Chumvi hufanya nini katika mwili wako?

Chanzo cha picha, Getty Images
Chumvi hufanya chakula chetu kiwe na ladha. Pia ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Sodiamu katika chumvi ni muhimu katika kudumisha kiwango sahihi cha maji katika mwili. Pia husaidia seli kunyonya virutubisho.
“Chumvi ni muhimu katika maisha,” anaeleza Paul Breslin, profesa wa sayansi ya lishe katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani.
"Chumvi ni muhimu sana kwa seli zote, ikijumuisha nyuroni zetu zote, ubongo, mgongo na misuli yetu yote. Pia ni muhimu kwa ngozi na mifupa.”
Na Profesa Breslin anaonya, ikiwa hatuna sodiamu ya kutosha tutakufa.
Upungufu wa sodiamu mwilini husababisha kuchanganyikiwa, hasira, misuli kutofanya kazi vizuri, kutapika, kukamata na koma.
Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza ulaji wa chumvi wa gramu tano kila siku, yenye gramu mbili za sodiamu.
Lakini wastani wa ulaji wa chumvi kimataifa ni karibu gramu 11 kwa siku. Hilo huongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa, saratani ya tumbo, unene, maradhi ya mifupa na ugonjwa wa figo.
WHO inakadiria watu milioni 1.89 hufa kila mwaka kutokana na matumizi ya chumvi kupita kiasi.
Wanaoongoza kutumia chumvi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika nchi nyingi, utumiaji wa chumvi kupita kiasi hutokana na kiasi kilichofichwa katika vyakula vilivyochakatwa.
Watu wa Kazakhstan hutumia karibu gramu 17 za chumvi kwa siku, zaidi ya mara tatu ya kiasi kilichopendekezwa.
Maryam anaishi Astana, mji mkuu wa Kazakhstan. Anasema, “ni kutokana na urithi wetu. Kwa karne nyingi tulizunguka misituni, tukiwa na nyama ambazo zilipaswa kuhifadhiwa kwa kutumia chumvi."
"Familia zilihifadhi nyama kwa msimu wa baridi. Wanaweza kuhifadhi ng'ombe mzima, kondoo na hata nusu farasi."
Miaka minane iliyopita, binti wa Maryam alikuwa na matatizo ya kiafya. Daktari wake alimshauri apunguze vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta na chumvi nyingi. Familia iliacha mara moja kuongeza chumvi kwenye chakula chao. Na hatimaye Familia ya Mariyam ilizoea maisha bila kuongezwa chumvi.
Chumvi mwilini

Chanzo cha picha, Getty images
Tunapokula chumvi, ladha yake hugunduliwa kwenye ulimi wetu na kaakaa laini la koo.
“Chumvi hutia nguvu mwili na akili zetu,” anasema Profesa Breslin.
Sodiamu huyeyuka kwenye mate. Kisha huingia kwenye seli za ladha na kuamsha seli moja kwa moja.
“Chumvi hupeleka mawimbi ya umeme ambayo huamsha mawazo na hisia. Kwa hivyo mwili na akili zetu huchangamka.”
Athari katika mwili

Chanzo cha picha, Maryam (contributor)
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Athari ya chumvi kwenye mwili inategemea muundo wa vinasaba wa mtu. Zaidi ya watu bilioni moja duniani kote wanakabiliwa na shinikizo la damu. Kupunguza ulaji wa chumvi kunaweza kusaidia kuzuia hilo na kutibu.
"Unapokuwa na chumvi nyingi, jambo la kwanza ambalo mwili wako hufanya ni kuiyeyusha. Kwa hivyo shinikizo la damu hupanda ili kusukuma maji ya ziada,” anaeleza Claire Collins, Profesa wa Lishe na milo katika Chuo Kikuu cha Newcastle nchini Australia.
"Ikiwa una udhaifu wowote katika mishipa yako ya damu, kama ile ya ubongo, inaweza kupasuka na kusababisha kiharusi."
Nchini Uingereza, wastani wa matumizi ya chumvi umepungua hadi gramu nane kwa siku, ambayo bado ni zaidi ya viwango vilivyopendekezwa. Upunguzaji huo unatokana na kanuni walizowekewa watengenezaji wa chakula kupunguza viwango vya chumvi.
Ulaji wa chumvi unaopendekezwa hutofautiana kutoka nchi hadi nchi. Kipimo cha mkojo kinaweza kugundua ikiwa mwili wako una chumvi nyingi au kidogo.
Namna ya kupunguza chumvi

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata kama kiwango chako cha chumvi ni cha juu, kupunguza kunaweza kuwa sio rahisi sana. Lakini Prof Collins anatuhimiza tule mkate au pasta au chakula kingine chochote ambacho kina kiwango cha chini cha chumvi.
"Ikiwa unapika chakula chako mwenyewe weka mitishamba na viungo badala ya chumvi."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












