Rigathi Gachagua: Wabunge wapiga kura kuamua hatma ya naibu wa Rais
Mbivu na mbichi kujulikana baada ya ya Spika wa bunge kutangaza kwamba wabunge sasa watapiga kura ili kuamua kuhusu hatma ya naibu wa rais Rigathi Gachagua
Muhtasari
- Ofisi za Save the Children zavamiwa Guatemala
- ‘‘Gachagua hana heshima kwa wamama aliita mbunge wetu malaya’’
- Hoja ya kumtimua mamlakani Naibu wa Rais Kenya: Haya ndiyo unayopaswa kujua
- Hezbollah yarusha makombora zaidi ya 100 kaskazini mwa Israel
- Rais wa Korea Kaskazini, Kim amuita Putin 'rafiki wa karibu zaidi'
- Rigathi Gachagua: Hoja ya kumuondoa madarakani Naibu wa Rais wa Kenya yaanza kujadiliwa bungeni
- Israel inasema imeongeza operesheni ya ardhini kusini mwa Lebanon
- Israel yasema ilimuua kamanda wa Hezbollah huko Beirut
- Cissy Houston, mwimbaji nguli na mama wa Whitney Houston, afariki dunia
- Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon asema nchi yake imetelekezwa na jumuiya ya kimataifa
- 'Jinsi Israeli inavyojilinda ni muhimu,' asema Kamala Harris
- Israel yaadhimisha mwaka mmoja tangu shambulio la Hamas huku mapigano yakiendelea
Moja kwa moja
Na Asha Juma, Lizzy Masinga, Dinah Gahamanyi &Seif Abdalla
Habari za hivi punde, Bunge la Kenya laidhinisha Gachagua kuondolewa madarakani
Hatimaye bunge limefanya uamuzi wa kumuondoa naibu wa rais wa Kenya Rigathi Gachagua kupitia kura iliopigwa.
Katika kura iliopigwa kuamua hatma yake, wabunge 281 waliunga mkono hoja ya kumuondoa kiongozi huyo madarakani huku wabunge 44 wakipiga kura ya kupinga na mbunge mmoja akikataa kupiga kura.
Habari za hivi punde, Bunge linapiga kura kuamua hatma ya Rigathi Gachagua
Gachagua aweka hatma yake kwa bunge
Naibu Rais Rigathi Gachagua ameweka matumaini yake kwa Wabunge wanapojiandaa kupiga kura kuhusu hoja yake ya kuondolewa madarakani.
Gachagua amesema anaheshimu na anaamini Bunge litafanya uamuzi sahihi.
Naibu huyo alikuwa akiwahutubia wabunge alipofika mbele ya Bunge kujibu tuhuma zilizowasilishwa kwenye hoja yake ya kuondolewa madarakani.
"Angalia, tafakari, na tumia dhamira yako na ufanye uamuzi yanayofaa," alisema.
"Ninaheshimu sana Bunge na uwezo wake wa kufanya uamuzi sahihi." Kiongozi huyo alitetea hatua yake ya kuzungumzia madai hayo siku moja kabla ya kufika mbele ya Bunge.
Gachagua alihutubia taifa katika mahojiano na wanahabari katika makazi yake rasmi ya Karen Jumatatu usiku.
'Hoja ya kuniondoa madarakani ni hafifu' - Gachagua
Kuhusu hoja iliowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Mwinge Mutuse, bwana Gachagua amesema kwamba madai hayo hayajafikia kiwango cha kumuondoa madarakani.
Amesema kwamba hakuna hata siku moja uchunguzi umefanywa dhidi yake kwa makosa chini ya sheria hiyo ama hata kuitwa ,kuandikisha taarifa kuhusu uchunguzi wowote.
Amesema kwamba kama Mkenya mwengine yeyote yule katiba inampa haki ya kutokuwa na hatia kuhusiana na makosa ya jinai hadi kinyume chake kitakapothibitishwa katika mahakama ya sheria chini ya kiwango maalum cha ushahidi.
Bwana Gachagua aliongezea kwamba kutokana na kutokuwepo kwa uchunguzi wowote dhidi yake haamini kwamba kunaweza kuwa na sababu zozote kuamini kwamba alifanya makosa yoyote, vinginevyo hilo lingewachiwa vyombo vya upelelezi pamoja na vyombo vya uchunguzi nchini.
‘’Kwa hivyo, ni jambo lisilowezekana kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 145(1)(b) ya Katiba kutegemea maoni ya Mheshimiwa Mutuse Eckomas Mwengi bila ya kuwepo mapendekezo yoyote kutoka kwa mpelelezi .
Alisema Gachagua: Madhara halisi ya kushtakiwa kwa msingi wa madai ya makosa ya jinai ambayo ushahidi wake haujajaribiwa katika mahakama ya sheria au na vyombo vinavyotoa mamlaka ya kuchunguza kama vile DCI, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Shirika la Urejeshaji Mali, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa itakuwa kuniondoa kwenye uwezekano wa kushika wadhifa wa umma kuhusiana na Kifungu cha 99(3) bila ya utaratibu wa kisheria .
Shirika la Ujasusi Kenya lilishindwa kuwajibika kabla ya maandamano - Gachagua

Chanzo cha picha, Kenya National Assembly
Kuhusu madai ya kuhujumu Shirika la Ujasusi nchini kenya, Bwana Gachagua amejitetea akisema kwamba , kitengo hicho cha serikali kilipaswa kujua kwamba Wakenya walikuwa wanapinga muswada wa fedha wa mwaka huu hivyobasi kilipaswa kumuarifu rais kabla ya maandamano yaliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu na uvamizi wa bunge.
Anasema iwapo kitengo hicho kingewajibika vya kutosha serikali ingeweza kubadili mipango yake na kuzuia maafa yaliotokea.
Anasema kwamba matamshi yake kuhusu kitengo hicho aliyoyatoa mjini Mombasa hayakuwa tofauti na kinachoendelea katika nchi nyingine wakati kitengo kama hicho kinashindwa kuwajibika.‘
''Taifa limeshuhudia matukio ya kusikitisha ya mauaji kadhaa, utekaji nyara na watu kupotea. Ninaamini kwamba kama idara ya upelelezi ya Taifa ingefanya kazi kwa bidii, matukio haya yasingeshuhudiwa’'.
Amesema kwamba chini ya Katiba ya Kenya, mashirika ya serikali yanapaswa kuwajibika kwa Wakenya .
Aliongezea kwamba pia anafahamu kuwa Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa mstari wa mbele kuwashtumu maafisa ambao wanaonekana kutoelewa kazi yao.
‘’Hivi majuzi, bosi wangu, Rais, alilalamika hadharani kuhusu watu wasio wajibika serikalini. Pia ninakumbuka kwamba bosi wangu, alipokuwa Naibu Rais, pia alimpigia simu aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Bw. Mutyambai.
Bwana Gachagua anasema kwamba Iliripotiwa na vyombo vya habari kwamba IMF ilikuwa tayari imeonya kuhusu machafuko yaliotarajiwa kufanyika kutokana na watu kutoridhika na Mswada wa Fedha wa 2024.
‘Sikumtishia jaji yeyote, nilichukua hatua za kisheria’ - Gachagua

Chanzo cha picha, Kenya National Assembly
Kinyume na madai katika hoja maalum, kwamba kiongozi huyo alimtishia jaji Esther Maina hadharani na kuonya kumchukulia hatua, Gachagua anasema kwamba badala yake alichukua hatua kama Mkenya mwengine yeyote kuwasilisha ombi kwa tume ya Utumishi wa mahakama akiomba jaji huyo atimuliwe.
‘’Nilichukua hatua halisi za kisheria zinazopatikana kwa kila raia wa Kenya chini ya Kifungu cha 168(2) cha Katiba kinachoruhusu mtu yeyote Kuwasilisha Ombi kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama ili Jaji yeyote aondolewe na nikawasilisha malalamiko ya kisheria mbele ya Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) mwezi Machi 2024’’ alisema Gachagua.
'Mali inayodaiwa ni yangu ni ya ndugu yangu marehemu' - Gachagua
Naibu wa rais nchini Kenya ameanza kujitetea dhidi ya madai ya kumtaka kuondoka madarakani.
Akizungumza punde tu baada ya kuwasili bungeni , Gachagua amesema kwamba madai ya umiliki wa hoteli ya Olive Garden jijini Nairobi, Vipingo Beach Resort iliopo Kilifi and Queens Gate Serviced Apartment Spar and Resort, ni ya uwongo na kwamba mali hiyo inamilikiwa na ndugu yake ambaye ni marehemu.
'Baada ya kifo chake, marehemu kaka yangu aliwacha wasia ambao, baada ya kunitambua kwamba nilikuwa mwaminifu aliniteua kuwa mmoja wa Wasimamizi wa mali yake '.
Gachagua anasema kwamba katika wasia huo, marehemu kaka yake alielekeza hoteli hizo ziuzwe na mapato yagawanywe . Bwana Gachagua alisema kwamba licha ya kuwa mmoja ya waliotajwa kurithi mali hiyo hamiliki hoteli yoyote
Habari za hivi punde, Rigathi Gachagua: Naibu Rais wa Kenya aanza kujitetea bungeni dhidi ya hoja ya kumtimua madarakani
Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ameanza kujitetea mbele ya Wabunge nchini humo ambao wamekuwa wakijadili hoja ya kumuondoa madarakani, kwa tuhuma mbali mbali ikiwa ni pamoja na uhaini, kupata mali kinyume cha sheria na kutoa kauli zinazochochea ukabila.
‘Alaumiwe Rais Ruto, si Gachagua’

Chanzo cha picha, Kenya National Assembly
Mambo yanaendelea kupamba moto bungeni nchini Kenya.
Hata hivyo, si wabunge wote wanaunga mkono hoja ya kuondolewa kwa naibu rais Rigathi Gachagua.
Wapo wanaomuunga mkono bwana huku wakipinga kutimuliwa kwake.
Mbunge Makali Mulu akichangia hoja bungeni alidai bwana Gachagua ananyanyaswa kutokana na msimamo wake na kuwa rais William Ruto ndiye anayefaa kulaumiwa.
‘’Mtu wa juu zaidi katika suala la uongozi ni Rais, sio Naibu Rais. Kwa hiyo katika hali ambayo uamuzi unafanywa na Naibu Rais haungi mkono, swali ni je, unafaa kuwa ukimnyanyasa Naibu Rais au Rais? Kwa hiyo kwa misingi ya bomoabomoa hiyo, Mheshimiwa Spika, itakuwa si haki kabisa kuanza kusema ni Naibu Rais ambaye hamtii Rais. Hebu tuwe waaminifu sana kwetu binafsi. Huo ndio ukweli wa mambo mheshimiwa Spika.’’
Kiongozi mtarajiwa wa Hezbollah 'pengine' aliuawa, Israel yasema
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant anasema kwamba kiongozi mkuu wa Hezbollah Hashem Safieddine "huenda" aliuawa katika shambulizi wiki iliyopita.
Ilielezwa kuwa Safieddine anaweza kuwa kiongozi ajaye wa kundi hilo, baada ya binamu wa kiongozi wa zamani, Hassan Nasrallah kuuawa mwezi uliopita katika shambulio la anga la Israel.
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kwamba Safieddine aliuawa katika shambulio la bomu la Israel huko Beirut lakini haijathibitishwa.
Wakati wa amri fupi na Jeshi la Ulinzi la Israeli, Gallant pia anasema vikosi vya Hezbollah "vimepigwa na kuvunjwa" tangu kuuawa kwa Nasrallah, jambo ambalo Hezbollah ilikanusha hapo awali.
Hezbollah haijasema chochote kuhusu mahali alipo Safieddine tangu mashambulizi hayo yalipotokea.
Ofisi za Save the Children zavamiwa Guatemala

Chanzo cha picha, AFP
Polisi nchini Guatemala walivamia ofisi tano za kikanda za shirika la misaada la Uingereza Save the Children siku ya Jumatatu kama sehemu ya uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji wa watoto.
Waendesha mashtaka waliomba taarifa kutoka kwa mamlaka ya Marekani mwezi Aprili kuhusu madai ya kuhusika kwa shirika hilo katika kusafirisha watoto kuvuka mpaka, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Shirika la Save the Children lilisema "linafahamu shughuli" katika ofisi zao, na likakanusha madai ya waendesha mashtaka.
Mwendesha mashtaka anayesimamia kesi hiyo, Rafael Curruchiche, na mwanasheria mkuu wa nchi hiyo, Consuelo Porras, hapo awali waliidhinishwa na Marekani na Umoja wa Ulaya kwa mashambulizi dhidi ya demokrasia
Katika taarifa kwa BBC, Save the Children ilisema kuwa inashirikiana na mamlaka lakini "haijawezesha uhamisho wowote wa watoto au vijana kutoka Guatemala".
"Kufuatia madai ya awali dhidi ya shirika letu mwaka huu, hakuna ushahidi uliopatikana", shirika hilo liliongeza.
Mapema mwaka huu, kundi la misaada lilisema "limeshtushwa na kushangaa" baada ya ofisi yake kuu kuvamiwa wakihusishwa na madai hayo.
‘Gachagua hana heshima kwa wanawake’

Chanzo cha picha, Parliament of Kenya
Imekuwa ni siku ya kauli kali katika bunge la Kenya huku idadi kubwa ya wabunge wakitoa hoja kali za kuunga mkono hoja kumtimua mamlakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua.
Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, ambaye aliwasilisha hoja ya kuondolewa mamlakani dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, Jumanne aliwasilisha kanda za video za Naibu Rais mnamo Februari 2023 alipotoa maoni yake kuhusu serikali kuwa 'kampuni' ambapo baadhi ya Wakenya ni 'wenye hisa nyingi ' na wengine 'hawana hisa'.
Mbunge huyo alisema maoni ya Gachagua yana hatari ya kuigawanya nchi na kuitumbukiza katika siasa mbaya za ukabila.
Mbunge Boss Sholei, Naibu Spika wa bunge na mbunge wa kiti cha wawakili wanawake wa jimbo la Uasin Gishu, pia alimshutumu Gachagua kwa uhaini kwa kumhujumu rais katika mikutano yake.
Bi Sholei alianza kwa kujitetea dhidi ya shutuma za upendeleo zilizotolewa na Gachagua ambaye alimshutumu kwa kutumia kiti chake kama Naibu Spika wa bunge : “Nataka nithibitishe kuwa sina upendeleo hata kidogo, nilipotoa kauli hizo nilizitoa kama mbunge wa Uasin Gishu na si kwa kama Naibu Spika , unaweza kunituhumu kwa upendeleo tu nikitoa kauli zangu kama Naibu Spika ," alisema Bi Sholei.
Sholei alikariri kauli anazodaiwa kuzitoa Bwana Gachagua katika mikutano alizodai zinalenga kuchochea utengano miongoni mwa Wakenya : "Wakati alipokuwa akitoka kanisani Meru, DP alisisitiza kwamba ikiwa ataondolewa, jamii za Wakenya wenyeji wa Mlima Kenya zitaiasi serikali na kuwa na vurugu. huo pia ni uhaini," aliongeza.
Mbunge wa Kaunti ya Likoni Mombasa katika pwani ya Kenya, Mishi mboko pia hakutafuna maneno huku akimshutumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kushindwa kutekeleza maadili ya kiapo chake na kuwakosea heshima wanawake.
‘‘Gachagua hana uwezo kwasababu alisema anapambana na matumizi ya dawa za kulevya, lakini alipofika pwani alikuwa anawanyanyasa viongozi tu’’ alisema Bi Mboko.
‘‘Gachagua hana heshima kwa wamama aliita mbunge wetu malaya’’, aliongeza mbunge huyo wa Likoni.
‘‘Gachagua amezungumzia kwamba nchi yetu ni kama kampuni na washikadau ,na washikadau hawa ni wale ambao tu wamepiga kura katika serikali ya Kenya Kwanza, hivyo alikiuka katiba’’ alisisitiza.
Kwa sasa sasa linajadili hoja hiyo kama hoja nyingine yoyote kabla ya kumpa naibu wa rais fursa ya kujitetea.
Unaweza pia kusoma:
Hoja ya kumtimua mamlakani Naibu wa Rais Kenya: Haya ndiyo unayopaswa kujua,

Chanzo cha picha, https://deputypresident.go.ke
Bunge la Kenya kwa sasa linajadili hoja hiyo kama hoja nyingine yoyote kabla ya kumpa naibu wa rais fursa ya kujitetea, na baadaye kupiga kura kuthibitisha hoja 11 moja baada ya nyingine au kuzikataa zote. Ufuatao ni muhtasari wa matukio muhimu kuhusu hoja hiyo:
- Naibu Rais wa Kenya Geoffrey Rigathi Gachagua anatarajiwa kufika mbele ya Bunge la kitaifa mwendo wa saa kumi na moja jioni ya Jumanne Octoa 8 ili kujitetea dhidi ya mashtaka 11 yaliyowasilishwa.
- Kikao maalum kilianza saa tatu asubuhi, ambapo mbunge wa Kibwezi magharibi Mwengi Mutuse alieleza kwa kina mashtaka 11 dhidi ya Gachagua ambazo anahisi zimevunja sharia na katiba ya Kenya.
- Ripoti ya maoni ya Wakenya kuhusiana na hoja hii iliwasilishwa Bungeni ambapo pia takwimu ya jinsi walivyopiga kura zilionyeshwa kwa Wabunge.
- Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, mbunge wa Kilifi Owen Baya aliunga mkono hoja hiyo baada ya hapo wabunge wengine wakapata fursa ya kuchangia hoja hiyo bungeni.
- Bunge likirejea kwenye kikao cha pili mwendo wa saa nane unusu, hoja hiyo itaendelea kujadiliwa hadi pale atakapowasili Naibu Rais na mawakili wake, kwa kikao maalum cha kujieleza na kujibu maswali ya wabunge.
- Kikao hiki cha kamati ya bunge zima kinasimiwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula.
- Baada ya saa mbili za kujieleza na kujibu maswali, Gachagua ataondoka bungeni na kuwaacha wabunge wakijadili majibu yake, kwa muda.
- Usiku wa leo, Spika Wetangula anatarajiwa kutangaza rasmi kwamba kikao maalum cha bunge kiko tayari kupigia kura hoja hiyo ya kumuondoa kazini Naibu Rais Gachagua.
- Atawaomba viranja wa bunge kupiga kengele ya kuidhinisha kura hiyo kupigwa.
- Kura huweza kupigwa kwa njia ya siri kupitia mashine za Kompyuta wanapoketi Bungeni. Kila mbunge ana kadi maalum yenye taarifa zae muhimu ambayo ataitumia kupiga kura , kisha matkeo yatangzwe kwenye Bunge kupitia {screen} iliyopo bungeni.
- Ili kupitishwa, wabunge 235 ambao ni thuluthi mbili ya wabunge wote nchini Kenya wanatarajiwa kukubaliana na hoja hiyo. Ikiwa raundi ya kwanza haitaafikia hili, basi wabunge watarudia kupiga kura.
Unaweza pia kusoma:
Habari za hivi punde, Hezbollah yarusha makombora zaidi ya 100 kaskazini mwa Israel
Hezbollah wanasema wamerusha makombora kuelekea miji ya Haifa na Krayot kaskazini mwa Israel, wakisema kuwa wamerusha "safu kubwa ya makombora".
Jeshi la Israel pia lilisema liligundua kurushwa kwa roketi 85 kutoka Lebanon mara baada ya saa sita mchana, na nyingi kati ya hizo zilinaswa lakini "ajali kadhaa ziligunduliwa katika eneo hilo".
Makombora mengine 20 yalibainika yakivuka kutoka Lebanon kwenda katika eneo la Israel.
Huduma ya gari la wagonjwa ya Magen David Adom ya Israel inasema mwanamke mwenye umri wa miaka 70 alijeruhiwa na wakati ilisambaza video inayoonesha jengo lililogongwa.
Vyombo vya habari vya Israel pia viliripoti kuwa jengo la Kiryat Yam huko Haifa limeharibiwa.
Haifa, jiji la tatu kwa ukubwa nchini humo, lina wakazi wapatao robo milioni. Iilipigwa jana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miaka 20.
Rais wa Korea Kaskazini, Kim amuita Putin 'rafiki wa karibu zaidi'

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ametuma ujumbe wa siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin, akimtaja kuwa "rafiki wake wa karibu zaidi".
Kim akimpongeza Putin kwa kutimiza miaka 72, aliongeza kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaimarishwa.
Uhusiano kati ya Pyongyang na Moscow umeongezeka tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, katika hatua ambayo inaitia wasiwasi Magharibi.
Katika hatua nyingine siku ya Jumanne, Kim alisema Pyongyang itaharakisha hatua za kuifanya nchi yake kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya kijeshi yenye silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa mtandao wa Yonhap News ukinukuu vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini KCNA, Kim alisifu uhusiano kati ya nchi zote mbili, akisema umekuwa "usioshindwa na wa milele", tangu ziara ya Putin huko Pyongyang mwezi Juni.
"Mikutano na uhusiano wa kindugu kati yetu... utatoa mchango chanya katika kuimarisha zaidi msingi wa milele wa urafiki wa DPRK na Urusi," aliongeza, akimaanisha Korea Kaskazini kwa jina lake rasmi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea.
Mapema mwaka huu, Putin na Kim walitia saini makubaliano ya kuahidi kwamba watasaidiana katika tukio la "uchokozi" dhidi ya nchi zote mbili - ingawa haikuwa wazi ni nini kilimaanisha uchokozi.
Kim ameshutumiwa kuisaidia Urusi katika vita dhidi ya Ukraine kwa kuipatia silaha badala ya msaada wa kiuchumi na kiteknolojia.
Rigathi Gachagua: Hoja ya kumuondoa madarakani Naibu wa Rais wa Kenya yaanza kujadiliwa bungeni

Chanzo cha picha, Rigathi Gachagua/X
Bunge la Kitaifa nchini Kenya limeanza kujadili hoja ya kuondolewa madarakani kwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.
Hatua hii inawadia baada ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse kuwasilisha sababu 11 kupitia hoja ya kutaka kumuondoa madarakani mnamo tarehe 26 Septemba.
Baadaye, naibu wa rais atakuwa na fursa ya kujitetea.
Gachagua amekanusha shutuma zote dhidi yake katika kikao na wanahabari siku ya Jumatatu.
Mchakato huo umeanza kwa kuwasilishwa kwa Ripoti ya zoezi la Ushirikishwaji wa Umma ambalo liliendeshwa kuhusu kuondolewa kwake madarakani, ambapo Wakenya walitoa maoni yao kwa kila tuhuma 11 zinazomkabili Gachagua.
Iwapo hoja hiyo itapata uungwaji mkono wa thuluthi mbili (233) ya wabunge 349, itawasilishwa kwa Seneti.
Hata hivyo ikiwa wabunge 117 wataikataa, naibu wa rais atasalia madarakani.
Pia unaweza kusoma:
Israel inasema imeanza operesheni ya ardhini kusini-magharibi mwa Lebanon
Jeshi la Ulinzi la Israel limetangaza hivi punde kwamba limeanza operesheni ndogo ya ardhini dhidi ya Hezbollah katika sehemu ya magharibi ya kusini mwa Lebanon tangu jana.
Operesheni ya ardhini ya Israel kusini mwa Lebanon ilianza tarehe 30 Septemba - hadi sasa, ilikuwa imelenga upande wa mashariki wa mpaka.
IDF pia inasema ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa akiba wa IDF kutumika katika operesheni za mapigano kusini mwa Lebanon.
Hezbollah inasema imerusha makombora zaidi kaskazini mwa Israel
Wakati huo huo, Hezbollah inasema ilirusha makombora zaidi kaskazini mwa Israel usiku kucha.
Kundi hilo linasema lililenga maeneo yenye makombora ya Israel huko Dishon na Dalton kaskazini mwa Israel.
Pia inasema ilirusha makombora kwenye "mkusanyiko wa vikosi vya adui" huko Yir'on, makazi mengine kaskazini mwa Israel, karibu na mpaka wa Lebanon.
Mapema usiku, Hezbollah ililenga makazi ya Waisraeli magharibi zaidi, ilisema kwenye mtandao wake wa Telegraph ya lugha ya Kiingereza.
Soma zaidi:
Israel yasema ilimuua kamanda wa Hezbollah huko Beirut huku mashambulizi ya anga yakiendelea

Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Israel linasema kuwa limemuua kamanda wa Hezbollah katika shambulio lililofanyika jana katika eneo la Beirut.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel vinasema Suhail Hussein Husseini alitekeleza jukumu "muhimu" katika kusafirisha silaha kati ya Iran na Hezbollah.
Bado hatujaona uthibitisho wowote wa kifo chake kutoka kwa Hezbollah.
Kulikuwa na milipuko zaidi jana usiku katika mji mkuu wa Lebanon, huku vyombo vya habari vya Lebanon vikiripoti angalau mashambulizi 10 ya anga huko Dahieh - kitongoji cha kusini mwa Beirut kikichukuliwa kuwa ngome ya Hezbollah.
Kaskazini mwa Israel, ving'ora vya kuonya mashambulizi ya roketi viliendelea kusikika usiku kucha na miji kadhaa zaidi ilitangazwa kuwa maeneo ya kijeshi yaliyofungwa.
Hapo awali Hezbollah ilisema ililenga viunga vya Tel Aviv kwa roketi, na Israel ilisema Hezbollah ilikuwa imerusha makombora 190 kufikia Jumatatu.
Soma zaidi:
Cissy Houston, mwimbaji nguli na mama wa Whitney Houston, afariki dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
Cissy Houston, mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili na mamake Whitney Houston, amefariki dunia Jumatatu asubuhi akiwa na umri wa miaka 91, familia yake ilisema katika taarifa.
Houston, mwimbaji aliyeshinda Tuzo ya Grammy mara mbili, alifariki nyumbani kwake New Jersey alipokuwa katika huduma ya wagonjwa wa Alzheimer, binti-mkwe wake Pat Houston alisema.
“Mioyo yetu imejaa uchungu na huzuni. Tumempoteza mama wa familia yetu,” alisema, akiongeza kuwa mama-mkwe wake alikuwa “mtu hodari na imara” katika maisha ya familia hiyo.
Houston alifurahia kazi ya uimbaji yenye mafanikio ya miongo kadhaa, ambapo aliigiza pamoja na wasanii maarufu kama Elvis Presley na Aretha Franklin.
