Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu ugonjwa wa preeclampsia ambao umewashangaza wanasayansi
Hali hii husababisha vifo vya akina mama zaidi ya 70,000 kila mwaka, lakini sababu zake bado ni kitendawili kwa wanasayansi.
Baada ya maisha mazuri ya riadha ambayo yalimfanya ashinde medali saba za dhahabu za Olimpiki na medali 14 za dhahabu za ubingwa wa dunia, Allyson Felix alifikiri ujauzito ungekuwa rahisi kama ilivyo kawaida katika riadha.
"Maisha yangu yote, nimeutunza mwili wangu na kuutegemea kwa kila kitu na haujawahi kuniangusha," Felix alisema. "Nimejifunza mengi na kila mara niliuliza mengi. Kwa hivyo nilidhani ningeweza kuzaa mtoto mzuri wa asili na nikachagua njia ya kulala usingizi.
Lakini wakati wa uchunguzi wa kawaida akiwa na ujauzito wa wiki 32, Felix alipatwa na mshtuko alipopata habari kwamba alikuwa na preeclampsia kali, matatizo ya ujauzito ambayo husababisha shinikizo la damu na uharibifu wa viungo vya ndani, na alihitaji kulazwa hospitalini mara moja.
Siku iliyofuata, madaktari walimfanyia upasuaji wa dharura na binti yake, Cameron, alizaliwa miezi miwili kabla ya wakati wake, akitumia mwezi wa kwanza wa maisha yake katika kitengo cha wagonjwa mahututi wa watoto wachanga.
Hadi wakati huo, hakukuwa na dalili zozote za matatizo ya afya yanayohatarisha maisha kwa Felix au mtoto wake, isipokuwa uvimbe fulani kwenye miguu yake.
"Haikunisumbua hata kidogo, lakini niligundua kwamba nilikuwa nikipoteza protini na nikaanza kuwa na matatizo ya shinikizo la damu," mama huyo alisema. “Ilikuwa inatisha. Lakini hatimaye familia yetu ilirudi nyumbani.
Ingawa Cameron sasa ni mtoto mwenye afya njema mwenye umri wa miaka mitano, Felix anafahamu vyema kwamba kuna hadithi kama zake, lakini ziliishia kuwa janga.
Mnamo Aprili 2023, mchezaji mwenzake Tori Bowie, bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 100 na mshindi wa medali ya dhahabu ya kupokezana vijiti katika Olimpiki ya Rio 2016, alifariki wakati wa kujifungua kutokana na matatizo yanayohusiana na preeclampsia alipokuwa na umri wa miaka 32 pekee.
"Tulikuwa kwenye timu kadhaa za kupokezana vijiti pamoja. Tulishindana katika mbio kadhaa, na kifo chake kilikuwa cha kushangaza sana," mwanariadha huyo alisema, na kuongeza kuwa "ilisikitisha sana kwa mtu ambaye nilifahamiana nae sana."
Ufumbuzi wa fumbo hatarishi
Eclampsia inakadiriwa kusababisha zaidi ya vifo 70,000 vya uzazi na vifo vya vijusi 500,000 kila mwaka, huku vifo vingi vikitokana na kiharusi au uzazi kutokana na shinikizo la damu.
Kifo kutokana na sababu hizi kinaweza kutokea bila tahadhari wakati wowote wakati wa ujauzito.
Wanawake wengine hupata preeclampsia kabla ya wiki 34, wakati wengine hupata preeclampsia katika hatua ya mwisho.
Wanawake wanaweza pia kupata preeclampsia katika wiki sita za kwanza baada ya kujifungua.
Eclampsia inakadiriwa kusababisha zaidi ya vifo 70,000 vya uzazi na vifo vya vijusi 500,000 kila mwaka, huku vifo vingi vikitokana na kiharusi au uzazi kutokana na shinikizo la damu.
Kifo kutokana na sababu hizi kinaweza kutokea bila tahadhari wakati wowote wakati wa ujauzito.
Wanawake wengine hupata preeclampsia kabla ya wiki 34, wakati wengine hupata preeclampsia katika hatua ya mwisho.
Wanawake wanaweza pia kupata preeclampsia katika wiki sita za kwanza baada ya kujifungua
Wanasayansi wamegundua baadhi ya dalili kwa nini hii hutokea. Kuvimba sana, ambayo huanza ndani ya tumbo, huharibu mifumo ya mawasiliano kati ya mwili wa mama na kijusi.
Hasa, huathiri urekebishaji wa mishipa ya damu ndani ya tumbo la uzazi ili kulinda kondo , eneo ambalo husambazia kijusi virutubisho na oksijeni inayohitaji.
Mtiririko wa damu usio wa kawaida kupitia kondo la nyuma, ambayo husaidia mwili wa mama kudhibiti shinikizo la damu, hatua kwa hatua husababisha shinikizo la damu na preeclampsia.
"Wakati wa ujauzito, moyo wa mama unapaswa kusukuma damu zaidi kwa mtoto na kondo.
Kiasi cha damu inachosukuma kila dakika ni mara moja na nusu hadi mbili zaidi ya mimba ya kawaida,” alisema Ian Wilkinson, mtaalamu wa tiba na profesa katika Chuo Kikuu cha Cambridge ambaye anaongoza watafiti wa Uingereza unaoangazia Preeclampsia unaoitwa "BOBBY."
Kuna hali ambazo huongeza hatari ya kupata preeclampsia, ikiwa ni pamoja na wanawake wanaougua magonjwa ya kuwa na kinga ndogo, wajawazito wenye umri wa zaidi ya miaka arobaini, na wanawake walio na uzito mkubwa wa mwili kwa sababu hawawezi kukabiliana na uzito unaoongezeka mwilini wakati wa ujauzito.
Hata hivyo bado kuna siri kubwa kuhusu kwa nini baadhi ya wanawake wanapata preeclampsia, ambayo mara nyingi hutokea bila dalili, na kwa nini wengine haiwatokei hivyo na kwa nini viwango ni asilimia 60 zaidi kati ya wanawake weusi hasa.
Watafiti wanasema hii inaweza kuwa kutokana na lishe duni na ukosefu wa huduma za afya kutokana na ukosefu wa bima ya afya.
"Kuna ubaguzi wa kimuundo, ambapo wagonjwa wengine hawapati huduma katika hatua za mapema na uchunguzi, haswa kwa sababu ya mahali wanapopata huduma zao za afya," alisema Garima Sharma, mtaalamu mkuu wa magonjwa ya moyo na uzazi kwa wanawake katika Mfumo wa Afya wa Inova huko Fairfax, Virginia.
Wakati huo huo, Sharma anaamini kuwa hii hatoshi kueleza kwa nini hali hiyo hutokea.
Ingawa madaktari bado wanategemea sana vipengele vya hatari ya kiafya kama vile umri, rangi na historia ya matibabu ili kutathmini uwezekano wa preeclampsia, tathmini kulingana na sababu hizi hazina usahihi.
Lakini kwa ujio wa uchunguzi mpya zaidi, sahihi zaidi, wanasayansi hivi karibuni wanaweza kutambua vyema zaidi ni nani aliye hatarini zaidi na ni nini kinachoweza kusababisha.
Utaitambuaje preeclampsia
Ingawa wataalamu wa magonjwa mengine kama vile saratani au maambukizo sugu wanaweza kuchukua vipimo vya tishu za ndani za mgonjwa kwa uchunguzi zaidi, hakuna njia rahisi ya kutambua mabadiliko yanayotokea kwenye tumbo la uzazi la mwanamke mjamzito.
"Hatuwezi kuchukua mara kwa mara sampuli ya kondo la mwanamke mjamzito kwa sababu hiyo huongeza hatari ya kuharibika kwa mimba," alisema Lana McMullins, profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Teknolojia Sydney. "Na wanyama hawapati preeclampsia, kwa hivyo kutumia mifano ya panya, kwa mfano, ni vigumu sana."
Badala yake, watafiti wamelazimika kujaribu kugundua viwango visivyo vya kawaida vya molekuli fulani katika damu kama njia ya kugundua ikiwa kuna kitu kibaya.
Uchunguzi umeonyesha kuwa seli za kondo kwa wanawake walio na viwango vya juu vya uvimbe kwenye tumbo la uzazi, haswa, huonesha usambazaji dhaifu wa damu kwa kutoa protini inayojulikana kama tyrosine kinase 1 (sFlt-1).
Mara moja katika mfumo wa damu, viwango vya juu vya protini hii huwa na athari ya sumu, na kuweka kizuizi kati ya mama na kijusi kiwe rahisi zaidi kwa kuvimba.
"Protini hii huwa katika viwango takriban mara 100 zaidi ya kawaida kwa wagonjwa walio na preeclampsia," alisema Craig Mello, profesa wa biolojia katika Chuo Kikuu cha Massachusetts Medical School na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya 2006. "Kwa hivyo inaweza kutumika kama nyenzo ya uchunguzi kabla ya hatua ya kushindikana kwa chombo hicho basi mwanamke anaweza kuwa katika hatari ya kupata preeclampsia."
Mwaka jana, Thermo Fisher Scientific, kampuni ya utafiti wa kimatibabu wa sayansi ya viumbe, ilipokea idhini ya FDA kwa uchunguzi mpya wa preeclampsia. Mbinu mpya ya uchunguzi inasaidia kuharakisha maendeleo ya teknolojia za matibabu zinazotumiwa kutambua na kutibu athari kali za hali hiyo.
Katika suala hili, kifaa cha uchunguzi kinatafuta viwango vya juu vya protini sFlt-1 ikilinganishwa na viwango vya chini vya protini nyingine, viwango vya chini ambavyo ni sababu ya ukuaji wa kawaida wa placenta.
Kipimo hicho kimepangwa kutumika kutabiri kwa haraka ikiwa mwanamke mjamzito aliyelazwa hospitalini akiwa na shinikizo la damu atapatwa na preeclampsia kali ndani ya wiki mbili zijazo.
Mbinu mpya ya uchunguzi ilithibitishwa kuwa na ufanisi katika utafiti wa 2022 uliohusisha zaidi ya wanawake wajawazito 700 katika hospitali 18, na wale waliogunduliwa wakipata ufuatiliaji na huduma ya haraka kabla ya dalili kuwa mbaya zaidi.
Ingawa teknolojia mpya ya uchunguzi inaaminika sana kuokoa maisha, Cindy Anderson, profesa wa afya ya uzazi na mtoto katika Chuo Kikuu cha Uuguzi cha The Ohio State University, anahisi kuna haja ya uchunguzi wa hali ya juu zaidi ambao unaweza kutambua dalili za hatari za preeclampsia mapema.
Ikiwa dalili za mwanzo za preeclampsia zinaweza kutambuliwa kabla ya kondo la nyuma kutengenezwa kikamilifu, hali hiyo bado inaweza kuzuilika.
"Baada ya wiki tisa, kondo la nyuma hutengenezwa," Anderson alisema. "Je, tunaweza kuona dalili hizi mapema, na kisha kuingilia kati kutibu au kuzuia ugonjwa huo?"
Ili kufanikisha hili, kundi la wanasayansi linabuni teknolojia mpya ambayo imekuwa ikiendelea kwa kasi katika miaka michache iliyopita
Kipimo cha kondo
Katika maabara huko Sydney, McMullins na timu yake wanakusanya tabaka za chembe hai za kondo, zilizounganishwa pamoja, ili kuunda miundo inayofanana na tishu asilia.
Wazo lao ni kuiga baadhi ya kile kinachotokea katika hatua za mwanzo za preeclampsia nje ya mwili wa binadamu, jaribio lisilo na mfano. Timu inaita teknolojia hiyo kitaalamu "placenta-on-a-chip."
"Tulijaribu kuunda mifano ambayo inaweza kuiga kile kinachotokea katika placenta ya binadamu inapokabiliwa na hali ya preeclampsia," McMintz alisema. “Kwa mfano, tulitumia chembe za plasenta, ambazo ni tabaka za seli zinazowezesha uundaji wa kondo katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito. “
Matumaini, McClements alisema, ni kwamba siku moja utafiti utasababisha alama mpya za kibaolojia ambazo zinaweza kuunda msingi wa vipimo vya damu vya baadaye kwa wanawake wajawazito katika miezi ya mwanzo.
Lakini kuwa na mfano halisi zaidi wa preeclampsia kunaweza kurahisisha watafiti kupima matibabu yanayoweza kubadilisha mwenendo wa ugonjwa.
"Wanawake wawili kati ya watatu walio na preeclampsia wako katika hatari ya kufa kutokana na mshtuko wa moyo na ugonjwa wa moyo na mishipa," aliongeza. "Kuna hitaji la dharura la kutafuta matibabu mapya ya kuzuia magonjwa wakati na baada ya ujauzito."
Hadi sasa, matibabu pekee yaliyopendekezwa kwa wanawake wajawazito walio katika hatari kubwa ya preeclampsia ilikuwa dawa aina ya aspirin ya kiwango cha chini kuanzia wiki 12 za ujauzito na kuendelea hadi kujifungua.
Uchunguzi umeonyesha kwamba wastani wa asilimia 60 ya wanawake wanaoanza matibabu ya aspirini kabla ya wiki 16 hawana dalili za preeclampsia.
Lakini bado tuna asilimia 40 ya wagonjwa ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo, na wanawake wengi ambao hawapati matibabu yoyote kwa sababu madaktari wao hawakushuku kuwa walikuwa katika hatari ya preeclampsia.
"Kuna wagonjwa wengi ambao hawapati matibabu, na hata hawajajadiliana nao," Andrew Shennan, profesa wa masuala ya uzazi katika Chuo cha King's London London alisema.
Urejeshaji wa dawa, mchakato wa kutafuta matumizi mapya ya dawa zilizopo au ambazo hazijatumika ambazo zimeonekana kuwa salama kwa wanawake wajawazito, kunaweza kuboresha huduma ya wagonjwa wa preeclampsia, mchakato ambao unaweza kuharakishwa kwa kupima dawa hizo kwenye seli za kondo, McClements alifafanua. .
Vizuizi vya pampu ya protoni, vinavyotumiwa sana kutibu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula,kiungulia au vidonda vya tumbo, vinafikiriwa kuwa vinaweza kuzuia ukuaji wa uvimbe unaodhuru ambao husababisha hatua za mwanzo za preeclampsia.
Watafiti pia wamependekeza kuwa eculizumab, dawa ya kingamwili ya monoclonal inayotumiwa kutibu ugonjwa wa damu, inaweza kupunguza hatari ya preeclampsia ikiwa inatumiwa na wanawake wajawazito katika miezi ya mwanzo.
"Kwa sasa tunafanyia kazi metformin, dawa ya kisukari ambayo inaweza kuwa tiba inayowezekana," McClements alisema. "Kuna utafiti mzuri ambao umeonyesha kuwa metformin inaweza kuchelewesha kuzaliwa kwa mtoto katika kesi za preeclampsia kali ya mapema, na kwa hivyo inaweza kuzuia kuzaliwa kabla ya wakati."
Jaribio lingine la kuzuia ugonjwa huo ni kuacha uzalishaji wa protini inayofahamika kitaalamu kama sFlt1 kwenye kondo. Mwaka jana, FDA iliidhinisha dawa mpya ya majaribio iitwayo CBP-4888, iliyotengenezwa na kampuni ya Massachusetts inayoitwa Comanche Biopharma, kwa majaribio ya tiba.
Dawa hiyo inajulikana kama RNA inayoingilia (siRNA), ambapo inaweza kudhibiti usemi wa vinasaba na utendakazi wa seli ili kusimamisha uzalishaji wa protini maalum kwa hali hii sFlt1.
"Moja ya mambo makuu kuhusu chembechembe hizi ni maisha marefu," alisema Melo, ambaye ni mshauri wa kisayansi wa Comanche Biopharma.
"Dozi moja inaweza kudumu kutoka miezi sita hadi mwaka, kwa hivyo tunatarajia dozi moja kutosha."
Kufikia sasa, kampuni imekamilisha uchunguzi wa usalama wa dawa hiyo kwa watu waliojitolea katika umri wa kuzaa.
Kama hatua ya kusonga mbele, kampuni hiyo inalenga kuifanyia majaribio mengine miongoni mwa wanawake wajawazito 50 wenye preeclampsia, ambayo huenda ikafuatiwa na ugunduzi makubwa zaidi nchini Marekani na pengine hata Uingereza, Australia, Ujerumani, Ghana, Kenya na Afrika kusini.
Preeclampsia imeenea kwa kiasi kikubwa kwa wanawake wenye rangi ya ngozi,” alisema Allison August, afisa mkuu wa tiba kutoka kampuni ya dawa ya Comanche BioPharma. "Kwa hivyo tunapofanya tafiti zetu nchini Marekani, tunaenda kwenye vituo vya kusini mwa Chicago, Alabama na St. Louis, mahali ambapo tunajua kuna maambukizi makubwa ya preeclampsia.
Kwa sababu idadi hii ya watu ina uhitaji mkubwa wa matibabu.
Ingawa ana matumaini kuhusu baadhi ya mafanikio, McClements anatumai kuwa uwekezaji zaidi utaelekezwa kwenye utafiti wa preeclampsia katika siku zijazo kutokana na athari kubwa na mara nyingi isiyotambulika ambayo huathiri watu.
"Ukilinganisha kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya saratani, afya ya wanawake inawakilisha asilimia 1-2 tu ya hiyo. Lakini mwisho wa siku, sisi sote tunatokana na ujauzito.
Wanawake ni nusu ya idadi ya watu lakini pia ni akina mama kwa nusu nyingine. Tunajua kwamba kujifungua kwa mama aliye na preeclampsia kuna athari ya muda mrefu kwa afya ya watoto. Kwa hivyo suluhu inapaswa kupatikana,” alisema.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Yusuf Jumah