Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanajeshi wa Ukraine hawaamini kama vita vitakoma hivi karibuni
Wakati Moscow ikizingatia usitishwaji wa vita kwa muda, vikosi vyake vya kijeshi vinaendeleza mapambano katika mstari wa mbele.
Majadiliano ya kidiplomasia yanaweza kuwa magumu na ya kasi ndogo.Lakini katika uwanja wa vita, yanaweza kupimwa kwa maisha yaliyopotea.
Katika hospitali ya kijeshi mashariki mwa Ukraine, majeruhi wanawasili kwa wingi wakiwa katika gari ya wagonjwa.
Hapa, kuna utofauti wa wazi kati ya diplomasia inayofanyika mbali na mapigano na ukatili wa vita, ambapo miili ya binadamu bado inapasuliwa, inakatwa vipande, na kuharibiwa na mabomu na risasi.
Tunaona askari wa Ukraine majeruhi takriban ishirini wakipakiwa kwenye basi ili kupelekwa hospitali huko Dnipro; baadhi wanatembea lakini wakiwa majeruhi, wengine wakiwa wamebebwa kwenye machela.
Basi hili limetengenezwa na vifaa vya matibabu ili kufuatilia majeruhi wanapohamishwa kwa mwendo kasi kwenye barabara zenye vichochoro vikali.
Wanaume walioko kwenye basi walikuwa majeruhi wasio na majeraha makubwa. Wengi waliguswa na vipande vya risasi.
Sababu ya majeraha yao ni silaha inayotumika sana na kutisha zaidi kwenye mstari wa mbele:
Hakuna hata mmoja wa askari tuliowahoji anayeamini kwamba vita hivi vitakwisha hivi karibuni.
Maksym, mwenye umri wa miaka 30, yuko kwenye machela, akipokea dawa kwa njia ya mishipa ili kupunguza baadhi ya maumivu kutokana na majeraha mengi aliyonayo mwilini mwake.
Anasema amesikia kuhusu usitishaji mapigano kwa muda wa siku 30, lakini anaongeza: "Ninamchukulia Putin kama muuaji, na wauaji hawakubaliani hivyo kirahisi."
Urusi haiwezi kuaminika
Vova, ameketi jirani, anaeleza akimaanisha uwezekano wa kusitisha mapigano: "Siamini." Anasema kuwa karibu na mji uliozingirwa wa Pokrovsk, walikuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya Urusi kila siku. "Nina shaka kutakuwa na suluhu," ananiambia.
Askari mwingine aitwaye Maksym anasema hii ni mara ya pili anajeruhiwa. "Sidhani kama kuna usitishaji mapigano," anasema. "Nilikuwa na marafiki wengi ambao hawako nasi tena."
"Ningependa kuamini kila kitu kitakuwa sawa, lakini huwezi kuamini Urusi.
Basi la matibabu linaendeshwa na Kikosi cha Matibabu cha Jeshi la Kujitolea la Ukraine, linalojulikana kama Hospitallers. Wanasafirisha makumi ya askari waliojeruhiwa kila siku.
Sofiia, mwanafunzi wa udaktari mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akifanya kazi na timu hiyo kwa muda wa miezi 18 iliyopita. Yeye, pia, ana shaka juu ya uwezekano wa kusitisha mapigano: "Siwezi kuamini, lakini ninatamani sana ingelitokea," anasema.
Ananiambia kwamba alipopata habari kwamba Marekani na Ukraine zimekubali kushinikiza kusitishwa kwa mapigano, ndege zisizo na rubani za Urusi ziliruka juu ya kambi yake na zilinaswa na vikosi vya ulinzi wa anga vya Ukraine.
Kwake, kuzungumza juu ya amani ni kama kuzungumza juu ya mambo yanayokwenda sambamba.
Sofia anasema kwamba "angalau ni vyema kwamba Ukraine na Marekani zinazungumza tena." Lakini kuhusu matumaini ya kusitisha mapigano, anaangazia yaliyopita.
"Ukiangalia majaribio yote ya kusitisha mapigano ambayo tumekuwa nayo hapo awali, hayakufaulu. Je, hili litafanikiwaje?" anauliza.
Daktari mwenzake, Daniel, alijiunga na Hospitallers kutoka Sweden. Anasema anaelewa jinsi taifa dogo linaposhambuliwa na jirani yake mkubwa. Babu yake alipigania Ufini dhidi ya Urusi wakati wa Vita vya pili vya dunia.
Daniel alipofika Ukraine, alizoea kuwauliza wanajeshi waliojeruhiwa walitaka kufanya nini baada ya vita.
Hafanyi tena. "Hakuna anayetaka kujibu hilo," anasema, "kwa sababu hawataki kukatishwa tamaa. Hawathubutu kuwa na matumaini."
Danieli hakatai usitishaji mapigano. Lakini anaongeza: "Hatuwezi kumwamini Putin kufanya jambo lolote ambalo halina faida kwake."
Ukraine ina uzoefu mkubwa wa kufanya mazungumzo na Urusi.
Ufaransa na Ujerumani zilisuluhisha usitishaji vita wa 2014 na 2015, wakati vikosi vinavyoungwa mkono na Moscow vilipochukua kwa mara ya kwanza sehemu za mashariki mwa Ukraine Crimea.
Mazungumzo hayo hayakufaulu. Wala haikuzuia Urusi kufanya uvamizi wake kamili wa Ukraine miaka minane baadaye.
Vikwazo kwenye uwanja wa vita
Kunaweza kuwa na mazungumzo ya amani, lakini wanaume wa 68th Jaeger Brigade ya Ukraine bado wanajiandaa kwa vita.
Tunatazama wakijitumia ujanja wao wa kumtoa askari aliyejeruhiwa chini ya moto uliosababishwa na upande wa adui.
Wengi tayari wamelazimika kuifanya maisha halisi.
Kwa mbali tunasikia sauti ya milio ya risasi. Tuko kilomita 16 tu kutoka mstari wa mbele, ambapo watarejea hivi karibuni.
Wamepokea taarifa chache chanya katika siku za hivi karibuni. Vikosi vya Ukraine vinavamiwa huko Kursk.
Mnamo Agosti mwaka jana, shambulio hilo la kushtukiza ndani ya eneo la Urusi lilionekana kama hatua ya busara na ya kuamsha ari.
Sasa inahatarisha kuwa kikwazo kikubwa cha kimkakati.
Kursk inaweza hivi karibuni kusitisha kuwa hoja ya mazungumzo yajayo na kuwa mzigo mzito, na kusababisha hasara zaidi kwa Ukraine.
Mojawapo ya mambo machache mazuri ni kwamba Marekani imeanza tena usaidizi wake wa kijeshi.
Hii ni muhimu kwa Brigade ya 67, ambayo inatumia vifaa vinavyotengenezwa na Marekani.
Wanaendesha mafunzo yao kwa kutumia gari la kivita la MaxxPro lililotolewa na Washington.
Ivan, dereva aliyevalia bendera ndogo ya Marekani kwenye sare yake, anasema amefarijika kwamba utawala wa Trump umekubali kubadili kikwazo hicho.
Gari lake linahitaji matengenezo ya mara kwa mara. "Natamani wangeendelea kusaidia," anasema.
Lakini Ivan bado hana uhakika kama Rais Trump anaweza kuaminiwa.
"Nina shaka," anasema. Kuhusu kumwamini Rais Putin, anajibu: "Hapana. Kamwe."
Hapa, hata usitishaji mapigano wa muda unaonekana kuwa mbali sana.