Wasichana walioandika barua kwa damu yao wenyewe na kumfanya baba yao kuhukumiwa kifungo cha maisha

Miaka sita baada ya kuandika barua kwa kutumia tone la damu yake , akiomba haki kwa mamake , ambaye alichomwa moto akiwa hai , mwanamke mmmoja nchini India ameona jinsi muuaji alivyoadhibiwa.

Kutokana na ushahidi wa Latika Bansal- ambaye sasa ana umri wa miaka 21 pamoja na dadake, mahakama moja imemuhukumu baba yao na mume wa mwathiriwa Manoj Bansal kifungo cha maisha jela.

Mwanamke huyo mwenye umri mchanga alisema katika kesi hiyo kwamba baba yao alikuwa akimpiga mama yao kwa kushindwa kujifungua mtoto wa kiume.

Bansal alikana madai hayo na kusema kwamba mkewe alifariki kwa kujiua – madai ambayo mahakama ya Bulandshahr , katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh haikuamini.

Upendeleo wa mtoto wa kiume

Upendeleo wa watoto wa kiume nchini India una mizizi yake katika Imani za tamaduni tofauti duniani.

Tamaduni zinasema kwamba mtoto wa kiume atabeba sifa za familia hiyo na kuwaangalia wazazi wake uzeeni, huku watoto wa kike wakiwa hawana gharama kutokana na mahari itakayolipwa wakati wa harusi , na kwamba pia huondoka na kuacha familia zao ili kujiunga na familia za waume zao.

Wakati wa kesi hiyo ,madada hao walisema kwamba walikuwa wakimuona baba yao akimnyanyasa mama yao kwa madai ya kuzaa wasichana pekee.

Mahakama hiyo pia iliambiwa kwamba mwathiriwa alilazimishwa kuavya mimba mara sita , baada ya vipimo haramu vya kubaini jinsia ya kijusi kuonesha kwamba alikuwa na mimba ya mtoto wa kike.

Kutokana na usaidizi wa familia

Dadake anasema kwamba maisha yake yalibadilika asubuhi ya Juni 14 2016 , wakati babake – akisaidiwa na watu wengine wa familia ,ambao wanakana madai hayo , walimwagia mafuta ya taa mama yao na kumchoma moto.

''Mapema mwendo wa saa kumi na mbili na nusu alfajiri, tuliamshwa na kelele za mama yetu . Hatukuweza kumsaidia kwasababu mlango wa kuingia chumba chetu ulikuwa umefungwa kutoka nje. Tulimuona akiungua''.

Akikumbuka baada ya wito wake kwa maafisa wa polisi na huduma ya dharura kupuuzwa, latika alisema kwamba alimuita mjombake na bibi yake , ambao waliwasili haraka na kumpeleka mama yao hospitalini.

Daktari aliyemtibu Anu Bansal alidai kwamba asilimia 80 ya mwili wake ulikuwa umeungua. Kiwango cha majeraha yaliotokana na moto kilimfanya kuaga dunia.

Katika barua hiyo maarufu

Tukio hilo la mauaji lilipewa kipaumbele baada ya wasicha hao wakati huo wakiwa na umri wa miaka 15 na 11 – kuandika barua kwa kutumia damu yao kwa aliyekuwa Waziri mkuu Akhilesh Yadav , wakiwashutumu maafisa wa polisi wa eneo hilo ambao walibadilisha mashtaka kutoka mauaji hadi kujiua mwenyewe.

Afisa wa polisi alisimamishwa kazi kwa kutofanya uchunguzi wa kina kabla ya Waziri huyo mkuu kuagiza uchunguzi mpya kufanywa.

Imechukua miaka sita , mwezi mmoja na siku kumi na tatu kupata haki, Sanjay Sharma , wakili aliyewawakilisha madada hao wawili katika kesi hiyo aliambia BBC.

''Hili ni tukio nadra ambapo wasichana walianzisha kesi dhidi ya baba yao na hatimaye kupata haki'', alisema, akiongezea kwamba katika kipindi cha miaka sita , wasichnaa hao walihudhuria vikao vya kesi hiyo zaidi ya mara 100 na hakuna hata wakati mmoja walikosa kuhuduria.

Sharma alisema kwamba hakuwatoza hata shilingi moja familia hiyo kwasababu hawakuwa na raslimali na kwamba alitaka kuwavutia wanawake zaidi walionyanyaswa kwa kushindwa kujifungua Watoto wa kiume.

''Hii sio kwasababu ya mauaji ya mwanamke pekee. Ni uhalifu dhidi ya jamii'', alisema. Sio uwezo wa mwanamke kuamua kuhusu jinsia ya mtoto, hivyobasi ni kwanini anyanyaswe na kuadhibiwa? Hii ni makosa''.