Utafiti: Kutumia kifaa cha skrini kwa muda mrefu ukiwa kitandani kunahusishwa na usingizi duni

Muda wa kusoma: Dakika 4

Utafiti uligundua kuwa watu wanaotumia muda mwingi kutazama skrini kitandani au wakati wa kulala wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa kulalamika kukosa usingizi au kuwa na ugumu wa kulala.

Utafiti huu unatokana na uchunguzi wa zaidi ya wanafunzi 45,000 nchini Norway.

Utafiti unaonyesha kuwa kila saa ya ziada ya muda wa kutumia kifaa inahusishwa na ongezeko la asilimia 63 ya hatari ya kukosa usingizi na dakika 24 chini ya usingizi.

Walakini, watafiti walisema walipata tu uhusiano kati ya wakati wa kutumia kifaa na usingizi duni na hawakupata kuwa wakati wa kutumia kifaa lazima husababisha usumbufu wa usingizi.

Wataalamu wanasema kwamba kuweka simu yako kabla ya kulala, kufanya kitu cha kupumzika, na kuanzisha utaratibu kunaweza kukusaidia kulala vizuri.

Utafiti huu unatokana na data iliyokusanywa kupitia Utafiti wa Kitaifa wa Wawakilishi wa Wanafunzi wa 2022, ambao uliwachunguza wanafunzi kati ya umri wa miaka 18 na 28.

Watafiti walitaka kuchunguza uhusiano kati ya muda uliotumiwa kutazama skrini kitandani na ubora wa usingizi.

Pia walitaka kutathmini athari za matumizi ya media ya kijamii kwenye usingizi, kinyume na shughuli zingine za skrini.

Dk. Gunhild Janssen-Jytland wa Taasisi ya Afya ya Umma ya Norway, mwandishi mkuu wa utafiti uliochapishwa katika jarida la Frontiers, anasema kwamba aina ya shughuli kwenye simu ya mkononi, kompyuta au kifaa kingine wakati wa usingizi inaonekana kuwa na athari ndogo kuliko muda wa jumla wa kutumia kifaa.

"Hatukupata tofauti kubwa kati ya muda wa kutumia kifaa na matumizi ya mitandao ya kijamii, na kupendekeza kwamba muda wa kutumia kifaa yenyewe ni sababu kubwa ya usumbufu wa usingizi," aliongeza.

Usingizi au mitandao ya kijamii

Katika Utafiti wa Afya na Ustawi wa Norway wa 2022, washiriki waliulizwa ikiwa walitumia kifaa chochote cha kidijiti baada ya kwenda kulala.

Walipewa chaguo la kutazama filamu au kipindi cha televisheni, kuangalia mitandao ya kijamii, kutafuta mtandao, na kucheza michezo ya kidigital.

Kati ya wale ambao walisema walitumia skrini kitandani kabla ya kulala, asilimia 69 walisema waliangalia mitandao ya kijamii.

Washiriki pia waliulizwa ni usiku ngapi kwa wiki walirambaza kwenye mitandao ya kijamii na kwa muda gani, na ni mara ngapi walipata ugumu wa kuamka au kulala, pamoja na uchovu au ugumu wa kuamka mapema asubuhi.

Kw hiyo, wale ambao walisema walipata shida hii usiku mara tatu kwa wiki au usiku mmoja kwa wiki kwa angalau miezi mitatu walitambuliwa kuwa wanasumbuliwa na ukosefu wa usingizi.

Ingawa utafiti huu ulipata uhusiano kati ya kutazama skrini wakati wa kulala na usumbufu wa usingizi au kukosa usingizi, watafiti wanasema hii haimaanishi kuwa ndio sababu.

Dk Jetland anasema: "Utafiti huu hauwezi kubainisha sababu - kwa mfano, ikiwa wakati wa kutumia kifaa husababisha kukosa usingizi au ikiwa wanafunzi walio na usingizi hutumia muda mwingi kutazama skrini.

Pia anabainisha kuwa utegemezi mkubwa wa utafiti juu ya data ya uchunguzi kuhusu uzoefu wa kibinafsi unaweza kumaanisha kuwa ni ya upendeleo na matokeo yake hayapaswi kuzingatiwa kuwa ya uwakilishi wa ulimwengu.

Joshua Piper, mtaalamu wa usingizi katika kampuni ya afya ya Uingereza ya ResMed, alisema utafiti huo ulipata "ushahidi muhimu na unaokua" wa athari mbaya za kutumia vifaa vya kielektroniki katika usingizi.

Aliiambia BBC: "Inakuibia kiwango na ubora wa usingizi wako, na hii inaweza kuwa ni kwanini watu wengine wanapata shida kupata usingizi na wengine wana shida kulala."

Watu wanaweza kujaribu kupunguza athari kwa kurekebisha mwangaza wa skrini katika eneo lao la kulala au kwa kuwezesha hali ya giza, lakini Bwana Piper anasema tafiti za awali zimeonyesha kuwa kurambaza (scroll) kwenye simu za rununu, kompyuta na vifaa vingine kunasumbua zaidi na kuvuruga usingizi kuliko mwangaza wenyewe wa skrini.

Vidokezo vya usingizi bora

Inakadiriwa kuwa mtu mmoja kati ya watatu nchini Uingereza ameathiriwa na kukosa usingizi.

Matatizo ya usingizi ni miongoni mwa matatizo ambayo watu hulalamikia, na mara nyingi matumizi ya simu usiku wa manane, kuvinjari katika wavuti, au kuangalia maudhui hasi na yasiyo na maana kwa muda mrefu hutajwa kuwa sababu ya kukosa usingizi.

Kutumia mitandao ya kijamii au kuvinjari maudhui ya mtandaoni kitandani sasa kunazidi kuwa jambo la kawaida, na maoni bado yamegawanyika kuhusu athari zake kwa afya ya kimwili na kiakili. Lakini wataalam bado wanapendekeza kwamba watu waache kutumia vifaa vya kidijitali muda mfupi kabla ya kulala.

Wanasema pia kwamba kujenga tabia ya kwenda kulala na kuamka kwa wakati mmoja kila siku kunaweza kusaidia kuboresha usingizi.

Mashirika ya misaada ya afya ya akili kama vile Mind and Rethink yanapendekeza kufanya shughuli ya kukufanya utulie kabla ya kulala, kama vile mazoezi ya kupumua, kusoma kitabu, au kuoga, badala ya kujilazimisha kulala.

Pia wanapendekeza kuepuka kafeini (kama vile kahawa), pombe, au milo mizito kabla ya kulala, na kuongeza kuwa ikiwezekana, fanya mazoezi rahisi na ufanye eneo lako la kulala na chumba kuwa kimya.

Mtaalamu wa usingizi Dk Kate Lederle aliiambia BBC kwamba mfiduo wa mchana wa asili, hasa asubuhi, ni muhimu sana kwa kusaidia kudhibiti saa ya ndani ya mwili wetu.

Aliongeza kuwa kutafuta njia ya kupumzika kutoka kwa siku ya kuchosha na yenye shughuli nyingi kiakili, kama vile kufanya shughuli ya kufurahisha ambayo haisisimui sana, inaweza kuchukua jukumu muhimu katika usingizi mzuri.

Waandishi wa utafiti wanasisitiza hitaji la utafiti zaidi juu ya mada hii. Wanasema hii inapaswa kujumuisha ufuatiliaji wa muda mrefu wa mifumo ya usingizi na pia kuchunguza mambo kama vile usumbufu wa usingizi unaosababishwa na arifa kutoka kwa vifaa usiku.

Wanasema, "Juhudi kama hizo zinatoa mwanga juu ya athari za utumiaji wa skrini wakati wa kulala wakati wa kulala na zinaweza kufahamisha mapendekezo yanayolengwa kwa wanafunzi na wengine."