Kisiwa cha Marekani kisicho na magari, ni baiskeli na farasi tu

Muda wa kusoma: Dakika 3

Katikati ya eneo linalojulikana kama "mji mkuu wa magari duniani", kuna kisiwa ambacho hakiruhusu gari hata moja. Hakuna honi, hakuna misururu ya magari, wala moshi wa injini. Badala yake, kuna sauti ya kwato za farasi, baiskeli zinazopita taratibu na upepo laini unaovuma kutoka Ziwa Huron.

Hiki ni Kisiwa cha Mackinac, kilichopo kaskazini mwa jimbo la Michigan nchini Marekani. Ni kisiwa kidogo chenye wakazi wapatao 600, farasi takribani 600, na mtindo wa maisha unaoonekana kana kwamba ni wa kurithi kutoka karne iliyopita.

Michigan ni eneo ambalo majina makubwa ya magari kama Ford, General Motors na Chrysler yanapotengenezwa, jambo linalolifanya litambulike kimataifa kama kitovu cha tasnia ya magari. Lakini dakika 20 tu kwa feri kutoka bara, kisiwa cha Mackinac Island kimechagua njia tofauti kabisa.

Kwa zaidi ya miaka 100, kisiwa hiki kimeishi bila magari, kikiendeleza utamaduni wa utulivu, subira na mwendo wa polepole, sifa ambazo leo zimekifanya kuwa kivutio cha kipekee kwa wasafiri kutoka duniani kote.

Kwa nini Mackinac haina magari?

Simulizi ya kukosekana kwa magari kwenye kisiwa cha Mackinac inaanzia mwishoni mwa karne ya 19, wakati magari yalipoanza kuonekana Marekani. Kwa mujibu wa simulizi za wenyeji, mwaka 1898 gari moja lililipuka kwa kishindo, lilisababisha farasi waliokuwa karibu kuogopa sana.

Tukio hilo liliwaacha viongozi wa kijiji wakiwa na hofu kubwa. Farasi walikuwa ndiyo njia kuu ya usafiri na uti wa mgongo wa uchumi wa kisiwa. Hivyo, mamlaka zilichukua uamuzi wa kupiga marufuku magari ndani ya kijiji.

Miaka miwili baadaye, marufuku hiyo ilipanuliwa na kutumika kwa kisiwa chote. Tangu wakati huo, hakuna gari la injini lililoruhusiwa kuingia na hata leo, marufuku hiyo bado ipo.

"Farasi ndiye mfalme hapa," anasema Urvana Tracey Morse, mfanyabiashara ambaye ameishi kisiwani kwa miongo kadhaa. Kauli hiyo imekuwa kama falsafa ya maisha ya kisiwani Mackinac.

Kisiwa kinachoendeshwa na farasi

Zaidi ya karne moja baadaye, farasi bado ni moyo wa maisha ya kila siku ya wananchi wa kisiwa cha Mackinac. Wakati wa majira ya kiangazi, farasi wapatao 600 hutumika katika shughuli mbalimbali, kuanzia kusafirisha watalii hadi kazi nzito za usafi.

Taka hukusanywa kwa magari ya farasi, mizigo huwasili kwa magari ya kukokotwa, na hata vifurushi vya kampuni kubwa kama FedEx husafirishwa kwa njia hiyo hiyo ya jadi.

Kila mwaka, zaidi ya watalii milioni 1.2 hufika kisiwani humo wakati wa kiangazi. Hata hivyo, kadiri msimu wa vuli unavyokaribia, farasi wapatao 300 huanza kurejeshwa bara, ishara ya mwisho wa msimu wa watalii.

Farasi wachache hubaki kisiwani wakati wa baridi kali ili kuendelea kutoa huduma muhimu, wakati feri zinapokatishwa mara kwa mara kutokana na barafu katika Ziwa Huron

Kabla ya watalii, kabla ya magari

Kisiwa cha Mackinac kilikuwa na umuhimu mkubwa muda mrefu kabla ya kuwasili kwa watalii au wageni kutoka Ulaya. Kwa mamia ya miaka, jamii za asili za Anishinaabe zilitumia eneo hili kama kituo cha uvuvi, uwindaji na biashara.

Walikiita Michilimackinac, likimaanisha "mahali pa kasa mkubwa", kutokana na mwonekano wa miamba na misitu yake, iliyofanana na kasa akichomoza majini.

Ngome ya kijeshi iliyojengwa na Waingereza mwaka 1780 bado ipo hadi leo, ikiwa ni ushahidi wa historia ndefu ya kijeshi ya kisiwa. Wageni wanaweza kushuhudia maonesho ya mizinga na watendaji waliovalia mavazi ya kihistoria.

Zaidi ya hayo, maeneo ya mazishi ya watu wa asili yenye umri wa hadi miaka 3,000 yamegunduliwa kisiwani, yakikifanya kuwa mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi katika ukanda wa maziwa makuu.

Maisha bila magari yanawezekana?

Asilimia 80 ya kisiwa cha Mackinac ni hifadhi ya taifa, yenye misitu ya kale, miamba ya chokaa na mandhari yanayovutia. Wageni hutembea kwa miguu, kuendesha baiskeli au kupanda magari ya farasi kufikia vivutio kama Arch Rock.

Zaidi ya baiskeli 1,500 hukodishwa kisiwani, na kwa wengi, baiskeli ndizo njia rahisi na ya haraka zaidi ya usafiri. Barabara kuu inayozunguka kisiwa imegeuzwa kuwa njia ya baiskeli na matembezi.

Kwa wakazi kama Morse, kuishi bila magari ni sababu kuu ya kuchagua kubaki kisiwani mwaka mzima, licha ya baridi kali ya majira ya baridi.

"Unaposhuka kutoka kwenye mashua na kusikia sauti ya kwato, unahisi kama umerudi nyuma kwa wakati," anasema Hunter Hoaglund. "Bila farasi, mahali hapa pasingekuwa palivyo."