Vijidudu tumboni na vinywani mwetu: Siri ya usingizi bora?

Chanzo cha picha, Getty Images
Bakteria wanaoishi kwenye matumbo na midomo yetu huenda wanadhibiti jinsi tunavyolala usiku.
Sasa, wanasayansi wanapanga kuwatumia ili kutusaidia kulala vizuri zaidi.
Unapolala kitandani usiku huu, mwili wako utakuwa na shughuli nyingi.
Katika kila inchi ya mwili wako hata ndani mabilioni ya viumbe vidogo wanajongea na kusongamana wakigombea nafasi.
Lakini kama wazo hilo linakutisha kiasi cha kukukosesha usingizi, zingatia hili: viumbe hao huenda pia wakawa msaada wako wa kupata usingizi bora.
Utafiti unaochipuka unaonyesha kuwa jamii za bakteria, virusi na fangasi (microbiota) walioko katika miili yetu wanaweza kuathiri usingizi wetu.
Kulingana na muundo wa mfumo huu wa viumbe hai kwa kila mtu, usingizi unaweza kuwa bora au kudhoofika.
Cha kuvutia zaidi, uelewa huu unaweza kufungua njia mpya za kushughulikia matatizo ya usingizi yanayosababishwa na kuvurugika kwa saa ya mwili ambayo kitaalamu huitwa circadian rhythms.
Ingawa watu wengi kwa sasa hutegemea dawa za usingizi kudhibiti usingizi sugu, huenda siku zijazo bakteria rafiki wakatumika kusaidia watu kulala, hata kutibu (obstructive sleep apnoea) hali ambapo kupumua hukatizwa wakati wa usingizi.
Hii italeta maana mpya kwa dhana ya "usafi wa usingizi."
"Kwa muda mrefu, dhana kuu imekuwa kwamba matatizo ya usingizi huvuruga microbiome zetu," anasema Profesa Jennifer Martin kutoka Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, na mjumbe wa bodi ya American Academy of Sleep Medicine.
"Lakini sasa kuna ushahidi unaoonyesha kwamba uhusiano huu huenda ni wa pande mbili."
Mnamo Mei, utafiti mpya uliowasilishwa katika kongamano la wanasayansi wa usingizi ulifupisha kile ambacho tafiti mbalimbali zimeanza kugundua: kwamba vijana na watu wazima wachanga wenye utofauti mkubwa wa bakteria midomoni walipata usingizi wa muda mrefu zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Utafiti pia unaonyesha kuwa watu wenye tatizo la usingizi lililothibitishwa kitaalamu wana utofauti mdogo wa bakteria tumboni ikilinganishwa na wanaolala vizuri.
Hali hii huashiria kinga dhaifu ya mwili na matatizo katika uchakataji wa mafuta na sukari, hali inayoweza kuongeza hatari ya kisukari, unene uliopitiliza, na maradhi ya moyo.
Utafiti mwingine uliowashirikisha watu 40 waliovaa vifaa vya kupima usingizi kwa mwezi mmoja huku microbiome zao zikichunguzwa, ulibaini kwamba kutopata usingizi ulihusishwa na upungufu wa utofauti wa bakteria wa utumbo.
Aidha, watu waliokuwa na tofauti kubwa kati ya ratiba zao za usingizi kati ya siku za kazi na wikendi, hali ijulikanayo kama social jetlag, walionekana kuwa na microbiome tofauti kabisa na wale waliokuwa na ratiba thabiti ya usingizi, kwa mujibu wa uchambuzi wa kampuni ya afya ya teknolojia ya Zoe nchini Uingereza.
"Midundo ya circadian huvurugika kwa watu wanaolala kwa kuchelewa na kulala wikendi, wanaofanya kazi kwa muda mrefu kama vile maafisa wa usalama, wahudumu wa afya wa dharura, wanajeshi, au wale wanaokula chakula karibu na muda wa kulala," anasema Profesa Kenneth Wright kutoka Chuo Kikuu cha Colorado Boulder.
"Hii inaweza kusababisha matatizo ya mmeng'enyo wa chakula na magonjwa ya kimetaboliki, ambayo ni ya kawaida miongoni mwa wafanyakazi wa zamu, na microbiome iliyovurugika inaweza kuchangia hayo yote."
Inawezekana pia kuwa watu wenye usingizi wa mang'amung'amu hufuata lishe duni, jambo linaloweza kuathiri microbiome zao, anasema Profesa Sarah Berry wa Chuo cha King's College London na mwanasayansi mkuu wa Zoe.
Anataja utafiti mwingine unaoonyesha kuwa watu wanaolala kwa muda mfupi huongeza ulaji wao wa sukari bila kujitambua.
"Sehemu ya nadharia ni kwamba ukipata usingizi wa mang'amung'amu, vituo vya ridhaa kwenye ubongo wako huongezeka shughuli, na hivyo unatafuta 'tiba ya haraka'," anasema. "Ubongo wako unakushawishi kutaka wanga rahisi ili upate nguvu za haraka."
Lakini mabadiliko ya lishe si sehemu pekee ya tatizo.
Berry na wenzake walibaini spishi tisa za bakteria zilizoongezeka na spishi nane zilizopungua miongoni mwa watu wenye mishemishe nyingi kwa siku.
Hata hivyo, lishe ilieleza mabadiliko ya spishi nne pekee kati ya hizo.
Profesa Jaime Tartar wa Saikolojia na Neurosayansi kutoka Chuo Kikuu cha Nova Southeastern, Florida, ambaye hakuhusika katika utafiti wa Zoe, anasema anazidi kushawishika kuwa baadhi ya bakteria huathiri moja kwa moja usingizi.
Anataja kundi la Firmicutes, mojawapo ya makundi makuu ya bakteria tumboni.
Katika utafiti alioufanya kwa wanaume 40, waligundua makundi 15 tofauti ya Firmicutes yaliyoonyesha uhusiano na viwango mbalimbali vya usingizi.
"Hatuna majibu yote kwa sasa, lakini inaonekana kuwa baadhi huimarisha usingizi na mengine huuvuruga," anasema.
Katika baadhi ya visa, usingizi usio wa kutosha unaweza kusababisha mabadiliko ya microbiome kupitia kudhoofisha kinga ya mwili, jambo linaloweza kupelekea matatizo ya usingizi wa muda mrefu.
Hata hivyo, watafiti kama Martin na Tartar wanaamini kuwa baadhi ya matatizo ya usingizi huweza pia kusababishwa na kutokuwa na usawa wa bakteria tumboni au mdomoni.
Wanaamini baadhi ya bakteria huathiri ubora wa usingizi kwa kuingilia midundo ya mwili na kudhibiti kiwango cha ulaji wa chakula mambo yote yanayohusiana na usingizi.
Ushahidi kwa hili unatokana na mfululizo wa tafiti kuhusu upandikizaji wa kinyesi.
Katika utafiti mmoja wa 2024, wanasayansi walipandikiza kinyesi chenye bakteria kutoka kwa binadamu kwenda kwa panya.
Panya waliopokea kinyesi kutoka kwa watu wenye shughuli nyingi kwa siku na wanaokosa usingizi walionyesha tabia za kukosa usingizi, wakibaki macho zaidi katika saa zao za kawaida za kulala.
Katika utafiti mwingine, panya waliopokea bakteria kutoka kwa binadamu katika awamu mbalimbali za shughuli walionyesha ongezeko la uzito na matatizo ya kudhibiti sukari.
Tafiti ndogo kutoka China zimeonyesha kuwa upandikizaji wa kinyesi unaweza kusaidia wagonjwa wenye matatizo sugu ya usingizi.
Hata hivyo, watafiti wanasema utafiti wa kitabibu wa kisayansi (randomised, double-blind clinical trial) unahitajika kuthibitisha matokeo hayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lishe pia inaathiri sana usingizi.
Wanaume 15 walipopewa lishe yenye mafuta na sukari nyingi kwa wiki moja, walionyesha mabadiliko katika shughuli za umeme za ubongo wakati wa usingizi mzito (deep sleep), ingawa ukubwa mdogo wa kundi hilo haufanyi iwe rahisi kutoa hitimisho thabiti.
Vilevile, utafiti mwingine uliohusisha watu waliotumia antibiotiki ulionyesha kupungua kwa usingizi wa aina ya non-REM, kipindi muhimu ambapo mwili hujijenga upya na kuimarisha kumbukumbu, ingawa matokeo haya hayakuhusu aina zote za antibiotiki.
Mabadiliko ya uwiano wa bakteria tumboni yanaweza pia kubadilisha kiasi cha kemikali wanazozalisha wanaposaidia kumeng'enya chakula, jambo linaloweza kuathiri ubora wa usingizi, anasema Tartar.
Tunajua kwamba baadhi ya bakteria wa utumbo huzalisha viambajengo vya neva kama gamma-aminobutyric acid (GABA), dopamini, norepinephrine, serotonini, pamoja na asidi fupi kama butyrate—vyote vina nafasi katika usingizi.
"Ingawa hutengenezwa tumboni, vinaweza kuathiri ubongo," anasema Tartar.
Iwapo viumbe hawa hupungua, athari zao kwenye ubongo pia hupungua.
Kwa upande mwingine, bakteria wanaotumia mafuta yaliyo na sukari ili kuunganisha molekuli za uchochezi zinaweza kuongezeka.
Baadhi ya kemikali hizi za kichochezi, ikiwa ni pamoja na asidi fulani ya nyongo, zinadhaniwa kuwa na uwezo wa kutatiza midundo ya ubongo yaani circadian rhythm.
Martin anasema vivyo hivyo vinaweza kuwa kweli kwa vidudu vidogo vya mdomo.
"Iwapo vijidudu hai vya mwili haina uwiano, hali hiyo inaweza kusababisha uvimbe wa ndani na wa mwili mzima, jambo linaloweza kusababisha njia ya hewa kuwa nyembamba, kuongezeka kwa homoni za msongo wa mawazo, pamoja na athari nyingine nyingi zinazoweza kuvuruga usingizi kwa muda mrefu," anasema Profesa Martin.
