Olenivka: Je nini kilitokea katika Gereza 120?

Chanzo cha picha, Reuters
Mnamo saa za mapema za tarehe 29 Julai, zaidi ya wafungwa 50 wa kivita wa Ukraine waliuawa katika shambulio dhidi ya Gereza la 120 katika eneo linalokaliwa na Urusi.
Ukraine na Urusi zinalaumiana kuhusu shambulio hilo. Wataalamu wa uchunguzi wanaiambia BBC kwa nini madai Urusi kuhusu matukio hayo hayana msingi.
Onyo:Makala haya yana picha na maelezo ya kutisha.
Matukio ndani ya jengo la magereza yanashtua. Picha za miili iliyoungua iliyolala kati ya mkusanyiko wa vitanda vya chuma. Nje, miili zaidi, iliyowekwa kwenye sakafu.
Takriban wafungwa 50 wa vita vya Ukraine (PoWs) waliuawa na 73 kujeruhiwa katika shambulio lililoshtua taifa na kusababisha maandamano ndani ya Ukraine na nje ya nchi. Mauaji hayo yalifanyika katika eneo lililojitangaza kuwa Jamhuri ya Watu wa Donetsk c (DPR).
Olenivka, kijiji kilichopo karibu, kimekuwa chini ya udhibiti wa waasi wanaoungwa mkono na Urusi tangu vita vilipozuka eneo la mashariki mwa nchi mwaka 2014.
Baada ya kutathmini kwa karibu picha kutoka kwa vyanzo vya Urusi, tulizungumza na wataalam wa silaha na wanasayansi wa mahakama, katika juhudi za kubaini kilichotokea, na kile ambacho hakikufanyika katika Gereza la 120.
Pia tuliwahoji wafungwa saba wa zamani ambao waliachiliwa huru wiki kadhaa kabla ya shambulio hilo kutoka Olenivka na ambao wanatoa picha mbaya ya maisha yalivyokuwa katika majuma kadhaa kabla ya shambulio hilo.
Wizara ya ulinzi ya Urusi haikujibu ombi letu la kupata maoni yake. Gereza hilo, linalojulikana rasmi kama koloni la adhabu la Volnovakha, lilifunguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 1999.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Inatumiwa kuwazuilia maelfu ya wafungwa - kuaanzia raia waliojitolea hadi wapiganaji wa Kiuraine - wote wamekamatwa na vikosi vinavyoungwa mkono na Urusi katika eneo lililojitangaza kuwa Jamhuri Huru ya Watu wa Donetsk (DPR) kusini mwa Ukraine.
Lakini miongoni mwa wafungwa hao kulikuwa na mamia ya wapiganaji kutoka kikosi cha Azov.
Kikosi cha kujitolea kilichoanzishwa mwaka wa 2014 chenye asili ya mrengo wa kulia, kikosi hicho kilirekebishwa baadaye na kujumuishwa katika Walinzi wa Kitaifa wa Ukraine.
Baada ya utetezi wao wa muda mrefu wa kulinda mji wa bandari wa kusini wa Mariupol mapema mwaka huu, uliishia katika mazingira ya baada ya vita na ujenzi wa kiwanda cha chuma cha Azovstal wa jiji hilo, walipata sifa yao kama miongoni mwa wapiganaji shujaa zaidi wa Ukraine.
Kulingana na maafisa wa Ukraine na orodha ya vifo iliyotolewa na Urusi inaonekana wengi wa waliouawa na kujeruhiwa walikuwa kutoka kitengo cha kijeshi cha Azov.
Wakitangaza habari za tukio hilo la Olenivka, jeshi la Urusi liliishutumu Ukraine kwa shambulio hilo, na kusema kuwa lilitekelezwa kupitia mfumo wa roketi za usahihi uliotolewa na Marekani unaojulikana kama Himars.
"Majukumu yote ya kisiasa, jinai na kimaadili kwa mauaji dhidi ya Waukraine yanabebwa na Zelensky [rais wa Ukraine], utawala wake wa uhalifu na Washington, ambayo inawaunga mkono," alitangaza msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Luteni Jenerali Igor Konashenkov kupitia televisheni ya serikali.

Maafisa wa Urusi walionyesha vipande vya roketi za Himars, zinazodaiwa kupatikana kwenye eneo la tukio.
Denis Pushilin, Kiongozi wa eneo la DPR linalotakaka kujitenga na ambaye anayeunga mkono Urusi, alidai kuwa majeshi ya Ukraine iliwaua askari wake wenyewe ili kuficha ushahidi wa uhalifu wa kivita. Hususan, mashambulio dhidi ya raia, ambayo Pushilin alidai, yaliamrishwa na Zelensky mwenyewe.
"Ushahidi uliotolewa wafungwa ulikuwa ushahidi kamili," Pushilin aliiambia Televisheni ya Urusi. "Kyiv aliamua kuiharibu."
Picha ya satelaiti iliyopigwa siku moja baada ya mlipuko huo inaonyesha jengo moja lililoharibiwa vibaya na mlipuko huo.
Wafungwa wa zamani wa gereza hilo wanasema jengo hili lilikuwa katika eneo la viwanda mbali na kambi kuu walimokuwa wakiishi.
BBC iliwasiliana na wataalamu kadhaa wa silaha na kuchunguza ushahidi uliopo - picha za satelaiti na video ya jengo lililolengwa - ili kuchunguza madai ya Urusi kwamba Ukraine ililenga kambi hiyo kwa makombora ya mizinga. Matokeo yao yalikuwa yanalingana kwa kushangaza. "Hakuna njia ambayo uharibifu ulisababishwa na huo [mfumo wa roketi nyingi za kurusha]," anasema Bob Seddon, afisa mkuu wa zamani wa ufundi wa jeshi la Uingereza. Uharibifu unaoonekana kwenye picha, alisema, ulijilimbikizia sana. Kwa vitisho vyote visivyoweza kuelezeka ndani, jengo lenyewe linabaki bila kujeruhiwa. Mfumo wa roketi nyingi za kurusha kama Himars, alisema, ungesababisha uharibifu mkubwa zaidi.
Zaidi ya hayo, ndani ya jengo hilo, miili iliyoonyeshwa kwenye picha iliyotolewa na vyombo vya habari vya Urusi, yote ilikuwa pamoja badala ya kutawanyishwa, anasema Dk Shehan Hettiarchy, daktari bingwa wa upasuaji na mkurugenzi mkuu wa majeraha katika Chuo cha Imperial cha London. Badala yake, inaonekana kama njia fulani ya uchomaji moto ilitumika, anasema mtaalamu mwingine - Dk Saleyha Ahsan, daktari wa Uingereza aliye na uzoefu mkubwa katika maeneo yenye migogoro. Kwa ushahidi mdogo uliopo, Pete Norton, mhadhiri wa teknolojia ya milipuko na usalama katika Chuo cha Ulinzi cha Uingereza huko Shrivenham, anasema "malipo ya vilipuzi, ikiwezekana kuongezwa kwa wingi wa mafuta" iliwekwa ndani ya jengo hilo. Kuhusiana na dhamira ya kutumia kifaa kama hicho, tovuti ya CAT-UXO, ambayo inajishughulisha na uhamasishaji wa vilipuzi, ilisema:
"Kifaa kama hicho kingeweza kutumika kusababisha uharibifu wa moto au kuharibu ushahidi wa mahakama."
Ushahidi mmoja tata ambao hatuuweza kuthibitisha ikiwa ni simu, ambayo inadaiwa kunaswa na idara za kijasusi za Ukraine.
Saa chache baada ya Urusi kuilaumu Ukraine kwa kutekeleza shambulio hilo, raia wa Ukraine walitoa rekodi hiyo kwa umma.
Ndani yake, wasemaji wawili ambao hawakutajwa majina wanajadili jinsi waajiri 200 wa Azov walivyohamishwa kutoka kwenye kambi zao hadi kwenye ghala lililojitenga siku mbili tu kabla ya shambulio hilo.
Mmoja wa watu hao anasema makombora ya Kirusi ya "grad" yalirushwa angani, ili kuficha sauti ya mlipuko ndani ya ghala na kwamba "uwezekano mkubwa zaidi walitega kifaa hicho cha vilipuzi mapema."
Walipoulizwa na BBC kwa maelezo zaidi, mamlaka ya Ukraine ilikataa kutoa maoni.

Bila kufikia eneo la uhalifu, haiwezekani kusema kwa uhakika kile kilichotokea ndani ya ghala usiku huo. Lakini kwa kuchunguza picha kutoka nje ya jengo hilo, kuna ushahidi zaidi wafungwa hao walikuwa wakizuiliwa katika mazingira duni.
Wataalamu wa uharibifu wa vita katika Huduma za Ujasusi za McKenzie wanasema baadhi ya watu kutoka nje ya gereza hilo huenda tayari walikuwa wamefariki kabla ya moto huo.
Kwa tahadhari kwamba uchunguzi wao unatokana na video moja, wanasema baadhi ya miili "inaonekana kuwa dhaifu na iliyonyong'onyea."
"Hali mbaya ya miili inaonyesha kiwango cha utelekezaji katika Gereza la Olenivka," wanasema.
Wachambuzi wa vyanzo huria kutoka SOAR, kampuni ya kuchora ramani ya satelaiti, wanaelekeza kwenye ushahidi mwingine kutoka kabla ya mlipuko huo, unaoonyesha dalili za ardhi iliyovurugwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habaroi maafisa wa Ukraine walisema kuwa picha zilionyesha ushahidi wa makaburi yaliyokuwa yakichimbwa na kwamba gereza hilo lilikuwa likijiandaa kuwazika majeruhi.

