Jinsi ujumbe uliofichwa miaka 132 iliyopita kwenye chupa ndani ya ukuta wa mnara ulivyopatikana

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wahandisi wamepata chupa yenye ujumbe wa miaka 132 ndani kabisa ya kuta za mnara wa taa unaofahamika kama Corsewall Lighthouse kusini mwa Uskochi.

Chupa hiyo ilipatikana ndani ya Mnara wa taa wa Corsewall uliopo kaskazini zaidi ya eneo la mwambao wa Rhins of Galloway.

Ugunduzi huo ambao hutokea "mara moja katika maisha" unasemekana kuwa ni ujumbe wa kwanza kuwahi kupatikana kwenye chupa kwenye mnara wa Corsewall Lighthouse Uskochi.

Umeandikwa kwa kutumia ncha ya nyoya na wino, na barua hiyo iliyoandikwa tarehe 4 Septemba 1892 inaonyesha majina ya wahandisi watatu ambao waliweka aina mpya ya mwanga katika mnara huo wenye urefu wa futi 30

Pia ina majina ya walinzi watatu huo.

Chupa ya inchi 8 (20cm) iligunduliwa na Ross Russell, mhandisi wa mitambo wa taasisis ya Northern Lighthouse Board, wakati wa ukaguzi.

Aliiona baada ya kutoa paneli kwenye kabati. Timu ya wahandisi iliiondoa ndani ya mnara huo kwa kutumia kibano kilichotengenezwa kwa kamba na mpini wa ufagio.

Lakini walingoja hadi mlinzi wa mnara , Barry Miller, alipowasili kabla ya kuifungua.

" Nashukuru kwa [wahandisi] kufanya hivyo," alisema.

Chupa ina msingi usio wa kawaida wa mbonyeo, kumaanisha kuwa haiwezi kusimama wima, na imetengenezwa kwa glasi, iliyojaa viputo vidogo vya hewa.

Inafikiriwa kuwa wakati mmoja ilikuwa na mafuta.

Mfuniko wa chupa ulikuwa kizibo, ambacho kilipanuka kwa muda na kushikamana na glasi, wakati waya ulioishikilia ulipokuwa umeshika kutu.

Wanaume hao walilazimika kukata sehemu ya juu ya kizibo na kuzibua kizibo kwa uangalifu sana.

Bw Miller, mwenye umri wa miaka 77, aliambia BBC Scotland News kwamba mikono yake ilikuwa ikitetemeka alipoifungua.

"Lilikuwa jambo la kusisimua sana, ilikuwa kama kukutana na wenzetu wa zamani. Ilikuwa kama tuko nao," alisema.

"Ilikuwa kama kuwagusa. Ilikuwa ni kama wao ni sehemu ya timu yetu badala ya sisi kuwa wanne tu, sote tulikuwa tunashiriki kile walichoandika kwa sababu kilikuwa kinaonekana na unaweza kuona mtindo wa mwandiko wao.

"Ulijua walichokifanya. Walijua wameficha mahali ambacho haitapatikana kwa muda mrefu sana."

Je barua hiyo ilisema nini?

Taa hii iliwekwa na Mhandisi wa James Wells, John Westwood Millwright, James Brodie Engineer, David Scott Labourer, wa kampuni ya James Milne & Son Engineers, Milton House Works, Edinburgh, kuanzia mwezi Mei hadi Septemba na ikawashwa tena Alhamisi usiku tarehe 15. Septemba 1892.

Wafuatao wakiwa walinzi kituoni kwa wakati huu, John Wilson Principal, John B Henderson msaidizi wa 1, John Lockhart msaidizi wa 2.

Lenzi na mashine imeyotolewa na James Dove &Co Engineers Greenside Edinburgh na kujengwa na William Burness, John Harrower, James Dods. Wahandisi wenye kampuni iliyo hapo juu.

'Nilishangaa sana'

Ross Russell, kutoka eneo la Oban, ambaye aliipata chupa hiyo pamoja na wenzake Morgan Dennison na Neil Armstrong, alisema ulikuwa ugunduzi wa ajabu.

"Barua hiyo ilikuwa ya kusisimua, nilishangaa sana," Ross alisema.

"Kuwa mtu wa kwanza kugusa chupa baada ya miaka 132 lilikuwa ni jambo la kusisimua. "Ni jambo linalopatikana mara moja katika maisha."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi