Jinsi mshahara wa Mkenya 'utakavyopigwa panga' ifikiapo mwezi Julai

Na Abdalla Seif Dzungu

BBC Swahili

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Sarafu za Kenya

Huku Wakenya wakiendelea kukumbwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ongezeko la gharama ya juu ya maisha hakuna matumaini ya afueni kupatikana hivi karibuni .

Hatua hii inajiri baada ya serikali kutangaza kuongeza ada ya Hazina ya kitaifa ya Bima ya afya {NHIF} na Ile ya Hazina ya kitaifa ya Hifadhi ya Jamii {NSSF} .

Viwango vya sasa, ambapo wafanyakazi wanaolipwa hulipa kati ya Sh150 na Sh1,700 kulingana na malipo yao ya kila mwezi, vinaondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kiwango kisichobadilika cha asilimia 2.7 ya mshahara wao.

Vilevile kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha, kila mfanyakazi atalazimika kulipa asilimia tatu ya mshahara wake ili kuhudumia hazina mpya ya Maendeleo ya Makaazi.Serikali imesisitiza kuwa malipo hayo sio kodi bali ni akiba ingawa makato hayo yatalindwa na sheria na kutolewa kwa mishahara ya wafanyakazi .

Licha ya lalama za wafanyakazi wengi na waajiri kuhusu athari za tozo hiyo ,serikali inasisitiza kwamba mpango huo ni muhimu kwa sababu utaunda nafasi za ajira kwa mamilioni ya watu wasiokuwa na ajira nchini .

Hata hivyo kumekuwa na uhaba wa maelezo sahihi ya jinsi watu watakavyonufaika na miradi hiyo ya nyumba hasa ikizingatiwa kuwa wasiokuwa na kipato hawatochangia ilhali baadhi ya wanaolazimika kuchangia huenda wanalipa madeni ya ujenzi wa nyumba zao binafsi .

Hazina mpya ya maendeleo ya Makazi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna hitaji kubwa la makazi bora ya bei nafuu nchini Kenya

Akizungumza na waandishi wa habari mapema siku ya Jumatano, katibu wa kudumu katika wizara ya makaazi na maendeleo ya mijini Charles Hinga alisema kwamba ada hiyo itatumika kama hakikisho kwa wawekezaji ambao serikali inataka kujihusisha nao katika ujenzi wa nyumba.

"Baadhi yenu mnauliza kwa nini hatuwezi kutoa fedha hizo kwa hiari? Lakini inapoendeshwa kwa sheria, nikipata bilioni kwa mwezi, ina maana naweza kwenda nje kuwaita wawekezaji na kuwaambia kwamba mradi sheria ipo, nitakusanya fedha baada ya miaka mitatu. ," alisema.

Huku akiifananisha ada hiyo na ushuru wa mafuta unaolipwa na Wakenya, katibu huyo alisema serikali isingeweza kujenga barabara ikiwa haina uhakika wa mtiririko wa pesa kila mwezi kuzipatia kampuni za ujenzi wa barabara.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa X ujumbe

Ruto awasihi wabunge

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wabunge wa Kenya
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Athari ya ada hizo inatarajiwa kuanza kuwa mzigo kwa wafanyakazi wote nchini kufikia mwezi Julai 2023.

Rais William Ruto mnamo Jumanne aliwahimiza wabunge washirika wa muungano wake wa Kenya Kwanza kuunga mkono mapendekezo yake makali ya ushuru na mipango ya kutatua madeni ya umma.

Hatua ya Rais ya kuwahimiza wabunge wake kuunga mkono ajenda yake ilikuja huku maseneta wakirejelea vikao vyao baada ya mapumziko marefu na wenzao wa Bunge la Kitaifa wanaotarajiwa kurejea Jumanne ijayo.

Siku ya Jumatatu rais Ruto aliwaleta wataalam, wakiwemo Makatibu Wakuu na wajumbe wa Baraza la Mawaziri ili kuwaelimisha wabunge kuhusu mapendekezo na ajenda zake za ushuru.

Rais Ruto anatazamia kukarabati uchumi ulio na deni kubwa alilorithi kutoka kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, ambaye aliharakisha kukopa ili kufadhili miradi ya miundombinu ya gharama kubwa.

Licha ya kuahidi kuboresha maisha ya Wakenya maskini wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana, Ruto sasa anachukua hatua isiyopendwa ya kuongeza ushuru.

Hii ina maana kwamba iwapo unapokea mshahara wa Sh. 100, 000 za Kenya kwa mwezi unapaswa kujiandaa kupunguziwa angalau Ksh. 4,380 zaidi kulingana na mapunguzo hayo.

Kwa mujibu wa hesabu zilizofanywa na gazeti la Business Daily, mishahara ya wafanyikazi hawa wanaotoka katika familia za tabaka la kati jijini Nairobi kulingana na hesabu ya matumizi ya Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) - itapungua kutoka wastani wa sasa wa Sh76,041 hadi Sh71, 661.

Mbali na kuathiri kiwango kikubwa cha mishahara ya Wakenya mpango huo pia huenda ukawaongezea mzigo wenye makampuni na kusababisha wafanyakazi wengi kupoteza kazi zao iwapo baadhi ya kodi hizo zitaidhinishwa na bunge.

Kulingana na mabadiliko hayo mapya yaliopendekezwa na rais William Ruto ,ambayo lengo lake ni kulinda afya ya wafanyakazi pamoja na familia zao , yatalenga makundi yote ya mapato huku wale walio na mishahara ya chini ya Sh20,000 wakikatwa Sh2,630.

Tayari, waajiri wameanza kutekeleza viwango vipya vya Hazina ya Kitaifa ya hifadhi ya jamii {NSSF}.

Viwango vilivyorekebishwa vya NSSF vimesababisha ada ya NSSF kupanda hadi Sh1,080 kutoka Sh200 za sasa. Hii ina maana kwamba mwajiri pia analazimika kuipatia serikali kiwango kama hicho.

Watakaotozwa zaidi

Ingawa wafanyikazi wote wataona mshahara wao ukipunguzwa na mabadiliko haya, watu wanaolipwa kiwango cha juu cha mshahara watalazimika kulipa asilimia 35 ya ziada ya kodi ya PAYE (Pay As You Earn) kwenye mapato ya zaidi ya Sh500,000.

Hii itawafanya wale wanaopata Sh600,000 kwa mwezi walipe Sh22,904 kutoka katika mshahara wao, huku serikali ikitafuta nyongeza ya Sh350 bilioni za kodi katika mwaka ujao wa kifedha.

Serikali ya Kenya Kwanza inasema kwamba ongezeko la akiba kupitia NSSF litasaidia sio tu kuwapa wafanyakazi faida katika maisha yao ya uzeeni bali pia kuiwezesha seriikali kupata fedha za ndani iwapo inataka kukopa.

Katika Bajeti ijayo ya Fedha inayoanza Julai, mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini Kenya KRA inalenga kukusanya Sh2.89 trilioni, ikiwa ni ongezeko kutoka kiwango cha sasa cha Sh2.53 trilioni.

Serikali inatarajia makusanyo ya kodi ya mapato—ambayo ni pamoja na PAYE na kodi ya mapato ya biashara inayolipwa na wafanyabiashara—kuongezeka kwa Sh194.2 bilioni hadi Sh1.2 trilioni katika mwaka wa fedha unaoishia Juni mwaka ujao.

Hadi sasa mazingira magumu ya biashara yameifanya serikali kushindwa kukusanya kodi PAYE katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu wa fedha.

Gharama ya maisha

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanaharakati wamekuwa wakitoa wito kwa serikali kuingilia kati ili kupunguza gharama ya maisha mateso ya watu

Mabadiliko ya hivi punde katika Mswada wa Fedha, 2023, yakiidhinishwa na wabunge, huenda yakaongeza shinikizo la mfumko wa bei unaohisiwa na Wakenya kwani gharama ya juu ya maisha inapunguza uwezo wao wa kununua.

Tayari kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametishia kuitisha maandamano kwa kile alichokitaja kuwa "tsunami ya ushuru".

Mapema mwaka huu kiongozi huyo, aliongoza mfululizo wa maandamano ya kupinga serikali kuhusu gharama ya juu ya maisha mbali na madai mengine ya wizi wa kura katika uchaguzi wa mwaka jana.