Kujiondoa Urusi kwenye mkataba wa nafaka kutakavyo athiri bei ya chakula Afrika

Jumanne ya Julai 18, Urusi ilijiondoa katika makubaliano na Ukraine ya kuruhusu mauzo ya nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Mkataba huo unaoitwa Black Sea Grain Initiative uliotiwa saini tarehe 22 Julai 2022, uliruhusu Ukraine kusafirisha nafaka kwenda sehemu mbalimbali duniani.

Viongozi wa Afrika na duniani wamezungumzia hatua hii ambayo italeta athari kwa bei ya bidhaa za nafaka zinazozalishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala, alieleza kusikitishwa kwake kujiondoa Urusi na kusema biashara ya Bahari Nyeusi ni kwa ajili ya chakula, malisho na mbolea ambayo hufanya bei ya bidhaa kutopanda duniani.

Mchambuzi wa masuala ya uwekezaji kutoka Nigeria, Victor Aluyi alisema uamuzi huo utaathiri bei ya bidhaa za vyakula kutokana na ukweli kwamba vyakula vikuu vingi vinavyoliwa Afrika vinazalishwa kutokana na ngano.

Aluyi aliongeza uamuzi huu utaathiri Afrika kwani mataifa yake yanategemea zaidi uagizaji wa bidhaa kutoka nje na hivyo kufanya bei ya bidhaa kupanda.

Huku ni kusalitiwa

Serikali ya Kenya pia ilionyesha kusikitishwa na hatua ya Urusi na kuielezea kama ni kusalitiwa kwa watu ambao nchi zao zinakabiliwa na ukame.

Nchi hiyo iko katika eneo linalokumbwa na ukame. Zaidi ya watu milioni 50 nchini Somalia, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini wanahitaji msaada wa chakula kutokana na kukosa mvua kwa miaka kadhaa mfululizo.

Kwa nini mpango wa nafaka ni muhimu? Ukraine ni mojawapo ya wauzaji wakubwa duniani wa alizeti, mahindi, ngano na shayiri. Vizuizi vya Urusi vinamaanisha kuwa tani milioni 20 za nafaka zitakwama kwenye bandari za Bahari Nyeusi.

Vilevile, hatua hiyo inatishia kusababisha uhaba wa chakula kwa mataifa kadhaa ya Afrika na Mashariki ya Kati ambayo yanategemea sana uagizaji wa nafaka za Ukraine.

Baada ya Ukraine na Urusi kusaini makubaliano ya usafirishaji wa nafaka, bei ya chakula duniani ilishuka kwa takriban 20%, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa.

Kwa nini Urusi inakataa kusaini tena mkataba?

Wakati Umoja wa Mataifa ulipojadili makubaliano kati ya nchi hzio mbili, Urusi iliambiwa itasaidiwa kuongeza mauzo yake na nafaka na mbolea.

Ingawa mataifa ya Magharibi hayajaziwekea vikwazo bidhaa za kilimo za Urusi, Urusi inasema vikwazo vilivyowekwa dhidi ya makampuni, benki za kimataifa vinaathiri uzalishaji wa ndani.

Urusi inataka benki ya kilimo inayomilikiwa na serikali, ya Rosselkhozbank, irudishwe tena kwenye mfumo wa malipo wa haraka wa Swift. Benki ya Umoja wa Ulaya inazuia benki zote za Urusi kuwepo katika malipo ya haraka ya Swift tangu Juni 2022.

Umoja wa Mataifa ulipendekeza Urusi iunde kampuni tanzu ya benki ya kilimo, ambayo inaweza kuruhusiwa kutumia Swift - lakini Urusi ilikataa chaguo hilo. Urusi ilisema itajiunga tena na makubaliano hayo ikiwa nchi za Magharibi zitatimiza masharti yake.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema atajaribu kumshawishi rais wa Urusi Vladimir Putin kujiunga tena na makubaliano hayo watakapokutana mapema mwezi Agosti.