Mafuriko Manyara: 'Hakuna kilichobaki, watoto wetu wote wamekwenda'

Marieta amepoteza wanafamilia wanane
    • Author, Alfred Lasteck, Manyara na Lizzy Masinga, Dar es Salaam
    • Nafasi, BBC Swahili

Marieta Banga, ambaye alipoteza watu wanane wa familia katika maporomoko ya matope Wilaya ya Hanang Kaskazini mwa Tanzania anasema hakuna kilichosalia, bado ana uchungu.

Banga anasema, "Tulisikia kelele nyingi, tukakimbilia nje, tukaona matope na mafuriko. Baadaye, baada ya mvua kuacha, tulikwenda kutazama upande wa juu na kuona hakuna nyumba iliyobaki...

“…hakuna kilichosalia, na watoto wetu wote walikuwa wamekwenda. Watoto wa kaka yang, sita kati yao na mama yao pia walikuwa wametoweka. Jamaa mwingine ambaye tunakaa naye hayupo, na kufanya jumla ya watu wanane. Walisombwa na mafuriko makubwa,” anasema Banga.

Mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma ilisababisha maporomoko ya matope katika eneo la Katesh huko Hanang, na kuathiri mamia ya watu.

Wengi wa waliojeruhiwa na kufariki ni watoto na wanawake wakati maporomoko ya udongo yalipoharibu makazi kando ya mto Jorodom wilayani Hanang kaskazini mwa Tanzania.

Mamlaka ilithibitisha vifo 65, 24 kati yao wakiwa watoto, 26 walikuwa wanawake na 15 wanaume.

Wengine 117 walijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika vituo vitatu vya wilaya ya Hanang. Kati yao 56 walikuwa watoto, 31 wanawake na 30 wanaume.

Bi. Christina Bura

Christina Bura, mama aliyefiwa na mwanawe, matope yalipoporomoka ghafla alipokuwa amelala anasema;

"Mnamo saa kumi na mbili asubuhi, nilikuwa nimelala ndipo mume wangu aliponiamsha, akiuliza, 'hilo si tetemeko la ardhi?' Mimi na watoto wetu tulianza kukimbia nje, lakini tulijikuta tumezungukwa na matope kila mahali, na yalianza kutuburuta. Tulikwama kwa saa kadhaa, na wengine walikuwa wakiburutwa pembeni yetu. Tuliona ng'ombe na nyumba. Wakati wa tukio hili. , nimefiwa na mwanangu. Katika mtaa wetu, hakuna nyumba sasa, na hakuna ng'ombe. Hatuna mahali pa kuishi."

Mawe makubwa yaliyobebwa na mafuriko kutoka pande za milima yameporomoka kwenye nyumba na maduka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Hawakuua tu na kuwaacha wengine kujeruhiwa, nyumba na biashara pia hazikuweza kuhimili mtiririko wa maji ya mafuriko.

Esther Martin
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Esther Martin ni kiongozi wa Kanisa anasema asubuhi maporomoko ya udongo yaliharibu nyumba yao kwa nyuma na baadaye kuharibu kanisa lao katika mtaa huo.

Bi Esther anasema alikuwa na bahati, “Watu walikimbilia nyumbani kwetu, lakini mafuriko yalikuwa yakija. Ilitubidi kukimbia. Mume wangu na watoto walikuwa na bahati, lakini nilivutwa kwenye matope, miamba, na miti kwa karibu kilomita 2. Nilianza kuomba, nikisema sifi, na Mungu alinisaidia. Nilifanikiwa kuning'inia kwenye mti na kupanda juu."

Makazi ya muda yameanzishwa kwa ajili ya waathiriwa wa janga hilo.

Jumanne waliweka kambi ya muda katika Mkoa wa Manyara ambako waathiriwa wa mafuriko hayo ambao wengi wao nyumba zao ziliharibiwa na maafa ya mafuriko hayo walikuwa wakitafuta hifadhi.

Haya yanajiri huku timu za uokoaji zikiendelea kupakua tope na vifusi kuwatafuta waathiriwa wa mafuriko ambao huenda wamenasa humo.

Vikosi vya uokoaji pia vinatatizika kufukua vifusi vya udongo vilivyorundikana katikati mwa mji, kuharibu nyumba na kufunika magari na mali nyinginezo.

Gendabi

Mafuriko yameufanya mji mdogo uliokuwa umechangamka kuwa katika hali ya simanzi kutokana na uharibifu mkubwa wa mali.

Sabina Amsi aliyezaliwa na kuishi Katesh kwa zaidi ya miaka 50, anasema kuwa ni mara ya kwanza kupata maporomoko ya matope.

Bi Sabina, ambaye ni mfanyabiashara anasema, “Nyumba yangu iliathiriwa na maporomoko, na baada ya mvua kuisha, nilikuja kuona duka langu lilikuwa katika hali gani. Sikuweza kupata chochote. Hakuna hata kijiko nilichokuwa nikiuza.

Vifaa vingine vyote vya nyumbani ninavyotumia kuuza vyote havipo. Biashara yangu ilifikia karibu shilingi milioni 10 za Tanzania (USD 4000), na kila kitu kimekwisha. Sina kitu.”

Sababu ya maporomoko ya matope

Kijiji cha Gendabi

Mamlaka nchini Tanzania zilibaini mmomonyoko wa udongo kwenye Mlima Hanang kuwa chanzo kikuu cha maporomoko ya udongo.

Msemaji wa serikali, Mobhare Matinyi alisema mawe yaliyolegea kwenye mlima huo yalinyonya maji ya mvua na kusababisha shinikizo lililosababisha kuporomoka.

"Mlima Hanang unajumuisha mchanga wa volkeno…eneo hilo halikuweza kustahimili shinikizo hilo na hivyo sehemu ikaporomoka, na tope likaanza kutiririka kwenye mto Jorodom na kusomba miti, na kuathiri makazi kando ya mto," anasema Bw Matinyi.

Aliongeza kuwa uchunguzi uliofanywa tangu Septemba umeonesha kuwa shughuli zozote za volkano ndani ya eneo la mlima.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini limetoa tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa mwezi wa Desemba. Mlima wa Hanang ni mojawapo ya volkano nyingi za Tanzania zilizo tuli ndani ya eneo la Bonde la Ufa.

Hofu ilitanda Katesh kwamba mkasa huo unaweza kuwa mkubwa na kuongezeka kwa majeruhi kwa sababu watu wengi walikuwa bado hawajulikani walipo.

Mafuriko Manyara: Mashuhuda wazungumza

Maelezo ya video,

Imeandaliwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdala