Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Julia Pastrana: Mfahamu mwanamke wa karne ya 19 ambaye uso wake ulifunikwa na nywele
Mwanamke wa karne ya 19 huko Yuropa ametajwa kuwa mwanamke mwenye sura 'mbaya zaidi' duniani.
Jina lake ni Julia Pastrana. Uso mzima wa Julia ulikuwa umefunikwa na nywele kwa sababu ya ugonjwa adimu wa maumbile.
Alikuwa akifanya kazi kama mwanasarakasi.
Julia alikufa mwaka wa 1860. Baadaye, mume wake alichukua maiti yake na kusafiri nchi mbalimbali kwa miaka mingi. Hatimaye safari yake iliishia nchini Norway.
Miaka 150 baada ya kifo cha Julia, mabaki yake yalihamishiwa nchini kwao Mexico kwa mazishi.
Mabaki ya Julia yalizikwa mwaka 2013.
Je, Julia alikuwa anaugua maradhi gani?
Julia alizaliwa mwaka wa 1834. Alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya hypertrichosis. Kutokana na ugonjwa huu alikuwa na nywele zisizo za kawaida ambazo zilikuwa zimefunika uso na taya zake.
Julia aliitwa 'tumbili' au 'dubu' na kila mtu kwa sababu ya hali hii.
Katika miaka ya 1850 alikutana na mburudishaji Theoda Lant. Baadaye walifunga ndoa. Theoda alipanga maonyesho mengi ya muziki na densi yaliyofanywa na Julia.
Julia alikufa huko Moscow mwaka 1860 baada ya kuzaa mtoto wa kiume. Alizaliwa na ugonjwa wake, mtoto aliishi siku chache tu.
Safari ya mume wake na maiti ya Julia
Hadithi ya kutisha ya Julia haikuisha na kifo. Hata baada ya kifo chake, Theoda aliendelea kusafiri kwenda nchi tofauti na mwili wake. Hatimaye alifika Norway.
Tukio jingine lilitokea mwaka wa 1976. Mabaki ya Julia yaliibiwa. Mtu alichukua maiti yake na kuitupa kwenye takataka. Lakini polisi walifanikiwa kuyapata na kuyahifadhi
Mabaki yake yalihifadhiwa baadaye katika Chuo Kikuu cha Oslo.
Mwaka 2005, msanii wa Mexico Laura Anderson Barbata alizindua kampeni ya kurudisha mwili wa Julia nchini Mexico.
"Julia anastahili nafasi katika historia, eneo lenye kumbukumbu ya dunia, haki ya kurejesha utu wake," Laura aliambia New York Times.
Kuzikwa nyumbani
Mabaki ya Julia yaliwekwa kwenye jeneza lililopambwa kwa waridi na kuzikwa katika jiji la Sinaloa de Leva, Mexico. Watu walimiminika mjini kuliona.
"Julia alikabiliwa na ukatili wa wanadamu. Jinsi alivyoishi ni fahari," Gavana wa Sinaloa Mario Lopez alisema wakati wa mazishi yake.
"Mtu hapaswi kuwa bidhaa mikononi mwa mwingine," alisema Padre Jem Reyes Retan.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla