Korea Kusini: Kwa nini wengi wanatatizika kulala?

Chanzo cha picha, Getty Images
Korea Kusini ni moja ya nchi ambayo inakabiliwa na tatizo la kulala duniani, hali ambayo imeendelea kuathiri watu wake.
Ji-Eun alianza kutatatizika kulala wakati alipozidiwa na kazi kiasi cha kukosa muda wa kupumzika.
Kwa wastani alifanya kazi kutoka saa moja asubuhi hadi karibu saa nne usiku na alikuwa na shughuli nyingi kila siku. Wakati mwingine afisa huyo wa uhusiano mwema mwenye umri wa miaka 29-alijipata ofisini hadi saa tisa usiku.
Bosi wake mara kwa mara anampigia simu usiku wa manane kuomba amfanyie kazi ya dharura muda huo.
"Ilikuwa kama nimesahau jinsi ya kupumzika," anasema.
Katika kliniki ya Dream Sleep iliyopo wilaya ya Gangnam mjini Seoul, Dkt Ji-hyeon Lee, mtaalamu wa magonjwa ya akili aliyejikita katika masuala ya usingizi, anasema mara nyingi anakutana na wateja ambao wanameza hadi tembe 20 za dawa za usingizi kwa usiku mmoja.
"Huwa inachukua muda kidogo mtu kupata usingizi na kulala, rea wanataka kulala haraka kwa hivyo wanatafuta tiba," anasema.
Uraibu wa kutumia dawa za kulala ni janga la kutaifa. Hakuna takwimu rasmi lakini inakadiriwa kuwa Wakorea 100,000 wameathirika na dawa za usingizi.
Kando na kutatizika kulala baadhi yao huamua kunywa pombe wakiwa wametumia dawa- na matokeo ni hatari.

''Watu wanatembea wakiwa usingizini. Wanaenda kwenye jokofu na kula vitu vingi bila kujua, ikiwa ni pamoja na vyakula vibichi,'' Dkt Lee anasema. ''Kulikuwa na hata visa vya ajali za barabrani katikati mwa Seoul zilizosababishwa na mgonjwa aliyekuwa akitembea akiwa usingizini.''
Dk Lee amezoea kuona watu ambao wamekosa usingizi kwa muda mrefu wakisumbuliwa na kile kinachojulikana kama hypo-arousal. Baadhi ya wagonjwa wake wanamwambia imekuwa miongo kadhaa tangu wamelala kwa zaidi ya saa chache usiku.
''Wanalia [lakini] bado wanapata matumaini [wanapokuja hapa]. Ni hali ya kusikitisha sana,'' anasema.
Kufanya kazi kupita kiasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi
Korea Kusini ni mojawapo ya mataifa yanayokosa usingizi duniani. Pia ina kiwango cha juu zaidi cha visa vya watu kujitoa uhai miongoni mwa mataifa yaliyoendelea, unywaji wa juu zaidi wa pombe kali na idadi kubwa ya watu wanaotumia dawa za kudhibiti mfadhaiko.
Kuna sababu za kihistoria za takwimu hizi.
Katika miongo michache tu nchi hiyo imetoka kuwa mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani hadi kuwa mojawapo ya mataifa yaliyoendelea sana kiteknolojia duniani. Pia ina nguvu nyingi laini, na ushawishi wake unaokua kwenye utamaduni wa pop.
Mataifa yaliyo na mwelekeo kama huo, kama Saudi Arabia na UAE, yanaweza kutumia rasilimali zao za asili, lakini Korea haina utajiri kama huo uliofichwa. Ilijiendeleza kutokana na ari ya kujitolea kwa watu wake na utaifa wa pamoja unaowasukuma kufanya kazi kwa bidii na haraka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tokeo moja ni kwamba watu wake wanafanya kazi kupita kiasi, wana msongo wa mawazo na kukosa usingizi.
Sasa, tasnia nzima imekua ikihudumia wale ambao hawawezi kulala - na tasnia ya kulala inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola bilioni 2.5 mnamo 2019.
Sekta ya misaada ya usingizi inayoendelea
Mjini Seoul, maduka makubwa yamejitolea kuuza bidhaa za kulala, kuanzia mashuka mazuri hadi mto bora, wakati maduka ya dawa hutoa rafu zilizojaa dawa za kulala hadi za mitishamba.
Pia kuna mbinu za kiteknolojia za kukabiliana na tatizo kukosa usingizi. Zaidi ya miaka miwili iliyopita Daniel Tudor alianzisha programu ya kutafakari - Kokkiri - iliyolenga kuwasaidia vijana wa Korea waliofadhaika.
Ingawa Korea ni nchi ya Kibudha kihistoria, vijana hufikiria kutafakari kama tafrija ya wazee, si jambo ambalo mfanyakazi wa ofisini huko Seoul anaweza kufanya. Daniel anasema ilimbidi kuagiza tena na kupanga upya kutafakari kama wazo la Magharibi ambalo halitawavutia vijana wa Korea.
Taasisi zaidi za kitamaduni pia zimejiunga na mkakati huo.
Hyerang Sunim ni mtawa wa Kibudha ambaye husaidia kuendesha mahali pa kuishi mjini Seoul ambapo wasio na usingizi wanaweza kushiriki katika kutafakari na kupata mafundisho ya Kibudha.

Hapo awali aina hizi za mapumziko madogo zilitolewa kwa wastaafu ambao walitaka mafundisho na maombi. Sasa washiriki wanaelekea kuwa Wakorea wadogo, waliotimiza umri wa kufanya kazi. Lakini mahekalu haya ya Kibudha pia yamekosolewa kwa kujinufaisha kutokana na warsha kama hizo.
''Bila shaka kuna wasiwasi… lakini nadhani manufaa yanazidi,'' alisema Hyerang Sunim.
''Kijadi imekuwa nadra kuona vijana wakija na kutafuta mafundisho ya Kibudha. Na wanapata mengi kutokana na mwingiliano wao na kukaa hekaluni.''
Haja ya mabadiliko ya kimsingi
Lee Hye-ri, ambaye alihudhuria warsha kama hiyo ya Wabudha baada ya shinikizo za kazini kuwa nyingi, anasema amejifunza kuwajibika kwa ajili ya mfadhaiko wake.
''Kila kitu kinaanzia kwangu, matatizo yote yanaanzia kwangu. Ndicho nilichojifunza hapa.''
Lakini kufikia suluhisho la mfadhaiko na kukosa usingizi kama jambo la kushughulikia kibinafsi kunaweza kuwa tatizo.
Wale wanaoamini kuwa tatizo linasababishwa na utamaduni wa kufanya kazi usio kupita kiasa na shinikizo za kijamii wamekosoa mbinu hii ya ubinafsi wakisema ni sawa na kulaumu waathiriwa. Wakosoaji hawa wanasema kutafakari au kupumzika ni plasta inayonata na kwamba suluhu za kweli zinaweza tu kpatikana kupitia mabadiliko ya kimsingi kwa jamii.
Ji-Eun hatimaye alikosa usingizi hadi akaamua kuacha kazi. Siku hizi anafanya kazi kwa saa zinazohitajika zaidi kama mfanyakazi huru kumaanisha kuwa anaweza kufanya kazi nyumbani. Pia ametafuta usaidizi wa kitaalamu katika kliniki ya usingizi ya Dr Lee ili kudhibiti hali yake ya kukosa usingizi.













