Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, vita vya Ukraine na Urusi vinaelekea kumalizika?
- Author, Yogita Limaye
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Moshi mwingi unaonekana kwenye skrini kutoka katika kamera za ndege zisizo na rubani za Ukraine nje kidogo ya jiji la mashariki la Pokrovsk, mojawapo ya eneo la mistari ya mbele wa mapambano nchini Ukraine.
Sekunde chache kabla, makombora ya Ukraine yalishambulia maeneo yaliyo na wanajeshi wa Urusi, wakati wanajeshi hao walipokuwa wakitembea - wakijaribu kusonga mbele kuelekea kwenye barabara kuu inayoingia Pokrovsk.
Kuna mwanajeshi mmoja wa Urusi amejeruhiwa, au amefariki baada ya shambulio hilo.
Ni matokeo ya umwagaji damu katika vita ambavyo Urusi ilivianzisha. Maelfu wameuawa hadi sasa, "umwagaji damu usio koma" kama Rais wa Marekani, Donald Trump alivyosema.
Tuko katika nyumba ya vijijini iliyogeuzwa kuwa kituo cha amri cha kikosi cha 155 cha jeshi la Ukraine. Ni maili chache kutoka mstari wa mbele wa mapambano.
Kiwango cha uharibifu tunachokiona kwenye skrini ni kikubwa, nyumba na majengo yamesambaratishwa kabisa, ni uharibifu mkubwa zaidi kuliko tulivyoona miezi sita iliyopita.
Ni ushahidi wa vita vikali vya miezi kadhaa vya kuutetea mji wa Pokrovsk, mji muhimu kwa usafiri katika eneo la Donetsk.
Matumaini makubwa
Wiki hii, kuna matumaini makubwa ya kusitishwa vita, hata miongoni mwa wanajeshi wenye mashaka, kwani juhudi za kidiplomasia kutoka Marekani, Ulaya, Uturuki na nchi nyingine, zinaisukuma Urusi na Ukraine kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu.
"Nadhani kuna jambo litatokea kwani Urusi ilikuwa ya kwanza kutaka mazungumzo haya. Namaanisha tangu 2022, wamekataa kuwasiliana na yeyote," anasema afisa ambaye anataka aitwe Kozak.
"Nataka kuamini huu utakuwa mwanzo wa mwisho wa vita.
"Tumefanikiwa kuharibu maeneo yao ya vita na vituo vyao vya usambazaji vifaa. Urusi haina nguvu na sio imara kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Kwa hivyo nadhani kuna kitu kitatokea."
Yurii, 37, alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya teknolojia kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, yeye anasema. "Tunatamani vita hivi viishe. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba hatuwezi kuvizuia kwa sababu hatukuvianzisha."
Anatazama juu kwenye skrini na kuwaona askari wa Urusi wakisonga mbele tena. Yeye na wenzake wanachambua walipo na kutuma taarifa hizo kwa kitengo chao cha makombora.
Mstari wa mbele
Tunaendesha gari kutoka katika kituo hicho na kuelekea mstari wa mbele wa mapambano, katika njia yenye tope na eneo kubwa la uwanda. Matope yanaruka, huku gari letu likiteleza, tunaendesha kwa kasi kadiri iwezekanavyo.
Kasi hiyo ni mbinu ya kuzuia mashambulizi kutoka ndege zisizo na rubani, ambazo zimeongeza vifo kwa wanajeshi wa Urusi na Ukraine tangu zilipotumwa kwa wingi mwaka 2023.
Na teknolojia ya vita inazidi kubadilika. Tunapoingia kwenye eneo lenye silaha lililofichwa chini ya miti na vichaka, wanajeshi wanatayarisha shambulizi kutumia mzinga wa Ufaransa unaoitwa "Caesar." Mzinga huu ulitumwa nchini Ukraine tangu kuanza kwa vita, na Ufaransa imekuwa ikijaribu kuongeza uzalishaji wake.
Tunawauliza wanajeshi maoni yao kuhusu mapendekezo kwamba Ukraine huenda ikalazimika kutoa ardhi yake ili kupata amani.
"Inauma kusikia hivyo. Hata mimi natamani kwenda nyumbani kwa familia yangu. Binti yangu ana miaka minane na ninamkumbuka sana. Siamini kwamba tukiwaachia eneo fulani, wataacha vita, baada ya miaka kadhaa watarudi na kuanza tena," anasema Yurii.
"Mtu ambaye hajawahi kufika hapa, ambaye hajui athari ya uvamizi wa Urusi, kama wachambuzi wa viti ambao husema kuacha ardhi na vita vitaisha. Hawaelewi kamwe ni ndugu na marafiki wangapi tumepoteza. Hatupaswi kuacha hata mita moja ya ardhi yetu," anasema Kozak.
Gharama ambayo Ukraine imelipa kutetea ardhi yake inaonekana kila mahali, kuna picha za askari vijana wanaotabasamu, zimewekwa kando ya barabara kuu, kwenye kuta za ukumbusho katika viwanja katikati ya jiji, na kwenye safu za makaburi mapya yaliyochimbwa.
Kuiachia Urusi maeneo
Yana Stepanenko, amepoteza mtoto wake mwenye umri wa miaka 22. Vladislav alikuwa rubani wa droni katika jeshi la Ukraine. Aliuawa katika shambulizi la Urusi tarehe 21 Februari mwaka huu.
Kwa Yana, habari za kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja hazileti matumaini.
"Inaonekana kwangu vita hivi ni vya milele. Licha ya kuwa, natamani wapate suluhu. Kwa sababu watu wanakufa huku na kule (Urusi). Lakini Putin ana uchu. Njaa yake kwa ardhi yetu haitosheki," anasema Yana.
Baadhi ya sehemu za mkoa wa Zaporizhzhia kwa sasa ziko chini ya Urusi, mstari wa mbele wa mapigano ni chini ya maili 40 kutoka katikati ya mji. Na Urusi inataka udhibiti kamili wa mikoa ya Zaporizhzhia, Luhansk, Donetsk na Kherson kama sehemu ya makubaliano yoyote ya amani.
"Hapana. Nataka kuishi Ukraine, si Urusi. Tumeona walichofanya wakati wa uvamizi, walichokifanya katika maeneo kama Bucha - ukatili wao na mateso," anasema Yana.
"Fikiri hata eneo hili la makaburi hawajaacha kulishambulia," anazungumza, akionyesha shimo kubwa la bomu lililolipuka miezi kadhaa iliyopita.
Machozi yakimtoka, anasema, "natumai mtoto wangu hakufa bure. Kutakuwa na ushindi na Ukraine yote itakuwa huru."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi