Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zijue sababu za wanaume kufa mapema kuliko wanawake
- Author, Nick Triggle
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Dunia inaadhimisha Siku ya Afya leo ambapo kwa mujibu wa ripoti za Shirika la afya duniai inakadriwa kwamba karibu wanawake 300,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ujauzito au kujifungua, wakati zaidi ya watoto milioni 2 hufa katika mwezi wao wa kwanza wa maisha na karibu wengine milioni 2 zaidi huzaliwa wakiwa wamekufa. Hiyo ni takriban kifo 1 kinachoweza kuzuilika kwa kila sekunde 7.
Japo kuna hiyo idadi ya wanawake kufa na hiyo ya watoto lakini kuna hili kuhusu wanaume.
Mwezi huu serikali nchini Uingereza itazindua mpango juu ya afya ya wanaume. Wataalamu wanasema, hatua hiyo imechelewa kwa muda mrefu, na wanaume wana uwezekano mkubwa wa kufa kabla ya wakati wao kuliko wanawake.
Kuna changamoto juu ya afya ya wanaume - mchanganyiko wa tabia za hatari na ukosefu wa kujiamini na ujuzi wa kutafuta huduma za afya.
Vifo vya mapema
Huko Uingereza wanaume wana uwezekano mkubwa wa kuvuta sigara, kunywa pombe, kutumia dawa za kulevya na kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) na shinikizo la damu.
Mambo hayo huchangia kwa kiasi kikubwa, wanaume kufa mapema kuliko wanawake – ikielezwa kuwa hufa mapema kwa miaka minne kuliko wanawake. Pia wanaume wana uwezekano wa karibu 60% kufa kabla ya umri wa miaka 75 kutokana na ugonjwa wa moyo, saratani ya mapafu, ugonjwa wa ini na katika ajali.
Prof Alan White, ambaye alianzisha shirika la misaada la Men's Health Forum na kuanzisha kituo cha afya cha wanaume katika Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, anasema suala hili linahitaji kuchukuliwa kwa uzito zaidi.
Anatoa mfano wa janga la Covi 19, wanaume 19,000 zaidi ya wanawake walikufa kutokana na Covid.
Anasema ni rahisi kulaumu kwamba wanaume hawatunzi afya zao, kwa mtindo wao wa maisha, lakini anasema "ukweli wa mambo ni zaidi ya jambo hilo."
Prof White anasema: "Wanaume hawana ujuzi wa kutosha wa kushughulikia afya zao, hawazungumzi kuhusu afya na kuchukua hatua kulingana na dalili. Wengi hupita miaka bila kuona mtaalamu wa afya."
"Ni tofauti kwa wanawake. Hupata huduma ya uzazi wa mpango, hufanyiwa uchunguzi wa mlango wa kizazi na kuzaa kunamaanisha wanawake wengi wanawasiliana mara kwa mara na wahudumu wa afya kwa njia ambayo wanaume hawana."
Robo 3 ya wanaojiua ni wanaume
Mark Brooks, mshauri wa sera wa Kundi la Wabunge wa Vyama Vyote kuhusu Masuala ya Wanaume na Wavulana, anasema:
"Katika jamii tuna matarajio maalumu juu ya wanaume. Wanatakiwa wawe imara na kufanya mambo, kuwa na nguvu na ustahimilivu."
"Maisha ya wanaume katika maeneo maskini ni miaka 10 chini kuliko katika nchi tajiri - katika maeneo masikini wanaume wana uwezekano wa mara 3.5 zaidi kufa kabla ya umri wa miaka 75."
"Huwezi kupuuza utofauti wa majukumu linapokuja suala la kazi kama vile ujenzi na utengenezaji," anasema. "Jinsi huduma za afya zinavyoundwa hazifanyi kazi kwa wanaume."
"Mtu anayefanya kazi katika ujenzi au eneo la viwanda atapata shida sana kuchukua likizo iwe ni kwa uchunguzi wa afya au kwenda kumuona daktari."
Brooks angependa kuona wafanyakazi wakipewa haki ya mapumziko ya saa mbili ya kulipwa ili kwenda kupima afya zao na pia huduma za afya kutolewa katika maeneo ambayo wafanyakazi wameajiriwa, kama vile maeneo ya viwanda.
Anasema kuna tatizo pia la baadhi ya wanaume kuogopa kukabiliana na matatizo ya kiafya ambayo yanatokea katika miaka yao ya 40 na 50 - hupuuza dalili za mapema au kuficha magonjwa.
Anaongeza kuwa wasiwasi wa kukosa kazi na matatizo ya kifedha, pamoja na matatizo ya mahusiano, ni kichocheo kikubwa cha kuwepo kwa viwango vya juu vya kujiua vinavyotokea kwa wanaume. Robo tatu ya watu wanaojiua ni wanaume nchini Uingereza.
Tofauti za kikabila pia huchangia, anasema. Kwa mfano, wanaume weusi nchini Uingereza wana uwezekano maradufu wa kugunduliwa na saratani ya kibofu cha mkono, huku wanaume kutoka asili ya India au Bangladeshi wako katika hatari kubwa ya kupata kisukari.
Wanaume wanapenda afya zao?
Lakini haya yote hayamaanishi kwamba wanaume hawapendi afya zao, asema Prof Paul Galdas, mtaalam wa afya ya wanaume katika Chuo Kikuu cha York. "Wanaume wako tayari kuzungumza, lakini ili kufanya hivyo lazima hayo mazungumzo yawe kwenye msingi wa vitendo na shughuli."
"Shughuli hizo zinaweza kuwa ni kwenda matembezini, kuona marafiki, kucheza gofu na kuendeleza ujuzi wa kutatua matatizo ili kulinda afya ya akili. Afya bora ya akili huleta afya njema ya mwili."
Prof White anasema sasa ni wakati wa kujenga misingi hii –mkakati wa kitaifa wa afya ya wanaume ni muhimu. Lakini pia wanaume wenye waamke. Anasema kuna baadhi ya hatua rahisi kila mwanaume anapaswa kuzizingatia.
"Angalia ukubwa wa kiuno chako - ikiwa ni kikubwa, au ikiwa tumbo lako ni kubwa jaribu kufanya mazoezi. Toka nje zungumza na watu na fanya mazoezi.
"Chukua muda wako ili kupima afya yako au kuchunguzwa na daktari. Na, ukiona mabadiliko ya mwili au matatizo ya afya, tafuta usaidizi."