Mtoto mchanga aokolewa kutoka kwa vifusi vya jengo lililoporomoka Syria
Mtoto mchanga wa kike ameokolewa na waokoaji kutoka chini ya vifusi vya jengo kaskazini-magharibi mwa Syria ambalo liliharibiwa na tetemeko la ardhi siku ya Jumatatu.
Mama yake alipata uchungu punde tu baada ya janga hilo kutokea na akafanikiwa kujifungua kabla ya kufariki muda mfupi baadaye, ndugu zake wanasema.
Baba yake, ndugu zake wanne na shangazi pia walikufa kwenye janga hilo.
Video za kusisimua zilionyesha mwanamume mmoja akiwa amembeba mtoto huyo mchanga, akiwa ametapakaa vumbi, baada ya kuvutwa kutoka kwenye vifusi huko Jindayris.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Daktari katika hospitali iliyo karibu na Afrin alisema kuwa sasa kichanga hicho kiko katika hali nzuri. Jengo ambalo familia yake iliishi lilikuwa mojawapo ya takriban majengo 50 yaliyoripotiwa kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.8 huko Jindayris, mji unaoshikiliwa na upinzani katika mkoa wa Idlib ambao uko karibu na mpaka wa Uturuki.
Mjomba wa mtoto huyo, Khalil al-Suwadi, alisemakama ndugu walikimbilia eneo la tukio walipopata taarifa ya kuanguka kwa jengo walilokuwa familia ya kichanga hicho.
"Tulisikia sauti tulipokuwa tukichimba," aliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumanne.
"Tuliondoa vifusi na kumkuta mtoto akiwa na kitovu kinaning'nia [akiwa mzima], hivyo tukakikata na binamu yangu akampeleka hospitali."
Daktari wa watoto Hani Maarouf alisema mtoto huyo alifikishwa hospitalini kwake akiwa katika hali mbaya, akiwa na "michubuko na majeraha kadhaa mwilini mwake".
"Pia alifika akiwa na hypothermia kwa sababu ya baridi kali. Ilibidi tumpatie joto na kumpa kalsiamu," aliongeza.
Alipigwa picha akiwa amelala kwenye incubator au chupa maalumu ya joto akipewa dripu, wakati mazishi ya pamoja yalifanyika kwa mama yake Afraa, baba Abdullah na ndugu zake wanne.
Wao ni miongoni mwa watu 5000 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na tetemeko lililokumba Sysra na Uturuki.













