUOMA
"Wanaamini tukifanya hivyo, siku za usoni tungepata kazi zenye faida kubwa na kuishi maisha bora zaidi kwa sababu wanaona mfano. Sisi sote ni binadamu, watu wanaweza kujaribiwa."
Wagombea wengine 19 wa urais wanashindana na Bw Weah katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumanne wiki ijayo, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais Joseph Boakai, mfanyabiashara Alexander Cummings na wakili wa haki za binadamu, Tiawan Gongloe.
Mojawapo ya mwito mkubwa zaidi wa mahakama unatoka kwa Yekeh Kolubah, mwanajeshi mtoto wa zamani, aliyeajiriwa katika miaka ya 1990 na waasi wa NPLF wa Charles Taylor, na mbunge aliye madarakani kutoka Kaunti ya Montserrado.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anataka washukiwa wote wafikishwe mahakamani - yeye mwenyewe akiwemo.
"Tunaitaka mahakama ya uhalifu wa vita vya kiuchumi... kwa sababu nataka kwenda huko na niweze kujinuasua na tuhuma. Niwajulishe watu makosa niliyofanya na niadhibiwe kwa hilo."
Maarufu sana kwa vijana, mtoto huyo muasi aliyegeuka kuwa mwanasiasa, alitembea kwa kasi, kama mwanajeshi, kuketi kwenye kiti cha plastiki katika kituo chake cha waandishi wa habari kilichowekwa katika eneo maskini la Monrovia kwa mahojiano yetu.
Kama ilivyo kwa Bw Sonyah, anaamini mahakama ingeruhusu Liberia kusonga mbele na kupona: "Ikiwa hatutafanya hivi, hiyo ina maana kwamba bado tunahimiza vita. Sababu tunafanya vurugu ni kwa sababu hatujaadhibiwa.
"Nikienda jela kwa kuwafanyia watu unyama, kuua watu, unadhani nitashika bunduki tena?"
Anakerwa na kile anachosema ni kujaribu kumnyamazisha kuhusu suala hilo kwa kuahidiwa nafasi za juu zenye masilahi makubwa ndani ya kamati za bunge.
Waziri wa Habari, Ledgerhood Rennie aliiambia BBC kuwa rais hatazungumza lolote kuhusu madai hayo, akimtupilia mbali Bw Kolubah kama "mzushi anayejulikana kichaa".
Naibu waziri wa fedha, alidokeza kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu mahakama ya uhalifu wa kivita kimsingi uko mikononi mwa bunge.
“Watu wanapaswa kuwaambia wabunge wao kulifanya suala hilo kuwa muhimu zaidi wakati wa kampeni zao na kuendelea kuwa na nia thabiti kwalo," Samora Wolokolie aliambia BBC.
Bw Rennie alisema inaweza kuwa suala ambalo lazima liende kwenye kura ya maoni.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini kundi la Liberia la Global Justice and Research Project (GJRP), ambalo limekuwa likikusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita, linaamini kuwa serikali haina nia ya kuwezesha chaguo lolote.
Mkurugenzi wake Hassan Bility alisema barua iliyotiwa saini na zaidi ya asilimia 50 ya wabunge, akiwemo Bw. Kolubah, ya kutaka suala hilo kujadiliwa bungeni "ilipotezwa" mara mbili na spika wa Baraza la Wawakilishi.
"Amani ambayo Liberia inafurahia, siamini kuwa ni amani ya kudumu au endelevu kwa sababu hakuna njia za kuzuia," Bw Bility aliiambia BBC.
Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza tangu kuondoka kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliotumwa baada ya kumalizika rasmi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.
Bw Wolokolie anasema Rais Weah lazima apewe sifa kwa kuongoza nchi kupitia Covid-19 na kuunda nafasi za kazi katika sekta ya umma.
Wafuasi wake pia wanampongeza kwa ujenzi wa barabara ambao umefanyika nchini kote kwa miaka sita iliyopita - aliwahi kusema yeye ndiye dawa inayohitajika kutibu barabara mbovu, na kujipatia jina la utani la "Bad Road Medicine" yaani “Dawa ya Barabara Mbovu”.
Mwanasoka bora huyo wa zamani wa Fifa wa mwaka bado anaweza kuvutia umati mkubwa wa watu kwenye mikutano yake. Ana ubora wa nyota hiyo, na mashabiki wengi katika mji mkuu.

Chanzo cha picha, MOSES GARZEAWU
Wleh Potee, mfuasi wa rais ambaye anauza saa za mikono na miwani katikati mwa Monrovia, anabainisha kuwa mdororo wa kiuchumi si maalum kwa Libeŕia. Na ingawa mauzo yake yamepungua sana, anasema yeye na wafanyabiashara wengine wanamfurahia rais.
"Hapo awali, polisi walikuwa wakikamata bidhaa zetu na tulitumia fedha nyingi na muda mwingi kuzirejesha. Lakini chini ya utawala huu polisi hawatusumbui tena. Kwa hiyo kwa fedha kidogo tunazopata tunakuwa hatuna wasiwasi."
Na kuna kukiri kwamba kwa ujumla kumekuwa na uhuru zaidi wa kujieleza chini ya serikali ya Weah, ingawa Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari kadhaa kuelekea uchaguzi.
Lakini mchuuzi huyo mwenye umri wa miaka 46, ambaye ni mhasibu kitaaluma, pia anaunga mkono kuanzishwa kwa mahakama, akisema angekuwa na udaktari kufikia sasa kama isingekuwa athari za vita: "Wacha walete mahakama kushughulikia kila kitu".
Bw Sonyah anatumai kwamba yeyote atakayepigiwa kura kuwa rais, atasikiliza matakwa ya wananchi na wabunge na kuunga mkono msukumo wa uhalifu wa siku za nyuma kushughulikiwa kisheria ili kuhakikisha mustakabali mwema, usio na ufisadi kwa Liberia.
“Amani bila haki ni sawa na chai bila sukari,” anasema.















