Rais Ruto kuwalipisha 'Mahasla' kodi zaidi

Na Abdalla Seif Dzungu

BBC Swahili

.

Chanzo cha picha, Getty images

Maelezo ya picha, Sarafu ya Kenya

Wizara ya fedha Kenya inapendekeza ulipaji wa kodi ya juu zaidi huku utawala wa rais William Ruto ukihitaji fedha zaidi kufadhili miradi yake.

Hii inajiri siku chache tu baada ya Rais Ruto William Ruto kuongeza kodi ya asilimia 1.5 kufadhili ujenzi wa nyumba mbali na ile ya thamani ya bidhaa VAT kutoka asilimia nane hadi kumi na sita.

Licha ya serikali kutoa ahadi kwa Wakenya kwamba ingewapunguzia gharama ya maisha wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka uliopita, malengo yake yamebadilika na badala yake imeamua kuwatoza Wakenya kodi zaidi ili kutekeleza baadhi ya ahadi ilizotoa.

Ifuatayo ni orodha ya mapendekezo ya kodi ambayo serikali ya Kenya kwanza inapendekeza.

VAT kupanda hadi 18%

Miezi michache tu baada ya serikali kupandisha kodi ya thamani ya bidhaa hadi asilimia 16%, serikali sasa ina mpango mwengine wa kuongeza kodi hiyo kuwiana na kodi za mataifa mengine ya Afrika Mashariki. Majirani wa Kenya , Uganda na Tanzania wanalipa kodi ya 18%.

Ongezeko la kodi ya VAT itasababisha kupanda bei kwa bidhaa nyingi kwani kodi hiyo huangazia bidhaa zote.

Kodi ya Pombe , Sigara na vinywaji kuongezeka

..

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Sigara na Pombe

Baada ya watumiaji wa bidhaa hizi kuepuka ushuru wakati sheria ya fedha ya 2023 ilipopitishwa bungeni, sasa wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi baada ya serikali kupendekeza kuziongezea kodi.

Kiwango cha ushuru kwa sigara na bidhaa zingine za tumbaku zitawianishwa huku ushuru wa pombe ukiongezeka kutokana na kiwango cha kileo.

Iwapo pendekezo hilo litafanikiwa bei za bidhaa hizi huenda zikapanda

Wakenya wana hadi Oktoba 6, 2023, kuwasilisha maoni kuhusu mapendekezo kutoka kwa Hazina.

Kodi ya barabara kuzinduliwa

.

Chanzo cha picha, Nation Media Group

Maelezo ya picha, Barabara ya kuelekea Thika nchini Kenya

Hazina ya serikali imependekeza mabadiliko makubwa ya sera kwa kupendekeza kutekelezwa kwa ushuru wa kila mwaka wa Mzunguko wa Magari - ambao pia unajulikana kama ushuru wa barabarani - ulipwe na wamiliki wote wa magari wakati wa kulipia bima, katika mwaka ujao wa kifedha.

Kodi hiyo italipwa kila mwaka na wamiliki wa magari katika hatua ya kupata bima.

"Kutakuwa na kiwango cha chini cha ushuru kinacholipwa na wamiliki wote wa magari pamoja na kiwango chengine kulingana na uwezo wa injini ya gari,"yalisema mapendekezo hayo.

Kwa kuhusisha ushuru huo na ulipaji wa bima ya magari, serikali inalenga kuhakikisha utiifu miongoni mwa wamiliki wa magari, katika azma ya kurahisisha ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kuhifadhi barabara na maendeleo ya miundombinu.

Kodi ya mabwawa ya kuogelea shuleni

Kama sehemu ya kupanua ukusanyaji wa kodi, Hazina ya serikali imependekeza kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa huduma za Elimu ambazo kwa sasa hazitozwi kodi ili kufanya elimu ipatikane kwa wanafunzi.

Hata hivyo, Hazina inabainisha kuwa manufaa ya msamaha huo si sawa kwa wanafunzi wote kutokana na tofauti za ada zinazotozwa na huduma zinazotolewa.

Inasema baadhi ya shule hutoa huduma ambazo hazihusiani moja kwa moja na elimu kama vile kuogelea na hivyo kusababisha ukosefu wa haki kwa vile kuogelea ni huduma inayopatikana inapotolewa nje ya shule.

"Ili kuondoa ubaguzi huu, kuna haja ya kutoza VAT kwenye huduma za ziada.

Katika suala hili, serikali itachunguza kuanzishwa kwa VAT kwa huduma zinazotolewa na shule lakini hazihusiani moja kwa moja na elimu," Hazina inabainisha katika rasimu ya mapendekezo.

Hii ina maana kwamba huduma zote za kiuchumi zinazotolewa na shule zitavutia kodi ya VAT .