Ni wakati gani unapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya kushindwa kudhibiti mawazo?

Utafiti unaonyesha kuwa wengi kati yetu tutapata matukio yasiyofaa ghafla akilini mwetu wakati fulani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,
    • Author, Yasmin Rufo
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Je, umewahi kukaa kwenye mkutano usio na mvuto na kujiuliza: "Vipi kama nitaanza kupiga kelele?" Au unaendesha gari na unafikiri: "Vipi kama nitapata ajali?"

Matukio haya yanayosumbua yanajulikana kama "mawazo yanayojitokeza ghafla" ambayo wengi wetu tutayapitia mara kwa mara na kuhisi tunaweza kuyapuuza.

Lakini kwa baadhi yanaweza kuwa mawazo yanayowalemea ambayo husababisha tabia za kujirudiarudia.

Wakati Dkt. Nina Higson-Sweeney alipokuwa mtoto, aliamini kwamba familia yake ingepata madhara ikiwa angekuwa na mawazo "mabaya" alipokuwa akitembea kurudi nyumbani kutoka shuleni.

"Nilipokuwa nikipata mawazo ya ghafla, nilianza tena kutembea kutoka kituo cha basi," anasema. "Niliogopa sana kwamba kama nisingelifanya tena na kitu kikatokea, kingekuwa kosa langu."

Nina aligunduliwa na ugonjwa wa obsessive compulsive disorder, OCD akiwa na umri wa miaka 10 na sasa anafanya kazi kama mtafiti wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza ambapo ana utaalamu wa afya ya akili ya watoto na vijana.

Dr Nina Higson-Sweeney

Chanzo cha picha, Dr Nina Higson-Sweeney

Maelezo ya picha,

"Nadharia ni mawazo, hisia au hisia za mwilini zinazoingilia na zisizotakiwa, ilhali kulazimishwa (compulsions) ni matendo ya kurudiarudia na ya kifumbo yanayofanywa ili kupunguza au kuondoa wasiwasi unaosababishwa na mawazo hayo, " Nina anaiambia BBC.

Inakadiriwa kuwa OCD huathiri asilimia 1–3 ya watu duniani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mawazo yanayoingilia yanaweza kuwa yanasumbua sana, na mara nyingi hulenga mambo yanayohisiwa kuwa yanapingana kabisa na maadili au utambulisho wa mtu.

"Unaweza kuwa na mawazo kuhusu madhara yanayowapata wapendwa wako," anasema Nina.

"Inaweza kuwa ni kujiuliza kuhusu mwelekeo wa kingono, je, mimi ni mtu wa mapenzi ya jinsia moja? Je, mimi ni wa jinsia tofauti? Inaweza hata kufikia kiwango cha kupita kiasi kama kujiuliza, je, mimi ni mtu wa kuwafanyia watoto vitendo vya kingono?"

"Jambo la kawaida sana ni mawazo yanayoingilia kuhusu uchafuzi na hofu ya kuugua au kusambaza magonjwa," anasema.

OCD mara nyingi huanza wakati wa kubalehe au ujana, lakini baadhi ya watu hugunduliwa baadaye maishani kwa sababu wanaweza "kuishi kwa miaka mingi wakificha msongo wa mawazo," anasema.

Utafiti unaonesha kuwa kunaweza kuwa na sababu za kijenetiki katika kuibuka kwa OCD, pamoja na uhusiano na msongo wa maisha ya awali kama vile kunyanyaswa, kufiwa, au kusambaratika kwa familia.

Mwanasaikolojia Kimberley Wilson anasema karibu kila mtu hupata mawazo yasiyotakiwa wakati fulani maishani.

"Utafiti unaonyesha kuwa takribani asilimia 80 ya watu hupata mawazo haya," anaeleza.

Kwa watu wengi, mawazo hayo hupita haraka.

"Tunaweza kuangalia, kufikiri ni ya ajabu, kisha kuyaweka kando," anasema.

Lakini kama huwezi kuyaondoa mawazoni, hapo ndipo unaweza kuhitaji kutafuta msaada, anashauri.

"Mawazo yanayohusiana na OCD hayapiti, yanabaki akilini, na hayawi mawazo chanya kamwe. Mara nyingi huwa ya ukali, uhasama, na ni magumu sana kushughulikia. Hapo ndipo yanapochukua maisha yote ya mtu na kusababisha tabia za kulazimika."

Dalili zake zinaweza kuwa za kiakili, kama kuhesabu hadi namba fulani, au zinazoonekana wazi, kama kukagua matairi ya gari mara kwa mara hata kama unajua yako sawa.

Jinsi ya kudhibiti OCD

"Kwenye kesi hizi, mtaalamu anaweza kubaini ni nini kitakachokufaa zaidi," anasema Nina.

Mbali na msaada wa kitaalamu, Nina anasema kuna mbinu watu wanaweza kutumia kila siku kupunguza msongo wa mawazo.

Moja ya mbinu ni kujifunza kubaini mawazo. "Kutambua kwamba 'nina mawazo yaliyoingia ghafla' kujikumbusha kwamba si mimi," anaeleza.

Baadhi ya watu pia hupata msaada kwa kuona OCD kama kitu tofauti.

"Kuchora picha ya jinsi OCD inavyoonekana kunaweza kusaidia, kuna mimi na kuna OCD, na hivi ni vitu viwili tofauti."

Kujitunza pia ni muhimu. "Kula vizuri, kupumzika na kufanya mazoezi ya mwili kunaweza kusaidia kwa sababu OCD huwa mbaya zaidi ninapokuwa na msongo na nisipojitunza," anasema.

Leo, Nina bado anaishi na OCD lakini amejifunza kujikinga nayo.

"Sijawahi kuondokana kabisa na OCD, lakini naweza kufanya mambo nikiwanayo. Sasa nina mawazo madogo na ufahamu mkubwa wa jinsi ya kuyadhibiti. Lakini ninapokuwa na msongo, ni vigumu kudhibiti na bado yanaweza kusababisha tabia za kutodhamiria."

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga