Abiria waliokwama katika treni waokolewa baada ya siku mbili

DSCX

Chanzo cha picha, Prapurao Anandan/BBC

Maelezo ya picha, Safari iliyotakiwa kukamilika kwa usiku moja ilichukua zaidi ya siku mbili
    • Author, Prapurao Anandan
    • Nafasi, BBC

Jumapili iliyopita saa 02:25 usiku treni ya kuelekea Chennai, India iliondoka kutoka kituo cha reli cha Tiruchendur. Takribani abiria 957 walikuwa wakisafiri katika treni hiyo.

Lakini wasafiri hawakujua kwamba safari iliyotakiwa kukamilika kwa usiku mmoja ingechukua zaidi ya siku mbili.

"Mvua ilikuwa ikinyesha sana. Treni iliondoka na kufika kituo cha Srivaikundam karibu saa 3:15. Treni ilisimama kwa muda mrefu katika kituo cha Srivaikundam kwa sababu ya mvua kubwa na giza pande zote," anasema abiria Suresh.

"Mvua ilinyesha sana kwa hivyo nilikuwa nikiendesha kwa uangalifu sana. Kituo cha Srivaikundam ndipo ambapo treni husimama kwa kawaida," anasema dereva wa treni hiyo, Loco Shaju.

Karibu na mji wa Dadankulam, mmomonyoko wa udongo ulitokea kwa sababu ya mvua kubwa na changarawe zote chini ya njia zilisombwa na mafuriko, na kuacha njia ya reli ikining'inia.

Habari hizo zilifikishwa mara moja kwa dereva Shaju na akaagizwa asiendeshe treni kuondoka kituo cha Srivaikundam.

Mafuriko yalikuwa makubwa na hakuna msaada uliwafikia hata baada ya alfajiri.

“Wakati abiria waliokuwa ndani ya treni wakisubiri treni nyingine ipite, baadhi ya wafanyakazi wa reli walisema kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, kokoto kwenye njia ya reli zilisombwa na maji na treni isingeendelea na safari,” alisema abiria Suresh.

Suresh anasema treni ilisimama katika kituo cha treni cha Srivaikundam kwa siku mbili mfululizo huku abiria wakiambiwa wasitoke nje ya treni kwani maji ya mafuriko yalizunguka kituo cha reli na tatizo hilo lingetatuliwa baada ya saa chache.

''Siku ya Jumatatu asubuhi, abiria walikwenda kwenye duka jirani na kununua biskuti na maandazi,” anasema Suresh.

Msaada wa Wanakijiji

DFC

Chanzo cha picha, Prapurao Anandan/BBC

Maelezo ya picha, Shirika la Reli ya Kusini limesema vikosi vya uokoaji havikuweza kufika eneo hilo kwani barabara zilivunjwa na kujaa maji

Shirika la Reli ya Kusini limesema vikosi vya uokoaji havikuweza kufika eneo hilo kwani barabara zilivunjwa na kujaa maji katika maeneo kadhaa karibu na kituo hicho. Hii ilichelewesha zaidi shughuli ya uokoaji.

Suresh anasema wanakijiji wa Srivaikundam waliwasaidia abiria wa treni kukabiliana na uhaba mkubwa wa chakula:

"Wanakijiji walipika milo mitatu kwenye hekalu la Bhadrakaliamman karibu na kituo cha treni kuanzia Jumatatu asubuhi hadi Jumanne.''

Pia, wanakijiji walikamua ng’ombe kwa ajili ya watoto na wazee waliokuwa ndani ya treni, na kwenda katika kila kichwa cha treni hiyo na kuwaomba wenye watoto wanunue maziwa kwa wanaohitaji.

Uokoaji wa Abiria Waanza

REDFC

Chanzo cha picha, Prapurao Anandan/BBC

Maelezo ya picha, Vifurushi vya chakula vilitolewa kwa helikopta asubuhi ya Jumanne
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Akiendelea, Suresh anasema, "vifurushi vya chakula vilitolewa kwa helikopta asubuhi ya Jumanne. Lakini helikopta hazikuhusika katika kuokoa mtu yeyote. Baadaye jioni, timu ya uokoaji ilifika kwenye kituo cha reli na kufunga mlango na kumpeleka kila abiria katika kijiji cha karibu cha Vellore.''

Kutoka hapo, mabasi sita yanachukua abiria hadi kituo cha reli cha Wanchi Maniachi. “Zaidi ya watu 400 bado wanasubiria katika kituo hicho,” anasema.

Suresh anasema katika maisha yake hajawahi kukumbana na janga la asili kama hilo na yeye na familia yake wameteseka sana kwa siku mbili zilizopita.

Pia, eneo wanaloishi wanakijiji waliosaidia abiria wa treni hiyo limeathirika vibaya, hakuna timu ya uokoaji iliyofika kijijini hapo hadi sasa na Suresh ameomba vikosi vya uokoaji vya serikali kwenda kijijini hapo na kuwaokoa wanakijiji walioathirika.

Akizungumza na BBC, Kitamil Maheshwari kutoka wilaya ya Mayiladuthurai, ambaye alikuwa amekwama kwenye treni, anasema, ''watoto na watu wazima waliteseka na njaa. Tuliweza tu kununua vitafunio kutoka katika maduka ya karibu.''

''Tukio hili lingeweza kuepukika ikiwa treni ingezuiwa kama tahadhari kutokana na mvua kubwa,'' anasema, na kuongeza, ''abiria wote bado wako katika hali ya wasiwasi.''

"Siku ya Jumanne asubuhi, pakiti za chakula ndizo zilitolewa kutoka katika helikopta. Hawakufanya uokoaji. Baada ya hapo, timu ya uokoaji ya reli ilikuja na kuwachukua abiria kwa mabasi," Maheshwari anasema.

"Mara tu treni ilipofika kituo cha Srivaikundam, idara ya reli ilinionya nisiendelee na safari, kwa hiyo nilisimamisha treni hapo. Tuliweza kuepuka ajali kubwa," anasema dereva Shaju.

Anasema kukaa kwa siku mbili katika kituo cha reli ni jambo lisiloweza kusahaulika na wafanyakazi wa reli hiyo walifanya kazi nzuri na wanakijiji walio karibu walisaidia sana.

''Wakati wa maafa kama haya mtu anapaswa kushukuru kwa msaada na fursa bila kulaumu wengine," anasema Shaju.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi