Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Umuhimu wa Putin kwa Trump: Mkakati wa kuitenga China?
Rais wa Marekani Donald Trump anatafuta kuimarisha uhusiano na kufikia ukaribu zaidi na Urusi, jambo ambalo linaweza kubadilisha mkondo wa sera za nje za Marekani kwa miongo kadhaa.
Trump ameungana na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya Ukraine, alimshinikiza Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kukubali masharti magumu yaliyowekwa na Urusi, ambayo iliivamia nchi yake, na kuwaambia washirika wa Ulaya wasitegemee kuendelea kuungwa mkono na Marekani.
Hatua hizi zote zinatuma ujumbe wa kumuunga mkono Putin, na hivyo kuzua maswali kuhusu iwapo Marekani inaelekea kwenye mkakati mpya wa kidiplomasia, na iwapo kuna mpango wa mkakati mkubwa zaidi unaolenga kujaribu kuivuta Urusi mbali na China? Au je, tabia ya Trump inatokana tu na hisia binafsi na uhusiano wa karibu na Putin?
Je, utawala wa Trump umeegemea upande wa Urusi?
Dalili za kwanza za mabadiliko makubwa ya Marekani kuelekea Urusi zilionekana Februari 12, wakati Trump alipopigiwa simu na Putin na kufanya naye mazungumzo kwa dakika 90.
Baadaye Trump aliweka shinikizo kwa Rais wa Ukraine Zelensky kukubaliana na makubaliano ya amani, akitaka akabidhi ardhi kwa Urusi bila kutoa hakikisho la usalama kutoka upande wa Marekani.
"Tulikubali ushirikiano wa karibu sana, ikiwa ni pamoja na kufanya ziara kati ya nchi zetu mbili," Trump alisema kuhusu mazungumzo yake ya simu na Putin.
Trump pia alitangaza kwamba Ukraine haitapata uanachama wa NATO baada ya vita kumalizika, ahadi iliyotolewa na mtangulizi wake, Joe Biden, ambayo Urusi iliipinga vikali.
Trump kisha alimwita Rais wa Ukraine Zelensky "hafai" na "dikteta," na akamwambia wakati wa mkutano wao wa White House kwamba Ukraine "haipaswi kuanzisha" vita, maoni sawa na yale yaliyotolewa hapo awali na Putin.
Trump amejizuia kutoa msaada wowote wa Marekani kwa vikosi vya Ulaya, ikiwa vitaendelea na mpango wa kulinda amani nchini Ukraine baada ya kumalizika kwa mzozo huo, na kwa upande wake, Urusi imekataa kabisa wazo la kuwepo kwa vikosi vya Magharibi kwenye ardhi ya Ukraine.
Marekani pia iliunga mkono Urusi katika kura katika Umoja wa Mataifa kuadhimisha mwaka wa tatu tangu kuzuka kwa vita nchini Ukraine, na ilijiepusha na kuilaani Urusi kwa uvamizi wake katika ardhi ya Ukraine.
Je, Marekani inafanya juhudi kupata kibali cha Urusi ili kuitenga na China?
Hatua hizi za kuiunga mkono Urusi na kujitenga na washirika wa Ulaya zinaonyesha mabadiliko makubwa katika sera ya mambo ya nje ya Marekani katika kipindi cha miaka 80 iliyopita, ingawa bado haijafahamika iwapo juhudi hizi zinaashiria mkakati mpya wa sera ya kigeni ya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alikiambia chombo cha habari cha kihafidhina Breitbart mnamo Februari 25 kwamba Trump na utawala wake wanataka kuudhoofisha uhusiano wa Urusi na China.
Alisema: "Ninaamini kwamba Urusi itabaki katika nafasi ya mshirika wa pili kwa China, na kulazimishwa kutekeleza chochote China inachosema kwasababu ya kuitegemea, sio matokeo mazuri kwa Urusi, wala kwa Marekani, wala kwa Ulaya, na hata kwa ulimwengu wote."
Alibaisnisha kuwa hali hii itakuwa hatari kwa Marekani, kwasababu "ni inahusu mataifa mawili ya nyuklia yanayoshirikiana dhidi ya Marekani."
Rubio aliongeza kuwa Marekani inakusudia kukabiliana na mtandao wa biashara wa kimataifa wa China, unaojulikana kama "Belt and Road Initiative''
China ilijibu vikali matamshi hayo ya Rubio, huku msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian akisema: "Jaribio la Marekani la kuzusha mafarakano kati ya China na Russia linaelekea kushindwa. China na Russia zina mikakati ya maendeleo ya muda mrefu na sera thabiti za kigeni."
Mkakati huo wa Rubio unaolenga kuitenga Urusi na China ili kuihujumu, unaweza kuonekana kama kioo cha mafanikio ya awali ya kidiplomasia wakati wa enzi za Rais wa Marekani Richard Nixon, alipofanikiwa kuitenganisha China na Muungano wa Usovieti.
Kwa uzoefu wa Nixon, Marekani ilianzisha uhusiano wa karibu na China, ambao ulisababisha kutengwa kwa Urusi katika kesi ya Trump, ukaribu wake na Urusi unaweza kusababisha kutengwa kwa China. Waangalizi wameelezea mkakati huu kama "Kinyume cha mpango Nixon " au " Kinyume cha mpango wa Kissinger ."
Nixon alikuwa amekamilisha mkataba na China mwaka wa 1972, kwa maelekezo ya mshauri wake wa usalama wa kitaifa wa wakati huo, Henry Kissinger, kumaliza miongo kadhaa ya muungano kati ya China na Muungano wa Usovieti - wakati huo mataifa ya kikomunisti - katika uadui wao wa pamoja dhidi ya Marekani.
Baraza la washauri la Marekani mahusiano ya kigeni lilisema kuhusu mpango wa Rubio: "Watunga sera mashuhuri zaidi wa China katika Ikulu ya White House wanaonekana kuamini kuwa wanaweza kufanya kazi na Urusi kuitenga China na ulimwengu na kuzuia ushawishi wake unaokua duniani."
Klaus Weil, profesa katika taasisi ya uchumi ya London, alieleza kwamba Marekani "haitaki Urusi iwe koloni la kuipatia China malighafi, kwani hiyo ina maana kwamba Urusi inauza rasilimali zake kwa China kwa bei ya chini, jambo ambalo linaipa China faida zaidi ya Marekani."
Je, mpango wa "Reverse Kissinger Plan" utafanikiwa?
Huenda ikawa vigumu kwa Marekani kujaribu kuitenganisha Urusi na China.
Nchi hizo mbili zilitangaza urafiki wa "bila kikomo" siku kadhaa kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo 2022, na uhusiano wa kibiashara kati yao umeimarika tangu wakati huo.
Uchina ndio muagizaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi ya Urusi, na uagizaji wa takriban dola bilioni 62 mnamo 2024, kutoka theluthi mbili tu ya kiasi hicho mnamo 2021. Kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, nchi za Magharibi ziliiwekea vikwazo mafuta ya Urusi, na kuipa China fursa ya kununua mafuta hayo zaidi.
China pia ni muuzaji mkuu wa zana za nhali ya juu za kiufundi kwa Urusi, ikiwa ni pamoja na chipu za kompyuta, kama vile semiconductors (ambazo hutumiwa katika silaha).
Ripoti zilizochapishwa na taasisi za wasomi za Marekani, kama vile Taasisi ya Biashara ya Marekani na Shirika la Carnegie Endowment for International Peace, zinaonyesha kwamba chipu nyingi za kompyuta zinazoagizwa na Urusi zinatoka China.
Profesa Yang Zheng, wa Chuo cha Shanghai cha Utawala wa Kidunia na Mafunzo ya Maeneo, anaamini kwamba uwezekano wa upatanisho kamili kati ya Urusi na Marekani bado ni mdogo, kutokana na "muingiliano wa kutoaminiana kwa kihistoria na tofauti kubwa za kiitikadi" kati yao.
"Urusi itasalia kujitolea kwa uhuru wake na haitapunguzwa kuwa chombo tu cha sera za kigeni za Marekani," aliiambia BBC.
"Nadhani Putin anaweza kujifanya kujibu maasi ya Marekani kwa muda, lakini hatataka kuutoa uhusiano wake na China kwa chochote ambacho Marekani itakitoa," alisema Henrik Wachtmeister wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Uswidi.
"Urusi na China ni washirika wa asili katika suala la rasilimali, lakini uhusiano kati ya Urusi na Marekani ni wa ushindani, hasa katika sekta ya mafuta na gesi," aliongeza.
Je, Trump anaiunga mkono Urusi kwasababu za kibinafsi?
Allen anadokeza kuwa mwelekeo wa Trump kuelekea Urusi na Putin unatokana na mkakati mdogo wa kidiplomasia kuliko sababu "za kibinafsi" zilizoanzia muhula wa kwanza wa Trump, wakati Urusi ilishutumiwa kuingilia kampeni za awali za uchaguzi wa Trump, na Trump na timu yake walishutumiwa kwa kushirikiana nayo.
Wakati wa mkutano wake wa mwisho na Zelensky katika Ikulu ya White House, Trump alisema kumhusu Putin: "Nimemjua kwa muda mrefu ilibidi tupitie uzoefu huu pamoja, ambao unajulikana kama uongo wa Urusi."
"Trump anajiona yeye na Putin kuwa katika mashua moja, waathiriwa wa uwindaji wa maadui," Allen anasema.
"Tunafahamu vyema uhusiano mkubwa kati ya Trump na Urusi, ambao ulionyeshwa na shindano la Miss World (mlimbwende wa Dunia) huko, au kwa msaada wa kifedha wa Urusi ambao ulisaidia miradi ya mali isiyohamishika ya Trump kuendelea," Weil anasema.
Anahitimisha kuwa uhusiano wa Trump na Urusi "siku zote umekuwa mzuri."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi