Waridi wa BBC: Ulemavu ulivyopokonya ndoa yake kwa miaka 20

Jina la Stella Joel mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Tanzania , limepata umaarufu mkubwa nchini humo mapema mwaka huu mara tu baada ya mwanamuziki huyo kufunga ndoa na mume wake Dr. Frank Richard.

Harusi hiyo ilizua gumzo mtandaoni baada ya kufungwa katika mbuga ya wanyama huko Manyara.

Wengine walihoji usalama wa wageni dhidi ya wanyama, wengine walihoji gharama na mambo mengine mengi ambayo hawakuyataria kwa harusi kufanyika mbugani.

Si jambo la kawaida na inawezekana ilikuwa ni mara ya kwanza kwa baadhi ya watu kusikia au kushuhudia harusi ikifanyika katika mbuga ya wanyama.

Lakini ukiachia mbali shughuli ya harusi ya harusi ilivyostaajabisha, wengine walihoji kuhusu historia ya mapenzi yao,utofauti wa umri kuwa mwanamke ni mkubwa kuliko mwanaume na suala la mmoja kuwa mlemavu.

Ingawa uhalisia ni kwamba Stella ni mdogo kuliko mume wake, yeye ana miaka 48 , na mume wake anakaribia kufika 56.

Bi Stella amekuwa akiishi na ulemavu takriban miaka tisa huku hali hiyo ikiwa ni kizuizi kikuu kwa mengi, ikiwemo kuolewa wakati alikuwa bado ni binti mdogo.

"Nilipata ajali mbaya ya gari wakati nilipokuwa naelekea shuleni mkoani moshi ,ajali hiyo iliyotokea eneo la Dodoma ilisababisha mabadiliko makubwa katika maisha yangu .Nilipoteza uwezo wa kutembea baada ya miguu yangu miwili kuvunjika"anakumbuka Stella

Baada ya hapo msanii huyu anaeleza changamoto nyingi alikutana nazo wakati anatafuta tiba , anasema kwamba kwa miaka tisa aliyoishi akiwa anatembea kwa magongo na wakati mwengine gari la magurudumu mawili alilazwa katika hospitali tofauti kuanzia Bukoba , Dodoma na Dar es salam.

Licha ya kwamba alikuwa ana changamoto ya kutembea, Stella anasema kwamba alikuwa ni mwimbaji katika kanisa moja , na alikutana na Dr.Frank wakati wakiwa ni vijana wakiimba kwaya pamoja.

Mapenzi yao yalianzia hapo licha ya kwamba Stella anasema kwamba hakuwa na ukakamavu wa kujihisi kama mwanamke ambaye angependwa au kupendeka .

"Ajali ilibadilisha taswira ya maisha yangu sana , licha ya kwamba niliendelea kuwa na imani kwamba siku mmoja ningetembea , ukakamavu wangu kama kijana wa kike haukuepo .Kwa hiyo hata wakati tunaanza mahusiano na mume wangu nilikuwa sijajikubali kabisa "anasema Stella

Stella anakiri kwamba uhusiano wake wa kimapenzi na mume wake ulivunjika baada ya yeye kushika mimba ila hakuwa na ujasiri wa kumueleza wakati huo .

Waliachana wakati Stella akiwa na miaka 26 na hawakuonana tena , Mwanamke huyu alijifungua mtoto na kumlea bila ya kumjulisha mume wake kuhusiana na hayo .

Mwanamke huyu anakiri kwamba kwa upande wa mume wake ; ndugu, jamaa na marafiki walimshawishi dhidi kuachana naye kutokana na ulemavu wake , aidha anasema kwamba aliona kana kwamba mume wake wakati huo alisikiliza na uhusiano huo ukavunjika.

"Unajua kuna watu ambao walikuwa wanafahamu kwamba tulikuwa pamoja , wakati huo nilikuwa naishi kama mlemavu , na bila shaka unyanyapaa ulikuweko kuhusiana na hali yangu.

Mume wangu alikubali kusikiliza maoni ya watu , lakini siwezi kumlaumu kwani sasa tuko pamoja ,"anasema Stella.

Stella aliendelea na malezi ya mtoto wake na baadaye alipata ujauzito kwenye uhusiano mengine ambao ulivunjika pia.

Mwaka wa 1990 ndipo ulemavu wake wa miguu ulipotea na akaanza kutembea tena asiwe na habari kwamba Dr.Frank alikuwa ameanza kumtafuta tena akiwa na lengo la kumshawishi wafunge ndoa.

Bi.Stella anasema miaka miwili iliyopita walikutana tena kwa mara ya kwanza baada ya miaka 26 ya kutoonana wala kuzungumza, Stella alikuwa akilea mtoto wao pekee yake , huku mume wake akiwa hana habari kuhusiana na kwamba mahusiano yao ya miaka iliyopita walipata mtoto .

Wakati walikutana , mwaka wa 2020 Mume wake alimueleza kuwa alitamani waishi pamoja kama mume na mke , ni wakati huo pia Stella alimweleza kuhusu ujauzito alioupata wakati walipokuwa na uhusiano kipindi wako vijana .

Na hatimaye Stella Joel , na Dr. Frank Richard walifunga pingu za maisha mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka huu 2022 .

Sherehe za ndoa yao zilikuwa za aina ya kipekee iliyofungwa katika hifadhi ya wanyama huko Manyara Tanzania

Aidha Stella anasema alitamani sherehe ya kipekee ambayo ingetangaza nchi yake ndio maana aliamua kufanyia sherehe yao katika hifadhi ya taifa ya ziwa Manyara .