Huenda ufumbuzi wa kichefuchefu wakati wa ujauzito ukapatikana hivi karibuni - Utafiti

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sote tumekumbana na kutapika katika hatua fulani maishani mwetu, iwe ni kutokana na hali ya kula chakula chenye sumu au pengine ni virusi vinavyoambukiza sana vinavyosababisha kutapika na kuhara maarufu kama norovirus kwa kiingereza ambayo huenea.

Na kila mtu anaweza kukubaliana kuwa ni hsli ya kutisha.

Hata hivyo, fikiria ikiwa kichefuchefu na kutapika vinavyoendelea vilitarajiwa kwa awamu muhimu katika maisha yako, na jinsi hali hiyo ingekuathiri kimwili, kiakili na kihisia.

Huu ndio ukweli wa wanawake wanne kati ya watano wanaopata kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito.

Hata kwa wanaopitia hili kwa kiasi cha wastani, hii inamaanisha dalili zisizofurahisha kama vile kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, na kutapika.

Kwa asilimia tatu ya wanawake wanaopata hali inayoitwa ‘hyperemesis gravidarum’, mambo ni mabaya zaidi, kwasababu huwa wanahitaji kulazwa hospitalini na kupata matibabu.

Hyperemesis gravidarum ni mkusanyiko wa dalili ikiwa ni pamoja na kichefuchefu kikali na kutapika ambako kwa kawaida mwanamke hawezi kula au kunywa, na hivyo kusababisha upungufu wa maji mwilini, upungufu wa virutubishi na kupungua uzito – matokeo yake ni kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Kulingana na Ofisi ya Takwimu ya Kitaifa, Mnamo 2022 hii ilisababisha karibu wanawake 20,000 kulazwa hospitalini.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo hadi hivi karibuni hakuna chochote kilichojulikana kuhusu sababu ya kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito.

Taarifa za dhana potofu zinaonyesha kuwa kadiri ulivyopata kichefuchefu na kutapika, ndivyo mimba inavyokuwa na afya njema - na hata hilo limehusishwa na idadi ya watoto ambao ulikuwa umebeba.

Hata hivyo, ushahidi wa ulimwengu halisi unaonyesha hakuna ukweli wowote kwa hili.

Ukweli ni kwamba, kuna aina mbalimbali za ukali na mifumo ya kichefuchefu na kutapika wakati wote wa ujauzito.

Ingawa mara nyingi hutambulika kama kuchafukwa na roho wakati wa ujauzito na kuhusishwa na kutokea nyakati za asubuhi, kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito vinaweza kutokea wakati wowote mchana au usiku.

Kawaida ni mbaya zaidi katika wiki 12 za kwanza na baadaye, hutulia.

Lakini kwa wanawake wengi, hili huendelea wakati wote wa ujauzito.

Hata hivyo, kumekuwa na mafanikio, baada ya zaidi ya miaka 20 ya kutafutia tatizo hili ufumbuzi kwa kutaka kujua hasa sababu ya kutokea kwa hali hii.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti huu umeendeshwa na Dk Marlena Fejzo, mtaalamu wa vinasaba katika Chuo Kikuu cha Southern California Keck School of Medicine.

Fejzo alipata hamasa ya kufanya utafiti huu tangu alipoteseka vibaya sana kutokana na kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito wake wa pili mwaka wa 1999. Hakuweza kula au kunywa bila kutapika, alipungua uzito haraka, na akawa dhaifu sana kiasi kutoweza kusimama au kutembea.

Hata hivyo, daktari wake alipingana na hilo akisema alikuwa akizidisha dalili zake ili kupata uangalizi. Hatimaye Fejzo alilazwa hospitalini na mimba ikaharibika ikiwa na wiki 15.

Akifanya kazi na kampuni ya kibinafsi, 23 and Me, ambayo huwawezesha watu binafsi kutuma sampuli zao za DNA ili kubaini afya zao na kufahamu taarifa zingine kama vile ukoo, Fejzo alifanya utafiti wa kinasaba na wanawake ambao walikuwa wajawazito hapo awali.

Alifahamu uhusiano kati ya wanawake ambao walikuwa na kichefuchefu kibaya na kutapika wakati wa ujauzito (uliohitaji mtu kuwekwa dawa kupitia njia ya mishipa) na usimbaji wa jeni kwa protini iitwayo GDF15, homoni inayofanya kazi kwenye shina la ubongo.

Uhusiano huu ulibainisha utafiti zaidi ulihitajika: kuelewa jukumu la protini ya GDF15 katika ujauzito.

GDF15 hutolewa kutoka kwa kondo la nyuma katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya ujauzito.

Pia kuna uwezekano ina jukumu la kuzuia mama asimkatae mtoto kibayolojia, na hivyo ni muhimu katika kuwezesha ujauzito kuendelea.

Hata hivyo, GDF15 imeonyeshwa kuwa kidhibiti cha uzito wa mwili na hamu ya kula kupitia ubongo. Inazalishwa kwa wingi kwa watu walio na saratani ambao wanakabiliwa na tatizo la hamu ya kula na kupoteza uzito.

Ukiongeza katika utafiti wa awali, utafiti ulioongozwa na Fejzo na Prof Sir Stephen O'Rahilly wa Chuo Kikuu cha Cambridge uliogundua kuwa viwango vya juu vya GDF15 vilipatikana kwa wanawake waliokuwa na kichefuchefu na kutapika sana wakati wa ujauzito.

Hata hivyo, athari ya homoni hii ilionekana kutegemea usikivu wa wanawake na kufichuliwa kabla ya ujauzito kwa GDF15. Wanawake ambao walikuwa na mfiduo mwingi kabla ya ujauzito hawakuwa na dalili za kichefuchefu au kutapika licha ya kuwa na viwango vya juu vya homoni ya GDF15.

Inakisiwa kuwa mfiduo wa muda mrefu wa GDF15 kabla ya ujauzito unaweza kuwa na athari ya kinga, na kufanya wanawake wasiwe na hisia ya kuongezeka kwa kasi kwa homoni inayosababishwa na mtoto anayekua tumboni.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ufahamu wa hili ni wa kipekee kabisa na hutoa sio tu uelewa na maarifa zaidi lakini pia unapendekeza matibabu yanayoweza kufanywa - kwa kuongezeka kwa mfiduo wa homoni kabla ya ujauzito, wanawake wanaweza kukosa hisia.

Kama vile jinsi baadhi ya watu hutibiwa kwa mzio wa chakula kupitia tiba ya mfiduo iliyodhibitiwa.

Kama vile kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito, hali nyingi za kawaida zinazoathiri wanawake hazieleweki vizuri licha ya kujitokeza kwa kiasi kikubwa.

Huduma ya afya ya wanawake si jambo la kawaida, na kuna mengi zaidi ya kuelewa na kujifunza kupitia aina hii ya utafiti.

Imeandikwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi