Kwanini mlo wenye chumvi kidogo una athari sawa na wenye chumvi nyingi?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Wanasayansi fulani wanasema kwamba mlo wenye chumvi kidogo athari yake ni sawa na wenye chumvi nyingi.

Video ya mpishi wa Kituruki Nusrat Gökçe akinyunyiza nyama chumvi maalum imezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii kwa muda sasa, na kumpa jina la utani "Saltbee," ingawa hakufikiria kuwa tukio hilo lingevutia nadhari.

Tunapenda kula chumvi; licha ya maonyo mengi, jambo ambalo linasababisha athari mbaya kwa afya zetu.

Sodiamu, kiungo kikuu katika chumvi, ni muhimu kwa ajili ya kudhibiti usawa wa maji katika mwili, kusafirisha oksijeni na virutubisho, na kufanya ishara za umeme katika neva. Watu wengi hutumia chumvi nyingi kuliko inavyopendekezwa, na maafisa wa afya ulimwenguni pote wanafanya wawezavyo kutushawishi tule chumvi kidogo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Miongozo ya lishe inapendekeza kwamba watu wazima wasitumie zaidi ya 6g ya chumvi kwa siku. Nchini Uingereza, watu hutumia takriban 8g kwa siku na Marekani ni karibu 8.5g.

Robo tu ya chumvi tunayotumia kila siku inatokana na chumvi tunayoongeza kwenye chakula, iliyobaki iko kwenye vyakula tunavyonunua, ikiwa ni pamoja na mkate, michuzi, supu na baadhi ya nafaka za kifungua kinywa.

Hali inakuwa ngumu zaidi watengenezaji wanapoorodhesha sodiamu kwenye lebo za vyakula badala ya chumvi, jambo ambalo hutufanya tufikirie kuwa tunakula chumvi kidogo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Chumvi huundwa na ioni za sodiamu na kloridi. Kuna takriban gramu 1 ya sodiamu katika gramu 2.5 za chumvi. "Umma kwa ujumla haujui hili na wanadhani sodiamu na chumvi ni kitu kimoja. Hakuna anayekuambia hivyo," anasema May Simpkin, mtaalamu wa lishe.

Utafiti umeonyesha kuwa kula chumvi nyingi kunaweza kuongeza shinikizo la damu, ambayo inaweza kusababisha kiharusi na magonjwa ya moyo.

Wataalam wanakubali kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa madhara ya kula chumvi nyingi. Tunapokula chumvi, miili yetu huhifadhi maji na hilo huongeza shinikizo la damu hadi figo ziweze kuinyonya.

Chumvi nyingi huweka shinikizo kwenye mishipa yetu kwa muda mrefu, na kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, tatizo la shinikizo la damu linachangia 62% ya ugonjwa wa moyo na 49% ya mishipa ya damu ya moyo.

Katika uchambuzi mkubwa kulingana na tafiti 13, zilizochapishwa kwa kipindi cha miaka 35, waligundua kuwa ulaji wa gramu 5 za chumvi ya ziada kwa siku huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo na mishipa kwa 17% na hatari ya kiharusi kwa 23%.

Soma zaidi:
.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kupunguza chumvi athari yake ni tofauti. Katika utafiti wa miaka minane wa shinikizo la damu na mambo mengine ya hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa na ulaji wa wastani wa chumvi, watafiti waligundua kuwa kupunguza ulaji wa chumvi kwa gramu 1.4 kwa siku kunapunguza shinikizo la damu, na kusababisha kupungua kwa 42% kwa hatari ya kiharusi na kupunguza 40% ya vifo vya magonjwa ya moyo.

Watafiti waligundua kuwa athari za kupunguza ulaji wa chumvi ilikuwa vigumu kuzitenganisha na tabia zingine za lishe na mtindo wa maisha.

Watu wanaotazama ulaji wao wa chumvi wana uwezekano mkubwa wa kuwa na lishe bora: kufanya mazoezi zaidi; kuvuta sigara kidogo na kunywa pombe kidogo.

Majaribio ya muda mrefu ya watu wanaotumia kiasi kikubwa cha chumvi ikilinganishwa na watu wanaotumia chumvi kidogo yanaweza kubainisha sababu na athari, lakini tafiti kama hizo ni nadra kutokana na gharama za kifedha na kuzingatia maadili.

"Inaweza kuwa vigumu kufanya jaribio lililodhibitiwa bila mpangilio ambalo linaonyesha athari ya matumizi ya chumvi kwenye mwili," anasema Francesco Cappuccio, profesa wa magonjwa ya moyo katika Chuo Kikuu cha Warwick Medical School nchini Uingereza na mtafiti wa utafiti wa miaka minane.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kuna ushahidi mwingi wa uchunguzi kwa hili. Mwishoni mwa miaka ya 1960, serikali ya Japani ilipoanzisha kampeni ya kuwashawishi watu wapunguze ulaji wa chumvi, ulaji wa chumvi kila siku ulipunguzwa kutoka gramu 13.5 hadi 12 kwa siku.

Katika kipindi hicho hicho, shinikizo la damu lilishuka na kulikuwa na kupungua kwa 80% kwa vifo vya kiharusi. Nchini Finland, ulaji wa chumvi ulipungua kutoka gramu 12 mwishoni mwa miaka ya 1970 hadi gramu 9 mwaka 2002, na kusababisha kupungua kwa 75 hadi 80% kwa vifo vya kiharusi na magonjwa ya moyo katika kipindi hicho.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Tofauti ya athari ya ulaji wa chumvi

Jambo lingine linalotatiza kuhusu athari za matumizi ya chumvi kwenye shinikizo la damu na afya ya moyo ni kwamba inatofautiana kati ya mtu na mtu.

Utafiti unaonyesha kwamba hili inategemea mambo kama vile asili ya kikabila, umri, uzito wa mwili, afya, na historia ya familia.

Utafiti fulani unaonyesha kwamba watu ambao huathirika na chumvi nyingi wako katika hatari kubwa ya shinikizo la damu.

Baadhi ya wanasayansi sasa wanasema kwamba mlo wenye chumvi kidogo ni chanzo cha shinikizo la damu sawa na ule wa chumvi nyingi. Kwa maneno mengine, hatari inaongezeka kwa kila upande.

Kwa mfano, uchambuzi mkubwa uligundua uhusiano kati ya ulaji mdogo wa chumvi na ugonjwa wa moyo na kifo. Watafiti wanaamini kuwa ulaji wa chini ya gramu 6.5 au kutumia zaidi ya gramu 12.5 za chumvi kwa siku husababisha athari mbaya ya kiafya.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti mwingine wa watu zaidi ya 170,000 ulikuwa na matokeo sawa: ulaji mdogo wa chumvi wa chini ya 7.5g kwa siku ulihusishwa na hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa moyo na mishipa na kifo kwa watu wenye shinikizo la damu na bila shinikizo la damu, ikilinganishwa na ulaji wa "wastani" wa hadi 12.5g kwa siku (vijiko 1.5 hadi 2.5 vya chumvi). Kiasi hiki cha wastani ni mara mbili ya kiwango kilichopendekezwa cha chumvi nchini Uingereza.

Andrew Mente, mwandishi mkuu wa utafiti huo na mtaalam wa magonjwa ya lishe katika Chuo Kikuu cha McMaster huko Ontario, Canada, anahitimisha kuwa kupunguza ulaji wa chumvi kutoka kiwango cha juu hadi wastani hupunguza shinikizo la damu lakini hakuna faida zingine za kiafya. Kuongezeka kwa ulaji wa chumvi kutoka ulaji mdogo hadi wastani kunaweza kuwa na athari sawa.

"Kiwango cha usawa yaani katikati ndio muhimu kwa virutubisho vyovyote, kwa sababu tunatumia sana chumvi, tunakuwa na sumu mwilini, na ikiwa tunatumia chumvi kidogo sana, tunakuwa na upungufu. Kiasi bora daima ni kile cha katikati, "anasema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Sarah Stanner, mkurugenzi wa kisayansi wa Wakfu wa Lishe wa Uingereza, alisema: "Kuna ushahidi mwingi kwamba kupunguza ulaji wa chumvi kwa watu wenye shinikizo la damu kunaweza kupunguza shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Idadi ya watu wanaokula kiasi kidogo cha 3g za chumvi kwa siku ni ndogo sana. Tafiti zingine zimeonyesha kuwa kiwango hiki cha chini ni hatari kwa mwili."

Stanner anasema kuwa kwa sababu ya chumvi katika vyakula tunavyonunua, ni vigumu kubainisha ni kiasi gani cha chumvi tunachokula.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Seo Matthews, profesa wa uchumi wa afya katika Chuo Kikuu cha Lancaster, anashauri kwamba ni bora kufahamu kiwango cha chumvi kilichotumika katika lishe yetu badala ya kujaribu kupunguza kabisa.

"Matatizo ya chumvi nyingi ni sawa na matatizo ya chumvi kidogo, lakini bado tunahitaji kufanya utafiti zaidi ili kuelewa hili," anasema Matthews. "Mwili wenye afya nzuri unaweza kudhibiti kiasi kidogo cha chumvi. Tunapaswa kufahamu kuwa chumvi nyingi ni hatari, lakini hatupaswi kuiondoa kabisa katika lishe yetu."

Licha ya onyo la hivi karibuni la utafiti kuhusu hatari za vyakula vyenye chumvi kidogo, pamoja na chumvi nyingi, hitimisho bora zaidi ambalo linaweza kutolewa kutoka kwa utafiti unaopatikana ni kwamba matumizi ya chumvi kupita kiasi bila shaka huongeza shinikizo la damu.