Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC:'Naumia ninapolinganishwa na mtoto' - Dorah
Na Anne Ngugi
BBC Swahili
Wanswekula Zacharia ndio jina halisi la msanii ambaye anajulikana na wengi nchini Tanzania kama Miss Dora .
Mwaka huu ametimiza miaka 27 na kwake yeye anasema kwamba ni muujiza kwamba yuko hai mpaka leo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Seli Mundu ama Sicke cell katika maisha yake ya utotoni , na hadi sasa anaishi na makovu ya ugonjwa huo .
”Nilipoanza kufahamu maisha nilijikuta kwamba sikuwa nakuwa kwa kimo kama watoto wengine , na hadi sasa muonekano wangu unaoneka nina mwili mdogo sana kuliko wanawake wa kawaida wa rika langu , Ila nimekubali jinsi nilivyo na ninajidhatiti kila siku kuyaishi maisha yangu kimamililifu”anasema Dorah .
Dorah ameshiriki michezo mIngi ya tamthilia nchini Tanzania ikiwemo Kapuni na Juakali iliyozidi kumpa umaarufu.
Katika tamthilia ya Juakali, Dorah anasema kwamba alikubali, kuigiza katika nafasi ambayo inagusia maisha yake angalau kwa kiasi fulani ili kudhihirishia ulimwengu mateso aliyopitia, kutengwa na kunyanyapaliwa.
”Kwa kweli sioni shida ikiwa watu wanaweza kujifunza kupitia maisha yangu halisi , kwani ninaamini kwamba itamuelimisha na kumpa matumaini angalau mtu mmoja ”anasema Dorah
Maisha ya Dorah
Dorah alizaliwa huko Singida nchini Tanzania , yeye ni mtoto wa pili kati ya watoto sita .
Mwanadada huyu anasema kwamba wakati anakua maisha hayakuwa mepesi kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo.
Wakati huo tayari alikuwa ameanza kuugua hali ambayo hawakujua kwamba ilikuwa ni ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell), ugonjwa ambao huathiri mfumo wa kinga na inakuwa rahisi mtu kuandamwa na magonjwa mbalimbali katika mwili kutokana na kukosa kinga dhabiti ya kujilinda.
Kwa mujibu wa Dorah, historia yake inavitu vingi na pia inahusu watu wengi ambao wamemlea na kumsaidia kufika alipo.
”Nilichukuliwa nikiwa binti wa miaka 8 na mtawa mmoja aliyekuja nyumbani kwetu kututembelea, baada ya kuona hali sio hali, wakaamua kunipeleka katika makazi ya watoto ambako nilianza masomo yangu na pia kuendelea kupewa huduma za matibabu kutokana na hali yangu”, anasema Dorah.
Aliendelea na masomo yake , huku akipewa matibabu , kulingana na msanii huyu alikuwa ameshauriwa na wataalam wa matibabu yake kwamba hali ya ugonjwa huo wa Seli mundu ingekwisha atakapokuwa mtu mzima .
Japo alipata wasamaria wema ambao walitembea naye katika kuhakikisha kwamba amepata matibabu na hali kadhalika amepata masomo anasema kwamba barabara ya kuishi maisha kwa muonekano alionao haikuwa rahisi , hasa kwa kuwa wengi ni wale ambao walimnyanyapaa licha ya miaka kusonga Dorah aliendelea kuwa na muonekano wa ‘kitoto’ na hilo lilimkosesha usingizi kwa miaka mingi.
Mwanamke huyu anasimulia siku zilizojawa na kiza kikuu ambapo baadhi ya watu katika jamii yake na hata watu waliokuwa karibu naye walimpa machungu mengi kwa kutumia muonekano wake kumdhalilisha .
”Hakuna mtu angependa kuwa tofauti na mwingine , sote tunatamani tuwe sawa kwa hivyo inauma kila wakati baadhi ya watu wakinilinganisha na mtoto , inauma sana kwa sababu nina akili za utu uzima na nina haki kama mwanamke mwengine yule ”Dorah alisema.
Ila siku zilivyozidi kwenda akajiunga na chuo kimoja kusomea uanahabari aliamua kupiga moyo konde na kukubali hatma yake kwamba huenda atakua kama wenzake
Seli Mundu ni ugonjwa gani?
Msanii huyu pia aligusia maisha yake ya mahusiano hasa ya kimapenzi na anasema kwamba yuko kwenye mahusiano ya kimapenzi ila hataki kuzungumzia zaidi ya hayo.
’Mwisho wa siku mimi ni mwanamke , anachotaka mwanamke mwingine mwenye umbo la kawaida hata mimi natamani, nina haki ya kuwa na mpenzi, kuheshimika, kwa hiyo inauma wakati mtu anatumia maumbile yangu kunidhalilisha na kuniumiza ila mwisho wa siku lazima niishi ”Dorah anasema.
Anasema kwamba watu wengine walitumia maumbile yake kumuona kituko na kwamba yeye akautumia muonekano huo huo kuigiza kwenye michezo ya tamthilia katika hali ya kuelimisha jamii , kwa kuwa anafahamu watu wengi ambao wanaishi na ulemavu mbali mbali wa kimwili huenda wanajikuta kwenye njia panda kutokana na unyanyapaa na kudhaniwa visivyo kila walipo.
”Huwa sipendi kukumbuka mbali, hata kwa ndugu zangu nikikumbuka walivyoninyooshea vidole za laana na pia waliniumiza kwa kuniita kituko, ni mengi (ya kuumiza nimepitia) ila acha tuishie hapo ”anasema Dorah.
Kwa sasa mwanadada huyu anatumia maumbile yake na kipaji chake sio tu katika uigizaji bali pia kutoa nasaha na kuwa kielelezo chema kwa watoto ambao wanazaliwa na mapungufu ya kimwili.
”Nitaelimisha watu , nitaonyesha watu kwamba binadamu aliyeumbwa na mwenyezi mungu anauwezo wa kukubadilisha kwa mfano kunyanyapaliwa na jamii na wengi, lakini leo hii Dorah amesimama na amekuwa kama kioo katika jamii licha ya changamoto nyingi tu ” .
Kwa mujibu wa wataalam wa maswala ya Damu Seli Mundu ni tatizo la chembechembe nyekundu za damu la kurithi ambapo kunakuwa na upungufu wa chembechembe hizo za damu kwa ajili ya kusafirisha oksijeni kuzunguka mwili mzima.
Kwa kawaidi, seli nyekundu za damu zenye uwezo wa kunyumbuka husafiri kiurahisi ndani ya mishipa ya damu.
Mgonjwa wa Seli Mundu huwa na seli nyekundu zenye umbo la mwezi mchanga.
Seli hizi ngumu , zinazonata huweza kuziba mishipa midogo ya damu, hali ambayo huweza kusababisha damu kwenda polepole au kuziba mtiririko wa damu na oksijeni kuelekea sehemu nyingine za mwili.
Hakuna dawa kamili kwa wagonjwa wengi wa Seli Mundu. Lakini tiba hutolewa ili kupunguza maumivu na kuzuia madhara yanayoweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa huu.
Dalili za Seli Mundu
Dalili za Seli Mundu huanza kuonekana mtoto akiwa na umri wa miezi mitano. Dalili huwa tofauti kwa watu tofauti na hubadilika na wakati. Dalili kubwa ni pamoja na upungufu wa damu mwilini. Mgonjwa pia kuwa seli nyekundu chache.
Kwa kawaida seli nyekundu huishi kwa siku 120 kabla ya kuhitaji kubadilishwa. Lakini seli za mgonjwa wa Seli Mundu huishi kwa siku 10 hadi 20, na kuacha pengo la seli nyekundu.
Bila ya kuwa na kiwango kizuri cha seli nyekundu, mwili haupati oksijeni ya kutosha hali ambayo husababisha uchovu wa mwili.
Kuchelewa kukua na pia kuchelewa kubalehe. Chembechembe nyekundu za damu huupa mwili oksijeni na virutubishi muhimu kwa ukuaji. Upungufu wa seli hizo huweza kusababisha ukuaji wa taratibu kwa watoto wadogo na kuchelewesha balehe kwa vijana.
Kupata vipindi vya Maumivu vya kujirudia mara kwa mara ni dalilili kuu ya ugonjwa huu. Maumivu hutokea wakati seli nyekundu za damu zinapoziba mtiririko wa damu kwenye mishipa midogo ndani ya kifua, tumbo na viungo. Maumivu huweza kutokea vile vile ndani ya mifupa.Maumuvu ya kupindukia huhitaji uangalizi hospitalini.
Kuvimba pia mikono na miguu kunakotokana na seli kuziba damu isifike kwenye mikono na migu pamoja na kupata maambukizi pia ya kila wakati, matatizo ya kuona.