Kadiri mapigano yanavyoenea Mashariki ya Kati, ndivyo mawazo ya amani yanavyopungua

- Author, Paul Adams
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mwaka mmoja uliopita Israel ilikumbwa na shambulio baya zaidi la kigaidi katika historia yake na kisha Gaza ikatumbukia katika mashambulizi ya mabomu. Mzozo wa Israel na Palestina, ukatawala tena vyombo vya Habari.
Zaidi ya Wapalestina 41,000 wameuawa. Watu milioni mbili wa Gaza wamefurushwa makwao. Katika Ukingo wa Magharibi, Wapalestina wengine 600 wameuawa. Nchini Lebanon, watu milioni moja wamekimbia makazi yao na zaidi ya 2,000 wameuwawa.
Zaidi ya Waisraeli 1,200 waliuawa siku hiyo ya kwanza. Tangu wakati huo, Israel imepoteza wanajeshi zaidi 350 huko Gaza. Waisraeli laki mbili wamelazimika kuondoka katika makazi yao karibu na Gaza na kwenye mpaka wa kaskazini na Lebanon. Takribani wanajeshi 50 na raia wameuawa na maroketi ya Hezbollah.
Kuenea kwa mgogoro

Chanzo cha picha, Getty Images
Huko Mashariki ya Kati, wengine wamejiunga na vita. Juhudi za Marekani za kuzuia mzozo huo usizidi kuongezeka, zinazohusisha ziara za rais, diplomasia na kutumwa kwa vikosi na silaha nyingi za kijeshi, zote zimeambulia patupu. Makombora yamerushwa kutoka Iraq na Yemen.
Israeli na Iran zimeshambuliana. Na Marekani imeonekana kuwa na ushawishi mdogo. Mzozo unapozidi kuenea na kubadilika, huelekea kwenye majanga makubwa zaidi.
Maisha ya watu wa Gaza, kabla na baada ya Oktoba 7, yanakaribia kusahaulika huku vyombo vya habari vikitarajia vita kamili Mashariki ya Kati.
Baadhi ya Waisraeli ambao maisha yao yalivurugwa siku hiyo mbaya wanahisi kupuuzwa vivyo hivyo.
"Tumepuuzwa," anasema Yehuda Cohen, baba wa mateka Nimrod Cohen. Anasema Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ndiye anahusika kwa "vita visivyo na maana ambavyo vimewakutanisha maadui wote dhidi yetu".
Mashambulizi ya Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sio Waisraeli wote wenye mtazamo kama huo wa Cohen. Wengine wanaona mashambulizi ya Hamas ya mwaka mmoja uliopita kama utangulizi wa kampeni pana ya maadui wa Israel ya kuliangamiza taifa la Kiyahudi.
Israel imejibu kwa kushambulia vifaa vya mawasiliano, mauaji ya viongozi, makombora ya masafa marefu na operesheni za kijasusi ambazo nchi hiyo imekuwa ikijivunia kwa muda mrefu.
"Hakuna mahali popote ndani ya Mashariki ya Kati, Israel haiwezi kufika," Netanyahu alitangaza kwa ujasiri wiki iliyopita.
Kura za maoni zilikuwa chini kwa waziri mkuu kwa miezi kadhaa baada ya Oktoba 7. Sasa zimepanda tena. Je, ni leseni ya kushambulia zaidi?
"Hakuna hata mmoja wetu anayejua ni lini vita vitaisha na kila mtu atakuwa wapi wakati huo," anasema Simon Gass, balozi wa zamani wa Uingereza nchini Iran.
Marekani bado inahusika, hata kama ziara za kwenda Israel za Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom), Jenerali Michael Kurilla ni za usimamizi wa mgogoro kuliko utafutaji wa njia za kidiplomasia.
Huku uchaguzi wa urais ukiwa umesalia wiki nne tu, hali ya kisiasa ya Mashariki ya Kati ni mbaya kuliko hapo awali.
Kwa sasa, changamoto kubwa ni kuzuia vita vya kikanda.
Kuna maoni jumla, miongoni mwa washirika wa Israel, kwamba ina haki ya kujibu shambulio la kombora la balestiki lililofanywa wiki iliyopita na Iran.
Hakuna Muisraeli aliyeuawa katika shambulio hilo na Iran ilionekana kulenga shabaha za kijeshi na kijasusi, lakini Netanyahu hata hivyo ameahidi jibu kali.
Amani bado iko mbali

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya wiki za mafanikio makubwa katika mbinu, waziri mkuu wa Israel anaonekana ana matarajio makubwa zaidi.
Katika hotuba ya moja kwa moja kwa watu wa Iran, alidokeza kwamba mabadiliko ya kiutawala yanakuja Tehran. "Iran hatimaye itakuwa huru, na muda huo utakuja mapema zaidi kuliko watu wanavyofikiria, kila kitu kitakuwa tofauti," alisema.
Kwa baadhi ya waangalizi, usemi wake una mwangwi wa kusikitisha kama ule uliotolewa na wahafidhina mamboleo wa Marekani katika kipindi cha uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq mwaka 2003.
Utawala wa Iran unataka dunia isiyokuwa na Israel, lakini unajua kwamba haina uwezo wa kulifanya hilo pekee yake, hasa katika wakati ambapo Hizbullah na Hamas - washirika wake katika kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani" - wanashambuliwa.
Na Israel, ambayo ingependa sana kuliondoa tishio la Iran, pia inajua haiwezi kufanya hivyo peke yake, licha ya mafanikio yake ya hivi karibuni.
Mabadiliko ya serikali ya Tehran hayako kwenye ajenda ya Joe Biden, wala ya makamu wake wa rais, Kamala Harris.
Kuhusu Donald Trump, wakati mmoja alionekana kuwa tayari kushambulia Iran - baada ya Tehran kuiangusha ndege isiyo na rubani ya Marekani Juni 2019 - rais huyo wa zamani alirudi nyuma dakika za mwisho (ingawa aliamuru kuuawa kwa jenerali mkuu wa Iran, Qasem Soleimani, miezi saba baadaye).
Huku mabaki mengi yakiwa yametapakaa barabarani, na matukio bado yanaendelea kwa kasi ya kutisha, watunga sera - na sisi wengine - tunatatizika kuelewa hali hiyo.
Wakati mzozo uliozuka Gaza ukiendelea mwaka wake wa pili, mazungumzo yote ya jinsi Gaza itakavyo kuwa na kutawaliwa baada ya mapigano kumalizika - yameachwa, au kuzamishwa na kelele ya vita vikubwa.
Kwa hivyo mjadala wowote wa maana wa utatuzi wa mzozo wa Israel na Wapalestina, ni lazima kwanza ujadili mzozo ambao umetufikisha hapa tulipo.
Muda ambao Israel itahisi imefanya uharibifu wa kutosha kwa Hamas na Hezbollah, na uchaguzi wa rais wa Marekani ukimaliza, diplomasia inaweza kupata nafasi nyingine.
Lakini hivi sasa, hayo yote bado yako mbali sana.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