Njia ya hewa inapozibwa au kupungua upana wake, husababisha matatizo kama vile kuzuiwa kwa usingizi na kukoroma.
Tunajua pia kuwa bakteria wa utumbo huzalisha viambajengo vya neva (neurotransmitters) vinavyohusika moja kwa moja na mchakato wa usingizi.
Kwa kuzingatia haya yote, kuna uwezekano kwamba probiotic (tembe zenye aina mahususi ya bakteria hai) au prebiotic (viambato vya chakula visivyomeng'enywa vinavyolisha bakteria wazuri tumboni) vinaweza kutumika kutibu baadhi ya matatizo ya usingizi.
Profesa Tartar anarejelea utafiti mmoja ulioonyesha kuwa probiotic ya aina ya Lactobacillus casei Shirota iliboresha usingizi kwa wanafunzi 94 wa udaktari waliokuwa katika kipindi kigumu cha kitaaluma, ikilinganishwa na dawa ya kutuliza.
Jinsi utafiti ulivyofanywa
Kwa upande wake, Profesa Sarah Berry anasema kuwa kampuni ya Zoe imekamilisha hivi karibuni utafiti wa wiki sita uitwao BIOME study, uliowahusisha watu 399 wenye afya kutoka Uingereza.
Utafiti huo (ambao bado unakaguliwa na wataalamu wengine) ulihusisha makundi matatu ya washiriki waliopokea aina tofauti za vyakula:
Kundi la kwanza lilipatiwa mchanganyiko wa prebiotic ulioitwa "nishati bora kwa microbiome", uliokuwa na zaidi ya viambato 30 vya vyakula asilia kama vile matunda ya baobabu na uyoga wa aina ya lion's mane.
Kundi la pili lilipokea probiotic ya kila siku yenye bakteria Lactobacillus rhamnosus.
Kundi la tatu (kundi udhibiti) lilipatiwa vipande vya mkate vilivyokaushwa (croutons) vyenye kiasi sawa cha kalori kama mchanganyiko wa prebiotic.
Ikilinganishwa na kundi la croutons, idadi kubwa zaidi ya waliotumia mchanganyiko wa prebiotic waliripoti kuwa usingizi wao umeboreshwa.
Hata hivyo, matokeo haya yalitokana na ripoti binafsi za washiriki badala ya vipimo vya moja kwa moja.
Tiba iliyopendekezwa
Ingawa Profesa Martin anavutiwa na matokeo hayo, anasisitiza umuhimu wa tafiti kubwa zaidi na za kudhibitiwa vizuri, ambazo zitalinganisha athari za prebiotic na probiotic na tiba zilizokwisha kuthibitishwa kuwa na mafanikio katika kutibu matatizo ya usingizi.
Miongoni mwa tiba hizo ni:
- Tiba ya kitabia ya utambuzi (Cognitive Behavioural Therapy – CBT)
- Dawa mbalimbali zinazotumika kitabibu
"Mimi huwa mwangalifu sana kupendekeza mtu kutumia dola 30 (takribani pauni 22) kununua bidhaa za afya ambazo bado hazijathibitishwa kitaalamu, ilhali tunajua kuna tiba za kisayansi zilizothibitishwa kufanya kazi," anasisitiza Martin.
Hata hivyo, anafurahia wazo la kuchunguza iwapo probiotics zinaweza kuwasaidia watu wenye hali nyepesi ya kukosa usingizi, pengine kwa kuchanganywa na vifaa maalum vya mdomoni vinavyosogeza taya ili kusaidia kupunguza tatizo la kupumua wakati wa usingizi.
Kwa kuwa takribani asilimia 20 hadi 30 ya watu wanaosumbuliwa na kukosa usingizi hawajibu ipasavyo kwa tiba ya CBT, Martin anajiuliza kama probiotic au prebiotic zinaweza kuwasaidia.
"Ningependa sana kuona tafiti zinazolenga kundi hilo la wagonjwa," anasema. "Katika taaluma ya tiba ya usingizi, tunakabiliana na changamoto kubwa ya kuwasaidia watu hawa, wengi wao wakiwa hawapendi kutumia dawa zinazowalaza."
Lakini iwapo sayansi ya vijidudu vidogo itathibitika kuwa na athari ya moja kwa moja kwa ubora wa usingizi, basi hiyo inaweza kuwa habari njema kwa watu wa aina mbalimbali.
"Uvunjifu wa mdundo wa moyo circadian ni jambo la kawaida sana katika jamii ya sasa," anasema Profesa Wright.
"Huenda kutokana na kuongezeka kwa uchovu baada ya safari za anga (jetlag), kazi zenye ratiba zisizo za kawaida, mitindo ya maisha ya kisasa, au magonjwa yanayohusiana na umri. Kwa hivyo, watu wengi wanaweza kufaidika na matibabu yatokanayo na vijidudu hai vidogo."
Kwa hakika, huu unaweza kuwa mtazamo mpya kabisa kuhusu wadudu wa kitandani.