Chanzo cha picha, Reuters
Hata hivyo, picha hizi pekee hazitoshi kuthibitisha aina yoyote ya eneo la mazishi au nia yakufanya hivyo. Pia tulizungumza na wafungwa saba wa zamani katka Gereza la 120. Walioachiliwa wiki chache kabla ya mlipuko huo hakuna hata mmoja wao aliyejua ni kwa nini waliachiliwa ghafla pamoja na makumi ya wafungwa wengine.
Wote walielezea msongamano, usafi duni na vitisho vya askari magereza. Wote walisema wiki chache za kwanza zilikuwa ngumu zaidi.
"Ungeweza kusikia wafungwa wakipigwa kila wakati. Wakati huo huo, muziki ulikuwa ukichezwa ili kuficha sauti ya watu wanaopiga kelele kwa maumivu," alisema Konstanyn Velychko, dereva wa kujitolea ambaye alikamatwa akiwasaidia watu kuondoka Mariupol.
Baada ya kuhamishiwa katika kambi ya kawaida, wote walisema hali iliimarika.Lakini wakati wote kulikuwa na hofu ya kuadhibiwa.
"Mkuu wa gereza aliniambia kuwa sisi ni watumwa wake," anasema Ruslan, mhandisi aliyezuiliwa kwa karibu siku 100 kwa kuwasaidia raia wa Ukraine kukimbia mapigano huko Mariupol. Kabla ya Olenivka yeye na wengine BBC ilizungumza nao walisema walizuiliwa katika vituo vingine katika eneo linalojiita DPR na walielezea mazingira hali mbaya waliyokumbana nayo. Chakula kilikuwa rasilimali ya thamani, wanasema wafungwa wa zamani, huku mlo wa wastani ukiwa na nusu glasi ya maji, kipande cha mkate na vijiko vichache vya nafaka. Lakini kati ya wafungwa wote, sema ni wapiganaji wa Azov ambao walikuwa na hali mbaya zaidi. Viktor, afisa wa polisi wa Ukrain, anasimulia akingoja kwenye foleni kuona daktari. Mpiganaji wa Azov mwenye umri wa miaka 20 pia alikuwa kwenye foleni. "Mtu wa Azov alipigwa alipofika. Ilikuwa ni ukatili sana hakuweza kuinuka kutoka kwa magoti yake," anasema Viktor (tulibadilisha jina lake kwa usalama wake).

Chanzo cha picha, Reuters
"Kisha mmoja wa walinzi wa gereza akapaza sauti: "Tazama, wameleta nyama mpya!" Wakamfanya asafishe mfereji wa maji machafu kwa mikono yake mitupu. Mwezi mmoja baadaye, Viktor anakumbuka mamia zaidi ya wapiganaji wa Azov waliofika gerezani. Baada ya kujisalimisha kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichozingirwa mnamo 16 na 17 Mei 2022 askari wengi walihamishwa moja kwa moja hadi Gereza la 120.
Walipofika, waliwekwa katika kambi tofauti, mbali na wafungwa wengine, anasema Viktor. Unyanyasaji wa wafungwa wa Azov haukukoma, wanasema wafungwa wote wa zamani. "Waliwachukia sana," anasema Ruslan. Katika mahojiano yaliyorekodiwa baada ya mlipuko, Ruslan anadai aliwasikia wakipanga mashambulizi hayo. "Nilisikia mara kwa mara jeshi la Urusi na walinzi wa DPR wakijadili ikiwa wanaweza kuweka watu wote wa Azov kwenye kambi moja na kuwarushia makombora."
Siku chache tu baada ya kundi hilo kuwasili, tarehe 18 Mei Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilifika "kutathmini mahitaji ya" PoWs lakini hawakuruhusiwa kuzungumza na wafungwa kwa misingi ya mtu mmoja-mmoja, waliiambia BBC.
Mwezi mmoja baadaye, bila ya kupata idhini ya kufikia jela hilo au miili ya waliouawa, familia za wahasiriwa wanasema hawana imani na majina yaliyotolewa na Urusi.
Ukraine imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuruhusiwa kuingia ili kuchunguza kile Rais Zelensky amekitaja kuwa "uhalifu wa kimakusudi wa kivita." Wakati Shirika la Msalaba Mwekundu linajaribu kwa haraka kuwasaidia waliojeruhiwa katika mlipuko huo.
"Kipaumbele chetu hivi sasa ni kuhakikisha majeruhi wanapata matibabu ya kuokoa maisha na miili ya waliopoteza maisha inashughulikiwa kwa heshima," walisema katika taarifa.












